Michael Mwanda

 

Kutokujiamini na kushindwa kuziendesha taasisi za umma nchini kwenda sawa na wakati, kumechangia kwa kiasi kikubwa mashirika mengi kufa na kuporomoka kiuchumi.
Watafiti  wa masuala ya kiuchumi wanasema kujiamini na ubunifu ni nyenzo muhimu kwa pande mbili kati ya viongozi wenye nia thabiti na uzalendo unaolenga maslahi ya nchi na wananchi wote, bila kuwabagua katika makundi kati ya wachache wenye kujilimbikizia mali na mafukara walio wengi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Michael Mwanda, anasema madhumuni ya kuanzishwa kwa bodi hiyo ni kuboresha kazi za taasisi hiyo.
Anasema bodi hiyo ilianzishwa mwaka 2012 na jukumu walilopewa na Serikali ni kuboresha taratibu za kazi za TPDC ili iende kulingana na wakati uliopo tofauti na ilivyokuwa awali.
“Unapofanya mageuzi mahali popote na kama baadhi ya watu wakiguswa kwa namna yoyote ile, lazima malalamiko yajitokeze tu,” anasema Mwanda.


Pamoja na hayo, anasema lengo la kuboresha Shirika hilo la umma lijiendeshe kwa faida, lilikuwa ni pamoja na kuwaajiri wataalamu wapya wenye sifa zinazohitajika kulingana wakati huu.
Mwenyekiti huyo anasema kwamba walitangaza nafasi za kazi za watendaji wa shirika ikiwamo nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji ambayo iliombwa na watu 40, hata hivyo aliyekuwa na sifa zaidi yao ni James Mataragio ambaye ndiye Mkurugenzi mpya wa TPDC.  
Ni miaka 20 sasa tangu kugunduliwa kwa gesi asilia nchini kwa kuishirikisha Serikali kwa upande mmoja na wadau mbalimbali, baada ya kuendesha tafiti za namna ya kutumia rasilimali hiyo.
Utafiti wa mwisho wa rasilimali hiyo ulikamilika mwaka 1991 ambapo mradi wa kusafisha gesi asilia kisiwani Songo Songo pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi hiyo hadi jijini Dar es Salaam ulibuniwa.
Hata hivyo, anaongeza kwamba pamoja na ubunifu wa mradi huo, Serikali ilikopa fedha kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Rasilimali ya Ulaya (EIB) dola za Marekani 225,347,062 ili kukamilisha utekelezaji wa mradi na kukabidhi visima namba 3,4,5,7 na 9 kwa kampuni ya Songas kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania  (TPDC).


Anasema lengo ni kupunguza utegemezi wa umeme unaozalishwa kwa kutumia maji, ambao mara kwa mara unaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwamo ukame.


“Matumizi ya gesi asilia yatapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuzalisha umeme na kupunguza gharama za uzalishaji viwandani na matumizi ya majumbani,” anasema.
Anasema kuwa mradi wa bomba la kusafirisha gesi asilia ni mali ya Watanzania wote na hivyo kila mmoja anapaswa kuhakikisha uharibifu wowote haujitokezi katika miundombinu hiyo.


Kazi za utafutaji wa gesi asilia na mafuta nchini zilianza miaka ya 1950 ambapo kampuni ya Agip ilifanya ugunduzi wake wa kwanza katika kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi mwaka 1974, na kufuatiwa na ugunduzi mwingine katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara mwaka 1982.
 Pamoja na utafiti huo gesi asilia iliyopatikana haikuendelezwa kwa kuwa ilionekana haina manufaa yoyote kiuchumi kwa kipindi hicho.


Mwaka 2006, Kampuni ya Artumas ilifanikiwa kuendeleza kitalu cha Mnazi Bay kwa kufufua kisima namba 1 kilichokuwa kimegunduliwa na kampuni ya Agip na kujenga mtambo mdogo wa kusafisha gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 2.1 kinachotumika kuzalisha umeme kwenye mitambo ya TANESCO mkoani Mtwara. Umeme unaozalishwa katika mtambo huo unahudumia mikoa ya Mtwara na Lindi.


 Baada ya ugunduzi huo, TPDC iliendelea kufanya utafiti na kuchimba visima mbalimbali kwa ajili ya kuthibitisha kiasi kilichopo katika maeneo ambayo gesi asilia iligundulika. Hadi kufikia Novemba 2014 kiasi cha gesi asilia kilichopatikana ni futi za ujazo trilioni 53.28 (53.28TCF).
 Meneja wa mradi wa bomba la kusafirishia gesi asilia, Mhandisi Kapuulya Musomba, anasema kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa mwaka 2007 Mkuranga ni futi za ujazo (0.2 TCF), mwaka 2008 Kiliwani kufikia futi za ujazo (0.07 TCF), mwaka 1974 Songo Songo (2.5TCF), 1982 Mnazi Bay (5TCF), 2012 Ntorya (0.178 TCF) na mwaka 2010-2014 katika kina kirefu cha bahari (45.28TCF).


Anasema ili kuhakikisha kuwa nchi inanufaika na rasilimali ya gesi asilia iliyogunduliwa, Serikali kupitia TPDC inakamilisha mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi katika maeneo ya Madimba mkoani Mtwara na Songo Songo mkoani Lindi pamoja na bomba la kusafirisha gesi hiyo.
Ujenzi wa bomba hilo litakalosafirisha gesi asilia kutoka Mtwara kupitia Somanga Fungu mkoa wa Lindi, Pwani hadi katika kituo kikubwa cha kupokea gesi kilichopo Kinyerezi Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 99.


Katika eneo la Madimba ujenzi wa mitambo mitatu yenye uwezo wa kusafisha futi za ujazo wa gesi milioni 70 kila mmoja kwa siku, na mitambo miwili yenye uwezo wa kusafisha kiasi hicho hicho cha ujazo kila mmoja katika eneo la Songo Songo inaendelea kujengwa.
Mwaka 2011 Serikali ya China kupitia Benki yake ya Exim imechangia kiasi cha dola za Marekani 1,225,327,000 ikiwa ni asilimia 95 huku Serikali ya Tanzania ikichangia asilimia 5 kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo.


Mtambo wa kusafisha gesi asilia wa Songo Songo unagharimu dola 151,735,000; Mnazi Bay dola 197,877,000 na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi hadi Dar es Salaam dola 875,715,000.
Ujenzi wa bomba hilo ni kiwango cha asilimia 14.5 ikiwa chini ya kiwango cha wastani wa gharama za kimataifa ama kile ambacho kingetozwa na kampuni za nchi za Magharibi.
 Kwa mujibu wa taarifa ya Interstate Natural Gas Association of America (INGAA) ya Machi 2014,  wastani wa gharama za ujenzi wa bomba la gesi asilia kwa mwaka 2011 zilikuwa dola za Marekani 94,000 kwa inchi-maili sawa na dola za Marekani 54,421.4.