Kesho ni Desemba Mosi, siku ambayo imetengwa na kufahamika kimataifa kama ‘Siku ya Ukimwi Duniani’ ambapo kwa Tanzania maadhimisho hayo huratibiwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS).

TACAIDS ilianzishwa Desemba 1, 2000 na Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ikipewa jukumu la kuratibu mwitikio wa Tanzania kwa janga la Virusi Vya Ukimwi (VVU) na ukimwi.

Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ni kutathmini hali na mwelekeo wa udhibiti wa ugonjwa huu uliotangazwa kama janga la taifa mwaka 1999. 

Kwa maana hiyo, kesho Watanzania tutaungana na dunia kutazama tumetoka wapi, tuko wapi na tunaendelea vipi na mapambano dhidi ya ugonjwa huu uliosababisha watu wengi kupoteza maisha na kuacha mfadhaiko kwa jamii.

Madhumuni mengine ya siku ya kesho ni kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARV) pamoja na kupinga unyanyapaa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye atakayeliongoza taifa kesho katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi yatakayofanyika jijini Mwanza chini ya kaulimbiu; ‘Jamii ni Chachu ya Mabadiliko – Tuungane Kupunguza Maambukizi Mapya ya VVU’.

Kaulimbiu hii inasisitiza ushiriki na ushirikishaji wa jamii katika shughuli za udhibiti wa ukimwi kuanzia kwenye upangaji mikakati, upatikanaji na utoaji wa huduma za VVU na ukimwi.

Tanzania kama taifa huru tumejiwekea malengo ya kuhakikisha ugonjwa huu unatoweka katika jamii yetu ifikapo mwaka 2030, yaani miaka kama tisa tu kutoka sasa.

Ingawa miaka tisa inaweza kuonekana kuwa ni michache, tukiamua na kuweka mikakati thabiti kama taifa tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuutokomeza ugonjwa huu ndani ya kipindi hicho.

Elimu ya namna ya kujikinga dhidi ya ukimwi, ugonjwa uliogunduliwa mara ya kwanza nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980, imetolewa na kusambazwa kiasi cha kutosha.

Maana yake Watanzania wengi kama si wote wanafahamu namna ya kujiepusha na ugonjwa huu. Wanafahamu tabia zote zinazosambaza ugonjwa wenyewe. Wanayafahamu madhara ya ukimwi kijamii.

Kwa hiyo kilichobaki kwa sasa ni kuwapo kwa nia ya dhati ya kuyatekeleza yote yanayotakiwa katika mapambano hayo. 

Utekelezaji huu sasa uchukuliwe kama ni shuruti ili ifikapo mwaka 2030, jamii au walau kizazi kijacho kiusome ukimwi kwenye vitabu vya historia.