*Tume ya Haki za Binadamu yabainisha matumizi mabaya ya ofisi

*Ashirikiana na mwindaji kuhujumu biashara za mwekezaji

*Atuhumiwa kupokea ‘rushwa’ ya visima Uchaguzi Mkuu 2020

*Mwenyewe ang’aka, asema; ‘tusiongee kama wahuni, nendeni mahakamani’

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Hadhi ya uongozi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, imechafuka; JAMHURI limebaini.

Taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inasema Mnyeti, ambaye sasa ni Mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza amekuwa akikiuka maadili ya uongozi na utawala bora wakati akiwa mkuu wa mkoa.

Taarifa hiyo ipo katika jalada namba HB/S/1556/2021/SC01/DSM (nakala tunayo) iliyosainiwa ma Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji (mstaafu) Mathew Maimu, imetokana na malalamiko yaliyowasilishwa Februari 12, 2021 na mfanyabiashara, Dk. Hamis Kibola, anayemiliki kitalu cha uwindaji katika Pori Tengefu la Simanjiro mkoani Manyara kupitia Kampuni ya HSK Safaris.

Malalamiko dhidi ya Mnyeti

Katika malalamiko yake Tume ya Haki za Binadamu, Dk. Kibola, anamtuhumu Mnyeti na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Emboret, Belinda Sumari, kushirikiana na mwindaji mwenye asili ya Kiarabu, Saleh Al Amry, kuhujumu biashara zake na kukiuka haki zake za msingi kama binadamu. Mnyeti na Belinda ni watumishi wa umma.

“Mnyeti alipanga njama kwa ustadi mkubwa akishirikiana na Al Amry anayefanya biashara ya uwindaji ili kunufaika na kitalu hicho. Al Amry akapeleka tuhuma (kwa Mnyeti akiwa Mkuu wa Mkoa) kuwa HSK Safaris inajihusisha na ujangili.

“Mateso yakaanzia hapo. Taarifa zikapelekwa Polisi. Mnyeti akaingilia kati na kuunda Tume (kamati) ya Uchunguzi,” analalamika Dk. Kibola.

Dk. Kibola anasema yeye na Al Amry walianza kushirikiana kibiashara kwenye kitalu hicho mwaka 2016. Al Amry alijihusisha na utafutaji wageni pamoja na uendeshaji wa shughuli zote za kitalu, kabla ya kutofautiana Juni 2019.

Dk. Kibola analalamikia hatua ya Mnyeti ya kuunda kamati ya kumchunguza ilhali akijua hana mamlaka hayo kisheria; kisha yeye na Belinda kumzuia kuingia kwenye kitalu anachokimili kihalali, kwa takriban miezi minane. 

Chanzo cha ugomvi huo ambao JAMHURI limewahi kuandika, kinatajwa kuwa ni masilahi kati ya washirika wa kibiashara kwenye kitalu hicho, Al Amry na Dk. Kibola. 

“Maelekezo ya Mnyeti kwa Belinda pamoja na utekelezaji wake vilifanyika bila barua wala maandishi rasmi kama taratibu za serikali zinavyoelekeza, hivyo kutia shaka uhalali wa amri na maelekezo yote,” yanasomeka malalamiko ya Dk. Kibola kwa Tume ya Haki za Binadamu.

Baada ya Mnyeti kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kumchunguza Dk. Kibola, akawasiliana na Kikosi Kazi (Task Force) Dhidi ya Ujangili na kukielekeza kufanya uchunguzi wa tuhuma za ujangili dhidi ya HSK Safaris.

Desemba 19, 2019 kikosi kazi hicho kilimkamata Dk. Kibola na watu wengine kadhaa wakiwamo wawindaji mahiri (professional hunters).

Dk. Kibola alitolewa Dar es Salaam hadi Arusha na kuwekwa rumande siku saba katika Kituo cha Polisi cha Utalii bila kupelekwa mahakamani.

Anasema kwenye sakata lote la kuandamwa na Mnyeti, amewekwa rumande kwa nyakati tofauti kwa siku 30.

Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu

Baada ya kupokea malalamiko hayo, THBUB ikaanza kufanya uchunguzi na kuukamilisha Oktoba 25, 2021.

Miongoni mwa watu waliohojiwa na kutokana na hadidu rejea tano zilizokuwapo ni mlalamikaji, Dk. Kibola; walalamikiwa, Mnyeti na Belinda, Kaimu Katibu Tawala Manyara, Said Mahiye na aliyekuwa Katibu wa RC (Mnyeti), Ibrahim Mbogo.

Wengine ni Wakili wa Serikali Mkoa wa Manyara, Peter Ngasa; Kamanda wa Polisi Manyara, Mareson Mwakyoma; Kamanda wa Polisi Wilaya ya Simanjiro, Juma Majata na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi.

Tume pia katika kutafuta haki na ukweli, imewahoji Ofisa Tarafa wa Emboret, Chausiku Baha; Ofisa Upelelezi Mkoa wa Arusha, ACP J. Mwafulango; aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mnyeti, SP Said Mchaki; Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Utalii Arusha, ASP Zegela; Saleh Salum Al Amry pamoja na Mhifadhi Wanyamapori TAWA Kanda ya Kaskazini, Emmanuel Pius.

Yaliyobainika

Katika Sura ya Tatu ya taarifa hiyo, tume imebaini kuwa Mnyeti alimwelekeza Belinda kumzuia mlalamikaji asiingie katika kitalu chake cha uwindaji pamoja na kuwa na vibali vyote halali.

Uchunguzi wa Tume umebaini kutofuatwa kwa taratibu za mawasiliano za utendaji kazi serikalini kwa kufuata ngazi za uongozi; kwamba kwa utaratibu Mkuu wa Mkoa alipaswa kumjulisha Katibu Tawala Mkoa ambaye angemjulisha Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Simanjiro naye angemjulisha Ofisa Mtendaji wa Kata kwa utekelezaji.

Pamoja na utaratibu huo kutozingatiwa, maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kuhusu zuio hilo hayakutolewa kwa maandishi bali kwa njia ya simu kwenda kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Emboret. 

“Mwenye dhamana ya kuweka zuio kuingia katika kitalu cha uwindaji ni Waziri wa Maliasili na Utalii. Kwa mujibu wa kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Sura 283, mwenye mamlaka ya kufuta kitalu cha uwindaji ni waziri. Hivyo, mkuu wa mkoa hakuwa na mamlaka kisheria kuweka zuio kwenye masula ya uwindaji,” inasema taarifa hiyo na kuendelea:

“Ofisi ya TAWA Kanda ya Kaskazini walipohojiwa na Tume Julai 3, 2021 walieleza kuwa hawakujua kuhusu kuwapo kwa suala la zuio na wala hawakushirikishwa katika jambo lolote lililomhusu mlalamikaji.”

Uchunguzi umebaini kuwa kamati aliyounda Mkuu wa Mkoa haikuwa na mamlaka ya kufanya uchunguzi wa masuala ya uwindaji wa wanyamapori kwa kuwa yako nje ya mamlaka yake kisheria. Pamoja na kamati hiyo kufanya uchunguzi mapendekezo yake hayakuwafikia walengwa ambao ni mlalamikaji na Wizara ya Maliasili na Utalii.

“Hata muundo wa Kamati hiyo haukuhusisha taasisi zinazojihusisha na shughuli za usimamizi wa wanyamapori,” inasomeka taarifa hiyo na kuongeza:

“Kwa ushahidi huo ni kuwa Mkuu wa Mkoa hakuwa na mamlaka ya kuunda kamati ya kuchunguza shughuli za uwindaji wala hakuwa na mamlaka ya kuweka zuio. Ni wazi kuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa (Mnyeti) alifanyakazi nje ya mipaka yake kisheria.” 

Tume pia imebaini kuwapo kwa uvunjifu wa haki za binadamu uliofanywa na Mnyeti dhidi ya Dk. Kibola,  kumzuia kuingia kwenye kitalu anachokimiliki kinyume cha Ibara 24(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kuwa kila mtu ana haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi ya mali yake kwa mujibu wa sheria.

“Pia kumuweka mlalamikaji mahabusu kwa siku kadhaa katika Kituo cha Polisi Utalii Arusha na Orkasumet –  Simanjiro bila kufikishwa mahakamani kwa agizo la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kulimnyima mlalamikaji kuwa huru kwa mujibu wa Ibara ya 17(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” inasema taarifa.

Haki nyingine iliyokiukwa ni ya kumzuia kuingia kitaluni kwa miezi minane.

Misingi ya Utawala Bora iliyokiukwa

Katika suala hilo, ripoti inasomeka: “Kitendo cha Mnyeti kutoa taarifa zisizo na uthibitisho ni kinyume cha maadili. Wakati Mnyeti alieleza kuwa aliweka zuio kwa maandishi, uchunguzi umeonyesha hakukuwa na maandishi bali taarifa zilizotolewa kwa mdomo.

“Wakati Mnyeti alieleza kuwa alipokea barua ya malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na uwindaji haramu kwenye kitalu cha HSK Safaris Ltd, uchunguzi umeonyesha hakukuwa na barua ya malalamiko iliyowasilishwa na wananchi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

“Uwepo wa uhusiano kati ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara (Mnyeti) na Saleh Salum Al Amry kuna ashiria harufu ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

“Al Amry alichimba visima vya maji katika Jimbo la Misungwi kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Mnyeti sasa ni Mbunge wa Misungwi.”

Mbali na uadilifu, tume imebaini Mnyeti alikiuka utawala wa sheria, kufanya kazi pasipo kushirikisha wadau kama TAWA katika suala husika na kukosa uwajibikaji kwa kushindwa kujibu barua kadhaa alizoandikiwa na mlalamikaji.

Katika hitimisho, tume imebaini kuwa zuio lililowekwa na Mnyeti kwa kumtumia Belinda limemsababishia hasara mlalamikaji na kushindwa kumudu kulipa tozo mbalimbali za uendeshaji wa kitalu.

Mnyeti ang’aka

JAMHURI limemtafuta Mnyeti kutaka kufahamu ukweli uliowekwa na tume, hasa kuhusu mwenendo wake akiwa mkuu wa mkoa na kuwapo kwa harufu ya rushwa katika uchaguzi uliopita.

Baada ya kupokea simu, Mnyeti akasema: “Tume ni ya nani? Ni Tume ya serikali, kaka, tusiongee kama wahuni ‘otherwise’  kuna kitu kingine mnatafuta.

“Kama wamesema kuna rushwa sijui ya Saleh, jambo muhimu ni waende mahakamani! Kwa nini mnazungukazunguka?

“Ni mwaka mzima sasa mnaandika, mara kwenye ‘jamiiforum’ mara kwenye JAMHURI. Mwambieni Kibola aende mahakamani.”

Alipoambiwa na mwandishi wa habari hii kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya Kibola na utafutaji wa ukweli kama ulivyoanikwa na tume, Mnyeti akasema:

“Mimi namjua huyo (Dk. Kibola) ananunua waandishi. Sasa, mwambie kuwa haki haipatikani kwenye magazeti, bali mahakamani.

“Atafute mwanasheria, hata yeye si ana PhD ya sheria! Aende mahakamani tukutane huko. Kama kuna visima vimechimbwa, mwambie aende mahakamani, Mnyeti yupo, hajatoroka nchi na atahudhuria vikao vyote hadi mwisho.

“Nikikutwa na hatia nitaadhibiwa. Sasa mnataka nini? Wewe nipigie simu muda wowote brother nitakujibu.”

Kwa upande wa Al Amry, hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi alioandikiwa kutaka kufahamu msimamo wake.

Akizungumza na JAMHURI, mlalamikaji, Dk. Kibola amesema: “Kwanza, ninamshukuru Mungu kwamba haki imetendeka. Tume imethibitisha kwamba nilionewa kwa muda mrefu.

“Pili, ninaishukuru serikali kwa kusimamia haki na kuhakikisha inatendeka. Huu ndio utawala bora. Watu wengi sana wamedhulumiwa haki na kutendewa vibaya kutokana na tamaa za viongozi wachache.”