Laiti tungekuwa tunahangaishwa na mambo serious, kwa hakika taarifa ya dada Aisha Twalibu, mlinzi wa kampuni binafsi pale Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ndiyo ingepamba mijadala kwenye vyombo vya habari na mitaani kwetu kote.
Huhitaji kuelezwa ukweli kwamba mtu yeyote anayefanya kazi ya lindo kama alivyo Aisha ni mtu mwenye maisha ya kawaida mno. Huwezi kumpata mlinzi kama yeye akiendesha VX yake au akiwa na watoto wanaosoma shule za kimataifa.
Aisha akiwa kazini kwake, akatupa jicho na kumuona mgeni mmoja kwenye taasisi hiyo akipoteza bulungutu la Sh milioni 10.
Fikiria noti 1,000 za Sh 10,000 kila moja zinaokotwa na mtu maskini tu. Yawezekana kiasi hiki ni kidogo kwa huyo mwenye nacho, lakini kwa Aisha ni kikubwa na chenye kumfanya hata ashawishike kuacha kazi na kukimbia kwa kiwewe. Sina hakika endapo hata mshahara wake unakaribia 200,000 kwa mwezi!
Aisha akaweka kando hisia zote za umaskini wake, ugumu wa maisha, shida za ndugu zake na njaa zote zinazomkabili.
Kama walivyo wanawake wengine wengi anapenda kujiremba ili awe na mvuto wa kike. Anapenda avae vizuri, ajipodoe na ikiwezekana aitunze vizuri familia yake.
Amekwenda kulinda ili apate pesa, lakini ghafla anajikuta pesa anayokutana nayo si ya mshahara. Haina jasho!
Maisha aliyonayo Aisha yangemshawishi asiwe radhi kuruhusu pesa iliyoangukia kwake imponyoke. Lakini pamoja na mahitaji yote hayo, pamoja na umaskini wake, bado dhamira yake akahakikisha anaibakiza kwenye utu na upendo.
Akaziokota hizo fedha, akamrejeshea mwenyewe. Haya mambo ya moral principles yametoweka sana katika jamii yetu. Aisha ameonyesha kuwa utajiri si wa mali pekee, bali ni wa roho na maadili pia.
Hatujui huyo aliyepoteza hilo bulungutu alikuwa anakusudia kulifanyia nini, lakini fikiria kama ndilo alitaka kulitumia kumlipia gharama za matibabu mgonjwa wake, kisha Aisha akatoweka nalo!
Simjui Aisha lakini inawezekana kabisa akapokea matusi kuanzia kwa watumishi wenzake, majirani, marafiki hadi ndugu zake.
Wapo watakaomcheka na wengine hata kumkatisha tamaa kwa kusema bahati hairudi mara ya pili! Kwa wote hao, awapuuze.
Aisha ametukumbusha kuwa pamoja na dhiki zote zinazotukabili Watanzania, bado miongoni mwetu tunao binadamu wenye utu, upendo na huruma.
Nyoyo za aina hii ndizo zilizowatofautisha Watanzania na watu wa mataifa mengine mengi, hasa haya ya Afrika – Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tukio la Aisha linafanana na la kijana mwendesha bodaboda Emmanuel Tuloe wa nchini Liberia aliyeokota bulungutu la dola 50,000 za Marekani (Sh milioni 115) na kuzirejesha kwa mwenyewe – mwanamama Musu Yancy.
Oktoba, mwaka huu Rais George Weah alimwita Ikulu akamtuza kijana huyo dola 10,000 za Marekani, bodaboda mbili mpya na nishani ya juu ya taifa hilo.
Nampongeza kwa dhati Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohamed Janabi, kwa kumtuza Aisha Sh 500,000.
Ameonyesha njia. Sasa ni wajibu wetu sisi wengine kuona Aisha tunamzawadia nini. Aisha ametupatia Watanzania zawadi ya somo la uadilifu na upendo. Hili ni somo kubwa.
Viongozi wetu wakuu wa nchi bila shaka hili tukio hawatalipa kisogo. Aisha amewapa ajenda nzuri ya wao kuhimiza maadili mema katika jamii.
Wampongeze kama shujaa na wamtuze kama Mtanzania aliyefanya tukio la kutukuka na la kupigiwa mfano.
Waonyeshe kuwa maskini si kigezo cha kuwa na roho mbaya ya ubinafsi. Naogopa kumwambia Rais Samia amtuze, maana nitaonekana nampigia debe, lakini Aisha amekoleza kwa kuonyesha wanawake si tu wanaweza kuongoza nchi, bali wanaweza kuongoza kwa uadilifu.
Wamtuze huku wakionya juu ya tabia mbaya za wakora ambao wamefikia kiwango cha juu cha ukora kwa kuwapora majeruhi na maiti ili kuchukua fedha na mali.
Viongozi wa dini wamtumie Aisha kama kielelezo cha uadilifu. Wawaonye waumini wao wadokozi walio radhi kuiba hadi sadaka na zaka. Wamtumie Aisha kama rejea ya mahubiri yao.
Polisi wamtumie Aisha kufufua ule utaratibu wa lost and found . Wawe na vitengo vya kupokea mali zilizopotezwa na wenyewe, kisha wakafanya kila linalowezekana kuwapata wahusika. Wafanye kazi hiyo kupitia taarifa zisizolipiwa kwenye vyombo vya habari. Haya yapo sana kwa mataifa yaliyostaarabika. Polisi wetu wakifanya hivyo watakuwa wamejijengea sifa na heshima kubwa kwa wananchi.
Aisha na Tuloe wametukumbusha kuwa kuishi kwa upendo ni jambo linalowezekana. Kumjali binadamu mwingine kwa kumtendea wema wa aina hii ni fadhila duniani na mbinguni.
Tukio la Aisha linaweza kumbadilishia maisha yake, tofauti kabisa na wanaodhani alistahili kutoweka na hilo bulungutu.
Kwa sifa na vigezo vyote, Aisha anastahili tuzo ya kitaifa ya kutambua na kuheshimu uzito wa alichokifanya. Rafiki yangu mmoja ameandika: “Aisha hakutaka kunywa uji wa mgonjwa”. Hongera sana Aisha Twalibu.