DAR ES SALAAM

Na Dk. Boniphace Gaganija

Nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Bernard Membe kwa kuelezea namna alivyofitiniwa na Rais Dk. John Magufuli na kupoteza nafasi ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. 

Pongezi hizi ni za dhati kwa sababu kwa maelezo ya Membe, Watanzania wanapata nafasi kuelewa jinsi mambo yanavyotendeka kwenye ofisi za serikali yetu. 

Lakini pia imetusaidia baadhi yetu kumwelewa Membe na huenda pia imetusaidia kujua moja ya sababu za Membe kuenguliwa mapema kwenye kinyang’anyiro cha urais 2015. 

Kwenye maelezo yake kuna chembechembe za utovu wa nidhamu kwa viongozi wake kama nitakavyoelezea katika ufafanuzi na uchambuzi wa maelezo yake.

Mheshimiwa Membe, umeelezea vizuri sana faida za kifedha ambazo Watanzania wangelizipata kwa kupitia nafasi hiyo kama wewe ungeliupata ukatibu mkuu wa Jumuiya ya Madola. 

Lakini katika mchakato wako wote, sijaona popote wewe binafsi ukienda au ukisema ulionana na viongozi wako wakuu nchini. 

Kwa maana ya marais waheshimiwa Jakaya Kikwete na Dk. Magufuli. 

Lakini pia sijaona kama ulifanya jitihada za kuonana nao wakakataa au ukazuiwa kuwaona. Pia sioni kwenye maelezo yako kama Mheshimiwa Abdulrahman Kinana ulikwenda kumuona wewe binafsi au kumshirikisha kabla ya mchakato wako kuuanzisha. 

Kwenye maelezo yako umesema Mheshimiwa Kikwete alitaarifiwa, akaridhia. Ni nani ulimtuma kumpa taarifa Rais Kikwete? 

Kwa nini mtu huyu hukumtuma kuonana na Rais Magufuli? 

Dk. Magufuli alikuwa ni waziri mwenzako, nini kilikuzuia kwenda kumjulisha harakati zako? Kama ulikuwa unamwogopa, kwa nini hukuwatumia wazee wetu; Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa walikuwapo, ambao wangeliweza kukupatanisha na Rais Magufuli kwa manufaa ya nchi, kwa nini hukwenda kuwaona? 

Mheshimiwa Kinana alizungumza na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, lakini pia Kinana na yeye inaonekana haukuzungumza naye wakati ndiye alikuwa Katibu Mkuu wako wa CCM, chama kilichokuweka madarakani. 

Naona mchakato wako umejaa maswali mengi sana. Yawezekana ulizungumza mengi na vyombo vya habari, na labda mhariri hakuyafafanua na ndiyo maana kumekuwa na giza nene kwenye kinachosemeka au kilichoandikwa.

Jambo jingine la msingi kwenye maelezo yako ni suala la kamati iliyokuwa inaongozwa na Mama Liberata Mulamula. 

Kutokana na maelezo yako kamati hii ilikuwa ya kukupigia kampeni kwa nchi mbalimbali ili upigiwe kura. Kamati hii umeeleza ilisambaratishwa na Magufuli. 

Je, wakati mnaunda kamati hii, mlizingatia misingi ya diplomasia? Kuwa ili kamati iweze kufaya kazi yake, itabidi kupata ridhaa ya viongozi wa nchi na vyombo vya ulinzi na usalama, kwa sababu suala la ukatibu mkuu wa Jumuiya ya Madola ni la kitaifa. 

Kutokana na maelezo yako sijasoma popote ambapo timu yako ilizingatia ushirikishwaji wa viongozi na vyombo husika. 

Kwa mantiki hii, Rais Magufuli ilikuwa ni halali kwake kuchukua uamuzi wa kuifuta kamati hiyo. 

Na kwa mtazamo huu huu, hadhi ya Balozi Mulamula iliingia dosari kwa kujihusisha kimyakimya kutekeleza jambo la kitaifa kinyume au nje ya utaratibu. 

Kwa nia hiyo hiyo njema kwa taifa, Magufuli alitenda vema kumweka kando Balozi Mulamula.

Mheshimiwa Membe, ni dhahiri kabisa kuwa ulikerwa sana na azima ya Serikali ya Awamu ya Tano kujikita kwenye kazi ya kujenga miundombinu ya usafirshaji. 

Kwa maelezo yako unaonyesha dhahiri kuwa ulikuwa na hasira sana juu ya jambo hili kwa kiwango cha kupofuka macho usione au kuangalia maeneo mengine ya msingi yaliyofanywa na serikali hiyo. 

Mfano, hukuona usambazaji wa umeme vijijini, elimu bure, mrejeo wa mikataba ya madini, ukusanyaji wa kodi, kuondoa wafanyakazi hewa, kuongeza udahili wa wanafunzi shule za msingi hadi vyuo vikuu, kusimamia uuzaji wa mazao, elimu bure n.k. 

Lakini nimekushangaa zaidi kwa kukasirishwa na uboreshaji wa miundombinu ya barabara. Kwa sababu moja ya chanzo cha umaskini kwa wananchi wa Jimbo lako la Mtama ni shida ya usafiri na usafirishaji, miundombinu chakavu ya shule, zahanati na huduma mbaya za kijamii ambazo Rais Magufuli alizisimamia kwa dhati na ujenzi wake tumeuona. 

Wananchi wa Kigoma bado wana changamoto kubwa sana ya usafiri na usafirshaji. Tangu Awamu ya Nne juhudi kubwa zimewekwa kwa wanachi wa Kigoma na sasa wameunganishwa kwa barabara za lami na mikoa mingine, umeme bado wanatumia majenereta. 

Lakini dhamira ya Rais Magufuli ilikuwa ni kuwaondolea kabisa shida ya usafiri wana wa Tanzania, ndiyo maana alinunua ndege na kujenga barabara. 

Tumshukuru Mungu haukupata kuwa Rais wetu, kwa maana miundombinu ya usafirishaji isingelikuwa kipaumbele kwako, hivyo wananchi wa Kigoma na Jimbo la Mtama wangeliendelea kutaabika na barabara za vumbi na matope. 

Kwa kuhitimisha, binafsi nakuona kama mtu uliyemchukia Rais Magufuli kwa sababu nyingine na si kwa haya uliyosema, kwa kuwa yanakuegemea mwenyewe.

Mungu ibariki Tanzania.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Boniphace Gaganija, ni daktari wa binadamu, msomi wa ngazi ya uzamivu (PhD) anayepatikana kwa simu namba 0787 766 401