Dodoma
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ana matumaini kuwa iwapo dhana ya Uchumi wa Buluu itaeleweka vema kutakuwa na nafasi nzuri ya kurekebisha na kuboresha sheria na taratibu za Mahakama katika safari ya kuujenga uchumi wa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma uliokwenda sambamba na uzinduzi wa Nembo pamoja na Bendera ya Mahakama.
Amesema kwamba kwa lugha nyingine sheria na taratibu za Mahakama zilizopo lazima ziendane na mipango iliyopo ya serikali yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia Uchumi wa Buluu.
“Mimi binafsi nitafurahi sana kama wanasheria kutoka pande zote mbili za muungano mtakuwa na mijadala ya dhati kuhusu kwa kiasi gani, sheria na taratibu za kimahakama zinavyoweza kuboresha kwa lengo la kufanikisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ya ujenzi wa Uchumi wa Buluu,” amesema Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Mwinyi amerejea kauli aliyoitoa Novemba 11, 2020 katika hotuba ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kwamba Wazanzibari hawana budi kuigeuza bahari kuwa ndilo shamba lao, kwani huko ndiko fursa za ajira za Zanzibar mpya zilizopo ambapo pia huo ndio msingi wa dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.
Amesisitiza kwamba Zanzibar haikujaaliwa ardhi kubwa kwani ni nchi ya visiwa, idadi ya watu wake ikiongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 56, ambapo mwaka 1964 Wazanzibari walikuwa laki tatu tu na sasa wapo takriban milioni 1.6.
Katika hotuba hiyo Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wanasheria na wataalamu wa sheria, viongozi wa Mahakama na watumishi wa sekta ya sheria kuielewa na kuifanyia kazi mipango mikuu ya uchumi wa Tanzania na kuwa huru kutoa ushauri wa kisheria serikalini kwa lengo la kuifanikisha.
Dk. Mwinyi amesema serikali zote mbili zinatambua kwamba zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwazo cha kufikia matarajio ya kiuchumi na ustawi wa jamii, na kwamba sheria hizo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko zifanikishe mipango ya uchumi wa kisasa.
Hivyo, amewahimiza wadau hao wa sheria kutumia utaalamu wao kuzishauri serikali kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo zina kasoro na kufanya hivyo kwa masilahi mapana ya Tanzania na Watanzania wote.
Rais Mwinyi amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar dhamira ya serikali ni kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia matumizi sahihi ya rasilimali za bahari au kama unavyofahamika Uchumi wa Buluu, ambazo ni jitihada za dhati kabisa za kujenga uchumi utakaowasaidia wananchi wa Zanzibar.
Ameeleza kwa upande wa pili ambako kuna dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupunguza umaskini na kuwa na uchumi unaolingana na ushindani wa karne ya 21.
Kutokana na juhudi hizo, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kwamba ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa dhamira na jitihada hizo za serikali zote mbili kutategemea uwezeshaji na mchango mkubwa wa sekta ya sheria, hasa kupata ushauri wa kutoka kwa wanasheria wa hapa nchini.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Sheria kukumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji wa haki.
Ameeleza kwamba amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria kwa vile anatambua kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni kuwapo kwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu, uzembe, kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili.
“Nafahamu kwamba sheria ina umuhimu mkubwa katika kujenga umoja wetu, amani yetu, udugu wetu, na pia mshikamano wetu, mafanikio ya kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji hutegemea kuwapo kwa misingi ya utawala wa sheria na uhuru wa Mahakama,” amesema Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuridhishwa na hatua ya ushirikiano iliyopo baina ya Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar, ambapo uhusiano huo ni wa muda mrefu tangu mwaka 1965.
“Nafurahi kuona kuwa ushirikiano huo unaendelezwa kwa kupeana uzoefu na utaalamu utakaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu, hivyo natoa wito kuuendeleza kwa lengo la kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji na kuongeza kasi ya ufanisi katika mahakama zetu,” amesisitiza Dk. Mwinyi.
Naye Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, ameeleza kwamba Wiki ya Sheria itakuwa na mambo mbalimbali ya kisheria hadi tarehe 29 na Siku ya Sheria itakuwa Februari 1, 2022, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Amewakaribisha wananchi kwenda katika maonyesho hayo yaliyozinduliwa na Rais Dk. Mwinyi ili waweze kupata mahitaji yao mbalimbali ya kisheria.
Jaji Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuimarisha sheria, ikiwa ni pamoja na kuimarisha Uchumi wa Buluu ambao utahitaji mabadiliko ya sheria huku akiahidi mashirikiano makubwa katika kuhakikisha dhana hiyo inafikia malengo yaliyokusudiwa sanjari na kuimarisha mashirikiano ya kimahakama kati ya pande mbili hizo.
Pia amewasisitiza wananchi kuwa na utamaduni wa kujisomea, hasa katika sheria, huku akiwataka wajitayarishe kwa kutumia mfumo wa “akili bandia” katika kutoa ushauri wa kisheria, jambo ambalo linakwenda na wakati uliopo hivi sasa pamoja na kupunguza gharama za kuendeshea kesi.
Mapema asubuhi, Rais Dk. Mwinyi aliongoza matembezi ya kilomita saba yaliyoanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki, jijini Dodoma na kupita katika maeneo mbalimbali na hatimaye kuishia katika viwanja vya ‘Nyerere Square’, ambapo Mama Mariam Mwinyi naye alishiriki kikamilifu.
Baada ya kufika katika eneo hilo la uzinduzi huo, Rais Dk. Mwinyi alitembelea mabanda ya maonyesho pamoja na kuzindua rasmi bendera na nembo ya Mahakama.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.