Mwaka mmoja uliopita tulichapisha makala hii ya aliyekuwa mmoja wa wakurugenzi wa JAMHURI, Mkinga Mkinga – akishawishi mamlaka za nchi ziinusuru Ngorongoro. Maandishi yake yameendelea kuwa muhimu hasa wakati huu ambao tishio la kuiangamiza hifadhi hiyo ya kipekee duniani likiongezeka. Kutokana na umuhimu wa maudhui, na katika kumuenzi Mkinga, tumeona ni vema tuirejee makala hii kwa manufaa ya uhifadhi nchini…

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro linahitaji uamuzi mgumu kutoka kwenye mamlaka ya Rais kulinusuru. Eneo hili la urithi wa dunia linakwenda kutoweka kutokana na kuzidiwa na idadi ya watu na mifugo.

Nasema uamuzi kutoka kwenye mamlaka ya Rais kwa sababu ambazo ziko dhahiri kwamba sheria iliyoanzisha eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatambua kwamba eneo hilo la ardhi yapo matumizi mseto.

Katika eneo hilo kunatakiwa mzani usiegemee sehemu yoyote kati ya masilahi ya wanyamapori, binadamu wanaoishi humo, na ikolojia ya eneo husika.

Mwishoni mwa Desemba, 2020 baadhi ya wahariri na waandishi wa habari waandamizi walishiriki warsha iliyoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambapo pamoja na mambo mengine, mada kadhaa ziliwasilishwa na kuonyesha namna tatizo la wingi wa watu na mifugo linavyoongezeka.

Hifadhi ya Ngorongoro ambayo imetengwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni Eneo la Urithi wa Dunia, ilianzishwa mwaka 1959 baada ya kugawanywa kwa lililokuwa Pori la Akiba la Serengeti.

Wakati wa warsha, mjadala wa tishio la Hifadhi ya Ngorongoro kuzidiwa idadi ya watu na mifugo ulianza kabla ya mada kuwasilishwa.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk. Freddy Manongi, alisema endapo hali iliyopo sasa ikiachwa iendelee kwa miaka 10, Ngorongoro itakuwa taabani.

Tayari serikali imeshaanza kuchukua hatua kadhaa ikiwamo kuundwa kwa timu ya uchunguzi mwaka jana kulikofanywa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo. Ilimaliza kazi Mei mwaka huo huo na kuwasilisha ripoti kwa waziri.

“Kitu kikubwa ambacho walishauri (nitasema kimoja) walipendekeza kitu kinaitwa zoning scheme – kwamba tujaribu kugawa eneo hili na maeneo yanayozunguka eneo hili. Tugawe katika kanda na kila kanda itathmini shughuli zinazofanyika na idadi ya shughuli za uhifadhi ndani ya eneo hilo.

“Wamependekeza tutenge maeneo, kwamba yawepo maeneo ya shughuli za maendeleo na maeneo ya shughuli za uhifadhi. Hilo ndilo jawabu… hiyo itatusaidia kutenganisha maisha ya binadamu na maisha ya wanyamapori na itawapa fursa wenyeji kuendelea kutokana na maeneo watakayokuwa wamepewa na uhifadhi nao uendelee kutokana na maeneo ambayo yatakuwa yametengwa kwa ajili ya uhifadhi,” anasema Dk. Manongi.

Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro imekipa chombo hicho dhima kuu tatu: Mosi, kusimamia uhifadhi wa wanyamapori na malikale; Pili, kuendeleza wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi, na Tatu, kuendeleza utalii.

Kwa mujibu wa sensa maalumu iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2017 idadi ya watu ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka kutoka watu 8,000 mwaka 1959 hadi takriban watu 100,000 mwaka jana.

Dk. Manongi anazungumzia hali hiyo: “Hatujui baada ya miaka 10 hali itakuwaje. Binadamu wanaendelea kuongezeka kwa sababu mbalimbali. Lile lengo la uwiano kati ya uhifadhi na maendeleo tumeona limefikia hatua mbaya kiasi kwamba mpango wowote wa uhifadhi unaathiri wenyeji na hicho si kitu kizuri; na mipango yoyote ya maendeleo ya binadamu inaathiri uhifadhi na huo ndio uwiano tuliotakiwa kuwa nao kati ya maendeleo ya binadamu na uhifadhi.

“Tumeanza kuona kwa kweli hii ‘model’ inafikia mahali pagumu. Tunajiuliza sasa tufanyeje? Hatujapata uamuzi, lakini itabidi tuendelee kufikiria jinsi ya kuelezea masuala ya maendeleo, lakini pia masuala ya uhifadhi ili tuhakikishe kwamba huo uwiano unakuwapo kwa sababu kwa kweli bila hivyo baada ya miaka 10 ninaamini model hii ya multiple use (matumizi mseto) itakuwa imefikia sehemu ngumu sana. Kwa kweli kuna haja hapa tulipo kuanza kuiangalia upya ili tuweze kufanya uamuzi mpya.

“Suala ni je, tunaweza vipi kuweka uwiano wa maendeleo endelevu ya binadamu, lakini pia maendeleo endelevu ya uhifadhi? Je, tunaweza ku-balance vipi? Nadhani mwisho wa kikao (wahariri) mtatusaidia mawazo ili kwa pamoja tuweze kuendelea na juhudi za kuangalia upya hii ‘model’.

“Kila kinachofanywa kwa manufaa ya uhifadhi kinaathiri binadamu ndani ya hifadhi, na kila ruhusa unayotoa kwa wenyeji inaathari katika uhifadhi. Ile timu imeliona kabisa hilo wazi. Na kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa wahifadhi kuhusu idadi ya watu na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu, na kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa jamii kuhusu shughuli za uhifadhi kwa maana zinawaumiza.

“Wiki iliyopita kuna diwani mmoja alinitumia picha ya fisi ameua kondoo 38, ninadhani alikuwa na ugonjwa wa rabies (kichaa), kwa hiyo wakanipigia simu wakasema fanya mpango tuzuie mambo kama haya ambayo huwezi ukayazuia kitaalamu… ni vigumu kweli kweli. Lakini si hiyo tu, kwa kweli kuna athari nyingi sana za uhifadhi zinazotukabili,” anasema.

Athari nyingine ni kuwapo kwa magugu vamizi ndani na nje ya kreta yanayosadikika kuenezwa na binadamu na mifugo.

Wakati mamlaka za nchi zikijitahidi kuinusuru Hifadhi ya Ngorongoro, baadhi ya wananchi wanaofaidika na shughuli za ufugaji katika eneo hilo wanapinga kwa nguvu zote mipango ya ama kuwapunguza au kuwaondoa hifadhini.

Ripoti ya CAG

Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka wa fedha 2018/2019 ilionyesha hatari inayoinyemelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Taarifa ya CAG inatathmini ya uwezo (Carrying capacity), hivyo inasaidia kutambua idadi ya watu, wanyama, pamoja na mimea ambayo kwa pamoja huweza kuishi katika eneo fulani bila kuharibu na kuhifadhi mazingira.

“Ukaguzi wa Hifadhi ya Ngorongoro ulibaini kwamba hakuna tathmini iliyofanyika kwa pamoja inayoonyesha uwezo au idadi ya binadamu, wanyama wafugwao, wanyamapori, pamoja na mimea ambayo huweza kuishi katika eneo hili la Hifadhi ya Ngorongoro bila kuharibu mazingira.

“Mabadiliko ya mitazamo ya watu, tamaduni na maendeleo katika jamii ndani ya eneo la Ngorongoro yameleta mkanganyiko na ugumu wa kufanya uamuzi ndani ya hifadhi, hususan kwenye suala zima la kuhakikisha wanyamapori wanaishi pamoja na binadamu bila kuharibu mazingira.

“Ninapendekeza Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ifanye upembuzi yakinifu utakaowezesha tathmini ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kujua uwezo wa bonde wa kuhifadhi watu, wanyama wafugwao, pamoja na wanyamapori na kupitia upya modeli mseto inayoruhusu binadamu, wanyama wafugwao, wanyamapori kuishi pamoja kwa kuhakikisha unalingana na uwezo wa eneo hilo na hali halisi.

Ongezeko la watu, shughuli za kibinadamu na wanyama wafugwao

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lina matumizi mbalimbali (multiple land use model) zikiwamo shughuli za kibinadamu, wanyama wa kufugwa na wanyamapori. Viumbe hawa wote kuishi pamoja katika eneo la hifadhi kama ilivyoainishwa katika Kifungu No. 3 cha Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ya Mwaka 2002.

“Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lina mchanganyiko wa binadamu pamoja na wanyamapori, jambo ambalo limeonekana kuwa si la kawaida, hivyo kuwa moja ya vivutio vya utalii na kuipa hifadhi hii sifa ya kipekee na yenye kutunzwa kwa umakini barani Afrika.

“Katika eneo hili, uhifadhi wa mazingira na maliasili unakwenda sambamba na maendeleo ya binadamu ambapo UNESCO wamelifanya eneo hili kuwa Urithi wa Dunia (The World Heritage Site).

“Pamoja na sifa za kipekee za eneo la Uhifadhi la Ngorongoro, mwingiliano kati ya wanyamapori na binadamu wa eneo hili la hifadhi unaleta changamoto zifuatazo za uhifadhi:

Uharibifu wa Mazingira

Hifadhi ya Ngorongoro imekumbana na changamoto ya uharibifu wa mazingira tangu kuanzishwa kwake mwaka 1959 kunakosababishwa na ongezeko la watu.

Taarifa ya sensa ya watu na wanyama wafugwao ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa idadi ya watu katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inakadiriwa kuwa ni zaidi ya 90,000 ikilinganishwa na idadi ya wenyeji 8,000 wakati wa kuanzishwa kwa hifadhi hiyo.

“Vivyo hivyo, idadi ya wanyama wafugwao inakadiriwa kuwa ni 799,462 ikilinganishwa na idadi ya wanyama wafugwao 261,723 waliokuwapo wakati wa kuanzisha hifadhi. Katika eneo la hifadhi, wanyama wafugwao wanashindana na kugombania malisho na wanyamapori.

Vilevile, ongezeko la wenyeji pamoja na wanyama wafugwao linaongeza shughuli za kibinadamu zinazochangia uharibifu wa mazingira. Haya ni kwa mujibu wa CAG.

Mheshimiwa Rais, ninaamini kabisa kwamba wewe ndiye huwa mtu wa kwanza kupokea taarifa ya ukaguzi ya CAG, hakika huwa unazisoma maana tumekuwa tukishuhudia hatua mbalimbali zikichukuliwa kutokana na mapendekezo yaliyomo.

Ombi mahususi kwako ni hili, iokoe Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kulinda ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti hadi kule upande wa pili wa Maasai Mara. Hifadhi zote hizo ikolojia yake inategemeana, hivyo kuiacha Ngorongoro iendelee kulemewa na watu na mifugo ni kudumaza na hatimaye kuua ikolojia ya hifadhi nilizozitaja.

Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa kazi ya kuhakikisha inaongeza idadi ya wataii kutoka milioni 2 wa sasa hadi milioni 5; pia kuhakikisha mapato yatokanayo na shughuli hiyo yanafikia au yanazidi dola bilioni 6 za Marekani. Hayo yameainishwa katika Ibara ya 67, 68 & 69 ya Ilani hiyo.

Mafanikio hayo hayawezi kufikiwa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa kuhakikisha kwamba hiyo maliasili inaendelea kulindwa kwa masilahi mapana ya Watanzania wa kizazi kilichopo na hata kijacho.