*Sh trilioni 3 hupotea kila mwaka kupitia miamala
KIBAHA
Na Costantine Muganyizi
Katika upande huu wa dunia ambako ni watu wachache wenye uhakika wa milo mitatu kamili kwa siku, Sh bilioni 1 ni fedha nyingi sana. Na ili ufikishe Sh trilioni 1 inabidi uwe na bilioni 1,000.
Kwa haraka na kwa kusikia tu, Sh bilioni 1 inaweza kuonekana au kuchukuliwa kuwa kiasi kidogo tu cha fedha. La hasha! Hizo ni fedha nyingi sana.
Ukitaka kujua kuwa Sh bilioni 1 ni fedha nyingi, toa Sh milioni 20 kwenye kiasi hicho. Utabaki na Sh milioni 980. Kama iko hivyo, basi ukitoa Sh milioni 20 kwenye Sh trilioni 1 unabaki na Sh milioni 980,000, yaani milioni laki tisa na themanini elfu.
Sasa pata picha Sh trilioni 3 ni kubwa kiasi gani. Kwa mujibu wa Kampuni ya Mastercard International, hizo ndizo fedha ambazo Tanzania hupoteza kila mwaka kwa kuendelea kutumia fedha taslimu katika miamala mbalimbali inayofanyika nchini.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wataalamu wa kampuni hiyo kigogo wa teknolojia bunifu na malipo ya kidijitali, wanasema fedha taslimu huigharimu Tanzania asilimia mbili ya pato lake la taifa kila mwaka.
Meneja wa MasterCard Afrika Mashariki, Shehryar Ali, amesema matumizi ya fedha taslimu nchini ni makubwa na gharama zake kwa taifa ni kubwa pia.
Ofisa huyo ameliweka hilo bayana wakati wa hafla ya MasterCard kuikabidhi Benki ya NMB tuzo maalumu kutambua mchango wake wa kusaidia kukuza na kuhamasisha matumizi ya kadi za malipo za MasterCard nchini na kama ishara ya kutambua juhudi zake za kusaidia kujenga uchumi wa kidijitali.
“Matumizi ya fedha taslimu yanayofikia hadi asilimia 90 ya miamala yote inayofanyika Tanzania yanaughalimu uchumi wa taifa asilimia mbili ya pato la taifa kwa sababu lazima fedha hizo zichapishwe, zihifadhiwe, zisafirishwe na zilindwe,” anafafanua Ali na kuhoji:
“Kama sasa hivi pato la taifa la Tanzania ni takriban dola za Marekani bilioni 64, je, asilimia mbili yake ni kiasi gani?”
Anasema wingi wa fedha hizo unadhihirisha umuhimu wa kuwekeza kwenye mifumo ya malipo ya kidijitali kama inavyofanya Benki ya NMB.
Asilimia mbili ya kiwango hicho cha pato la taifa ni sawa na dola za Marekani bilioni 1.28, sawa na takriban Sh bilioni 2,945.28 (takriban Sh trilioni 3).
Iwapo zikiokolewa, fedha hizo zinaweza kufanya mambo mengi ya kusaidia kulijenga taifa na kuboresha maisha ya wananchi katika huduma za jamii.
Kama kujenga chumba kimoja cha darasa kunagharimu kati ya Sh milioni 10 hadi 20, basi hasara inayotokana na matumizi ya fedha taslimu inaweza kugharamia ujenzi wa vyumba 150,000 hadi 300,000 vya aina hiyo.
Kwa kigezo cha makadirio ya matumizi ya serikali kwenye mwaka huu wa fedha, kiasi hicho pia kinatosha na kuzidi bajeti nyingi za wizara, idara za serikali na taasisi nyeti za umma pamoja na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo.
Mifano mizuri ni wizara za Maji, Habari na Kilimo ambazo katika mwaka wa fedha 2021/22 zimetengewa Sh bilioni 680.3, Sh bilioni 54.7 na Sh bilioni 13.8 mtawalia. Kwa mantiki hiyo, Sh trilioni 3 zinaweza kuendesha Wizara ya Kilimo kwa zaidi ya miaka minne!
Fedha hizo pia zinaweza kuiweka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika mikono salama kwa zaidi ya miaka 50 na ile ya Kilimo miaka 2,017. Zinatosha pia kusaidia kutekeleza karibu miradi 411 ya maji na usafi wa mazingira.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka huu, Waziri Jumaa Aweso, amesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya usambazaji maji na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ni Sh bilioni 7.3.
Umuhimu na faida za Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kidijitali ambao moja ya vigezo vyake vikubwa na kati ya sifa zake nyingi ni kufanyika kwa malipo kielektroniki ni mchango wa kiasi kitakachookolewa kwa kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika kutekeleza bajeti ya Serikali Kuu.
Matumizi ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha ni Sh trilioni 13.25, ambapo Sh trilioni 2.88 ni fedha za nje ikiwamo mikopo. Wakati ugharamiaji wa mradi wa treni ya umeme wa SGR utahitaji karibu Sh trilioni 1.2, ule wa umeme wa Julius Nyerere umetengewa Sh trilioni 1.44.
“Katika mwaka 2020/21, serikali inapanga kutumia jumla ya Sh trilioni 36.3 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh trilioni 23 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni asilimia 63 ya bajeti yote na Sh trilioni 13.3 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote,” anasema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alipowasilisha bajeti hiyo Juni mwaka huu.
“Bajeti ya maendeleo inajumuisha Sh trilioni 10.4 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.2 ya bajeti ya maendeleo na Sh trilioni 2.9 fedha za nje, sawa na asilimia 21.8 ya bajeti ya maendeleo.
Aidha, Sh trilioni 10.7 sawa na asilimia 29.5 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya kulipa fedha zilizokopwa kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imekamilika na inayoendelea,” anaongeza.
Meneja wa MasterCard, Ali, anasema ingawa matumizi ya fedha taslimu bado ni makubwa nchini, maendeleo ya malipo kufanyika kidijitali yamekuwa ni mazuri vilevile. Malipo hayo yamechagizwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya kadi za kidijitali zinazowezeshwa na mfumo wa msimbo (QR Code).
Wataalamu wa MasterCard wanasema mfumo huo unaofanya kazi kwa kutumia kamera ya simu janja ambayo inaskani msimbo (CODE) na kisha kukamilisha malipo ndani ya muda mfupi, unasaidia na kurahisisha miamala, kitu ambacho ni muhimu katika biashara.
Ingawa itachukua muda, huduma hii huenda ikaondoa kabisa haja ya mtu kutembea na fedha taslimu kwani huduma nyingi muhimu zimefikiwa nayo.
Kwa mujibu wa Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, kadi za malipo za NMB MasterCard ni salama.
Mponzi anasema ili kujenga uchumi imara wa kidijitali na kupunguza matumizi ya fedha taslimu, kuna haja ya wadau kuacha ubahili linapokuja suala la kuwekeza katika teknolojia mpya na za kisasa kama wao wanavyofanya.
“Benki ya NMB imekuwa kinara katika kuhamasisha matumizi ya kadi ya benki si tu kwa ajili ya kutolea fedha katika ATM, bali katika matumizi mbalimbali kama kufanya malipo katika sehemu za migahawa, supermarket, vituo vya mafuta na hata katika sehemu za starehe na hata kuagiza bidhaa kupitia mitandao,” anasema.