#Miaka 3 sasa amefungiwa kizuizini chumbani

#Anyimwa tiba, haruhusiwi kuona mkewe, watoto

#Rais Azali Assoumani kichwa ngumu, awa jeuri

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Aliyekuwa Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ahmed Abdallah Mohamed Sambi, amemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan akimuomba afanye awezavyo atolewe kizuizini anakoteseka tangu mwaka 2018.

Sambi yuko kizuizini kwa amri ya Rais wa sasa wa Comoro, Azali Assoumani, kwa kile kinachoonekana ni sababu za kisiasa. 

Taifa hilo lililoko katika Bahari ya Hindi linaundwa na visiwa vitatu vya Grande Comoro (Moroni), Anjouan na Moheli. Kisiwa cha nne, Mayotte mwaka 1974 wakazi wake walipiga kura na kuchagua kuwa sehemu ya koloni la Ufaransa.

Hatua ya Sambi kumuomba Rais Samia aingilie kati kumnusuru imetokana na Rais Assoumani kukaidi maombi ya Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), taasisi za kitaifa na kimataifa, na watu maarufu ndani na nje ya Bara laAfrika.

Duru kutoka serikalini zinasema Rais Assoumani amekuwa ‘kichwa ngumu’ kwani licha ya Rais Samia kumpelekea ujumbe mahususi kuhusu hatima ya Rais mstaafu Sambi, kiongozi huyo ameendelea kukaidi.

Sehemu ya barua ya Rais mstaafu Sambi kwa Rais Samia inasomeka hivi: “Mheshimiwa Rais, familia na mawakili wangu wamejitahidi kufanya kila linalowezekana ili niwe huru kutoka kizuizini, lakini hadi sasa imeshindikana. UN, AU kupitia Tume ya Haki za Binadamu – wote wametoa mwito niachiwe huru, lakini wamepuuzwa.

“Mheshimiwa, kwa miaka mitatu sasa nimetengwa na dunia. Kwa miaka yote hii nimezuiwa kuonana na mke wangu, watoto wangu wala mtu yeyoye awaye. Mtu pekee ninayeonana naye ni mtoto wa dada yangu.

“Nimefungiwa kwenye selo ndogo nyumbani, nanyimwa haki zote za msingi ambazo mtuhumiwa au mfungwa kama mimi ninastahili kuzipata kwa mujibu wa sheria za Comoro na kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu.

“Afya yangu imedhoofu, nimenyimwa matibabu kwa muda wote huo licha ya kutakiwa kuonana na madaktari na kupewa matibabu. Hii ndiyo sababu kuu iliyonifanya mheshimiwa nikuandikie barua hii ili unisaidie niweze kutibiwa.

“Daktari wangu Said Ali Petit, baada ya kunichunguza mara kadhaa ameshauri nipate vipimo na matibabu zaidi, lakini nimezuiwa kabisa. Hata jaji anayechunguza shauri langu Januari 2, 2020 alitoa kibali nipate matibabu, lakini uamuzi wake umepuuzwa. Mimi kama wengine nina haki za msingi za kibinadamu za kutibiwa, na zaidi kupata matibabu ya uhakika hata kama hayapatikani ndani ya nchi hii (Comoro).

“Mheshimiwa Rais, hali yangu ya sasa inanipa shaka mimi na jamaa zangu. Mimi kama rais mstaafu, kama raia, baba na mume, si haki kuzuiwa kizuizini na kunyimwa matibabu… kuwekwa kwangu kizuizini kumetokana na sababu za kisiasa, na mara zote nimesema sina kosa la kunifanya niwekwe jela. Kwa hiyo nakuomba ujadili suala langu la afya na mamlaka za nchi za Comoro ili nirejeshewe uhuru wangu.

“Mheshimiwa Rais, ili kupata ukweli juu ya mashitaka haya niliyofunguliwa, naambatanisha nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na barua niliyomwandikia Rais Azali Assoumani, na nyingine iliyoandikwa na marafiki zangu kuelezea mkasa ulionipata.”

Rais mstaafu Sambi pia ameiandikia AU barua, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Mahamat, akiomba umoja huo usaidie kumrejeshea uhuru aliopokwa na Rais Assoumani.  

Anasema Mei 12, 2018, alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Rais Azali Assoumani kubadili Katiba ya Comoro ili kumwezesha kuendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2029. Hatua hiyo, anasema ilikuwa inafuta utaratibu wa kikatiba wa kuwa na urais wa mzunguko kwa kila kisiwa kwa miaka mitano.

Anasema Mei 18, 2018, alikamatwa na kuwekwa kizuizini nyumbani kwake kwa amri iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

Hatua hiyo anasema ni kinyume cha sheria, kwani mwenye mamlaka hayo ni jaji. Anasema licha ya mamlaka za dola kutambua kuwa kuwekwa kwake kizuizini ni kinyume cha sheria, ziliridhia pengine kwa hofu na hila.

Sambi anasema watu mbalimbali wamezuiwa kumtembelea, akitoa mfano kuzuiwa kwa Balozi wa Marekani nchini Comoro ambaye alitaka kufanya hivyo, lakini akazuiwa.

“Bila kufunguliwa kesi wala kusikilizwa, wala bila kuwapo ushahidi wa makosa ninayotuhumiwa kwayo, Serikali ya Comoro imeamua niwekwe kizuizini kwa muda usio na ukomo, ikiwa ninadhulumiwa haki zangu za kibinadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa,” anasema Rais mstaafu Sambi kwenye barua ambayo JAMHURI ina nakala yake.

Anasema Serikali ya Comoro imekataa katakata asitibiwe licha ya Serikali ya Tanzania kupitia kwa Rais Samia kukubali kugharimia matibabu yake.

Chanzo cha Sambi kuwekwa kizuizini

Mwaka 2001 visiwa vitatu viliunda Katiba mpya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Comoro. Katiba hiyo, pamoja na mambo mengine, ilianzisha utaratibu wa mzunguko wa urais katika visiwa hivyo kwa miaka mitano, yaani The principal of rotating presidency between islands for five years.

Utaratibu huo ulianza vizuri ambapo kuanzia mwaka 2002 – 2006 alishika Rais Azali anayetoka Grande Comoro. 

Mwaka 2007- 2011 urais ulishikwa na Rais Abdallah Mohammed Sambi kutoka Kisiwa cha Anjouan, na mwaka 2012 – 2016 Jamhuri ya Comoro iliongozwa na Rais Dk. Ikililou Dhoinine kutoka Kisiwa cha Moheli.

Mwaka 2008 wakati Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Kisiwa cha Anjouan kilifanya jaribio la kujitenga na visiwa viwili vingine; jambo ambalo Umoja wa Afrika ulilikataa. Jeshi la Ulinzi na Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kibali cha Umoja wa Afrika lilikwenda kuzima jaribio hilo kwa kumwondoa kiongozi muasi Kanali Mohamed Bacar na kukirejesha kisiwa hicho kwenye utawala wa Jamhuri ya Comoro. 

Operesheni hiyo iliyojulikana kwa jina la Operesheni Comoro iliongozwa na Brigedia Jenerali Chacha Igoti. 

Baadaye alipanda cheo na kuwa Meja Jenerali kabla ya kustaafu miaka kadhaa iliyopita. Pamoja na JWTZ, Tanzania iliungwa mkono na wanajeshi kadhaa kutoka Sudan, Libya na Senegal zilichangia vifaa kama magari na gharama nyingine.

Mwaka 2017 Rais Azali aligombea tena urais na akashinda. Kipindi chake kilikuwa kiishe mwaka huu wa 2021. Mwaka 2018 akafanya mabadiliko ya katiba bila kushirikisha wananchi na Bunge. Akafuta kipengele cha mzunguko wa urais kwa visiwa wa miaka mitano mitano. Matatizo yakaanzia hapo.

Wananchi wakapinga, na Rais mstaafu Sambi akatoa kauli ya kulaani uvunjaji huo wa katiba. Kitendo hicho ndicho kilichosababisha akamatwe na kuwekwa kizuizini kuanzia Mei 18, 2018 na hadi sasa hajaachiwa.

Gazeti la JAMHURI limezungumza na baadhi ya watu wanaofuatilia siasa za Comoro. Mmoja kati ya watu hao amesema: “Rais Mstaafu Sambi hakufanya kosa lolote la kisheria la kustahili kuwekwa kizuizini. Hakutenda tendo lolote la jinai. Hakufikishwa kwenye chombo chochote kile cha kisheria. Haruhusiwi kutoka kwenda kokote kwa matibabu. Haruhusiwi kukutana na familia yake wala ndugu zake. Hapatiwi huduma yoyote.

“Kwa hali hiyo, na ikizingatiwa kuwa Rais Sambi ni mtu anayeheshimika kwenye visiwa vya Comoro na duniani kote, dunia wala Tanzania haiwezi kukaa kimya. Sisi Watanzania ambao ni jirani na nchi muhimu sana kwa visiwa vya Comorro lazima tupige kelele za kumtaka Rais Azali Assoumani, asikilize mwito wa viongozi wenzake akiwamo Rais wetu, Samia Suluhu Hassan. Tunatambua kuwa Septemba mwaka huu alimtuma Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kumpelekea ujumbe maalumu Rais Assoumani kumtaka amwachie huru Rais Mstaafu Sambi.

“Tunampongeza Mhe. Rais wetu na Mama yetu, kwa kazi aliyoianza na asichoke kumshauri Rais Azali amwachie Rais Mstaafu Sambi. Asiwe na kisingizio kuwa eti kesi hiyo ipo mahakamani. Haipo mahakamani! Hakuna kesi mahakamani, Rais Assoumani anauhadaa ulimwengu.

“Wala asiseme kuwa ana mpango wa kuitisha dialogue (mazungumzo) na wapinzani wote. Amejaribu, lakini wapinzani wamesema hawawezi kuonana naye kwa mazungumzo mpaka Rais mstaafu Sambi na wote waliowekwa kizuizini awaachie,” amesema na kuongeza:

“Lazima aheshimu katiba ya nchi yake. Hawezi peke yake kwa kutumia wanasheria kubadilisha katiba hata kama haipendi. Na wananchi na viongozi wao wakimpinga, hiyo si dhambi ya kustahili wananchi wake kuwaweka kizuizini. Wana Comoro wengi wa ndani na waishio nje wanataka amwachie Rais Sambi. Umoja wa Afrika unataka amwachie huru, nchi za SADC zinataka amwachie, na Tanzania inataka amwachie. Haiwezekani yeye tu Assoumani awe wewe yuko sahihi na wengine wote hao wawe hawako sahihi.”

Historia fupi ya Comoro

Comoro ina ukubwa wa kilomita za mraba 1,862 (bila kuhusisha Kisiwa cha Mayotte). Ni nchi ya tatu kwa udogo wa eneo katika Bara la Afrika. Idadi ya watu kwa sensa ya watu ya mwaka 2000 ilikadiriwa kuwa ni 798,000 (bila Mayotte). 

Ni nchi ya sita kwa kuwa na idadi ndogo ya watu katika Bara la Afrika – ingawa ni moja ya nchi zenye msongamano mkubwa wa watu. 

Kila kilometa moja ya mraba inakaliwa na wastani wa watu 275. Jina Comoro limetokana na neno la Kiarabu ‘qamar’, yaani mwezi.

Comoro ina milima mirefu. Hali ya hewa ni ya kitropiki. Ina misimu miwili mikuu ya mvua. Wastani wa joto ni nyuzijoto 29–30 °C kwa mwezi Machi. 

Kipindi cha mvua kinachoitwa ‘Kashkazi’ ni miezi ya Desemba na Aprili. Kipindi cha baridi huwa na nyuzijoto 19°C. 

Kipindi cha kiangazi (kusi) ni kuanzia Mei hadi Novemba. Kisiwa cha Ngazidja ndicho kikubwa katika Comoro, kikiwa na eneo linalolingana na visiwa vingine vyote vikiwekwa pamoja. Ndicho kisiwa chenye umri mdogo, kwa sababu hiyo kina miamba mingi. Kuna volkano mbili katika Kisiwa cha Ngazidja – Karthala (iliyo hai) na La Grille (iliyolala).

Mlima Karthala kilele chake ni urefu wa mita 2,361 (futi 7,748) kutoka usawa wa bahari. Hiki ndicho kilele kirefu katika Comoro. 

Karthala ni moja ya volkano hatari zilizo hai duniani. Mara ya mwisho ililipuka mwaka 2006. Matukio mengine mabaya ya kulipuka kwa volkano yalikuwa mwaka 1991 na Aprili, 2005.

Tukio la mwaka 2005 lilidumu kuanzia Aprili 17 hadi Aprili 19. Watu kadhaa walifariki dunia na wengine 40,000 waliokolewa. Hali hiyo ilisababisha kutoweka kwa ziwa lililokuwa limetokana na kreta, likiwa na urefu wa kilometa tatu na upana wa kilometa nne.

Sehemu za miji zenye watu wengi ni Moroni, Mutsamudu, Domoni, Fomboni, na Tsémbéhou. Kuna Wacomoro kati ya 200,000 hadi 350,000 nchini Ufaransa pekee. 

Idadi hiyo ni nusu ya walio nyumbani Comoro. Visiwa vya Comoro vina watu wenye mchanganyiko wa damu ya watu wa nchi na mabara mbalimbali, lakini wengi ni mchanganyiko wa Kiafrika-Kiarabu. 

Asilimia zaidi ya 99 ya Wacomoro ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Ingawa utamaduni wa Kiarabu ndio ulioenea, sehemu ndogo ya wananchi wa Mayotte, wengi wakiwa wahamiaji kutoka Ufaransa, ni Wakatoliki. 

Kuna Wamalagasi (madhehebu ya Kikristo) na Wahindi (madhehebu ya Ismaili) kwa idadi ndogo. Wachina wapo katika sehemu za Mayotte na Ngazidja, hasa Moroni. Pia kuna Wacomoro wengine wahamiaji kutoka Ufaransa na Ulaya hasa Wadachi, Waingereza na Wareno.

Lugha kuu Comoro ni Kicomoro au Shikomor inayofanana kwa maneno mengi na Kiswahili. Kila kisiwa kina jina lake kwa lugha hiyo hiyo – Shingazidja, Shimwali, Shinzwani na Shimaore – inategemeana na mzungumzaji anatoka kisiwa gani. 

Kiarabu ni lugha maalumu kwa ajili ya masomo ya Kurani; ilhali Kifaransa ndiyo lugha rasmi ya kufundishia shuleni na vyuoni. 

Lugha za Malagasi na Shibushi zinazungumzwa na robo tatu ya wakazi wa Mayotte. Asilimia 57 ya watu wote wanajua alfabeti za Kilatini, wakati asilimia 90 wanajua alfabeti za Kiarabu. Idadi ya wanaojua kusoma na kuandika kwa nchi nzima ni asilimia 62.5 (kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2008).

Ufaransa ilianza kutawala Kisiwa cha Mayotte mwaka 1843; na kufikia mwaka 1904 ikawa imevikalia visiwa vingine vya Moroni (Ngazidja, au Grande Comoro), Anjouan (Nzwani) na Moheli (Mwali). 

Mwaka 1974 ilipigwa kura ya maoni, na asilimia 95 ya wananchi wakataka wajitawale. Mayotte, yenye Wakristo wengi, ikapiga kura ya kubaki chini ya Ufaransa. Hadi leo ni sehemu ya Ufaransa.

Visiwa vilivyobaki, Julai 6, 1975 chini ya Rais Ahmed Abdallah, vikajitwalia uhuru. Mwezi mmoja baadaye Rais Abdallah alipinduliwa na Waziri wa Sheria, Ali Soilih. 

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa Comoro kukosa utulivu. Tangu wakati huo kumeshatokea mapinduzi mara 20 hivi. 

Mapinduzi manne kati ya hayo yalifanywa na mamluki wa Kizungu waliojiita Les Affreux au The Terrible Ones, chini ya kiongozi wao Mfaransa, Bob Denard. Denard aliikimbia Comoro mwaka1989 baada ya Ufaransa kupeleka askari wake 3,000 visiwami humo.

Uasi uliendelea. Agosti 3, 1997, baada ya mwezi wa maandamano, Kisiwa cha Anjouan kikajitangazia uhuru wake. 

Lengo kuu likawa kwamba wananchi katika kisiwa hicho walitaka kurejesha utawala wa Kifaransa kwa madai kwamba kitendo chao cha kujitenga na nchi hiyo kimesababisha hali yao ya uchumi kuwa mbaya.

Kisiwa cha Mohéli ambacho ndicho kidogo, pia kilifanya hivyo. Hata hivyo, Ufaransa ikakataa kutambua kujitenga kwa visiwa hivyo kutoka Muungano wa Comoro.

Septemba 1997 majeshi ya Rais Mohamed Taki yalijaribu kukikomboa Kisiwa cha Anjouan, lakini yakashindwa.

Mwaka 1999, Kanali Azali Assoumani, aliongoza mapinduzi, akampindua Rais wa mpito, Tadjidine. Akaahidi uongozi wa mpito wa kijeshi kwa mwaka mmoja, ahadi ambayo AU iliendelea kumkumbusha. Baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo Katiba mpya ikatungwa Machi 2002, na kuvifanya visiwa vitatu kuungana tena.

Kila kisiwa kikamchagua rais wake, na ilipofika Mei mwaka huo huo, Rais wa Muungano alichaguliwa kutoka Grande Comoro (Ngazidja au Moroni). Naye alikuwa ni kiongozi wa mapinduzi wa zamani, Azali. Februari, 2003 mapinduzi dhidi ya Azali yalipingwa.

Desemba 2003 saini ya makubaliano ya kugawana madaraka ziliwekwa ili kukifanya kila kisiwa kuwa na mamlaka fulani fulani ya ndani. 

Mwaka 2004 Bunge la Taifa lilichaguliwa. Mwaka 2006 Kiongozi wa Kiislamu, Ahmed Abdallah Sambi, akachaguliwa kuwa Rais wa Muungano wa Comoro.

Mei 2007 AU ilipeleka jeshi lake nchini humo kwa ajili ya uchaguzi wa Juni, mwaka huo. Bacar wa Anjouan, akajitangaza mshindi, lakini Serikali Kuu ilikataa kutambua ushindi wake. AU ikaitisha uchaguzi mwingine Oktoba na hapo ikawa imechukua hatua ya kuzuia mali zote za Bacar na maofisa wa serikali waliomuunga mkono. Machi 2008, vikosi vya AU vikiongozwa na Tanzania vilitua Anjouan na kumng’oa Bacar ambaye alivaa baibui na kutoroka.

Rais Dk. Ikililou Dhoinine alichaguliwa mwaka 2010 kwa kupata asilimia 61.1 ya kura zilizopigwa. 

Aliingia madarakani rasmi Mei 2011. Baada ya hapo ndipo akaingia Rais Assoumani na kubadili katiba. Moja ya mambo aliyofanya ni kumweka kizuizini Rais mstaafu Sambi ambaye ni mtu wa kuheshimiwa mno.