Na Bashir Yakub
Unapokwenda kufungua shauri la mirathi mahakamani haimaanishi kuwa unakwenda kuiomba mahakama kugawa mali za marehemu. Bali unakwenda kufungua mirathi ili utambulike rasmi kimamlaka na kisheria kuwa wewe ni msimamizi wa mirathi.
Mahakama haitakiwi kugawa mali za marehemu kwani mahakama si msimamizi wa mirathi. Mahakama ni chombo kinachomthibitisha msimamizi wa mirathi. Kazi ya kugawa mali za marehemu ni kazi ya msimamizi wa mirathi baada ya kuthibitishwa na mahakama.
Katika hili wapo watu wamekwepa kwenda hata mahakamani kumthibitisha msimamizi wa mirathi kwa kuhofia kuwa mahakama itagawa mali za marehemu. Hili si kweli, kwa sababu mahakama haigawi bali inamthibitisha msimamizi wa mirathi.
Na tunasema mahakama inamthibitisha msimamzi wa mirathi kwa kuwa msimamizi wa mirathi anateuliwa aidha na kikao cha ukoo/familia (kama hakuna wosia au upo lakini haukutaja msimamizi), au anakuwa ameteuliwa moja kwa moja na marehemu mwenyewe kwenye wosia.
Kwa hiyo ni jina la aliyeteuliwa na kikao cha ukoo/familia, au la aliyeteuliwa na marehemu kwenye wosia ndilo linalopelekwa mahakamani kwa ajili ya kuthibitishwa na kuwa rasmi msimamizi wa mirathi. Na bila uthibitisho huu wa kimahakama hauwezi kuwa au kuitwa msimamizi wa mirathi hata kama umetajwa na wosia.
Yote kwa yote, eneo muhimu katika makala hii ni kuwa mahakama haiwezi kuvaa kazi ya msimamizi wa mirathi. Haitagawa mali kwa kuwa jukumu hilo ni katika majukumu ya msimamia mirathi. Kwa msingi huu hauna haja ya kuhofia taratibu za kimahakama katika mirathi.
Hata hivyo yapo baadhi ya maeneo mahakama hasa za mwanzo zimejishughulisha na kugawa mali. Kama hili limetokea, ni kosa na yafaa uamuzi huo kupingwa. Katika Shauri la mirathi kati ya IBRAHIMU KUSAGA V EMANUEL MWETA (1986) TLR 26) Mahakama ya Mwanzo iligawa mali za marehemu ambapo rufaa ilipotua Mahakama Kuu Jaji Kapoor (kama alivyokuwa), alikitaja kitendo hicho kama kinyume cha sheria na hivyo kufuta uamuzi huo wa mgawo.
Basi yapasa hili tulielewe katika mipaka hii.
Wakili Bashir Yakub
+255 714 047 241