*Ni mfanyabiashara Arusha adaiwa kushiriki uwindaji haramu
*TAWA wapelekewa picha kuthibitisha uharibifu anaodaiwa kushiriki
*Amewahi kutozwa faini kwa kujaribu kutorosha madini
*Aomba JAMHURI lisiandike chochote akidai ‘haya mambo yananipa presha’, abadilika
ARUSHA
Na Mwandishi Wetu
Wakati Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikiendelea kukusanya ushahidi wa tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, mmoja wa washirika wake, Saleh Salum Al Amry, ameingia matatani.
Oktoba mwaka huu ripoti ya uchunguzi iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji (mstaafu) Mathew Maimu (nakala tunayo) ilimkuta Mnyeti pamoja na Mtendaji wa Kata ya Emboret mkoani Manyara, Belinda Sumari, na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na viashiria vya rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 (kwa Mnyeti pekee).
Mnyeti sasa ni Mbunge wa Misungwi, Mwanza, baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka jana ambao kwa mujibu wa Jaji Maimu, visima vilivyochimbwa na Al Amry jimboni humo; “vina harufu ya rushwa.”
Al Amry matatani
Al Amry, ambaye pia alihojiwa na THBUB, ni mfanyabiashara wa uwindaji wa kitalii aliyekuwa na uhusiano na Mnyeti wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Mnyeti, kinyume cha sheria, taratibu na utawala bora, aliunda ‘kamati ya uchunguzi’ akidai kuwa wananchi wa Simanjiro wamelalamika kuwapo uwindaji haramu kwenye kitalu kilichopo Pori Tengefu la Simanjiro kinachomilikiwa na Kampuni ya HSK Safaris Ltd.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba wakati kamati ya Mnyeti ikiundwa Desemba 6, 2019; siku mbili kabla, yaani Desemba 4, 2019, Al Amry na washirika wake waliwinda wanyama na ndege wengi huku ikidaiwa kuwa hawakuwa na leseni ya kuwindwa.
JAMHURI lina picha kutoka kwa chanzo cha habari cha uhakika ndani ya taasisi moja ya serikali mkoani Arusha zinazothibitisha kufanyika kwa ujangili mkubwa wakati kamati ikijiandaa kuwachunguza HSK Safaris Ltd., waliokuwa wamezuiwa kuingia kitaluni na Mtendaji wa Emboret, Belinda kwa maelekezo ya Mnyeti.
Zaidi ya picha 100 za matukio mbalimbali ya uwindaji haramu zimeshuhudiwa na mwandishi wa habari hizi.
Miongoni mwa picha hizo zinaonyesha wawindaji wenye asili ya Kiarabu wakiwa wamewashikilia ndege aina ya ‘kori bustard’ ambao hawaruhusiwi kuwinda.
“Hawa ndio ndege wakubwa wanaoruka na wapo katika hatari ya kutoweka, hivyo hakuna kibali cha kuwawinda. Hairuhusiwi kabisa,” anasema ofisa mmoja wa wanyamapori Mkoa wa Katavi aliyewasiliana na JAMHURI kutaka kufahamu msimamo wa kiserikali katika uwindaji wa ndege na wanyama nchini.
Picha hizo za Desemba 4, 2019, mbali na ‘kori bustard’, zinaonyesha wanyama kama swala jike na simba wenye umri mdogo wakiwa wameuawa.
Kifungu cha 56(1) cha Sheria Namba 5 ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kinasomeka: “A person shall not hunt the young of any animal or any female animal which is apparently pregnant or accompanied with youngs.”
Kwa tafsiri isiyo rasmi, maana yake ni kwamba hakuna anayeruhusiwa kuwinda mnyama ‘kijana’ (mdogo) wa aina yoyote au mnyama jike mwenye mimba au anayeongozana na watoto.
Katika hilo la wanyama jike, ofisa wanyamapori kutoka mkoani Katavi anafafanua: “Kwa sababu si rahisi sana kumtambua mara moja mnyama mwenye mimba, ndiyo maana haturuhusu uwindaji wa jike la mnyama yeyote ili kulinda kizazi cha wanyama hawa.”
Kosa kwa atakayefanya kitendo hicho ni: “…fine not less than twice of price of animal, imprisonment of not less than three years.”
“Hii ni kwa sababu wanyamapori ni hazina na maliasili ya taifa, ndiyo maana huwindwa kwa malipo rasmi serikalini yanayohusisha leseni na idadi ya siku za mawindo.
“Sasa kuhusu adhabu huwa tunachukulia gharama ya tozo za uwindaji wa kitalii ambazo huwa ni katika dola za Marekani. Na sheria inaweka wazi kuwa adhabu hizi zinaweza kwenda kwa pamoja; yaani faini pamoja na kifungo,” anasema.
Malipo ya leseni ya kuwinda simba, nyati, nyumbu na swala hufanyika kwa dola za Marekani huku thamani ya ‘kori bustard’ kwenye duru za kimataifa ikifika hadi dola za Marekani 10,000.
Ujangili kama uliofanyika kwenye Pori Tengefu la Simanjiro hulinyima taifa mapato huku kuuawa kwa wanyama majike na vijana kukivuruga maisha ya wanyama husika.
Pori Tengefu la Simanjiro lilitengwa mahususi na serikali ikizingatiwa kuwa ni eneo la mapito ya wanyama (ushoroba) nyakati na misimu tofauti.
Taarifa zinaonyesha kwamba idadi ya simba duniani imekuwa ikipungua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na magonjwa yanayowakabili pamoja na ujangili.
Macho ya wahifadhi kote ulimwenguni kwa sasa yanaitazama Tanzania kwa jicho la kipekee, kwa sababu asilimia 50 ya simba wote duniani wapo katika mapori ya Tanzania.
“Kanuni maalumu zimewekwa kuratibu uwindaji wa simba ili kuhakikisha simba wanaowindwa ni madume yaliyofikia umri mkubwa.
“Iwapo ujangili utashamiri Tanzania, basi idadi ya simba nchini itaathirika, hivyo kuathiri idadi ya simba wote duniani,” anasema.
Picha nyingine zinazomhusisha Al Amry na makosa katika taaluma ya uwindaji inamuonyesha yeye na watoto wake watatu wenye umri mdogo wakichezea bunduki ya uwindaji.
Mbali na kukiuka haki za watoto kwa kuwaruhusu kuchezea silaha hatari, picha hiyo pia inakiuka miongozo ya uwindaji inayokataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki uwindaji wa wanyamapori na hata kumsindikiza porini mwindaji anayekwenda kwa shughuli hizo na si utalii wa picha.
Pia ipo picha inayomuonyesha mwindaji mwenye asili ya Kiarabu akiwa amemshikilia swala hai.
Picha zapelekwa TAWA
Akizungumza na JAMHURI iwapo ana taarifa ya picha zilizopigwa kwenye kitalu chake na wawindaji wa kigeni wakiwa na Al Amry ambaye awali alikuwa akifanya naye biashara, Mkurugenzi Mtendaji wa HSK Safaris Ltd., Dk. Kibola, anasema siku zote ukweli na uongo hutengana.
“Baadhi ya picha hizi zilipelekwa kwenye kamati ya Mnyeti kama ushahidi dhidi yangu; kwamba mimi ni jangili. Ukweli ukidhihiri, uongo hujitenga.
“Unganisha doti na utaona kuwa kama haya yalifanyika siku mbili kabla ile kamati ya mkuu wa mkoa haijaanza kazi, kisha ujiulize jangili ni nani na msingiziwa ni nani,” anasema Dk. Kibola.
Mwanasheria huyo ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serikali ya UTT AMIS, anasema tayari baadhi ya picha za ujangili ameziwasilisha Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA). JAMHURI limeelezwa kuwa zimekwisha kupokewa.
“Ndiyo. Nimezipeleka TAWA kama Tume ya Haki za Binadamu ilivyoelekeza. TAWA wanapaswa kufanya uchunguzi,” anasema Dk. Kibola.
Kuhusu kumshitaki Mnyeti kama tume ilivyopendekeza, Dk. Kibola amesema: “Huyo (Mnyeti) asubiri tu, kwani muda wa zuio bado uko mbali. Acha mengine yajidhihirishe kwanza.”
Katika mapendekezo yake, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilipendekeza TAWA ifuatilie vitendo vya uwindaji haramu katika Pori Tengefu la Simanjiro Magharibi na kuchukua hatua stahiki ili kukomesha biashara hiyo.
Pamoja na picha hizo kupelekwa TAWA, kana kwamba haitoshi, miezi michache iliyopita Al Amry alijikuta katika misukosuko na vyombo vya dola akidaiwa kukutwa na ‘mzigo’ wa tanzanite na dhahabu bila kuwa na kibali.
Mmoja wa watu wa karibu na Al Amry amelithibitishia JAMHURI kuhusu kukamatwa kwake akisema:
“Baada ya kuhojiwa aliachiwa ikisemekana amelipa faini. Hakuwahi kufikishwa mahakamani!”
Azungumza na JAMHURI na kubadilika
Siku chache kabla ya kuchapwa kwa habari hii, juhudi za JAMHURI kuzungumza na Al Amry kwa njia ya simu zilizaa matunda Ijumaa ya Desemba 24, 2021.
Awali, kabla ya kuzungumza naye, JAMHURI lilimtumia maswali matatu; kwanza, ni kutaka kufahamu iwapo anazitambua picha tulizonazo.
Pili, kama wakati wa uwindaji huo walikuwa na leseni za kuua nyati na simba; tatu, JAMHURI lilitaka kufahamu ni mwindaji mahiri gani (professional hunter – PH) waliyekuwa naye wakati wa uwindaji na mwisho ni ukweli kuhusu kuhojiwa kwa kuwa na madini.
Al Amry aliomba kwanza atumiwe picha husika na mara baada ya kutumiwa siku hiyo hiyo ya Ijumaa, akampigia simu mwandishi wa JAMHURI na kusema: “Kwa sasa nipo porini. Unaonaje ukinisubiri hadi Jumapili saa tatu asubuhi tuzungumzie suala hilo?”
Al Amry alikutana na JAMHURI ofisini kwake asubuhi ya Jumapili (saa tano na nusu badala ya saa tatu kama ilivyokuwa awali) na kwanza akaomba taarifa hizo zisichapwe gazetini.
“Haya mambo yananipa ‘pressure’ kaka, kwani hatuwezi kuyaacha kwanza? Hebu nipe mhariri wako nizungumze naye,” anasema Al Amry.
Baada ya mwandishi kumsisitizia kwamba kinachohitajika ni majibu ya maswali aliyoulizwa, suala ambalo pia lilisisitizwa na mhariri; Al Amry hakutaka kuendelea na mazungumzo tena.