Na Deodatus Balile
Kashfa kubwa imeliandama Jeshi la Polisi nchini kutokana na mauaji ya kijana mfanyabiashara Musa Hamisi (25). Kuna taarifa mbili kuwa Hamisi aliuawa baada ya kuporwa Sh milioni 33.7, ilhali wengine wakisema ameporwa Sh milioni 70. Hamisi alikuwa mkazi wa Kijiji cha Ruponda, wilayani Nachingwea, mkoani Lindi. Inatajwa ameuawa Januari 5, mwaka huu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Marck Njera, kabla ya kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi, awali alisema mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 na mwili wa marehemu ulitupwa Kitongoji cha Majengo, Kijiji cha Hiari, wilayani Mtwara.
Polisi wanawashikilia Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje – Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango – Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu wa Polisi Msaidizi Nicholaus Kisinza – Mkuu wa Kikosi cha Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Mkaguzi wa Polisi John Msuya Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Juma Mbalu.
Sitanii, kabla sijaendelea kueleza nilichokisikia, naomba nimnukuu Rais Samia Suluhu Hassan katika maagizo aliyotoa wiki hii kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa: “Lakini kuna mauaji yametokea Mtwara. Na taarifa zilizopo ni kwamba jeshi lako ndilo lililofanya mauaji. Taarifa niliyonayo ni kwamba sasa jeshi limetengeneza kamati ya kufanya uchunguzi halafu walete taarifa. Haiwezekani jeshi lifanye mauaji, jeshi lichunguze lenyewe.
“Ndugu zangu wananchi na Watanzania, nimemwelekeza waziri mkuu, aunde kamati nyingine. Iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi halafu watuletee taarifa, lakini wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri nataka jeshi lako lijitafakari waone kama kinachotokea ndiyo misingi ya Jeshi la Polisi au ni vinginevyo.” Amesema watalinganisha taarifa hizi mbili ya Jeshi la Polisi na ya kamati aliyoiunda waziri mkuu, kisha waone hatua za kuchukua.
Kwa kweli hili sasa ni kaa la moto kwa polisi. Mara nyingi wananchi wamelalamika polisi kuwa wanabambikiwa kesi au polisi wanafanya mauaji ila yote hayo yalikuwa yanaoshwa na maji chini ya daraja. Polisi kimekuwa chombo pekee ambacho kinaweza kumwanzishia kesi mtu, halafu akilalamika, kusikilizwa ni kazi kweli kweli, kwa maana inabidi akalalamike kwao hao hao polisi.
Sitanii, vyanzo vyangu vimenieleza kilichotokea kwa kusema hivi: “Huyu kijana Hamisi inaelezwa kuwa alikuwa na wenzake wawili wakaiba dola huko Mwanza. Hamisi akarejea kwao Nachingwea, ila akawa anachukua kidogo anabadilisha kisha anakwenda kutanua Mtwara. Nyumbani kwao akawa ameanza kufanya ukarabati wa nyumba yao na vijana akawa anawasaidia ambao ni majirani zake.
“Siku moja akiwa Mtwara, wenzake wakamchoma. Akakamatwa na polisi. Walipomtesa akakiri kuwa na dola alizoiba na wenzake. Polisi wakamwambia awapeleke nyumbani Nachingwea. Akaondoka nao hadi Nachingwea. Alikuwa amewaambia zipo kwenye kopo na zimehifadhiwa ndani. Walipofika wakawa hawazioni. Wakamkamata baba yake, naye akapewa kibano kidogo, akasema ‘umenielekeza nizitoe ndani, kopo nimelihamishia nje.’
“Baba yake Hamisi akawapeleka nje lilipo kopo lenye dola, akawaonyesha. Inasemekana Hamisi alikuwa hata hajahesabu kiasi cha fedha zilizomo. Polisi waliondoka naye, wakaenda naye hadi Mtwara. Hapa kumbuka hawajatoa taarifa kwa RPC wa Mtwara au Lindi, wamevuka mipaka ya mikoa miwili wakaenda kufanya kazi na kurudi.
“Huyu kijana walipofika Mtwara wakampa Sh 100,000 wakamwambia ‘tawanyika, vinginevyo utapewa kesi kubwa’. Baada ya kumwambia hivyo akarudi Nachingwea. Akawaeleza vijana wenzake kilichotokea. Vijana wakamwambia ‘usikubali bora mkose nyote, kawasemee kwa mkuu wa wilaya.’
“Baada ya hapo Hamisi akaenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, akamweleza kila kitu. Mkuu wa Wilaya akamwandikia Mkuu wa Wilaya ya Mtwara barua. Kijana akaipeleka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara. Pale, vyombo vya ulinzi na usalama vikaanza kushirikishwa. Kijana akawasimulia kila kitu.
“Sasa taarifa zilizopo, hawa askari waligawana dola 4,000 kila mmoja. Walivyosikia limefika kwa wakubwa wao, wakaamua kwa pamoja wamuue huyu kijana. Taarifa zinasema wakamuua na kupeleka mwili wake porini karibu na mbuyu, ambako kuna fisi wengi, wakijua kuwa ataliwa ushahidi utapotea.
“Walipobanwa wakawapeleka askari wa uchunguzi katika eneo la tukio, zikakutwa mbavu na mguu mmoja. Kupima DNA ikaonekana ni masalia ya Hamisi. Sasa hapo iliishakuwa shida, askari wameanza kukamatwa, na ndipo huyu mmoja aliyejinyonga alipobaini kuwa jinsi alivyohusika hawezi kupona, akachukua uamuzi alioufanya.”
Sitanii, mtoa taarifa huyu anasema wakuu wa wilaya waulizwe katika uchunguzi huu, familia na wanavijiji wanaofahamu kilichotokea waulizwe na hao wakiisha kuulizwa, uchunguzi utapata majibu ya maana. Wanampongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kuelekeza Jeshi la Polisi lichunguzwe, kwani hii ni historia mpya. Mungu ibariki Tanzania.