DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Swali la msingi wanalojiuliza Watanzania wengi ni nini hasa kilichowaponza Job Ndugai, Profesa Palamagamba Kabudi, William Lukuvi, Geoffrey Mwambe, Profesa Shukrani Manya na Mwita Waitara? 

Wanajiuliza wakubwa hawa walikuwa wamesukaje mkakati ambao hapana shaka umevuja na  kuwafanya wang’oke katika nafasi zao za Spika wa Bunge, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Uwekezaji, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Naibu Waziri wa Madini.    

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema wanasiasa hao wameponzwa na hekaheka za mbio za urais za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025 kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan.

Hoja ya wachambuzi hao inakaziwa na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Januari 4, mwaka huu wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa matumizi ya fedha za maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona (Covid-19) kwamba baada ya kukaa katika nafasi hiyo kwa muda wa miezi minane, alikusudia kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Kwamba alikusudia kufanya hivyo baada ya kile alichokisema kuwa ni kuwasoma kwa muda, ndipo akatoa orodha mpya ya wateule anaowaona watamsaidia kuwaletea wananchi maendeleo.

“Nimeweka watu ninaoamini mtanisaidia kazi, wakuu wa mikoa nimekuwekeni nikiamini kule nilikowakasimia madaraka mtakwenda kusimamia kazi, na wengine wote makatibu wakuu na mawaziri,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Nimekaa nadhani huu ni mwezi wangu wa nane sijui, nilisema nilikuwa nawasoma nanyi mnanisoma, na siku niliyofanya mageuzi ya mawaziri kidogo nikasema hapa nimeweka koma, kazi inaendelea. Nataka niwaambie nitatoa listi mpya hivi karibuni, wote ninaohisi wanaweza kwenda na mimi nitakwenda nao. 

“Lakini kwa wale ninaohisi ndoto zao ni kule na wanafanya kazi kwa ajili ya mwaka 2025 nitawapa nafasi waende wakajitayarishe vizuri huko nje, kwa sababu nikiwatumia ndani itawasumbua, bora niwape nafasi wakajitayarishe tukutane huko mbele ya safari.”

Pia kuhusu nchi kukopa, Rais Samia akasema: “Huwezi kuamini mtu mzima na akili yako unaenda una-argue tozo na mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kama vile ndiyo kwanza umetokea Tanzania wakati toka tumepata uhuru ni mikopo kwenda mbele na katika mikopo yote huu ni mkopo mzuri ever.

“Mtu na akili yake anakwenda kusimama ana-argue, ni uhuru wake kusema chochote, lakini ni mtu tunayemtegemea, labda atakuwa na uelewa hasa kwa sababu bajeti zote, mikopo yote na taarifa zote za kiuchumi ndani ya nyumba yake ndiyo zinapita, lakini ni 2025 fever, wasameheni. 

“Ninalotaka kuwaambia nitajitahidi kila fursa nitakayoiona ninayoweza kutumia kuleta maendeleo Tanzania nitaitumia, wala sifanyi hivi kwa ajili ya uchaguzi wa 2025. Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili aende akasimame aseme yale, ni stress ya 2025.” 

Baada ya Rais Samia kutoa kauli hiyo, Januari 6, mwaka huu Ndugai akaandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya uspika.

Katika taarifa yake, Ndugai, akasema ameandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiuzulu nafasi hiyo kisha nakala akaiwasilisha kwa Katibu wa Bunge.

Pia wachambuzi hao wanasema kilichomponza Ndugai hadi akachukua uamuzi huo ni baada ya kunukuliwa Desemba 28, mwaka jana katika mkutano wa Kikundi cha Wanyusi akihoji wanaofurahia nchi kukopa huku deni likifikia Sh trilioni 70.

“Mama ameenda kukopa shilingi trilioni 1.3 hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa, haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe?

“Tutembeze bakuli ndiyo heshima, tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku. Tukasema pitisha tozo anayetaka – asiyetaka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.

“Sasa 2025 mtaamua, mkitoa waliopo nayo sawa, waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya kuongoza nchi hivi sasa deni letu shilingi trilioni 70. Hivi nyinyi si wasomi, je, hiyo ni afya? Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” amesema Ndugai. 

Katika hatua nyingine, Rais Samia, akathibitisha kwamba anachokisema ndicho anachokimaanisha baada ya Januari 8, mwaka huu kupangua Baraza lake la Mawaziri kwa kuwateua mawaziri wapya watano na kuwateua makatibu wakuu wapya saba huku miongoni mwa aliyeachwa akiwa ni Dotto James, aliyekuwa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mabadiliko hayo yalitangazwa Jumamosi ya wiki iliyopita katika Ikulu ya Dar es Salaam na mawaziri hao walitarajiwa kuapishwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma jana.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, amewataja mawaziri wapya walioteuliwa kuwa ni Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Hamad Masauni (Mambo ya Ndani), Dk. Pindi Chana (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Angelina Mabula (Ardhi) na Hussein Bashe (Kilimo).

Huku manaibu waziri wapya ni Anthony Mavunde (Kilimo), Jumanne Sagini (Mambo ya Ndani), Dk. Lemomo Kiruswa (Madini), Ridhiwani Kikwete (Ardhi) na Atupele Mwakibete (Ujenzi na Uchukuzi).

Waliohamishwa katika wizara zao za awali na kupelekwa mpya ni Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ummy Mwalimu (Afya), George Simbachawene (Katiba na Sheria), Profesa Joyce Ndalichako (Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Innocent Bashungwa (Tamisemi). Wengine waliohamishwa ni Profesa Adolf Mkenda (Elimu), Dk. Doroth Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu), Mohamed Mchengerwa (Utamaduni, Sanaa na Michezo) na Dk. Ashatu Kijaji (Uwekezaji, Viwanda na Biashara).

Naibu mawaziri waliohamishwa wizara ni Khamis Khamis (Muungano na Mazingira), Hamad Chande (Fedha na Mipango) na Mwanaid Khamis (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu).

Huku akiwa amefanya mabadiliko ya wizara tatu na kuunda wizara mpya ikiwamo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Wizara ya Afya na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Katika hatua nyingine, wachambuzi hao wanasema kilichowaponza kina Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Kabudi aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria; Mwambe aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji; Kitila aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara; Profesa Manya aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini na Waitara aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ni kwamba kwa muda mrefu sasa ama walikuwa wanajihusisha au kushiriki moja kwa moja katika siasa za makundi ya urais wa mwaka 2025 au walikuwa karibu na watu waliokuwa wanataka kuratibu mipango hiyo.

Pia wachambuzi hao wanasema Rais Samia amewadhibiti mapema wanasiasa hao huku akirejea kile kilichofanywa na mtangulizi wake, Rais Dk. John Magufuli, pale alipowaeleza baadhi ya mawaziri kuwa hawataweza kuupata urais.

Novemba 16, mwaka juzi Magufuli katika moja ya hotuba zake aliweka wazi kuwa hakuna mtu anayepanga kuwa rais wa nchi bali wapo watu wanapanga jina lake kutokana na mienendo yake.

Magufuli alitolea mfano wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuwa hakuna aliyejua kama angekuwa Rais wa Zanzibar, kwa kuwa katika utumishi wake akiwa serikalini hakuonyesha dalili za kuutaka.

Pia alimweleza Lukuvi kuwa pamoja na kukaa muda mrefu serikalini na kuwa mjumbe wa NEC hataweza kuupata urais.

“Sina hakika kama Lukuvi atapata urais, sasa hivi umri wake ni zaidi ya miaka 60, sitaweza kupendekeza jina la mtu anayenizidi umri.

“Hata Rais Kikwete alipopendekeza jina la mgombea wa urais hakupendekeza jina linalomzidi umri, hatutaweza kupendekeza kwenye kamati kuu kupitisha rais mwenye umri mkubwa,” alisema Magufuli.

Kwa upande wa Mwambe pia anatajwa kwamba huenda kingine kilichomng’oa katika nafasi yake ni kutoelewana na baadhi ya wanasiasa wenzake.

Huku baadhi ya wachambuzi hawakushangazwa kwa sababu wakati anateuliwa kuwa waziri, Rais Samia alimtahadharisha kuhusu kuibadilisha wizara hiyo.

Katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri alilolitangaza Machi 31, mwaka jana Rais Samia alimpa miezi mitatu ya kuunda wizara hiyo huku akisema kuwa wakishindwa atawabadilisha kisha akawaonya mawaziri kutodharauliana baina yao na manaibu waziri wao.

Akinukuliwa na gazeti moja linalochapwa kila siku hapa nchini, Katibu Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema mabadiliko hayo pengine yanatokana na utii.

“Maoni ya nani kaondoka na nani kabaki, Rais Samia ameangalia wale wanaomtii, na hiyo inatunyima kufanya uchambuzi, swali gumu litabaki vile alivyonukuliwa hao waliondolewa ndio wamo katika genge la mwaka 2025.

“Rais Samia ameteua watu ambao wako tayari kumtii. Ni mabadiliko yanayoakisi kinyang’anyiro cha mwaka 2025. Hatujaona jina kubwa linalotokana na ufanisi na uwajibikaji lakini yeye anazo taarifa,” amesema Ado.  

Pamoja na mambo mengine, hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kuwaonya wale wenye nia ya mbio za urais wa mwaka 2025.

Aprili Mosi, mwaka jana, Rais Samia wakati akimuapisha Balozi Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu Chamwino jijini Dodoma na mawaziri wapya aliwataka wanasiasa hao kuacha mara moja mawazo hayo na badala yake wafanye kazi kwa maendeleo ya taifa.

Rais Samia alinukuliwa akisema kuwa ni kawaida ikifika kipindi cha pili cha Rais aliye madarakani, wanasiasa huanza harakati.

“Nafahamu 2025 iko karibu na kawaida yetu kinapoingia kipindi cha pili cha Rais aliyepo, watu kidogo mnakuwa na hili na lile kuelekea mbele, nataka kuwaambia acheni!

“Twendeni tukafanye kazi, hili na lile tutajua mbele. Rekodi yako inakufuata katika maisha yako, kuna wengine wamekosa hizi nafasi kwa rekodi zao tu. Kwa hiyo rekodi yako inakufuata kwenye maisha yako,” amesema Rais Samia.

Pia amesema hatafumba macho katika kusimamia suala hilo na kwamba kila mwenye nia ya kugombea urais, basi aache mara moja kabla hajakutana na jicho lake wakati akiangalia rekodi.

“Na mimi nitakuwa na jicho kubwa sana kuangalia rekodi zenu na safari ya mbele yetu. Lakini nataka kuwaambia kila mwenye nia ya 2025, aache mara moja,” amesema Rais Samia.