DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Alhamisi Oktoba 29, 2020, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ilimtangaza Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa mshindi wa nafasi ya Rais wa Zanzibar, kwa ushindi wa asilimia 76.27 ya kura zilizopigwa.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dk. Mwinyi aliwashukuru Wazanzibari wote na kuwataka waungane kuijenga Zanzibar mpya.

“Wajibu ulio mbele yetu ni kudumisha amani, uchaguzi umekwisha turudi tuwe kitu kimoja, tuponye majeraha ya uchaguzi na kujenga Zanzibar mpya,” anasema Dk. Mwinyi.

Saa 4:30, Novemba 2, mwaka jana, Dk. Mwinyi aliapishwa kuwa Rais wa Nane wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, akimrithi Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

Siku chache baada ya kula kiapo, Dk. Mwinyi alitembelea Bandari ya Zanzibar kujionea ufanyaji kazi katika kitengo hicho muhimu katika kukuza uchumi wa Zanzibar.

Katika hatua za awali za mikakati ya serikali yake juu ya ukusanyaji kodi, mapato ya serikali na kukuza uchumi wa bluu visiwani humo, Desemba 5, mwaka jana, Dk. Mwinyi alikutana na wafanyabiashara wa kada mbalimbali wakiwamo wamiliki wa viwanda, wakulima wakubwa, wavuvi, wafugaji na wafanyakazi wa bandari.

 Katika mkutano huo, Rais Dk. Mwinyi anasema: “Hili ninataka kusema hadharani, tusifichane, tukifichana hatuwezi kujenga. Tukisema tunajenga sina maana ya kufukua makaburi wala sina nia ya kutafuta mchawi. Lakini ninasema kuanzia sasa kwenda mbele kila mtu lazima alipe kodi.”

Akifafanua kuhusu mazingira rafiki ya kodi, Rais Mwinyi anasema yeye si muumini wa kodi kubwa ila anaamini kujenga uchumi kwa kodi ndogo itakayochochea mnyororo wa shughuli nyingi za kibiashara kwa Wazanzibari. 

“Watu wanadhani kodi kubwa ndiyo pato kubwa. Kwa serikali ni kinyume chake, kwani kodi kubwa hupunguza wafanyabiashara. Watakaofanya biashara kwa kodi kubwa ni wachache. Ila tukipunguza, watakaofanya biashara ile ni wengi,” anasema.

Rais huyo wa nane ameanzisha Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi katika hatua ya kutimiza ahadi yake wakati wa kampeni, akiwataka Wazanzibari kutumia fursa hiyo muhimu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa zima.

Katika hatua za kuimarisha uwajibikaji na nidhamu kazini, Dk. Mwinyi alivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar baada ya kutoridhishwa na ufanyaji kazi wake.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Rais Mwinyi kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Malindi na eneo la Maruhubi kutafuta mwarobaini wa ucheleweshaji wa kutolewa mizigo bandarini hapo.

Tangu aingie Ikulu, Dk. Mwinyi amekuwa na mikakati mbalimbali inayolenga kupeleka huduma kwa wananchi na kunufaisha kundi kubwa la wananchi wa kipato cha chini kisiwani humo.

Desemba 17, mwaka jana, Mwinyi alikutana na kuzungumza na wajasiriamali kutoka Mkoa wa Kusini Pemba na kusema wavumilie wakati akifanya uamuzi mgumu kushughulikia ufisadi visiwani humo. 

“Nimekaa madarakani kwa mwezi mmoja na nusu lakini kila ninapogusa kumejaa ufisadi. Nitafanya uamuzi mgumu ila sitafukua makaburi wala kutafuta mchawi. Baada ya uamuzi  huo wenye nia ya kujenga uchumi imara kila senti ya fedha ya  serikali itaheshimiwa,” anasema.

Anasema yapo mambo yasipofanywa kwa uamuzi mgumu wakati huu huko mbele kutakuwa kugumu sana na maendeleo yaliyokusudiwa hayatafanikiwa, jambo litakalofanya wananchi waendelee kukabiliana na kero zilizopo na kusisitiza kwamba jambo hilo halikubaliki.

“Leo tukiwa tunatekeleza tuliyoyaahadi halafu kuna mtu anatubomoa, kumuachia itakuwa tumejitakia wenyewe.

“Nayasema haya kwa madhumuni ya kuwatayarishia wananchi kwa yatakayokuja kuyasikia katika kipindi kifupi kijacho. Kwani serikali imedhamiria kukuza uchumi wa Zanzibar,”  alieleza Dk. Mwinyi. 

Ndani ya siku 100 za  uongozi wake Rais Mwinyi aliahidi kuanzishwa kwa mahakama  ya  kushughulikia  wala  rushwa   na wahujumu uchumi,  hatua ambayo inaelezwa kuwa na tija katika vita ya kupambana na rushwa na ufisadi.

Aidha, katika kipindi cha mwaka mmoja Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi amefanikiwa kuleta maendeleo  makubwa katika sekta mbalimbali pamoja na changamoto zilizopo. 

Oktoba 8, mwaka huu Dk. Mwinyi alisema serikali yake imetenga jumla ya Sh bilioni 70 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo, hatua itakayowakomboa na kupambana na umaskini.

“IMF imetupatia Sh Bilioni 70 ili kuwawezesha wajasiriamali wetu kuzitumia kwa ajili ya biashara na kutaka serikali za mtaa kuwa na weledi wa hali ya juu katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Rais Dk. Mwinyi katika uongozi wake amefanikiwa kudumisha amani na utulivu, kuwaunganisha wananchi, kuhamasisha umoja na mshikamano na kufanikiwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa  (SUK) ambayo imeleta maridhiano, mshikamano na umoja madhubuti kwa Wazinzibari na Watanzania kwa ujumla.

Ndani ya mwaka mmoja serikali chini ya uongozi wa Rais Mwinyi imefanya jitihada kubwa na kuleta mabadiliko chanya kwa watumishi na viongozi wa umma katika utoaji huduma kwa jamii.

Katika utekelezaji wa uchumi wa bluu kumeshuhudiwa tukio kubwa la kihistoria la utiaji wa saini wa hati za maendeleo (MOU) wa ujenzi wa bandari kubwa na za kisasa za Mangapwani na Mpigaduri.

Zanzibar imesaini Mou na Serikali ya Oman kupitia mamlaka yake ya uwekezaji kuhusu bandari ya mafuta na gesi ya Mangapwani. Pia imesaini na Kampuni ya intertorco yenye makao makuu yake mjini Madrid Hipsania.

Mpango huo unahusu ujenzi wa bandari shirikishi ya uvuvi eneo la Mpigaduri – Unguja na bandari ya mkoani Pemba, pamoja na mradi wa ufuaji wa umeme kupitia nishati ya gesi.

Serikali ya Awamu ya Nane imefanikiwa kudhibiti mianya ya rushwa na kuzuia safari ambazo hazikuwa na masilahi kwa taifa, huku idadi ya wawekezaji ikielezwa kuongezeka siku hadi siku pamoja na kutokea kwa janga la ugonjwa wa Uviko – 19.

Rais Mwinyi amefanikiwa kuanzisha mahakama ya udhalilishaji na wanaotuhumiwa kudhalilisha hawapewi dhamana mpaka kesi zihukumiwe.

Tofauti na huko nyuma, mapato ya bandari kwa mwaka yameongezeka kutoka Sh bilioni 4 hadi kufikia Sh bilioni 2 kwa mwezi na kufanya mapato hayo kufikia Sh bilioni 24 kwa mwaka.

Ndani ya mwaka mmoja serikali ya Rais Mwinyi imeanzisha jumla ya miradi 97 yenye uwezo wa kutoa ajira 7,000, hatua inayotatua tatizo la ajira na kuinua uchumi wa taifa.

Ndani ya miradi hiyo kuna mradi mkubwa wa mkopo wa Benki ya Dunia ambao una uwezo wa kusambaza nyaya za umeme Zanzibar nzima, wenye thamani ya dola za Marekani milioni 150. 

Katika hatua nyingine, Serikali ya Awamu ya Nane imefanikiwa kuzipatia ufumbuzi kero 11 za muungano kwa kipindi kifupi, tofauti kabisa na mategemeo ya wengi. 

“Mgawanyo wa mapato ya kodi kwenye huduma za simu, sheria na uvuvi wa bahari kuu pamoja na ucheleweshaji wa mikataba ya miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa barabara ya Chakechake – Wete na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bunguni, masuala haya yameshapatiwa ufumbuzi,” amesema Rais Dk. Mwinyi.   

Hashim Yahya wa Morogoro anasema Rais Dk. Mwinyi amefanya uamuzi mgumu wenye tija kwa Zanzibar tofauti kabisa na wengi walivyosema ni mpole.

Mfuatiliaji huyo wa masuala ya siasa na kijamii anaongeza kuwa ndani ya mwaka mmoja Rais Dk. Mwinyi ameleta mabadiliko makubwa sana katika nyanja zote za maendeleo, Wazanzibari hawana budi kumuunga mkono kwa kuchapa kazi kwa bidii. 

0755-985966