Na Deodatus Balile, Naivasha, Kenya

Wiki iliyopita niliandika makala nikieleza na kusifia uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwatambua wafanyabiashara kama sehemu muhimu ya jamii ya Tanzania. 

Nimepata mrejesho mkubwa sana. Asanteni wasomaji wangu. Hata hivyo, kati ya mrejesho huo nimepata mrejesho kutoka namba moja ambayo kwa kweli nimetafakari sana kabla ya kuweka hapa ujumbe huo. Mtu huyo ameonyesha chuki ya wazi kwangu binafsi, lakini nikapata shida zaidi kuona kuwa mtu huyu ni mkabila.

Sitanii, nimewaza mno nikajiuliza nini kimemhudhi kwa mimi kusema ukweli kuwa kutambua kundi la wafanyabiashara ni mkondo sahihi wa kujenga uchumi imara wa taifa letu. 

Katika makala hiyo, nilisema hakuna serikali inayoweza kuendelea bila kukusanya kodi. Hakuna jinsi ya kukusanya kodi bila kuwa na wafanyabiashara wakubwa. 

Nilipendekeza kwa makusudi nchi hii iwezeshe baadhi ya wafanyabiashara tupate angalau wafanyabiashara 10 wenye uwezo wa kulipa kodi angalau Sh trilioni 5 au zaidi kwa mwaka kila mmoja, na hii ndiyo itailetea maendeleo ya kweli nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine duniani.

Mtu huyo akaniletea ujumbe mkali, na baadaye alianza kumwaga matusi, nikaishia kumshukuru. Kwa kuwa mtu huyo ni msomaji wa gazeti letu, imebidi niweke ujumbe alionitumia, mtanisamehe una baadhi ya maneno yenye ukakasi, lakini msomaji ukipata fursa ya kusoma makala hii, uingie kwenye mtandao wetu kama gazeti lililopita liko mbali (www.jamhurimedia.co.tz) usome makala hiyo niliyoiandika kisha upime iwapo nilistahili mashambulizi haya. 

Nauweka ujumbe wa msomaji huyu bila kuuhariri, ila nisameheni kwa lugha ya ukakasi iliyomo katika ujumbe huu.

“Hbr ndg Deodatus? naomba nisaidie wewe ni mwandishi wa habari au mwanaharakati? kuna makala unaandika zinaeleweka lkn zingne ni km unatafuta fadhila za viongozi fulani, naamini ipo siku utalipwa fadhila, lkn moja ya sifa ya uandishi ni kuhabarisha umma, kuna katabia ka kihaya kamekukaa sn” watu wenye mawazo finyu”. Kumbuka kila tabaka kwenye jamii lina faida na ndio wanaonunua gazeti lako na kufanya maisha yk yaende. Acha kubeza wt kwa kichaka cha kutaka fadhila,” anasema kupitia Na. 0789673100.

Najiuliza hii dhana ya hovyo kabisa ya kuhukumu watu kwa makabila yao itakoma lini? Kwa Kenya nisingeshangaa, ila nasikitika kuona hapo Tanzania bado kuna mtu anawaza kikabila. Hii ni bahati mbaya ya aina yake. 

Nimeweka ujumbe huu, mhusika apate fursa ya kujipima kama anaishi Tanzania yetu yenye kuthamini mawazo huru bila matusi au ametekwa kwenye dimbwi la chuki lisilostahili kuishi hapo nchini kwetu.

Sitanii, katika makala iliyopita nilisema nitaangalia wapi tumetokea, wapi tupo na wapi tunapoelekea. 

Kimsigi wazee wetu wakiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walipigania Uhuru wa Tanganyika. 

Ajenda kubwa ilikuwa ni kupata Uhuru. Kuna maneno mawili ya Kiingereza – freedom and independence. Yote haya kwa Kiswahili yanamaanisha Uhuru. Hadi leo ukiniuliza nadhani tulipata freedom, hatukuwahi kupata independence.

Kwa nini ninawaza hivyo? Wakati wa mkoloni Malkia wa Uingereza ndiye aliyefahamu fedha za kujenga barabara zinatoka wapi, mishahara ya watumishi wa umma inalipwa kupitia fungu lipi, maendeleo ya jamii kwa ujumla iwe afya, elimu au miundombinu. 

Walipoondoka tukapata Uhuru, hakika bendera yetu ilipandishwa. Hatukushuhudia tukikata mnyororo wa kuendelea kununua mafuta (petroli na dizeli) kutoka kwao. 

Hatukukata mnyororo wa kuzalisha kahawa tukaiuza nusu dola kwao, wakati kikombe cha kahawa London au New York kinauzwa dola 5. Kilo moja inatengeneza vikombe 500 vya kahawa.

Hapa ndipo nitaanzia wiki ijayo. Kama wazee wetu walivyopigania Uhuru (wa bendera – freedom), ni jukumu letu kupigania uhuru wa kiuchumi (independence) na kuondokana na utegemezi wa misaada (aid dependence). 

Wakati umefika tuwe na mkakati wa kufanya nao biashara badala ya kutegemea misaada (trading and not aiding). 

Hatuwezi kufanya hivyo bila kutoa elimu ya biashara, biashara ikawa taaluma badala ya kubaki kuwa urithi hapa nchini. 

Tukiiendea biashara kama taaluma, ni wazi tutashuhudia maadili ya hali ya juu katika kufanya biashara na ulipaji kodi bila shuruti, badala ya kuishi kwa mazoea. Tukutane wiki ijayo. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.