Neno CHOMBO katika lugha yetu ya Kiswahili lina maana au tafsiri nyingi katika matumizi. Katika tafsiri sahihi na sanifu CHOMBO lina maana sita kwa maelezo yaliyomo kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la pili la 2004.
Kamusi hiyo kwa ufupi inatoa maana zifuatazo: kitu chochote cha kufanyia kazi, samani, pambo la dhahabu la mwanamke, kifaa cha jikoni cha kupikia au kutilia chakula, kitu kinachotumiwa kusafiria baharini na mwisho ni muundo unaotekeleza kazi fulani na wenye madaraka fulani.
Maana hiyo ya sita isemayo ni muundo unaotekeleza kazi fulani na wenye madaraka fulani ndiyo ninaokusudia kuzungumzia. Ni jambo la kawaida kusikia watu katika mazungumzo yao kutaja mamlaka fulani ni chombo.
Mathalani Serikali, Kampuni, Polisi, Mahakama na kadharika huitwa chombo. Hata chama cha ngoma, michezo na cha siasa huitwa chombo. Kwa maelezo hayo, makala yangu inalenga kuzungumzia chama cha siasa, nacho ni Chama Cha Mapinduzi.
Chama Cha Mapinduzi ni chombo kilichoundwa kwa ridhaa ya wanachama wa Afro Shiraz Party na Tanganyika African National Union. Chombo hiki kina Baraka zote za kijamii na kisheria kama vile CHADEMA, CUF na NCCR- Mageuzi.
Chombo hicho Chama Cha Mapinduzi – CCM tangu kuasisiwa Februari 5, 1977 hadi sasa kutimiza miaka 38, kimekumbana na kupambana na mikasa kadha wa kadha katika makuzi na utendaji wa kazi zake za kisiasa.
Ni ukweli pia kimefurahia makuzi na utendaji kazi zake katika kuongoza na kushika madaraka ya kisiasa na kiserikali kupitia serikali zake. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ukweli ndani ya miaka 38 chombo hiki kimeendesha uongozi na utawala wake kwa kufurahisha wananchi kutokana na watendaji waadilifu na kuchukiza wananchi kutokana na watendaji wasio waaminifu.
Chombo hiki kimekumbwa na lawama kedekede za utendaji mbovu kwenye baadhi ya matawi, kata, wilaya, hadi mkoa. Achilia mbali utendaji wa kitaifa ambao ndiyo unaobeba lawama zote.
Uzembe, ufisadi, rushwa kutamalaki nchini ni baadhi ya lawama zilizomo ndani ya chombo hiki. Miaka 20 iliyopita, Horace Kolimba (marehemu) aliyekuwa Katibu Mkuu wa chombo hicho aliwahi kusema kuwa chombo kimepoteza dira.
Hata kama wanachama na wapenzi wa chombo hicho walikataa kauli ya Kolimba si kweli, hali halisi iliyochomoza baadaye ni nchi kutumbukia kwenye rushwa na ufisadi. Na mambo kuwa magumu ndani ya chombo chenyewe.
Muasisi mmoja wapo wa chombo hicho, Mwalimu Julius K. Nyerere katika hotuba zake na vitabu vyake ameeleza na kukemea chombo kwenda mrama. Hadi sasa chombo hicho hakijafaulu kurekebisha na kuondoa kasoro zilizopo.
Kasoro zinapatikana katika maeneo tofauti. Kwa mfano katika michakato ya chaguzi za viongozi ndani ya chombo chenyewe, hongo na rushwa zinatamba kama pia mchezoni, baadhi wanafurahia na baadhi wanachukia.
Katika uchaguzi wa viongozi wa chombo hicho uliopita, Makamu Mwenyekiti wake kwa upande wa Bara, Philiph Mangula alitangaza vita ya kukomesha rushwa ndani ya miezi sita chomboni.
Leo Katibu Mkuu wa chombo hicho, Abdulrahman Kinana anapita kila mkondo na kichochoro kuweka mambo sawa, chombo kisiende mrama, lakini baadhi ya wanachombo hawapendi na wanazidi kuweka vikwazo.
Cha ajabu hata msemaji wa chombo, Nape Nnauye anapotetea na kurekebisha matendo ya baadhi ya wanachombo ambayo hayamo katika maadili ya chombo, anaambiwa hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono.
Jamani uongozi ni hadhi. Unastahili kupewa heshima kwa daraja lake, Urais, Ubunge na Udiwani ni viti vyenye mamlaka na madaraka yake havithaminiwi na kuenziwa.
Si kila Mzaramo, Mmakonde na Msukuma anaweza kuwa diwani, mbunge au Rais. Tafakari.