Leo tunatimiza miaka 33 tangu kuuawa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Sheikh Abeid Amani Karume. Ni mojawapo ya matukio makubwa katika historia ya Zanzibar na historia ya Tanzania kwa ujumla. Maadhimiisho kama haya yanakuwa na madhumuni kadhaa, lakini napenda kuzungumzia historia kama nyenzo ya kujenga kinga ya uhuru wa kitaifa.
Historia ya taifa inaundwa na matukio yaliyopita na namna yale matukio yanavyohusishwa na watu wa taifa husika. Lakini fasili hii haihusishi matukio pekee, bali inajumuisha kumbukumbu, uvumbuzi, upangaji, uwasilishaji, na – muhimu sana – uchambuzi wa taarifa zinazohusu matuko yenyewe.
Hiki kipengele cha mwisho kinafanya matukio yale yale ya historia kubadilika kutegemea ni nani anayaandika. Lakini pamoja na kuwapo kwa kupindisha ukweli kwenye matukio ya kihistoria, bado yanaweza kubaki maeneo ambayo historia husimama yenyewe imara bila kuyumbishwa na matakwa ya wale wenye kukusudia kubadilisha ukweli. Hapa ni pale historia inakubalika kwa makundi ambayo hayakubaliani kuhusu vipengele vyote vya historia.
Matukio ya kihistoria mara nyingi yanahusisha watu katika nafasi mbalimbali ndani ya jamii. Ni watu na jinsi wanavyokabiliana na matukio ya nyakati zao, zaidi ya matukio yenyewe, ndiyo huumba historia.
Tunapozungumzia viongozi wetu waliotangulia, na hapa sizungumzii Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume pekee, wao nao wanachukuwa sehemu kubwa ya unapoelekea mkondo wa historia ya Tanzania. Wakati wa uongozi wao walichukuwa uamuzi ambao leo ni sehemu ya historia yetu. Lakini tunatambua kuwa ni binadamu kama mimi na wewe na hivyo hawatahusishwa mara zote na matukio chanya kwenye historia ya Tanzania.
Hata hivyo, kasoro zilizopo zisituzuie kutambua mambo muhimu ambayo wamefanya kusaidia kujenga Taifa la Tanzania. Itakuwa ni kosa kubwa mno kwa viongozi waliofuata baada yao kuacha kuona uongozi kama mwendelezo wa yale yaliyotarajiwa na wananchi wa Tanganyika baada ya tarehe 9 Desemba 1961, na yale yaliyotarajiwa na wananchi wa Zanzibar baada ya tarehe 12 Januari 1964; na badala yake kuona uongozi uliofuata kama nguzo inayoweza kusimama peke yake.
Kwa mfano mwingine, litakuwa ni kosa la kuona uongozi kama nafasi ya kuanza kujenga nyumba nyingine kwenye kiwanja kipya badala ya kuona uongozi kama fursa ya kuendeleza jengo ambalo tayari lilianza kujengwa kwenye miaka ya mwanzoni ya 1960.
Hatuwezi kudharau shinikizo kutoka nje ambazo zinatusukuma kila wakati kutafuta viwanja vipya vya kujenga utaifa na kuacha misingi ikiota majani, lakini kwa kukubali au kushindwa kusimama wenyewe; tunahatarisha uhuru wetu kama jamii na kama taifa.
Uhuru huu unaweza kuimarishwa iwapo tutaangalia historia yetu na kuibua watu na matukio ambayo tutayatunza kama hazina ya kutujengea imani kuwa tunao uwezo wa kukabili changamoto zinozotukabili.
Mojawapo ya maazimio yaliyopitishwa kwenye Mkutano wa Nane wa Umujumui wa Afrika uliofanyika Ghana mwezi uliopita ni kuhimiza Waafrika na watu wa asili ya Kiafrika kujipenda. Ni neno dogo lakini lina maana kubwa. Maana yake pana ni kuwa kama Waafrika na watu wa asili ya Afrika wanauonea aibu Uafrika wao, basi bila shaka ni watu ambao hawataweza kuona historia yao kama eneo muhimu la kuibua kumbukumbu ambazo zimewaficha watu na matukio ambayo yametoa mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali kama vile utamaduni, sayansi, siasa, na masuala ya jamii.
Usipojikubali, basi si ajabu hutayaona masuala chanya ndani ya utamaduni wako, ndani ya jamii yako, na – muhimu sana kwangu – ndani ya historia yako. Utatapatapa kutafuta kujishikiza kwenye utamaduni ambao si wako, kujitambulisha na jamii ambayo si yako, na kushabikia historia ya watu wengine. Kwa hali hiyo utakuwa unalea watoto ambao hawana misingi imara na wakipulizwa na upepo kidogo tu watageuka, kama bendera inavyogeuzwa mwelekeo na upepo.
Naheshimu mno kazi ya wasanii wa nchi yetu, lakini sijawahi kukatishwa tamaa na mwelekeo wa watoto wetu kama nilivyoshuhudia video ya mahojiano ya mtoto wa shule ya msingi aliyeulizwa ni nani Rais wa Tanzania na kujibu kuwa ni Diamond, msanii maarufu wa nyakati hizi.
Wakati wa mahojiano yale wengi walilaumu jibu lile kama ni tatizo la Serikali kutowekeza vyema kwenye sekta ya elimu. Kwangu ni kielelezo cha raia wa Tanzania wa miaka inayokuja. Iwapo mwanafunzi wa leo hamfahamu Rais Jakaya Kikwete, anayo nafasi ya kumkumbuka Mtemi Milambo, Kinjeketile, na wale maelfu ya
mababu zake waliopambana dhidi ya Wajerumani kwenye Vita ya Maji Maji? Atamkumbuka Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume? Tungepata ahueni kama Diamond siku moja angegombea urais na kufanya jibu ambalo leo siyo sahihi kuwa sahihi, lakini hatujui kama hilo litatokea. Hali kama hii inaashiria kuwa hakuna kiungo cha moja kwa moja kati ya historia yetu na Watanzania tunaotarajia watashika nafasi za uongozi katika miongo inayokuja. Hii ni hali ya hatari.
Tunapoadhimisha kumbukumbu ya Siku ya Karume leo tuongeze bidii katika kutambua na kusisitiza mchango muhimu wa viongozi wetu kwenye historia yetu, na mchango mkubwa wa mababu zetu kabla ya Uhuru wa kupambana na dhuluma na kutafuta haki. Ikitumika vyema, historia yetu ni ngao muhimu ya kulinda uhuru wetu.