‘Katiba mpya, mgombea
binafsi havikwepeki’
DAR ES SALAAM
NA DENNIS LUAMBANO
Kachero mbobezi, Bernard Membe, anasema hakuna wafanyabiashara walioumizwa na Serikali ya Awamu ya Nne ikilinganishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Anazungumzia mwenendo wa utawala wa Awamu ya Nne wa Jakaya Kikwete, ikiwa ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa habari zinazotokana na mahojiano maalumu na Gazeti la JAMHURI yaliyofanyika nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Katika toleo lililopita Membe aliyewahi kuwa Mbunge wa Mtama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2015, alielezea umuhimu wa viongozi wote kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kujua historia na taarifa zao, kwa kuwa baadhi yao si Watanzania.
Kuhusu wafanyabiashara anasema anaweza akasimama juu ya paa akaeleza kwamba hawakuumizwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ukilinganisha na walivyoumizwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
Pia anasema hakumbuki kama kuna watu waliumia kwa ajili yake kutokana na yeye kuwa msimamizi au mtu wa karibu wa Jakaya, kwa sababu ya nafasi yake ya Waziri wa Mambo ya Nje.
“Ukiwa katika nafasi hiyo hufanyi mambo ya nje tu, unashirikishwa na mambo mengine mengi, kumbuka nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nje, Ulinzi na Usalama,” anasema na kuongeza:
“Sikumbuki ukiondoa mpaka wa Malawi au kuwaumiza watu kisaikolojia. Mbali na kufunga mpaka wa Malawi na kuuweka katikati ya maji (Ziwa Nyasa) hadi leo na Banda akasema watu wanashindwa kwenda Likoma kuzika ndugu zao.
“Kwa sababu mpaka uko katikati, sikumbuki kama kuna mtu mmoja atasimama atasema jamani sikilizeni mimi nimeumizwa na ushauri wa Membe, mtu huyo ajitokeze, kwa sababu moja, mimi ni mseminari, namthamini Mungu.”
Pia anasema yeye hawezi kumuonea mtu bure hata siku moja, na mtu huyo hawezi kuwa mfanyabiashara maarufu hapa nchini Rostam Aziz.
Anasema Rostam amewasaidia mwaka 1995, ila akiwa na mfanyabiashara mwingine maarufu hapa nchini, Yusuph Manji, wamejiumiza wenyewe.
“Unajua suala la fedha za Akaunti ya EPA mimi nikiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nilisisitiza lazima hatua zichukuliwe, tusiseme kwamba kulikuwa na fedha za bure BoT, kwamba zile fedha hazikuwa na mtu,” anasema na kuongeza:
“Niliingilia hilo suala kama mshauri wa karibu wa Rais Kikwete na kuondoa hiyo dhana kwamba fedha za EPA hazikuwa na mwenyewe na ndiyo maana hata mbele ya umma hakuna aliyenishambulia na nilikataa ile hoja kwamba zile fedha si za serikali.
“Na tukisema hivyo tutatengeneza mwanya wa kila mtu kuzichukua jambo ambalo halitakuwa sahihi. Sasa kuna mtu alikuwa anaumia, sasa ni kama vita, ni kama Mwalimu Nyerere wakati wa Vita ya Kagera ukimuuliza ulipigana vita na watu 108 walikufa, je, wewe una dhambi? Atakwambia ile ilikuwa vita halali.
“Na mimi ukiniuliza kuna watu niliwaumiza nitakwambia ndiyo lakini kwa sababu ile ilikuwa ni vita halali, si kwamba niliwaumiza nikafurahi au niliwaumiza makusudi hapana, kwamba kusema fedha hizi hazina mwenyewe ndipo ameumia wakati ameshachukua.
“Wamenishughulikia kweli, usione mimi nimemshitaki Musiba kwamba alikuwa peke yake, hapana. Sikutaka tu kuwajumuisha katika hii kesi, nina macho kweli kama ya panzi, huyu Musiba hakuwa peke yake.
“Kuna watu walikuwa wananikomoa mimi kupitia kwake, kwa sababu nilikuwa ninajua, nikasema nichukue kichwa hicho na wengine niwaache.”
Urafiki wake na Lowassa ukoje?
Kuhusu urafiki wake na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anasema ni kaka yake kipenzi.
“Sikiliza, Lowassa ni mtu ambaye, kwanza kati yetu kila mtu anayepata matatizo anampelekea mwenzake salamu za kumtakia kila la heri, tunasalimiana vizuri sana,” anasema na kuongeza:
“Amenizikia dada yangu Esther vizuri sana, na sasa hivi namtumia mtoto wake Fred kila ninaposikia hali ya afya ya Lowassa inakwendaje, ninamtumia Fred ambaye ni Mbunge wa Monduli.
“Tuna uhusinao mzuri sana na Lowassa, lakini nguvu zilizoharibu uhusiano wetu hakuwa Rostam na hautasikia Membe amefanya chochote, kamwe, na kama yeye alifanya sawa.”
Anasema urafiki wao ni wa kujivunia. Anamtaja Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa ana tabia moja ambayo kama binadamu angeiga tungefika mbali.
Anasema Kikwete anaweza akawa na adui yake, lakini hataki kukuambukiza na wewe huyo adui.
“Anakwambia kabisa adui yangu mimi ni adui yangu… na Membe nikiwa ni rafiki wa karibu wa Jakaya, ninajua adui zake, na mimi ananiambia wale ni maadui zangu kwa mambo kadha wa kadha,” anasema.
Je, ni kweli kwamba mvutano wake na Lowassa ulisababisha Magufuli akapenya katika mbio za urais ndani ya CCM mwaka 2015?
Membe anajibu swali hilo: “Hapana, ukitaka kujua kilichotokea mwaka 2015, tukae kikao kingine cha mahojiano, inavutia sana, kwa sababu ngoja nikueleze, hali hiyo ilikuwapo hadi anateuliwa Magufuli, lakini asubuhi yake baada ya kuteuliwa ile usiku, Lowassa aliulizwa na viongozi wale wa CCM ambalo ni Baraza la Wazee.
“Kwamba wale wazee wameambiwa wakimteua mtu mwingine mbali na Membe hautatoka CCM na utaridhika na matokeo? Lakini aliwakatalia na aliwaambia kwamba wasipomteua yeye, kisha wakamteua Membe atahama CCM.
“Akawaambia, ‘tafadhali sikilizeni, nimesema hivi na ninasema hivi kwamba msiponiteua mimi kuwa mgombea wa kiti cha urais nitahama.’
“Ndivyo alivyosema, akasema asipitishe mtu maneno katikati ya kusema kwamba akiteuliwa Membe basi yeye atahama CCM – hata kidogo. Ni yeye mkimuacha ndiyo atahama.”
Madai ya Katiba mpya
Anaunga mkono mchakato wa nchi wa kutaka mabadiliko hayo. Anasema umuhimu wake upo na suala la Katiba mpya ni jambo la lazima kabisa, kwa sababu hiyo ni nyaraka pekee ambayo wananchi lazima washirikishwe.
“Hakuna nyaraka nyingine ikiwamo sijui mikataba, fanyeni huko serikalini, hii ni nyaraka pekee ambayo wananchi wanayo haki ya kushiriki kuitengeneza vizuri, na tunu za nchi lazima zisemwe maana msipotengeneza Katiba mpya mnaweza kuwa na fisi mle ndani,” anasema na kuongeza:
“Kwa hiyo suala la kuwa na Katiba mpya ni jambo la lazima kabisa, lakini kama sikosei Rais Samia Suluhu Hassan hajalikataa ila ana vipaumbele vyake kwanza vya kuvitekeleza kisha suala hilo litakuja baadaye.
“Si kwamba Rais Samia amekataa suala la Katiba mpya, analikubali, isipokuwa anangoja wakati mwafaka ufike kwa hiyo ni suala la kumuombea na kumshawishi ili aweze kusema ni lini shughuli za Katiba mpya zinaweza kuanza, lakini mimi ninaamini na nimefanya naye kazi analipenda kabisa suala la Katiba mpya.”
Pia anasema unapoingia katika nafasi ya urais unakuwa na changamoto nyingi za kuzizingatia, pengine hata kabla haujafika huko na ana imani kwamba Rais Samia analiona na kuna siku atalala, atamka na kuanza kuonyesha nia ya kuanza uchambuzi wake.
“Nawaomba Watanzania wenzangu tumpe muda Rais Samia, urais ni jambo moja kubwa mno na zito sana, kwa hiyo tumpe muda kidogo ili hatimaye alifanikishe,” anasema Membe.
Mgombea binafsi
Kuhusu suala la mgombea binafsi anasema ni gumu na ana hakika katika Katiba mpya inayopigiwa chapuo litajitokeza.
Anasema katika Katiba mpya inayoombwa suala hilo litajitokeza na linaweza kushinda na yeye ataheshimu uamuzi wowote ule.
“Si mbaya unajua, mimi nilipokuwa katika madaraka nilikuwa ninalilia vitu hivyo; kwanza mgombea binafsi kwa sababu kama wewe unajiamini katika chama kwanini usigombee?” anahoji.
Uraia pacha
Kuhusu uraia pacha anasema si tu kwamba utambue Watanzania waliopo nje ya nchi, bali wapewe haki au ruhusa hiyo, kwa kuwa kuna fedha zinazotoka nje kwa diaspora ila sisi Tanzania tunazikosa.
Anasema Kenya, Nigeria, Comoro na Ghana wanapata fedha nyingi kwa mwaka kutoka kwa diaspora, kwa sababu wameruhusu wananchi wao kama wana sifa za kuchukua uraia katika nchi hizo, wafanye hivyo.
Anasema Mtanzania akiwa na sifa na amepewa uraia wa nchi nyingine anakuwa analipwa zaidi kuliko mtu asiyekuwa raia, kwa sababu yeye anafanya kazi ndogondogo tu zinazompa fedha kidogo.
“Au mtu aliyepata uraia anapata zile kazi nzuri, anaweza kuwa ofisa mtendaji mkuu wa kampuni mahala, labda anapata dola 6,000 au 8,000 za Marekani kwa mwezi.
“Ile Serikali ya kule inailipa serikali yetu huku kwa sababu wewe umesomeshwa na sisi huku, sasa serikali ya kule inawajibika kuilipa Tanzania kwa watu wake wote ambao wameiacha nchi yao huku na kwenda kuitumikia nchi ya kule.
“Na matunda ya kule ya watu wako uliowasomesha kwenda kuitumikia nchi nyingine ndiyo maana mnalipwa fedha hizo ili isionekane kama vile wanatunyonya, ndiyo maana Kenya wanapata dola bilioni 1.4, Nigeria wanapata dola bilioni 2.6, Ghana wanapata dola bilioni 2 za watu wao wanaofanya kazi nje ya nchi – wanalipwa.”
Anasema Tanzania tunazikosa fedha hizo kwa sababu tumekataa Mtanzania yeyote kuchukua uraia kule, kwa kuwa ni kama adui wa nchi, na amenunuliwa na nchi, anatumiwa na nchi hiyo.
“Nilipokuwa Mambo ya Nje (waziri) nilikuwa ninawatania wenzangu kama mnakataa hilo ngoja niwaulize swali, kwanini Waziri wa Mambo ya Ndani hapa anatangaza katika magazeti watu wanaotaka uraia wa Tanzania na tunawapa?
“Sisi hawa wamekaa miaka 10 hawajafanya makosa na tunawapa uraia, lakini Mtanzania aliyekaa Uingereza miaka 10 unamwambia ole wako uchukue, hatufikirii sawasawa.”
Ameipokeaje hukumu dhidi ya Musiba?
Membe anasema ameifurahia hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa Oktoba 28, mwaka huu na kumuamuru Cyprian Musiba kumlipa fidia ya Sh bilioni sita kutokana na kumchafua.
Anasema hukumu hiyo imemsafisha kwa sababu aliumizwa, alidhalilishwa na kutenganishwa na jamii ya Watanzania na wanadiplomasia wenzake duniani.
Anasema alitwishwa kashfa kubwa za uhaini ambazo adhabu zake ni, ama kufungwa, au kunyongwa hadi kifo kwa kuwa aliambiwa anamhujumu Rais Magufuli, anafanya kampeni mapema kabla ya wakati, baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kutamka hivyo Geita alipozungumza na wana CCM.
Anasema aliambiwa amekwenda Zimbabwe kukutana na majenerali wastaafu kupanga njama za kuipindua serikali ya Magufuli, wakati yeye alikwenda kama mwangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2018 kwa mwaliko rasmi akiwa na timu ya watu 15.
Hata hivyo, anasema safari hiyo ‘ikageuzwa’ na kuwa ya kukutana na majenerali na akaambiwa yeye ni mtu hatari.
“Ikachukuliwa orodha ya watu 14 mimi ndiyo nikawa mkubwa wao, maana picha yangu ilikuwa kubwa, nikaambiwa nimekula fedha za Libya, kesi ambayo ilikwenda mahakamani na rufaa mara tatu, Membe hatajwi, hasemwi wala by implication,” anasema na kuongeza:
“Lakini nikatwisha mimi na pale Mahakama Kuu waliokuwa wanaanzisha kiwanda cha saruji Lindi ni Kampuni ya Meis Industries Ltd, alishinda ile kesi kukawa na appeal iliyofanywa, walikata rufaa mara tatu.
“Membe hata senti moja hakuchukua wala jina lake halikusemwa wakati kesi zote hizo zinasemwa, lakini ikaonekana fedha amechukua Membe, uongo mtupu.”
Pia anasema akazushiwa taarifa kwamba amekwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kukutana na wafanyabiashara, kukusanya fedha, na majeshi kwa ajili ya kuipindua Serikali ya Magufuli.
Anasema tangu aache uwaziri mwaka 2015 hajawahi kwenda DRC hata siku moja.
“Ukiniuliza niliipokeaje hukumu iliyotolewa Oktoba 28, mwaka huu na Mahakama Kuu, jibu langu ni kwamba nilifarijika, nilifurahi kwa sababu nilipata haki yangu na madai yote yaliyotolewa na mawakili wangu yalibeba msingi mkubwa wa kisheria.
“Na Mahakama Kuu ikatupilia mbali propaganda, uongo na udhalilishaji wote ambao walikuwa wanaufanyia biashara, nilifurahi sana,” anasema.