*Malori ya mafuta yapunguziwa mizani

*Hakuna kupima bandarini, yabakizwa 3

*Hofu ya mapato yaibuka, Waziri anena

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imefuta utaratibu wa malori ya mafuta yanayokwenda nje ya nchi kupimwa katika mizani zote, badala yake sasa yatapimwa kwenye mizani isiyozidi mitatu.

Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alilotoa mwishoni mwa mwaka jana.

Tayari limeanza kutekelezwa huku likiibua furaha kwa wasafirishaji, lakini hofu kwa wakusanya mapato ya serikali wanaodhani huenda mwanya huo ukatumika kushusha mafuta katika vituo vilivyopo nchini.

Utekelezaji wa agizo hilo la waziri ulielekezwa kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kupitia barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa wakati huo, Mhandisi Joseph Malongo. 

Barua hiyo ilikuwa na kichwa cha habari: “Kupunguza msongamano kwenye mizani na kupunguza muda wa kusafiri magari yanayosafirisha mafuta.”

Sehemu ya barua hiyo inasema kila ushoroba (njia za usafirishaji mafuta) kutoka au kuingia nchini itakuwa na vituo vitatu pekee vya kupima magari hayo.

“Wizara imefanya uchambuzi wa ushoroba ambazo magari yanayosafirisha mafuta hupita zinazoanzia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na maeneo yanayohifadhiwa mafuta jijini Dar es Salaam na kupendekeza vituo vitatu vya mizani kwa kila ushoroba, kwa kuzingatia njia za safari. Magari yanayoanzia safari za Bandari ya Dar es Salaam hayatapima uzito katika mizani ya Kurasini,” imeagiza barua hiyo.

Imeagizwa kuwa malori yatakayosafirisha mafuta endapo yatabainika kuzidi uzito katika mizani inayopima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion) yataingia kwenye kituo husika cha mizani ili kuhakiki uzito.

Waziri Profesa Mbarawa amezungumza na JAMHURI na kukiri kuanza kwa mabadiliko hayo. “Ni kweli tumeanza kwa majaribio kwa mwezi mmoja, na mafanikio yake yamekuwa mazuri.”

Ingawa anasema mabadiliko hayo ni kwa malori ya mafuta yanayopelekwa nje ya nchi, kwenye taarifa ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kumewekwa mchanganuo wa shoroba kwa magari yanayoshusha shehena ndani ya nchi, pia yanayopeleka nje ya nchi.

Nje ya nchi

Vituo vya mizani vitakavyopima uzito wa magari yanayosafirisha mafuta nje ya nchi: Barabara Kuu ya Tanga-Rusumo/Kabanga/Mtukula: Kwa magari yanayoanzia Tanga kwenda Burundi na Rwanda yanapima vituo vifuatavyo: Pongwe-Njuki-Nyakahura.

Kwa magari yanayoanzia Tanga kwenda Uganda yanapima vituo vya Pongwe-Njuki –Kyamnyorwa.

Barabara ya Dar-TANZAM: Magari yanayokwenda Malawi kupitia Barabara ya Dar es Salaam-Uyole- Kasamulu yanapima vituo vya mizani vya Vigwaza-Mikumi-Uyole.

Kwa magari yanayokwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Barabara ya Dar es Salaam-Tunduma yanapima vituo vya Vigwaza-Mikumi-Mpemba.

Njia ya Kati: Kwa magari yanayokwenda Burundi na Rwanda yatapima vituo vya Vigwaza-Njuki-Mpemba. Kwa magari yanayokwenda Uganda yatapima vituo vya Vigwaza-Njuki-Kyamnyorwa.

Ndani ya nchi

Njia ya Kati: Kwa magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na Mara yanapima vituo vya Vigwaza-Njuki-Tinde.

Kwa magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Rusoma na Kabanga vituo vitakavyopima uzito ni Vigwaza-Njuki-Mwendakulima.

Kwa magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Tabora na Kigoma yanapima mizani ya Vigwaza-Itigi-Ilolanguru.

Njia ya TANZAM: Kwa magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Songea-Ruvuma yanapima Vigwaza-Mikumi-Luhimba.

Magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Tunduma na Katavi sasa yanapima vituo vya Vigwaza-Mikumi na Nkangamano.

Njia ya Kusini: Magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Mtwara yanapima mizani ya Mkuranga-Mingoyo-Ndumbwe.

Magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Songea yanapima mizani ya Mkuranga-Mingoyo-Sisi kwa Sisi.

Magari yanayoanzia Mtwara hadi Songea yanapima vituo vya Ndumbwe-Mingoyo-Sisi kwa Sisi.

Njia ya Kaskazini: Magari yanayoanzia Dar es Salaam hadi Kilimanjaro yanapima uzito vituo vya Kunduchi-Msata-Himo.

Profesa Mbarawa anasema lengo la kupunguza vituo vya kupima uzito kwa malori ya mafuta ni kupunguza msongamano na usumbufu usio wa lazima.

“Kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu, tumefanya majaribio na kuona utaratibu huu unafaa.

“Lengo letu ni kuondoa usumbufu usio wa lazima, lakini kuwavutia wafanyabiashara kutumia bandari zetu kwa kuondoa ucheleweshaji. Nakuhakikishia hatua hii itasaidia sana kuvutia wafanyabiashara,” anasema.

Kuhusu hofu ya kuwapo ushushaji mafuta njiani, Profesa Mbarawa anasema: “Hilo ni jambo la uhalifu kama uhalifu mwingine. TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wanajua namna ya kukabiliana nalo…tunawaomba na wenzetu polisi barabarani wapunguze mikono (kusimamisha magari),” anasema.

Kwa upande wa wasafirishaji, uamuzi wa serikali wa kupunguza mizani umepokewa kwa shangwe na furaha.

Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Mohamed Abdullah, amezungumza na JAMHURI na kusema wameupokea uamuzi huo kwa mikono miwili, kwa sababu hali hiyo ilikuwa vikwazo vinavyowasumbua na kuwakatisha tamaa wafanyabiashara wengi.

“Tunashukuru sana, lakini bado tunapendekeza malori ya mafuta yasipite kabisa kwenye mizani kwa sababu yanatengenezwa kwa namna ambayo huwezi kuzidisha mzigo. Wakala wa Vipimo, Shirika la Viwango – kote huko malori huwa yanahakikiwa ujazo wake.

“Kama hivyo ndivyo unaona hakuna sababu ya kupita kwenye mizani kwa sababu huwezi kuzidisha kipimo kilichokwisha kuwekwa kwenye capacity (ujazo) ya matangi ya mafuta. Uzito wa mafuta unajulikana, ni tofauti kabisa na malori ya makontena. Kenya hawana mizani kwa malori ya mafuta, tunashauri hata sisi mizani iondolewe kabisa,” anasema.

Anasema pamoja na malori, mabasi ya abiria nayo hayana sababu ya kupita kwenye mizani kwa kuwa idadi ya abiria na uzito wa mizigo vinajulikana ni tani 5.5 kwa mabasi makubwa.

“Hata kwa hiyo mizani iliyobaki tunaomba vipimo vya mizani vifanane, maana sasa ukipima Vigwaza, ukapima Mikese na baadaye Mikumi utakuta vipimo vinasoma tofauti kwa shehena ile ile moja,” anasema Abdullah.

Lakini Profesa Mbarawa anatofautiana na Abdullah kwa kusema: “Tunajua sana Watanzania ni wataalamu wa kubadili mambo, unaweza kuleta gari ambalo kitaalamu linatakiwa libebe abiria sita, lakini utashangaa gari hilo hilo limefanyiwa ujanja ujanja linabeba watu 12. Kwa hiyo tutaendelea kupima ili kuwakabilia wakorofi wachache,” anahadharisha waziri huyo.

Abdullah anatoa angalizo kwa kusema kama nchi tusibweteke kuona kuna mizigo mingi bandarini kwa sasa, kwani ipo kwa sababu kadhaa, ikiwamo ile ya wafanyabiashara kukwepa vurugu za waasi  zilizoibuka Msumbiji, na mauaji yaliyotokea Afrika Kusini.

“Sasa hivi tunaona mizigo mingi, ni jambo zuri lakini tusibweteke, tuhakikishe kero na vikwazo vya kibiashara vinaondolewa zaidi ili kuwavutia wafanyabiashara wengi,” anasema.

Hata hivyo, kumekuwapo hofu miongoni mwa baadhi ya wadau kuhusu uamuzi huu wa serikali. Baadhi ya waliozungumza na JAMHURI kwa ahadi ya kutotajwa majina yao – kutoka TRA na TANROADS – wote wameonyesha shaka.

Ofisa wa TRA aliyezungumza na gazeti hili amesema: “TRA wakiamua wizi wa mafuta ukome, utakoma; wakiamua wizi uwepo, utakuwapo. Zile lakiri zinazofungwa kwenye malori zikizingatiwa hakuna mafuta yataibwa, lakini wenzetu wanaweza kuchukua lakiri wakaifunga kwenye RAV4 (gari dogo) wakaenda nalo hadi Tunduma na kwenye mfumo ikaonekana lori la mafuta limevuka mpaka. Wengine wanafunga kwenye bodaboda. Haya huyafanya bila ushirika na watu wa TRA.”

Mwingine amesema hatua hii ya kutopima kwenye mizani, hasa mzani wa Kurasini, itasababisha mafuta mengi yaishie kwenye vituo vya Mlandizi hadi Chalinze.

“Mizani haikuwa na kazi ya kupima uzito pekee, bali kuweka rekodi za mafuta – nani anasafirisha mafuta, anasafirisha kiasi gani, yanapelekwa wapi? Kumbuka wakati wa mizani kulikuwa na upotevu mkubwa – mwaka 2013 kuna kampuni zililipa faini ya mabilioni kwa udanganyifu, sasa fikiria hakuna kupima mizani.

“Mbaya zaidi malori haya yanapimwa kwenye mizani mitatu ambayo yote ni weigh in motion, maana yake rekodi zinazobaki ni za uzito wa gari lililopita, lakini hakuna rekodi za namba za gari, dereva, uzito, shehena inakopelekwa na kadhalika.

“TRA sasa wakitaka hizo rekodi kwa ajili ya kufuatilia ukwepaji kodi hawawezi kuzipata, kwa hiyo furaha ya kuleta mfumo huu inaweza kubadilika na kuwa kilio kwa uchumi wa nchi,” kimesema chanzo chetu.

Ushushaji mafuta nchini (dumping) ni miongoni mwa matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyolikumba taifa kwa nyakati tofauti. Hali hiyo ilitajwa kama kichocheo cha kuwapo kwa utitiri wa vituo vya mafuta hasa eneo la kuanzia Kibaha hadi Mlandizi mkoani Pwani.

Biashara ya mafuta imekuwa na changamoto nyingi, zikiwamo za uchakachuaji, hali iliyoifanya serikali ipandishe bei ya mafuta ya taa ili kuzuia hali hiyo.

Kadhalika, mfanyabiashara mmoja wa mafuta anasema uwekaji rangi katika mafuta si mwarobaini wa kudhibiti udanganyifu na wizi, bali ni mradi wa ‘wakubwa’ wanaoshirikiana na wafanyabiashara.

Kumekuwapo pia hali ya sintofahamu katika kuratibu kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini hasa kutokana na kuibuka kwa vita dhidi ya mita za mafuta katika bandari za Dar es Salaam na Tanga.

Mara kadhaa zimenunuliwa mashine kwa mabilioni ya shilingi, lakini zikakwama kufanya kazi kwa kile kinachotajwa kuwa ni hujuma za kuwezesha uchepushaji takwimu halisi za mafuta.

JAMHURI limeambiwa kuwa hata mita mpya zilizofungwa hivi karibuni katika Bandari ya Dar es Salaam hazipati matengenezo kama inavyostahili, hali inayotishia uhai wake.

Kwa mujibu wa takwimu za TAT, awali wastani wa magari yanayosafirisha mafuta kwenda nje ilikuwa 100 hadi 300 kwa siku, lakini miaka kadhaa iliyopita idadi ilishuka hadi magari yasiyozidi 100 kwa siku. Hali hiyo ilisababishwa na sababu mbalimbali ikiwamo ya masharti magumu ya kibiashara yaliyowekwa na waliokuwa viongozi wa TRA.

Malori ya mafuta yaliyotengenezwa kwa chuma hubeba wastani wa lita 33,000 hadi lita 35,000. Kwa magari ambayo matangi yake yametengenezwa kwa aluminiamu ujazo wake ni lita 38,000 hadi lita 42,000. Tani moja ya mafuta ya dizeli ni lita 1,250 hadi lita 1,280. Tani moja ya petroli ni lita 1,300 hadi lita 1,350. Tani moja ya Jet A-1 (mafuta ya ndege) na mafuta ya taa ni lita 1,350. Tani moja ya IDO ni lita 1,200, tani moja ya mafuta mazito yanayotumiwa na TANESCO (HFO) ni lita 1,000; pia tani moja ya maji ni lita 1,000.

Wastani wa mafuta yanayoingizwa nchini kila mwezi ni tani 350,000 hadi 400,000. Nusu ya mafuta hayo ni kwa matumizi ya ndani ya nchi, na nusu husafirishwa nje. Kati ya hayo yanayouzwa nchini, Dar es Salaam pekee inatumia nusu ya kiwango chote cha nchi.