Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu 

Kuna nyakati mtu unabaki ukicheka tu kutokana na hali inavyokwenda. Kuna golikipa mmoja amewahi kunichekesha sana.

Huyu ni Jeremiah Kisubi, golikipa wa Simba aliyetolewa kwa mkopo kwenda kwa wakata miwa wa Morogoro, Mtibwa Sugar ya Turiani. Kwa hakika Kisubi alinichekesha sana. 

Huyu jamaa, Kisubi, alikuwa miongoni mwa makipa wa Tanzania waliofanya vizuri sana msimu uliopita. Wakati huo akiwachezea maafande wa Tanzania Prisons. 

Umahiri wake uwanjani, hasa katikati ya milingoti mitatu, ukawavutia wakubwa wengi na hatimaye mabingwa watetezi wa soka Tanzania Bara, Simba ya Dar es Salaam, wakafanikiwa kumsajili katika kikosi chao.

Ndani ya kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi, Kisubi akakutana na wataalamu wengine kama mkongwe Aishi Manula, Beno Kakolanya na bwana mdogo Ally Salum. 

Wote hawa watatu ni wazuri sana golini, kwa namna yoyote ile haikuwa ajabu pale Kasubi alipojikuta akidondoka na kuwa chaguo la tatu nyuma ya Manula na Kakolanya.

Kabla ya kupelekwa Mtibwa Sugar kwa mkopo, nilisoma sehemu fulani na kukuta Kisubi akilalamika kutaka apate nafasi ya kucheza mbele ya Manula na Kakolanya. 

Amelalamika kweli kweli na ni haki yake kama mchezaji. Kwamba anahisi akiendelea kukaa benchi kiwango chake cha soka kitaporomoka, na hii ni hoja tosha kwa kuwa ndio ukweli wenyewe. Hapo Kisubi alikuwa na hoja ya nguvu.

Ni mawazo na nia ya kila mchezaji kushirikishwa katika kikosi cha kwanza cha timu iliyomsajili. Kisubi ana akili. Tena ana akili nzuri sana. Akili yake inamwelekeza kutaka kucheza kikosi cha kwanza cha Simba. 

Ni hapo ndipo ninapotamani au kutaka kujua, hivi aliposainishwa mkataba wa kujiunga na wababe hao wa soka nchini, Simba, alielezwa nini kuhusu nafasi yake ya kucheza kikosi cha kwanza?

Nina shaka isije kuwa kumbe hata hajausoma mkataba wake vizuri! Kwamba ametazama kiasi cha fedha kilichowekwa mezani, akachanganyikiwa na kukamata peni kisha akasaini mkataba wenyewe ambao nao ulikuwa mezani. 

Inawezekana mkataba wake na Simba unamtaka awe kipa namba moja mbele ya Manula, Kakolanya na Ally. Lakini ameusoma?

Kisubi anapaswa kujua Manula ndiye kipa namba moja wa Simba na Tanzania. Lakini hii haina maana kuwa alikuwa hawezi kuwa kipa namba mbili, tatu.

Inawezekana, lakini ilikuwa lazima Manula afanye makosa mengi ya kujirudia rudia kila mara, kisha Kakolanya na Kisubi wakapandisha viwango vyao. Kufikia hapo Manula angekaa benchi na tungeanza kumuona Kisubi kikosini.

Lakini kila nikimtazama Manula sikuiona nafasi ya kina Kisubi, labda awe anaumwa. Mwalimu kumpumzisha. Hapo Kisubi angekaa hata benchi kumngoja Kakolanya. 

Kisubi amefanya uamuzi wa kuomba kwenda kwa mkopo Mtibwa Sugar ili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Abuutwalib Mshery aliyejiunga Yanga. Huu ni uamuzi mzuri aliochukua. Tumpongeze.

Kisubi ni kipa mahiri, lakini kucheza Simba kikosi cha kwanza mbele ya Manula na Kakolanya alihitaji kufanya mazoezi ya ziada katika kiwanja cha mazoezi, huku akiomba kupewa nafasi ya kuonyesha alichonacho. 

Miaka mitano nyuma, lango la Simba halikuwa katika mikono salama sana. Kipa ambaye angefanya bidii katika kiwanja cha mazoezi angepata nafasi bila shida. Muda huu maisha ni tofauti. Manula ameishika vema nafasi.

Manula  ameweka pango kubwa la ubora baina yake dhidi ya makipa wengi wa nchini; si Kakolanya, si Kisubi. Wako wengi aliowaacha mbali.