Pyongyang

Korea Kaskazini

Korea Kaskazini imeonyesha picha inazodai kuwa zimechukuliwa kutoka katika jaribio lao la kurusha kombora lenye nguvu kubwa zaidi kuwahi kufanyika katika kipindi cha miaka mitano.

Picha hizo ambazo si za kawaida zimechukuliwa kutoka anga za mbali zikionyesha sehemu ya Rasi (peninsula) ya Korea na maeneo jirani.

Wiki iliyopita Serikali ya Pyongyang imethibitisha kufanyika kwa majaribio ya kombora linalofahamika kwa jina la ‘Hwasong-12 Intermediate Range Ballistic Missile (IRBM)’.

Likiwa katika kiwango chake cha juu kabisa, kombora hili linao uwezo wa kusafiri kwa maelfu ya kilomita, hivyo kuyaweka maeneo kama Guam yanayomilikiwa na Marekani katika dira ya kushambuliwa kirahisi. 

Majaribio ya wii iliyopita yamezusha hofu kwa jumuiya ya kimataifa. 

Katika mwezi mmoja tu wa Januari mwaka huu, Pyongyang imeweka rekodi kwa kufanya majaribio ya makombora saba – yaliyoambatana na milipuko mikubwa na ya kutisha iliyolaaniwa vikali na Marekani, Korea Kusini, Japan na mataifa mengine kadhaa. 

Tayari Umoja wa Mataifa (UN) umeshaizuia Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora na silaha nyingine za nyuklia, na kisha kuiwekea vikwazo. Lakini mara kwa mara taifa hilo lililopo mashariki mwa Bara la Asia limekuwa likipuuza. 

Jumatatu ya wiki iliyopita maofisa wa Marekani wamesema majaribio hayo ni hatua zinazohalalisha kurejeshwa upya kwa mazungumzo na Pyongyang.

Nini kilitokea katika majaribio ya Hwasong – 12?

Korea Kusini na Japan ndiyo yalikuwa mataifa ya kwanza kuripoti kufanyika kwa majaribio hayo baada ya kuyagundua kupitia mitambo yao maalumu ya kimfumo (anti-missile systems).

Wamekisia kuwa kombora hilo limeruka kwa kiwango cha kawaida cha IRBM, na kufika hadi umbali wa kilomita 800 huku likienda juu kwa umbali wa kilomita 2,000 kabla ya kutua baharini karibu na Japan. 

Likiwa kwenye kiwango chake cha juu kabisa, kombora hili linaweza kusafiri hadi umbali wa kilomita 4,000.

Majaribio hayo yamethibitishwa na Korea Kaskazini kupitia taarifa zilizosambazwa na vyombo vya habari vya umma, siku moja tu baada ya kufanyika.

Wakala wa habari wa serikali, KCNA, umesema majaribio ya kombora hilo yamefanyika ili; “kuthibitisha usahihi wake.”

Na kwamba lilielekezwa kwa makusudi kwenda kutua mbali; “kwa kuthamini usalama wa mataifa jirani.”

Wakala wa habari wa serikali ukaongeza kwa kuchapisha picha ukidai kuwa zimechukuliwa na kamera iliyowekwa kwenye ‘kichwa’ cha kombora.

Moja ya picha hizo inaonyesha wakati wa kurushwa kwa kombora na nyingine ikionyesha wazi wakati kombora likiwa katikati ya anga, likipigwa kutokea juu. 

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, hakuwapo kushuhudia kurushwa kwa kombora Jumapili ya mwisho ya Januari, tofauti na ilivyokuwa wiki tatu zilizopita, ambapo picha zilimwonyesha akishuhudia kurushwa kwa ‘hypersonic glide missile’, – kombora lililotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa zaidi kuzuia lisionekane na mitambo ya kung’amua makombora. 

Ni Korea Kusini pekee duniani ndiyo imefanya majaribio ya aina hii ya makombora; tena mara tatu!

Kwa nini Korea Kaskazini wanafanya hivi?

Mchambuzi wa Korea Kaskazini, Ankit Panda, anasema kutokuwapo kwa Rais Kim wakati wa kurushwa kwa kombora hili sambamba na lugha iliyotumiwa kwenye vyombo vya habari ni ushahidi tosha kuwa jaribio lililofanyika lililenga kuthibitisha iwapo mfumo wake unafanya kazi sawasawa na hakukuwa na lengo la kujitapa duniani kwa kuwa na teknolojia mpya. 

Hata hivyo, hii ni mara ya kwanza kwa taifa hili kurusha kombora kubwa la nyuklia tangu kufanyika kwa mazungumzo na Marekani chini ya utawala wa Rais wa zamani, Donald Trump – mazungumzo yaliyosababisha kupungua kwa shughuli za utengenezaji wa makombora.

Wakati wa mkutano wa nane wa Chama cha Congress mwezi uliopita, Kim Jong-un, amesema kuendelezwa kwa teknolojia ya kijeshi ya satelaiti na makombora yaendayo kwa kasi sana, pamoja na ndege za kushambulia zisizo na rubani (unmanned attack drones), ndiyo malengo makuu katika mipango ya miaka mitano ijayo ya taifa lake.

Tayari wamekwisha kujaribu makombora mawili yenye kasi kubwa mwezi uliopita na wataalamu wanaamini, kwa serikali kuonyesha picha zilizopigwa kutoka anga za mbali, wakati wowote watazindua satalaiti za upelelezi.

Kitendo hicho, kwa namna yoyote ile, lazima kitachukuliwa na Marekani na washirikka wake kama cha kichokozi kinachovuka mipaka. 

Satalaiti za roketi hutumia teknolojia karibu sawasawa na ile ya makombora ya kurushwa kutoka bara moja hadi jingine (intercontinental ballistic missile – ICBM) – tofauti pekee ni mzigo uliobebwa.

Picha zilizoonyeshwa na kudaiwa kuchukuliwa na kamera iliyofungwa kwenye kichwa cha kombora ni za kisasa na za aina yake, zinazoweza kuthibitisha kuwa Korea tayari wamepiga hatua kubwa katika kuingiza teknolojia kwenye makombora ya kijeshi. 

Ili kuwa na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa wa milipuko, kombora linapaswa kuhimili umbo kubwa na joto kali wakati linapokuwa likishuka kutoka angani kuelekea katika eneo lililolengwa. 

Bado wataalamu wanashikwa na kigugumizi kusema iwapo Korea Kaskazini wamefikia uwezo huo mkubwa. Lakini walau picha zinazoonyesha maeneo ya Ras ya Korea na Japan zilizopigwa kutoka anga za mbali kutawagutua majirani zao.

Kwa mara ya mwisho Hwasong-12 lilifanyiwa majaribio mwaka 2017, pale Pyongyang ilipolirusha mara sita; mara mbili kati ya hizo likirushwa kupitia anga la Kisiwa cha Hokkaido cha Japan, na kuacha hofu kubwa kwa wakazi wa kisiwa hicho.

Baada ya Rais Kim kukutana na Trump mwaka 2018, Korea Kaskazini walitangaza kusitishwa kwa muda kwa majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu. Lakini baada ya uhusiano kudorora mwaka mmoja baadaye, Kim akasema hakuna haja ya kuzingatia azimio la awali.

Wiki iliyopita, Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in, amesema kwa majaribio yaliyofanyika; “Korea Kaskazini imedhamiria kusitisha makubaliano.”

Zipo sababu nyingi za kuongezeka kwa shughuli za kijeshi kwa Korea Kaskazini mwaka huu, ambazo awali zilizinduliwa na Kim katika hotuba yake ya mwaka mpya.

Wachambuzi wanasema majaribio haya yanafanywa makusudi na Kim katika kuishinikiza Marekani kurejea kwenye meza ya mazungumzo, yakionyesha nguvu walizonazo dhidi ya mataifa mengine duniani.

Yanafanyika huku maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing inayotarajiwa kuanza wiki hii yakikamilika huku kukiwa na uchaguzi wa urais Korea Kusini mwezi ujao.

“Imekuwa ni tabia yao ya miaka mingi ya kujaribu kuwatia hofu Korea Kusini pamoja na rais ajaye,” anasema Dk. Daniel Pinkston, Profesa wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa Chuo Kikuu cha Troy anayeishi Korea Kusini.