Na Nizar K Visram

Uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika nchini Libya Desemba 24, mwaka jana umeahirishwa ghafla baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza kuwa maaandalizi yaliyofanywa hayatoshi. 

Tume ilitangaza siku mbili tu kabla ya uchaguzi, bila kusema sasa utafanyika lini.

Kati ya raia milioni saba nchini Libya, milioni 2.5 walijiandikisha. Tatizo lilionekana wakati tume ilishindwa kutangaza hata majina ya wagombea, kwa hivyo haikuwezekana kuendesha kampeni.

Siku ya uchaguzi ilipangwa kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo kama haukufanyika, maana yake serikali ya mpito inayotawala Libya sasa muda wake utamalizika, kwa hiyo haitakuwa na mamlaka ya kikatiba. 

Hii ni serikali ya mpito iliyoundwa Februari mwaka jana baada ya mkutano wa maridhiano uliofanyika chini ya Umoja wa Mataifa (UN). 

Kazi yake ilikuwa ni kuiongoza nchi hadi uchaguzi wa serikali mpya ya kudumu itakapochaguliwa. Swali sasa ni iwapo serikali ya mpito itaendelea au itahitaji mkutano mwingine wa usuluhishi? Mkutano huo utachukua muda kuitishwa na wakati huo huenda nchi isiwe na serikali. 

Katika hali hiyo ya ombwe, Libya inaweza ikatumbukia tena katika vurugu na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imekuwako tangu majeshi ya NATO na Marekani yalipompindua  Muammar Gaddafi mwaka 2011. 

Katika vurugu hiyo mataifa makubwa yako tayari siku zote kuchochea kwa kutoa silaha na askari mamluki.

Kwani mara baada ya uchaguzi kufutwa makundi ya wapiganaji yamekuwa yakikutana mjini Tripoli. Magari ya kivita yalionekana yakirindima karibu na Chuo Kikuu cha Tripoli na kwingineko.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa Oktoba 2020 baada ya mkutano ulioongozwa na UN. Kisha kundi lijulikanalo kama Jukwaa la Kisiasa la Libya likaandaa dira na mwongozo wa kuundwa kwa serikali ya mpito.

UN ilipanga mkutano wa usuluhishi pamoja na uchaguzi huru kama njia ya kuepukana na vita na nchi kumeguka. Lengo ni kuachia wananchi wajichagulie serikali yao badala ya makundi ya wapiganaji yaliyoibuka baada ya kuuawa kwa Gaddafi. 

Mara ya kwanza uchaguzi ulipangwa kufanyika mwaka 2014 lakini matokeo yake Libya ikagawanyika vipande viwili – serikali ya magharibi inayotambuliwa na UN, ikiwa na makao yake Tripoli na utawala wa mashariki ukiwa na ngome yake Benghazi.  

Katika mazingira kama haya uchaguzi mwingine ukapangwa hivi majuzi. Mtafaruku ukazuka miongoni mwa wagombea urais wapatao 100. Wawili kati yao ni maarufu zaidi. 

Mmoja ni Jenerali Khalifa Haftar, mbabe wa vita ambaye ni kamanda wa kikundi cha wapiganaji wa Benghazi. Wa pili ni Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa mkuu wa Libya aliyepinduliwa.

UN itabidi kuitisha mkutano wa kimataifa ili kusuluhisha mgogoro wa Libya kwa sababu huu si mgogoro wa Libya peke yake bali unachochewa na mataifa ya nje. 

Libya ni nchi yenye utajiri asilia unaomezewa mate na mataifa mengi. Ndiyo maana mataifa ya NATO yakiongozwa na Marekani yalimpindua Gaddafi. Matokeo yake nchi imeingiliwa na mataifa ya nje na mamluki wao.

Kwa mfano kuna video ikionyesha wapiganaji kutoka Syria waliotumwa na Uturuki kwenda kuisaidia serikali ya magharibi iliyo Tripoli (GNA). 

Video hii inaonyesha Wasyria hao wakiungama kuwa waliajiriwa kwa mshahara wa dola 2,000 kila mwezi na ahadi ya kupewa uraia wa Uturuki.

Mwandishi wa Kiarabu anayeishi Uingereza, Abdel Bari Atwan anasema GNA inasaidiwa na Uturuki na Qatar ambao wametuma mamluki 5,000 kutoka Syria. 

Kwa upande wa mashariki (Benghazi) Haftar anafadhiliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri, Urusi, Jordan, Ufaransa, Israel na Marekani, na anatumia mamluki kutoka Sudan, Chad na Urusi. 

Mamluki wa Syria hapo awali walitumiwa kumpindua Rais Assad wa Syria, wakashindwa na sasa wamehamishiwa Libya kuisaidia GNA. Kule Syria walitumiwa na Uturuki ikishirikiana na Marekani, Ufaransa, Saudi Arabia, Qatar na UAE. Sasa nchini Libya wakati Uturuki inaisaidia GNA nchi hizo zilizobaki zinamsaidia Haftar kuipindua GNA.

Haftar aliwahi kuwa jenerali katika jeshi la Gaddafi. Akatengana naye na kukimbilia Marekani ambako amepewa uraia wa nchi hiyo. Akatumiwa na Marekani pamoja na tawala za Kiarabu kumpindua Gaddafi. 

Baadaye akatengana na GNA na sasa anajaribu kuipindua serikali hiyo ya Tripoli. Kwa maneno mengine, nchi za NATO na watawala wa Kiarabu wako upande wa Haftar, Uturuki iko upande  wa GNA.

Katika kinyang’anyiro hiki Warusi pia wamo. Kampuni ya Wagner Group kutoka Urusi imeajiri mamluki wa Kirusi nchini Libya. Kila nchi inapigania masilahi yake, masilahi ya kudhibiti mafuta ya Libya na kunyakua tenda za mabilioni ya dola nchini humo. 

Israel nayo imejitosa kwa  kumuunga mkono Haftar. Tarajio lake ni kuwa iwapo Haftar atashinda basi Libya itaungana na Sudan, Morocco, UAE na Bahrain katika kusaini mkataba wa urafiki na Israel (Abraham Accords).

Ndiyo maana mwanzoni mwa Novemba mwaka jana Haftar alimtuma mwanawe, Saddam, kwenda Israel. Alichukuliwa kwa ndege ya Kifaransa (Dassault Falcon) kutoka UAE hadi Tel Aviv.

Gazeti la Kiisraeli (Haaretz) limeripoti kuwa Saddam Haftar alizuru Israel ili kuomba msaada wa kijeshi na kidiplomasia. Wakati huo ni kabla ya uchaguzi kufutwa na Haftar alikuwa anafanya kampeni ya kimataifa akitaka kuungwa mkono na mataifa ya NATO na Israel.

Saddam Haftar ana cheo cha kapteni katika jeshi la baba yake (Libyan National Army). Kwa mujibu wa ripoti ya UN na wanaharakati wa Libya yeye aliongoza kikosi cha wapiganaji wake, akavamia Benki Kuu ya Libya mwaka 2017 na akapora takriban dola nusu bilioni.

Jalel Harchaoui, mtafiti wa Shirika la Global Initiative, anasema kampeni ya kimataifa ni njia ya Haftar kuyaahidi mataifa hayo kwa kusema: “Mkinisaidia nikaambulia urais wa Libya basi  nitawafanyia moja, mbili, tatu.” 

Haftar amekuwa akifanya hivyo tangu mwaka 1987, akiwaomba wafadhili wake wamsaidie kunyakua nafasi ya Gaddafi. Wakati wote huo amekuwa akiwasiliana na majasusi wa Marekani (CIA) na wa Israel (Mossad).

 Hii ndiyo hali ya Libya ilivyo hivi sasa, ikiwa inawaniwa na mataifa ya kigeni yanayochochea vita na vurugu. Ni Libya ya Muammar Gaddafi aliyeuawa kikatili kwa msaada wa majeshi ya NATO yakiongozwa na Marekani. 

Walidai wanaondoa ‘udikteta’ na kuleta ‘demokrasia’.

Mwaka 1967 Gaddafi alirithi Libya ikiwa nchi maskini katika Afrika, ingawa ilikuwa na mafuta mengi. Wakati anauawa, Libya ilikuwa nchi yenye kiwango cha juu cha maisha kwa mujibu wa ripoti za kimataifa (Human Development Index).

Gaddafi aliunda kamati na mabaraza ya wananchi (Mu’tamar shaʿbi asāsi)takriban 800 nchini kote, yakiwa na mamlaka kamili ya kupitisha sera, sheria na bajeti. Kila mwananchi alikuwa na haki ya kuhudhuria, kutoa maoni na kupiga kura.

Mwaka 2009 Gaddafi aliwaalika wanahabari wa New York Times kutembelea Libya kwa wiki mbili wakiona jinsi mabaraza hayo yanavyofanya kazi. 

Mwishowe wakakubali kuwa wameshuhudia maelfu ya wananchi wakishirikishwa katika uamuzi wa kitaifa, kuanzia mambo ya nje hadi ujenzi wa shule. 

Mara nyingi ushauri wa Gaddafi ulikataliwa na uamuzi mbadala ukapitishwa kwa kura huru na wazi. Kwa mfano, alipendekeza  kufutwa kwa adhabu ya kifo lakini mabaraza yakamkatalia. Pia alipendekeza kuwa mapato ya mafuta yagawiwe nchini kote ili kila familia ipate gawio sawa. Hili pia lilikataliwa. 

Chini ya ‘udikteta’ wa Gaddafi wananchi walipata matibabu, umeme na elimu bila ya malipo, kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu ndani na nje ya nchi. 

Huu ndio ‘udikteta’ wa Libya uliopinduliwa na majeshi ya NATO. Badala yake wametengeneza nchi iliyogawanyika, huku wababe wa vita wakipewa msaada wa hali na mali na wafadhili wao kutoka nje. 

Wametengeneza nchi ambayo imegeuka kuwa kitovu cha wapiganaji wa Daesh (ISIS) pamoja na wakimbizi kutoka nchi za Kiafrika wanaojaribu kukimbilia Ulaya. Wengine wanaishia kupigwa mnada katika soko la watumwa nchini Libya. 

[email protected]

0693-555373