DODOMA
Na Mwandishi Wetu
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amepewa jukumu la kuunda kamati ya watu 10 kuratibu maazimio ya wadau wa siasa nchini.
Amekabidhiwa jukumu hilo wiki iliyopita jijini hapa baada ya Baraza la Vyama vya Siasa nchini kukutanisha viongozi wa vyama vya siasa kwa siku tatu.
Katika mkutano huo uliozaa hoja 80 zikiongozwa na madai ya Katiba mpya na kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara, wadau wamesema mfumo wa uendeshaji siasa nchini ulivurugika, hivyo unahitajika kusukwa upya.
Washiriki walikubaliana kuwa kwa mkutano kutoa maazimio bila kuunda kamati ya kuyaratibu, ingekuwa kazi bure, kwani isingefahamika hoja ipi itafanyiwa kazi na nani.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu (mstaafu), Mizengo Pinda, amesema wakati umefika kuondoa hofu na kumaliza hoja ya Tume Huru ya Uchaguzi ambayo imedaiwa tangu kitambo.
Akifungua mkutano huo, Jumatano wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka wanasiasa kujiepusha na vurugu, akisema: “Dhana ya kutumia ncha ya upanga kutafuta amani imepitwa na wakati, badala yake amani inapatikana kwa ncha ya ulimi.”
Ametoa mfano wa Zanzibar, ambapo Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi ameamua kutatua mgogoro wa kisiasa kwa njia ya mazungumzo, na sasa Wazanzibari ni wamoja zaidi kuliko wakati wowote, akisema hiyo ndiyo nguvu ya ncha ya ulimi.
Rais Samia amesema mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ni haki yao kikatiba na kisheria, isipokuwa kisichokubalika ni mikutano kuzusha vurugu na uharibifu wa mali za watu.
Amewataka wanasiasa na wadau wa siasa waliohudhuria mkutano huo kutoa mapendekezo wanayoamini yakifanyiwa kazi yatawezesha uwepo wa siasa za ushindani bila kupigana.
Baada ya mjadala wa siku tatu, wadau wa siasa walikubaliana kuwa hoja zilizotolewa ni nyingi, hivyo ni bora ikaundwa kamati ya watu 10 ambayo itachambua hoja za wadau na kuziweka katika muktadha unaotekelezeka, kisha ziwasilishwe kwenye mamlaka.
Mgongano wa hoja
Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa uliomalizika Ijumaa wiki iliyopita jijini Dodoma umeibua mgongano mkubwa wa hoja miongoni mwa wanasiasa.
Mgongano huo uliibuka pale Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kumuomba Rais Samia amsamehe Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anayeshitakiwa kwa tuhuma za ugaidi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
“Mwenzetu mmoja yupo ndani kwa sababu za kisheria, tunakuomba uone namna ya kufanya tuwe naye, atoke tuje kufanya naye siasa,” amesema Zitto.
Rais Samia akapokea ombi hilo kwa kusema siku zote demokrasia ni kuheshimu sheria.
“Heshima ya mtu inakuja kwa kuheshimu sheria. Unapotumia uhuru wako ujue mwisho wa uhuru wako ndiyo mwanzo wa uhuru wa mtu mwingine.
“Naomba tufanye kazi kwa kuheshimu sheria, kuna msemo unasema mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba, japokuwa kusameheana pia kupo,” amesema Rais Samia.
Pia amewataka wanasiasa kusahau yaliyopita na kuzika tofauti zao na yeye yuko tayari kusamehe na kuanza upya kwa masilahi mapana ya nchi. Huku akiliagiza Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukaa pamoja na wadau wa demokrasia nchini kujadili namna bora itakayotumiwa na vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara bila kuvunja sheria za nchi.
Aidha, amesema serikali yake iko tayari kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha sheria za vyama vya siasa pamoja na mambo yanayoshabihiana nayo ili kuimarisha demokrasia hapa nchini.
Katika hatua nyingine, wafuasi wa Chadema wamemshukia Zitto kupitia mitandao ya kijamii kwa kitendo chake cha kuomba Mbowe asamehewe.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ameandika kupitia akaunti yake ya Twitter: “Rais anatakiwa kusamehe waliopatikana na hatia tu. Hana mamlaka ya kusamehe watuhumiwa wa kesi kama hii. Tunataka afute mashitaka dhidi ya Mbowe bila masharti yoyote kwa sababu ni mtuhumiwa tu. Hatuombi asamehewe, hana hatia yoyote ya kusamehewa!”
Mbali na mgongano, pia mkutano huo wa siku tatu umeibuka na mapendekezo 80 yanayotakiwa kufanyiwa kazi huku madai ya Katiba mpya yakiibuliwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba.
Kupitia mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala, aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Warioba ameshauri suala la kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi na mikutano ya vyama vya siasa kufanyiwa kazi haraka.
“Kwanza ni mikutano ya vyama vya siasa. Rais ametoa mwelekeo, nina hakika mkizungumza vizuri tutamaliza.
“Kuhusu Katiba wananchi walishaamua, mchakato ukawapo, tukawa na rasimu, hakuna haja ya kusema turudi nyuma hatua zilizopita,” amesema Warioba.
Amesema mchakato wa Katiba mpya unaongozwa na sheria na ipo na akashauri ifanyiwe marekebisho ili kuendana na wakati na mahitaji.
Kuhusu tume huru ya uchaguzi, amekosoa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana akitaka sheria na kanuni za uchaguzi ziangaliwe upya.
Akizungumzia mapendekezo 80, Mukandala, amesema lipo suala la marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Polisi ili kuondoa vitendo vya uonevu kwa wanasiasa hapa nchini na umuhimu wa mkutano kama huo kwa wadau wa masuala ya siasa ya vyama vingi.
Alitaja jambo jingine lililopendekezwa katika mkutano huo kuwa ni umuhimu wa wadau wa siasa kufuata Katiba, sheria, kanuni na miongozo katika kutekeleza majukumu yao huku vyombo vya uamuzi navyo vinapaswa kutenda haki na kulinda amani.
Aidha, amesema elimu ya uraia nayo iwe endelevu na ianzie ngazi ya chekechea na isisubiri wakati wa uchaguzi huku serikali na vyombo vya dola viepuke upendeleo vinapohudumia vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla.
Akifunga mkutano huo, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekemea siasa za chuki na kuwataka Watanzania kufanya siasa za kulinda masilahi ya nchi na kukuza maendeleo yao.
Amesema si nchi nyingi duniani unaweza kukuta viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa vyenye itikadi tofauti wanaweza kukaa pamoja kujadili maendeleo ya mfumo wa vyama vingi nje ya Bunge.
Pia amesema utulivu wa kisiasa mara zote unatokana na majadiliano kwa watu kukaa pamoja na kuwasilisha mawazo yao kwa kuweka masilahi mapana ya nchi.