DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Je, unamjua mwanasheria wa kimataifa aliyepiga hatua tangu kuwa hakimu mkazi mwaka 1975 hadi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani nchini Tanzania na Shelisheli, na haikutosha akateuliwa tena na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Cambodia? 

Huyo si mwingine bali ni Jaji Dk. Steven Bwana aliyezaliwa saa mbili na dakika tano usiku wa Jumamosi ya Januari 9, 1949. 

Inadaiwa alipopewa jina hilo akatabiriwa atakuwa mtu mkubwa duniani na atapendwa na watu wote na ilipofika mwaka 1957 akaanza kusoma Shule ya Msingi Busamba iliyopo Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara.

Jaji Bwana amepata elimu yake ya msingi kwa tabu kwa kulazimika kutembea pekupeku kwa umbali wa kilomita tano kila siku.

Kwa mujibu wa mahojiano yaliyorushwa hewani hivi karibuni katika Kipindi cha Nyota wa Wiki cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jaji Bwana ambaye kwa sasa amestaafu, anasema miaka ile hawakuruhusiwa kuvaa viatu kwa kuwa watafanana na walimu wao.

Anasema mwaka 1961 alijiunga na Shule ya Msingi Mwisenge ambayo hata Mwalimu Julius Nyerere amewahi kusoma hapo na elimu yake ya sekondari ameipata katika Shule ya Sekondari Musoma, kisha Shule ya Sekondari Usagara kwa masomo ya kidato cha tano na sita, na mwaka 1971 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Kitivo cha Sheria na akahitimu Shahada yake ya kwanza ya Sheria mwaka 1974.

Hata hivyo, kujiendeleza kitaaluma haikuwa rahisi kwake, lakini akapambana hadi kupata shahada ya uzamili ya sheria katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Roma nchini Italia. 

Aidha, mwaka 1984 alioa mke raia wa Ujerumani, Angelika Hub, na kubarikiwa kupata watoto wanne.

“Mazingira ya kwenda shuleni yalikuwa magumu, nilikuwa ninatembea kila siku kilomita tano, hakuna viatu, hakuna nini, funza miguuni, hakuna kantini shuleni,” anasema na kuongeza:

“Maisha yalikuwa magumu, lakini ndiyo mazingira ya wakati huo. Hatukuwa tunaona ajabu kwa sababu ndiyo hali halisi iliyokuwa wakati huo. 

“Ndoto ya kuwa mwanasheria ilichipuka nilipokuwa kidato cha tano na cha sita, ndipo nilianza kufikiria kusomea sheria, kabla ya hapo nilitaka kuwa padre, kwa hiyo mke wangu nisingempata.”

Anasema baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha sita ndipo akachaguliwa kujiunga na UDSM. “Wakati huo hatukuwa tunachagua, ila serikali ndiyo ilikuwa inakupangia wapi pa kwenda.

“Kwa kweli sikuwa na mtu maalumu, nilitaka tu kwa sababu wakati huo walikuwa wanataka kama unachukua masomo ya sayansi ukishinda kwa kiwango fulani ama unakuwa daktari au mhandisi, na kama unachukua masomo ya sanaa, ukishinda kwa ngazi fulani unakwenda sheria,” anasema na kuongeza:

“Ama fani nyingine yoyote ile, ama uchumi au kitu kingine cha aina hiyo. Zaidi nilitegemea ushindi wa mtihani wangu wa kidato cha sita kuliko mtu fulani. Sikuwa ninamjua jaji yeyote, sikuwa ninamjua hakimu yeyote, nilikuwa nimetoka kijijini huko Musoma, kwa hiyo sikuwa ninamjua mtu.”

Jaji Bwana anasema kipindi hicho wakati anasoma wanasheria walikuwa wanaheshimika, walikuwa wakiogopwa na wakati mwingine wanadharauliwa kwa sababu ya mazingira ya kazi yenyewe wanayofanya.

“Kwa hiyo sikutegemea zaidi ya hapo, lakini mimi sikutegemea kuwa hakimu wala jaji hata siku moja, wala sikuwa na mtu ninayemhusudu kwamba na mimi nikisoma niwe kama mtu Fulani, sikuwa ninawafahamu,” anasema na kuongeza:

“Nilisoma sheria ili niwe nani, ni vigumu. Kwa sababu sikutaka kuwa hakimu, nilitaka nisome sheria labda niwe mkufunzi wa chuo kikuu, lakini malengo yangu yalikuwa nifanye kazi Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje,” anasema na kuongeza:

“Nilikazania eneo la sheria inayoelekea huko, masomo yanayokuwa yanaelekea upande huo na masomo yanayoelekea kwenye ujaji na uhakimu sikuyapenda kabisa wala sikuyatilia mkazo.”

Anasema siku alipoambiwa amepangiwa na serikali kwenda kuwa hakimu alisononeka, kwa sababu hakuipenda kazi hiyo.

“Kwa sababu sikupenda kuhukumu watu, hasa kuhukumu adhabu ya kifo. Nilijua nikiwa hakimu siku moja nitakuwa jaji nitakuwa na mamlaka ya kutoa hukumu ya kunyongwa watu, sikupenda sana hiyo,” anasema na kuongeza:

“Lakini basi ndiyo hivyo siku ya siku ilipofika nilipoambiwa hivyo nikalalamika lakini jibu nililopewa lilinikatisha tamaa kabisa.

“Nakumbuka tulikuwa Kivukoni Chuo cha Wanasheria wote, tulikuwa tunapatiwa mafunzo na kila mmoja alipoambiwa alipopangiwa na mimi niliambiwa ninakwenda kuwa hakimu, nikaenda kumuona mtaaluma chuoni pale kuonyesha kutoridhika kwangu na kupangiwa kazi hiyo.

“Majibu yake yalikuwa yananichanganya baada ya zaidi ya kuniambia wewe Ndugu Bwana umekaa na sisi miezi mitatu tunakufahamu na hakuna kazi inayokufaa kufanya kama uhakimu, nilichanganyikiwa na baadaye maishani nilikuja kuona labda alikuwa anasema ukweli.”

Anasema baada ya hapo akawa hakimu pale Kivukoni, Dar es Salaam na baadaye akahamishiwa Kisutu, lakini ile ndoto yake ya kujiendeleza zaidi alikuwa bado anayo.

Anasema baada ya kupata shahada ya kwanza baba yake alipenda aendelee kusoma zaidi, ndipo akajiandikisha kwa shahada ya pili kwa shida hivyo hivyo lakini akaja kufaulu masomo yake.

Pia anasema akatafuta uwezekano wa kusoma shahada ya uzamivu na baada ya kuhangaika kuitafuata akaipata pamoja na ya nne na aliporudi akawa makao makuu ya mahakama akiwa ni Msaidizi wa Jaji Mkuu wa zamani Francis Nyalali.

Katika hatua nyingine anasema alipopata kazi ya uhakimu haikumshinda wala haikuwa ngumu, kwa sababu yeye ni mpiganaji na si mtu wa kukata tamaa na hakukubali kushindwa. 

“Nilipoteuliwa kuwa hakimu siku ya kwanza mahakamani nilikuwa kichekesho, lakini ndiyo kazi yenyewe hiyo,” anasema na kuongeza:

“Tulipangiwa mahakimu wawili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni wakati huo lakini kwa sasa ni Mahakama ya Biashara, siku ya kwanza hakimu mfawidhi akanipangia mimi na yeye kuingia mahakamani.

“Kwa hiyo nikajua ndiyo nitaanza kujifunza kuona jinsi kazi zinavyofanywa. Tumeingia mahakamani na yeye ameshughulikia kesi ya kwanza, ya pili na ya tatu. Ghafla akaiambia kadamnasi ya watu waliokuwa wamejazana mahakamani kwamba yeye ana dharura, anamwachia Hakimu mpya, Steven Bwana, aendelee na kesi.

“Nilishituka kwa sababu tulikuwa wawili tu tuliokaa pale mbele, sasa sikujua nianzie wapi wala nifanye nini, lakini Waswahili wanasema ‘Mungu hamtupi mja wake’.

“Kwenye benchi la mawakili pale kulikuwa na Wakili mmoja anaitwa Otoni Ochilwa alikuwa mkimbizi kutoka Malawi na ndiye aliyetufundisha chuo kikuu masomo yanayohusiana na kazi za uhakimu, alikuwa amekaa pale mbele na aliniona jinsi nilivyoshituka akacheka.

“Sasa nikachukua faili moja kati ya mafaili aliyoyashughulikia mwenzetu Elias Kazimoto, sasa ni marehemu, alikuwa ameandika nini, amefanya nini? Tulipokuwa tunasikiliza yale mafaili matatu ya kwanza sikuyazingatia kwa sababu nilikuwa ninajua huu ni mfano tu ninaonyeshwa, haikuningia akilini.

“Basi, kwa sababu ambazo sizijui, tukaanza mawasiliano ya macho na yule wakili. Pale tunachukua faili ananielekeza nini cha kufanya kwa alama ya macho tunaelekezana. Alikuwa anatumia macho. Mahali ambapo sipaelewi alikuwa akinielekeza kwa alama ya macho na mimi ninajua, kwa sababu kwa kutumia macho mnaelewana.”

Anasema siku hiyo ilikuwa ngumu maishani mwake, kwa kuwa alishughulikia mafaili zaidi ya 10 na kesi zikatajwa na baada ya kumaliza waliporudi ofisini Hakimu Kazimoto akamcheka, kwa kuwa hakuwa na safari wala dharura. 

“Kwa sababu kumlaumu siwezi, alikuwa mkubwa wangu, nikamjibu nimemudu hivyo hivyo watanisahihisha wenye mamlaka ya kufanya hivyo. Akasema hiyo ndiyo njia ya kujifunza uhakimu,” anasema na kuongeza:

“Na kuanzia hapo kwa kweli nilikuwa nimejifunza. Pia kulikuwa na hakimu mwingine mwandamizi, Mama Stella Longway, bado yungali hai, jaji mstaafu, na yeye alikuwa anatufundisha nini cha kufanya kabla ya kesi au faili ufanye nini, basi ndiyo nikazoea hivyo.

“Mfumo wa kujifunza uhakimu kwa njia ambayo nimefundishwa mimi sikuwahi kuitumia, japokuwa njia ile ingeboreshwa zaidi walau angeniambia kabla ya kuingia mahakamani, walau tungepata mafunzo fulani kabla ya kuingia mahakamani, si kwenda kushitukizwa tu mahakamani. Ninafikiri haikuwa sahihi, hakunitendea haki.

“Njia niliyotumia kuwafundisha mahakimu ni  kuzungumza kwanza kabla ya kwenda mahakamani, ninamwambia aina ya kesi tuliyonayo mbele yetu inategemea nini, sheria husika inafanyaje, ushahidi uliopo mbele yetu utakuwaje, aina gani ya maswali tuyatarajie na tukitoka mahakamani tunarudi tunaizungumzia tena unaonaje, ilikuwaje, umelewa, nini kimekukwaza, kitu cha namna gani? Hiyo ndiyo njia nilikuwa ninaitumia, nadhani imewasaidia wengi.”

Anasema kwa sasa utaratibu umebadilika hadi mtu anateuliwa kuwa jaji, lakini kwa miaka yao kwanza lazima uwe hakimu mwandamizi kwa kiasi fulani. Kisha tabia yako iwe imechunguzwa na umeonekana una tabia nzuri na Jaji Mkuu anashauriana na majaji wafawidhi na Mwanasheria Mku wa Serikali.

Pia mkuu wa Kitivo cha Sheria na vyombo vingine vya kisheria, ikiwamo Polisi, waone kweli huyu hakimu anafaa kuwa jaji.

Anasema huo ndio ulikuwa utaratibu wa wakati huo, ila kwa miaka hii kuna Tume ya Utumishi wa Mahakama inapokea mapendeezo hayo kisha yanatolewa uamuzi, yanafikishwa kwa Jaji Mkuu. Kwa nafasi moja iliyopo anapendekeza majina matatu kwa Rais ambaye anateua.

Anasema ujaji wake umeanzia Shelisheli mwaka 1994 baada ya mwaka 1991 kutokea nafasi aliyopendekezwa na anafahamu Jaji Mkuu wakati huo alifikiri anamhitaji kwa kazi fulani, kwa hiyo akamwomba Rais Ali Hassan Mwinyi asimteue.

“Rais Mwinyi hakukubaliana naye, ikabidi niulizwe, ndipo nikafahamu hayo, kwa hiyo akauliza kama nikakubaliana na mapendekezo ya Jaji Mkuu,” anasema na kuongeza:

“Nilikubali kiroho safi, kwa sababu yule alikuwa mkubwa wangu wa kazi, tulifanya naye kazi muda mwingi – miaka 15, miezi tisa, wiki mbili, siku tano na saa saba. Halafu pia mwaka 1993 nilipendekezwa kuwa Jaji Mahakama Kuu, ikatokea kuna kazi fulani, nilikuwa nimeanza kuisomea wakati huo nilikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani ambayo ni kama katibu mkuu katika wizara. 

“Kwa hiyo Jaji Mkuu alifikiria niendelee na kazi hiyo, ilipotokea nafasi ya Shelisheli kuna rafiki yangu hakimu alikuwa anafanya kazi huko, simtaji jina, bado yuko kazini, alipendekeza kwa mamlaka ya Shelisheli kwamba huyo mtu anafaa, baadhi yao walikuwa wananifahamu tulikuwa tunafahamiana.

“Kwa hiyo ikafanyika juhudi hadi hatimaye Serikali ya Tanzania ikakubali kuniachia kwa hiyo nikaenda kuwa Jaji kule mwaka 1994 hadi mwaka 1999. Baada ya hapo ndipo nikarudi na Rais mstaafu Benjamin Mkapa akaniapisha kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na nikahamishiwa Mahakama ya Biashara nikawa Jaji Mfawidhi mwanzilishi.”

Kuhusu kuulizwa kabla ya nafasi ya uteuzi wa ujaji ni utaratibu au si utaratibu, anasema kwa kipindi kile haukuwa utaratibu, kwamba vyombo vya dola vimependekeza baada ya kufanya uchunguzi wake na kuona kuna mtu anafaa lakini Jaji Mkuu anasita kumwachia kwa wakati huo hadi muda fulani.

“Unajua kipindi kile Rais Mwinyi alikuwa mtu wa haki, kwa hiyo alipenda kujiridhisha kama kweli na mimi mwenyewe nimeafiki, kwa sababu Jaji Mkuu alimwambia kwamba nimeafiki,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo alitaka kujiliridhisha kama ni kweli nimeafiki, ndiyo maana alitumia vyombo vyake kuniuliza nikakubali kiroho safi kabisa. 

“Nilipokuwa Jaji wa Mahakama Kuu wakati wa Mkapa mwaka 2004 Shelisheli ikaniomba tena niwe Jaji Mkuu katika Mahakama ya Rufani ya huko, lakini ile ya kwenda wiki mbili kila baada ya miezi mitatu kwa hiyo haikuwa na shida na niliruhusiwa na Rais kuendelea hadi mwaka 2009.

“Mwaka 2008 Rais Kikwete aliniteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na hiyo ndiyo nilikuwa nayo hadi nilipostaafu.”

Kuhusu swali la shauri lenye ugumu katika maisha yake alilokuwa anaulizwa, anasema inategemea aina ya kesi na mazingira yake na anatoa mfano mtu anaweza kusema kesi fulani ni ngumu lakini kwa misingi ya kisheria si ngumu.

Hata hivyo, anasema hakupata matatizo makubwa japo madogo yalikuwapo na hayakumtikisa. Pia kuna kesi moja ya kubaka walishinda na wameitolea mfano katika kitabu.

Anasema ni nini na jinsi gani ilivyokuwa inapindwa na walivyoirekebisha na kutoa msimamo halisi wa sheria inapaswa iwe.

Anasema kuamua shauri ukipangiwa ni lazima ufanye kazi hiyo ila ikitokea kama kuna shauri la ndugu yako hauruhusiwi kulisikiliza na katika maisha yake mashauri ya ndugu zake yamekwenda mengi na ameyakataa.

“Nilipokuwa Shelisheli nilikataa mengi na hapa pia nilipokuwa Mahakama Kuu nilikataa mengi, hapa nyumbani kwangu kuna sehemu ninahifadhi vitabu vyangu, mavazi na kuna sehemu nimehifadhi hukumu zangu,” anasema.