DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Watendaji wa serikali na halmashauri za wilaya, nyingi zikiwa ni za pembezoni mwa nchi, wamo kwenye wakati mgumu wakiwaza namna watakavyotekeleza kwa ufanisi maelekezo yaliyotolewa na Serikali Kuu, hasa kwa upande wa ujenzi wa madarasa.

JAMHURI limeelezwa kuwa tayari Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imetoa mwongozo unaoelekeza kuwa imetenga Sh milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa darasa moja nchi nzima.

Jumla ya madarasa 15,000 yanatarajiwa kujengwa nchini, ikiwa ni zaidi ya upungufu uliokuwapo wa madarasa 11,000.

Fedha zilizotengwa kwa kazi hiyo ni sehemu ya mkopo nafuu wa Sh trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Akizungumza na JAMHURI kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Hamad Mapengo, anasema mgawanyo wa fedha hizo haukuzingatia hali halisi ya jiografia ya Tanzania.

“Hofu yangu ni kwamba watekelezaji wa agizo hili wanaweza kujibana na kujenga madarasa kutokana na mgawo walioelekezwa wakati kwa hali halisi hilo haliwezekani.

“Ninasema hivi kwa sababu sisi tunaoishi maeneo ya pembezoni vifaa vya ujenzi hupatikana kwa bei kubwa sana. Sasa hii Sh milioni 20 inatakiwa itumike kujenga boma la darasa kuanzia msingi hadi ‘finishing’ na kuweka samani kama madawati na meza ya mwalimu, haiwezi kutosha kabisa,” anasema Mapengo.

Ofisa mmoja wa halmashauri hiyo anasema mwongozo waliopewa ni kujenga madarasa yote kwa matofali ya saruji (block). 

Mwongozo huo unamnyima raha Mwenyekiti Mapengo akisema: “Huku kwetu tunajenga nyumba kwa matofali ya kuchoma kwa sababu bei ya mfuko mmoja wa saruji ni kubwa sana. Ni zaidi ya Sh 22,000.

“Tungeruhusiwa kujenga kwa kuzingatia hali halisi ya maeneo yetu, wala kusingekuwa na hofu. Lakini matofali ya ‘block’, nondo na mabati hugharimu fedha nyingi sana. Sijui aina ya madirisha yanayotakiwa, kama ni ya vioo, ni hatari.”

Anatoa mfano wa eneo la Mwese lililopo zaidi ya kilomita 130 kutoka mjini, akisema kusafirisha nondo, saruji na mabati hadi huko ni gharama kubwa.

“Mwese hauwezi kupata mchanga wa kujengea, kwa hiyo unapaswa kwenda kilomita 50 hadi Kapanga kufuata mchanga. Ukifikiria hali hiyo, unajikuta ukipata hofu utakapopewa jukumu la kusimamia ujenzi,” anasema.

Mapengo anasema ipo tofauti kubwa kati ya gharama za ujenzi wa darasa la Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Kauli ya Mapengo inaungwa mkono na mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Igalukilo iliyopo Mnyamasi, Halmashuri ya Nsimbo mkoani humo, akisema wao watalazimika kusafirisha vifaa vya ujenzi kwa kilomita 94 kutoka mjini Mpanda.

“Unafuu pekee tutakaopata ni kwa madawati, kwa kuwa huku kwetu mbao zinapatikana kwa urahisi tofauti na Dar es Salaam. Lakini vifaa vingine vitatugharimu sana, ndiyo maana nina hofu huenda haya madarasa yakajengwa chini ya kiwango,” anasema mwalimu huyo akiomba hifadhi ya jina lake.

Utafiti wa JAMHURI umegundua kuwapo kwa hofu kama hiyo katika mikoa ya Kagera, Mara na Kigoma.

Hata hivyo, mkazi mmoja wa Dar es Salaam ambaye ni fundi ujenzi, Abraham Ngowi, anaamini kuwa Sh milioni 20 zinatosha kujengea darasa moja na hata kuliwekea samani.

“Watu waache mazoea. Fedha hizo ukipewa mtu binafsi ujenge nyumba yako zitatosha kabisa. Na nyumba ni tofauti na darasa, kwa kuwa darasa ni boma tu.

“Matofali 3,000 hadi 3,500 yanatosha kumaliza boma la darasa. Sidhani kama utahitaji mabati 100, lakini hata kama ni mabati 100, fedha zinatosha na utanunua madawati hata 40 kwa bei ya Sh 80,000 kwa dawati moja ukiwa Kigoma au Dar es Salaam,” anasema.

Kauli ya Ngowi inapingwa na Ofisa Ukadiriaji Majenzi (QS), akisema ni lazima kuwepo tofauti ya gharama na kwamba kuna maeneo watagharamika zaidi.

“Kuweka ‘flat rate’ ya Sh milioni 20,000 kwa nchi nzima si sahihi. Nadhani wangefanya utafiti na kuongeza kiasi fulani kwa maeneo ya pembezoni,” anasema ofisa huyo wa taasisi ya serikali.

JAMHURI limefika Ofisi ya Bodi ya Wabunifu na Wakadiriaji Majenzi zilizopo jengo la George’s maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam kutaka kupata kauli ya kitaalamu kutoka kwao.

Juhudi hizo ziligonga ukuta baada ya ofisa anayekaimu nafasi ya Msajili wa Bodi kukataa kuzungumzia suala hilo akisema si miongoni mwa majukumu aliyokaimishwa.

Kauli ya TAMISEMI

Ofisa Mawasiliano wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Nteghenjwa Mbwambo, amelieleza JAMHURI kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa si mradi wa kwanza kupelekwa kwenye mikoa na wilaya za pembezoni.

Anasema kuna miradi imetekelezwa kwa ubora wa hali ya juu huku gharama za utekelezaji wake zikiwa kwenye kiwango sawa katika maeneo yote.

“Bei iliyowekwa ni kutokana na tafiti iliyofanywa kwenye maeneo yote mijini na vijijini na ikajaribiwa na kuonekana kutosha,” anasema Nteghenjwa.

Ofisa huyo wa TAMISEMI anazitaja wilaya ambazo miradi kama hiyo imewahi kutekelezwa na kuonyesha mafanikio kuwa ni Uvinza mkoani Kigoma ambako kumejengwa kituo cha afya cha Kata ya Kalya (mwambao wa Ziwa Tanganyika).

“Kituo hiki kipo mbali sana, lakini serikali imefanikiwa kufikisha vifaa vya ujenzi na kujenga kituo cha afya,” anasema.

Pia anakitaja kituo kingine kilichopo Mpimbwe mkoani Katavi ambacho kimejengwa kwa gharama inayolingana na ile iliyotumiwa Kalya.

Nteghenjwa anapingana na watu wanaodai kuwa viwango vya fedha vilivyotengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi huo huenda vikashindwa kuendana na uhalisia unaotarajiwa.