TABORA 

Na Moshy Kiyungi

Ukimwona kwenye runinga akinengua huwezi kuamini kwamba mwanamuziki mkongwe wa DRC, Jenerali Defao, ana zaidi ya miaka 60 sasa.

Defao alizaliwa Desemba 03, 1958 Kinshasa, DRC, akiitwa Mutomona Defao Lulendo.

Ni mwanamuziki mwenye kipaji cha kutunga na kuimba kwa sauti nyororo tofauti na mwonekano wake, akianza muziki mwaka 1976 na Orchestra Suka Movema.

Baadaye akajiunga na Fogo Stars, kisha mwaka 1978 akahamia bendi ya Korotoro iliyokuwa na makazi magharibi mwa DRC.

Defao ni miongoni mwa wanamuziki waliounda  bendi ya Grand Zaiko Wawa mwaka 1981 iliyokuwa ikiongozwa na mpiga gitaa mashuhuri, Pepe Felix Manuaku.

Katika kutafuta maisha, akajiunga na Ben Nyamabo kuunda kikosi kipya cha Choc Stars pamoja na Debaba, Carlito, Bozi Boziana na Djuna Djunana.

Tungo zilizotolewa na bendi hii ziliipatia umaarufu mkubwa.

Choc Stars na Orchestra Shakara Gagna Gagna zilizokuwa zikiongozwa na Jeanpy Wable Gypson, zilimfanya Defao kuwa maarufu kitaifa.

Uimbaji na uwajibikaji wake jukwaani ulionyesha wazi kuwa Defao hakuwa na kipaji cha kubahatisha.

Siku zote hucheza sambamba na wanenguaji wake akiwa kivutio kikubwa kwa mashabiki, akinengua katika mitindo mbalimbali, ukiwamo ‘Ndombolo’ bila kuchoka.

Mwishoni mwa mwaka 1990, Defao aliondoka Choc Stars akidhamiria kuunda bendi yake, ndoto iliyotimia kwa kuunda bendi aliyoiita  Big Stars, akiwa na akina Djo Djo Bayenge, Debleu Kinanga, Adoli Bamweniko na Djo Poster aliyetokea Grand Zaiko.

Big Stars ilikuwa na wanamuziki wengi wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza muziki akiwa na mpiga solo chipukizi wakati huo, Jagger Bokoko, aliyetokea kuwa kipenzi kikubwa cha Defao.

Katika miaka mitano ya bendi hii, Defao alipata mafanikio makubwa baada ya kufyatua albamu zisizopungua 17, sita kati ya hizo ziliingia katika soko la Ulaya mwaka 1995.

Mifarakano kazini huwa haikosekani. Bendi hiyo baadaye iliteteleka baada ya kuondoka Djo Djo Bayenge na kumuacha Defao akiwa kiongozi.

Akiwa na Big Stars, Defao aliikarabati upya bendi na kutengeneza kikosi kipya  chenye wanamuziki mahiri, wakimuongeza Roxy Tshimpaka kutoka Choc Stars. 

Umaarufu wa Jenerali Defao ulisambaa maeneo mengi ya Afrika Mashariki na Kati miaka ya 1990, mashabiki wake wakiulinganisha na ule wa akina Papa Wemba, Koffi Olomide, Bozi Boziana na au King Kester Emeneya.

Hapana ubishi kwamba Defao ni mwanamuziki maarufu DRC, akibebwa na nyimbo za Georgina, Fammilie Kikuta, Nadine, Bana Kongo, Oniva na Filie zilizopigwa katika mitindo ya rumba na sebene mold.

Ubovu wa usimamizi ulimfanya Defao kubadili maprodyuza na kampuni za kurekodia, wakati mwingine akitoka na matoleo ya kazi zake zile zile kwa lebo tofauti.

Defao aliivunja Big Stars mwaka 2000 akiwa Kinshasa, akaamua kwenda ‘kutanua’ Paris, Ufaransa alikorekodi albamu ya Nessy de London, akiwashirikisha akina Nyboma Mwandido, Luciana de Mingongo, Wuta Mayi, Ballou Canta na Deesse Mukangi, wakafanya onyesho kubwa lililowavutia  wengi.

Defao, kwa kuwatumia waimbaji hao waalikwa, walifanya albamu ya De London kupanda chati zaidi, aliachia albamu nyingine nyingi zikiwa na nyimbo za Mandova, Ya Gege, Copinnage, Sam Samita, Salanoki Guerre De1, Animation na Nessy of London.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Defao baadaye akawa kimya katika muziki, hali hiyo ilitokana na sintofahamu za kisiasa nchini mwake iliyosababisha afungiwe kupiga muziki huko DRC wakati wa utawala wa Rais Laurent Kabila.

Defao alifika Tanzania katika ziara iliyogubikwa na matatizo lukuki mwaka 2000, alizidiwa akili na ‘promota’ aliyemleta, matokeo yake alikosa fedha za kujikimu pamoja na kulipia ‘visa’ yake.

Nguli huyo alikosa hata nauli ya kumrejesha kwao hadi alipopewa ‘lift’ na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) wakati lilipozindua safari kati ya Dar es Salaam na Lubumbashi.

Baada ya subira ya muda mrefu ya mashabiki wake, mwaka 2006 gwiji huyo aliibuka na albamu mpya yenye lebo ya Nzombo le Soi; na miaka minne baadaye alifyatua CD yenye lebo ya Pur Encore.

Mwaka 2012, Defao, kwa bahati nzuri alirudi ulingoni akiwa na albamu ya ‘The Undertaker’.

Mwanamuziki  huyo mwaka 2018 alikuwa akisikika akifanya maonyesho mengi Nairobi nchini Kenya.

 Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0767331200 na 0736331200.