TABORA
Na Moshy Kiyungi
Wiki mbili tu baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika maisha ya mkongwe wa muziki wa Afrika na raia wa DRC, Lulendo Matumona, maarufu Le Jenerali Defao, taarifa zikasambazwa kuwa amefariki dunia.
Katika toleo la gazeti hili la Desemba 14, 2021, ukurasa huu wa burudani ulipambwa na historia ya mwanamuziki huyo aliyefariki dunia Jumatatu ya Desemba 27, mwaka jana, siku 13 tu baadaye.
Defao alifariki dunia katika Hospitali ya Laquintinie, jijini Douala, Cameroon alikokuwa amelazwa.
Sababu za kifo chake zimegubikwa na utata kufuatia taarifa tofauti zinazoeleza kwamba kimetokana na Covid-19, huku taarifa nyingine zikisema kimetokana na shinikizo la damu.
Pia kuna taarifa kuwa amefariki dunia wakati akisherehekea kutimiza miaka 63 ya kuzaliwa kwake na nyingine zimebainisha kuwa Defao aliugua kwa muda mfupi ugonjwa wa kisukari.
Defao alikuwa Cameroon kwa ajili ya kutoa burudani ya muziki wakati wa kipindi cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Mkongwe huyu alizaliwa Desemba 3, 1958 huko Kinshasa, DRC, alikuwa mwanamuziki mwenye kipaji cha kutunga na kuimba kwa sauti nyororo tofauti na mwonekano wake, akianza muziki mwaka 1976 na Orchestra Suka Movema.
Hadi mauti yanamfika, alikuwa kiongozi wa Bendi ya Big Stars ya DRC.
Defao Mutomona alipenda sana kucheza jukwaani sambamba na wanenguaji wa bendi hiyo, wakicheza mitindo mbalimbali kama ‘Ndombolo’ bila kuchoka.
Kifo chake kimewatia majonzi na huzuni baadhi ya watu wakikumbuka vifo vya ghafla vya magwiji wa muziki wakiwa kazini kama Jean de Dieu Bialu Makiese, ‘Madilu System’ aliyeanguka Agosti 10, 2007 akapelekwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kinshasa na kufariki dunia siku iliyofuata akiwa na umri wa miaka 57.
Kifo kingine cha aina hiyo ni cha Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba ‘Papa Wemba’ ambaye mara baada ya kushika kipaza sauti jukwaani, alianguka ghafla wakati akitumbuiza jijini Abdjan, Ivory Coast.
Papa Wemba alifariki dunia Aprili 24, 2016 akiwa na umri wa miaka 67.
Mnenguaji maarufu wa Empire Bakuba, mbilikimo Aiyeny Bin Tumba ‘Emoro’ alifariki dunia ghafla baada ya kudondoka huko huko Abidjan mwaka 1992.
Historia ya Defao katika muziki inaonyesha kuwa alianza kujishughulisha mwaka 1976 akiwa katika bendi ya Orchestra Suka Movema.
Baadaye akajiunga na Fogo Stars, kisha mwaka 1978 akahamia bendi ya Korotoro iliyokuwa na makazi magharibi mwa DRC.
Defao ni miongoni mwa wanamuziki waliounda bendi ya Grand Zaiko Wawa mwaka 1981 iliyokuwa ikiongozwa na mpiga gitaa mashuhuri, Pepe Felix Manuaku.
Katika kutafuta maisha, akajiunga na Ben Nyamabo kuunda kikosi kipya cha Choc Stars pamoja na Debaba, Carlito, Bozi Boziana na Djuna Djunana.
Tungo zilizotolewa na bendi hii ziliipatia umaarufu mkubwa.
Choc Stars na Orchestra Shakara Gagna Gagna zilikuwa zikiongozwa na Jeanpy Wable Gypson, zilimfanya Defao kuwa maarufu kitaifa.
Uimbaji na uwajibikaji wake jukwaani ulionyesha wazi kuwa Defao hakuwa na kipaji cha kubahatisha.
Siku zote hucheza sambamba na wanenguaji wake akiwa kivutio kikubwa kwa mashabiki, akinengua katika mitindo mbalimbali, ukiwamo ‘Ndombolo’ bila kuchoka.
Mwishoni mwa mwaka 1990, Defao aliondoka Choc Stars akidhamiria kuunda bendi yake, ndoto iliyotimia kwa kuunda bendi aliyoiita Big Stars akiwa na akina Djo Djo Bayenge, Debleu Kinanga, Adoli Bamweniko na Djo Poster aliyetokea Grand Zaiko.
Big Stars ilikuwa na wanamuziki wengi wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza muziki akiwa na mpiga solo chipukizi wakati huo, Jagger Bokoko, aliyetokea kuwa kipenzi kikubwa cha Defao.
Katika miaka mitano ya bendi hii, Defao alipata mafanikio makubwa baada ya kufyatua albumu zisizopungua 17, sita kati ya hizo ziliingia katika soko la Ulaya mwaka 1995.
Mifarakano kazini huwa haikosekani. Bendi hiyo baadaye iliteteleka baada ya kuondoka Djo Djo Bayenge na kumuacha Defao akiwa kiongozi.
Akiwa na Big Stars, Defao aliikarabati upya bendi na kutengeneza kikosi kipya chenye wanamuziki mahiri, wakimuongeza Roxy Tshimpaka kutoka Choc Stars.
Umaarufu wa Jenerali Defao ulisambaa maeneo mengi ya Afrika Mashariki na Kati miaka 1990, mashabiki wake wakiulinganisha na ule wa akina Papa Wemba, Koffi Olomide, Bozi Boziana na King Kester Emeneya.
Hapana ubishi kwamba Defao ni mwanamuziki maarufu DRC, akibebwa na nyimbo za Georgina, Fammilie Kikuta, Nadine, Bana Kongo, Oniva na Filie zilizopigwa katika mitindo ya rumba na sebene mold.
Ubovu wa usimamizi ulimfanya Defao kubadili maprodyuza na kampuni za kurekodia, wakati mwingine akitoka na matoleo ya kazi zake zile zile kwa lebo tofauti.
Defao aliivunja Big Stars mwaka 2000 akiwa Kinshasa, akaamua kwenda ‘kutanua’ Paris, Ufaransa alikorekodi albamu ya Nessy de London, akiwashirikisha akina Nyboma Mwandido, Luciana de Mingongo, Wuta Mayi, Ballou Canta na Deesse Mukangi, wakafanya onyesho kubwa lililowavutia wengi.
Defao, kwa kuwatumia waimbaji hao waalikwa, walifanya albamu ya De London kupanda chati zaidi, aliachia albamu nyingine nyingi zikiwa na nyimbo za Mandova, Ya Gege, Copinnage, Sam Samita, Salanoki Guerre De1, Animation na Nessy of London.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Defao baadaye akawa kimya katika muziki, hali hiyo iliyotokana na sintofahamu ya kisiasa nchini mwake, iliyosababisha afungiwe kupiga muziki huko DRC wakati wa utawala wa Rais Laurent Kabila.
Defao alifika Tanzania katika ziara iliyogubikwa na matatizo lukuki mwaka 2000, alizidiwa akili na ‘promota’ aliyemleta, matokeo yake alikosa fedha za kujikimu pamoja na kulipia ‘visa’ yake.
Nguli huyo alikosa hata nauli ya kumrejesha kwao hadi alipopewa ‘lift’ na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) wakati ilipozindua safari kati ya Dar es Salaam na Lubumbashi.
Baada ya subira ya muda mrefu ya mashabiki wake, mwaka 2006 gwiji huyo huyo aliibuka na albamu mpya yenye lebo ya Nzombo le Soi; na miaka minne baadaye alifyatua CD yenye lebo ya Pur Encore.
Mwaka 2012, Defao, kwa bahati nzuri alirudi uliongoni akiwa na albamu ya ‘The Undertaker’.
Mwanamuziki huyo mwaka 2018, alikuwa akisikika akifanya maonyesho mengi Nairobi nchini Kenya.
Wakati wa Krismasi ya mwaka jana, Tanzania kulifanyika onyesho kubwa la kihistoria lililojulikana kama ‘Usiku wa Rhumba Kali’, onyesho lililowakutanisha wakongwe wa muziki wa dansi.
Mipango ya awali ya waandaaji wa onyesho hilo walipanga kuwakutanisha wakongwe wa Tanzania na wenzao wa DRC.
Kati yao jina la Defao lilikuwamo ambapo Novemba mwaka jana, mmoja wa waratibu wa Usiku wa Rhumba Kali, alizungumza naye kwa njia ya simu akimualika ili awe mmoja wa wanamuziki wageni mashuhuri.
Alikubali mwaliko na kusema atahudhuria bila kuhitaji malipo yoyote, ila tu gharama za kujikimu zitakazopangwa na waandaaji.
“Watanzania ni rafiki zangu, nitakuja kuimba pamoja na ninyi. Nitaimba Sala Noki, Kolza na Abdallah,” Defao alimwambia mmoja wa waratibu aliyewasiliana naye.
Bahati mbaya kamati ya maandalizi ilishindwa kupata wadhamini au wadau wa kulipia tiketi na gharama za kujikimu kwa kuwa malazi haikuwa shida kwa kuwa Hoteli ya Nefaland iliyopo Manzese Argentina ilikuwa tayari.
Mpango wa kumleta Defao ukafeli. Endapo mpango huo ungefanikiwa, basi Defao asingekwenda Cameroun na kufia huko, bali angetumbuiza Dar es Salaam sambamba na kina Tshimanga Assosa, Nguza Vicking na Komandoo Hamza Kalala. Na huenda hata asingefariki dunia.
Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi. Amina.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.
Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0767331200 na 0736331200.