Hakuna siri kwamba taifa linapita katika kipindi kigumu, cha kutisha na kusikitisha kikiacha maswali mengi yasiyo na majibu vichwani mwa Watanzania.
Ndani ya mwezi mmoja au miwili hivi kumetokea matukio ya ajabu ajabu yanayotishia usalama wa raia na mali zao huku wenye dhamana ya usalama wakibaki kimya.
Matukio ya mauaji yanayohusisha wanafamilia yamekwenda sambamba na mauaji yanayoweza kudhaniwa kusababishwa na ushirikina au kulipa kisasi.
Kwa bahati mbaya mamlaka husika, yaani Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi, hawajatoa ufafanuzi wa kuridhisha utakaoondoa hofu na kuleta matumaini kwa raia.
Iwapo tukio la vijana watano kukamatwa na polisi Desemba 26, mwaka jana na hadi leo hawajulikani walipo linatia doa Jeshi la Polisi, basi mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara wa madini yanayodaiwa kufanywa na askari polisi yanalichafua kabisa jeshi hilo.
Haiingii akilini watu waliopewa dhamana ya kusimamia usalama wa raia na mali zao wakapewa kila nyenzo za kazi kama usafiri na silaha leo wakageuka kuwa waporaji si wa mali tu bali hata uhai wa raia hao wasio na hatia.
Taarifa ambazo hazijakanushwa na mamlaka husika zinadai kuwa maofisa wa polisi wa Mtwara wamempora madini yenye thamani kubwa mfanyabiashara mmoja kisha kumdunga sindano ya sumu.
Hizi ni tuhuma nzito na za kutisha kuliko nyingine zote zilizowahi kuelekezwa kwa Jeshi la Polisi katika miaka ya hivi karibuni. Kumdunga raia sindano ya sumu! Askari hawa waliitoa wapi sumu hiyo?
Ni nani aliyewathibitishia kuwa ingemuua mtu huyo? Je, siku hizi mbali na bunduki, polisi wanafanya doria wakiwa na sindano za sumu? Kwa ajili ya nini? Wameanza lini?
Ukimya wa viongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi unatia shaka si tu kwa uwezo wao wa kuwasimamia askari, bali pia iwapo kweli wana dhamira ya dhati ya kusimamia usalama wa raia wa Tanzania.
Matukio kama haya ya Mtwara yanasababisha raia kukosa imani na Jeshi la Polisi. Kwamba kwa sasa kukamatwa au kukutana na askari polisi ni sawa na kutekwa na majambazi, ingawa kwa hakika majambazi hawana sindano za sumu.
Inawezekana kuwa ni maadili ya askari mmoja mmoja kama binadamu, lakini iweje askari zaidi ya watano wakapanga mbinu za uporaji kisha sisi tukasema ni kosa la mtu mmoja na si taasisi?
Kwa namna yoyote ile tukio hili limemchafua Waziri wa Mambo ya Ndani, Inspekta Jenerali wa Polisi pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.
Watu hawa wanapaswa kuwajibika ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchunguzi huru utakaorejesha imani ya raia kwa askari wa Jeshi la Polisi.