Na Christopher Lilai, Lindi

Uwazi, uwajibikaji na usimamizi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya madini nchini. Kwa kawaida, katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ushirikishwaji wa wananchi ni mdogo sana. Katika maeneo mengi, wananchi wanaona shughuli za madini zinaendelea bila ya wao kuwa na taarifa za kina kuhusiana na miradi hiyo.

Hali hiyo haijitokezi miongoni mwa wananchi wa kawaida tu. Katika baadhi ya maeneo, hata viongozi katika ngazi za mitaa, vitongoji, vijiji na kata wanakuwa hawana taarifa kuhusiana na miradi ya madini inayoendeshwa katika maeneo yao. 

Mara nyingi wafanyabiashara wanaojihusisha na miradi hiyo huwasiliana na uongozi wa wilaya, mkoa na wizara ili kupata mahitaji yao katika uendeshaji wa miradi hiyo.

Wananchi na viongozi wa ngazi za chini wanashindwa kuchukua hatua kwa sababu hawana uelewa wa ushiriki wao katika shughuli hizo.

Kwa maana hiyo, elimu zaidi inahitajika kwa wananchi na  viongozi hao wa ngazi za chini juu ya sheria ya madini na kanuni zake ili waweze kujua nafasi zao na haki zao.

Elimu hiyo ni muhimu pia ili kuwawezesha viongozi hao wa ngazi za chini kufanya uamuzi sahihi kuhusiana na miradi ya utafutaji na uchimbaji wa madini inayoendeshwa katika maeneo yao.

Elimu hiyo pia itapunguza au kuondoa kabisa mwingiliano wa majukumu kati ya wachimbaji vibarua na wachimbaji wadogo.

Kukosekana kwa elimu ya aina hiyo kwa watu wengi katika maeneo ya uchimbaji madini kuna dhihirisha kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa wahusika katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Meneja wa mgodi wa Mpiruka wilayani Nachingwea, Selemani Ngoso, anasema elimu ya kutosha inahitajika kwa wananchi, wachimbaji na viongozi ili kuondoa migogoro na utoroshaji wa madini. Anabainisha kuwa wachimbaji wengi wanaamini kuwa wanadhulumiwa mapato yao wanapouza madini kwenye masoko yaliyoanzishwa na serikali, kwani hawajui maana ya tozo na kodi.

Kwa upande mwingine migogoro inaendelea kwa sababu wachimbaji wengi, hasa wachimbaji wadogo hawajui maana ya umiliki wa eneo, hivyo kuwafanya wavamie maeneo yanayomilikiwa na watu wengine na wanapofukuzwa wanaona kama wanaonewa.

Matokeo yake, badala ya kuuza madini kwenye masoko maalumu, wachimbaji wengi wadogo wanatorosha madini yao na kuyauza katika masoko ya vichochoroni.

“Sijawahi kuona wataalamu wa madini wakija kutoa elimu hapa kwetu. Elimu ni muhimu sana huku migodini kwani baadhi ya migodi kwenye mikoa mingine imeanza kutoa kozi kabla ya  kuanza uchimbaji,” anasema Ngoso.

Ngoso anasema kukosa elimu na uwazi juu ya masuala ya madini kumesababisha hata waliolipwa fidia ya  maeneo yao kupisha uchimbaji wanarudi kwenye maeneo yao na kusababisha migogoro baina ya wachimbaji na wakulima.

Mmiliki wa machimbo ya Mibure wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi, Maiko Malibiche, naye anakiri kuwa licha ya kufanikiwa kupata leseni ya uchimbaji kwenye eneo lake ambalo lina madini ya dhahabu, bado hana elimu wala uelewa wa masuala ya madini, hivyo kuomba mamlaka zinazohusika kuwapatia elimu kuhusu sheria, kanuni na sera ya madini ili imsaidie kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria.

“Kwangu suala la ufahamu juu ya sheria ya madini na kanuni zake ni changamoto. Nimeanza na ninaendelea na shughuli za uchimbaji bila kujua iwapo ninachokifanya kinaendana na matakwa ya sheria na kanuni za madini. Kuna haja ya kutujengea uwezo sisi wachimbaji wadogo ili tufanye shughuli zetu kwa ufanisi,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Malibiche, uelewa wa sheria utasaidia sana hata katika ulipaji wa maduhuli ya serikali.

“Kwa sasa tunalipa lakini hatujui kama kinacholipwa ni sahihi au si sahihi,” anasema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashimu Komba, anasema kuwa kuna changamoto miongoni mwa viongozi na wawekezaji kuingia mikataba bila kujua taarifa muhimu zinazohusu uwekezaji. Kutojua taarifa na sheria zinasemaje kunachangia migogoro baina ya viongozi wa vijiji, wananchi, viongozi na wawekezaji.

Komba anasema kuwa viongozi wa serikali za vijiji wanatakiwa kuwashirikisha wananchi katika hatua zote kabla ya kuingia mikataba, kwani uzoefu unaonyesha ni viongozi peke yao wanaofanya uamuzi unaohusu masilahi ya wananchi bila kuwahusisha wananchi wenyewe.

“Wananchi wasifanywe kama mihuri ya kupitisha uamuzi  uliofanywa  na viongozi. Kutowashirikisha wananchi kunasababisha wawekezaji kwenye sekta ya madini kukiuka makubaliano, kwani huenda walipatikana kwa njia zisizo halali,” anasema mkuu huyo wa wilaya. 

Akizunguzia juu ya changamoto hizo hasa kutokuwapo kwa uwajibikaji, Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Lindi,  Mhandisi Jeremiah Hango, anasema ofisi yake imejitahidi kutembelea maeneo ya machimbo lakini changamoto kubwa ni ubovu wa barabara za maeneo ya uchimbaji. Kwa kuwa barabara nyingi katika maeneo hayo huwa hazipitiki muda wote, inakuwa vigumu kwao kuyafikia baadhi ya maeneo wakati wa masika.

Aidha, Hango anasema hali ya Ofisi ya Madini Mkoa wa Lindi kuwa pembezoni kumesababisha baadhi ya wateja kutofika  ofisini kufanyiwa mahesabu kwa ajili ya malipo hasa kwa wale wanaotoka Wilaya ya Kilwa.

Anasema hata wale wanaofika ofisini hapo wamekuwa wanalalamika kuwa wanatumia muda mwingi kusafiri.

“Hili la mahali ofisi zetu zilipo zinatukwamisha hata sisi kufaya safari za kukagua machimbo mara kwa mara hasa wilayani Kilwa, kwa sababu ofisi haina mafuta ya kutosha kufanya safari hiyo ndefu,” anasema.

Kuhusu soko la madini lililopo wilayani Ruangwa, Mhandisi Hango anasema soko hilo linawahudumia wachimbaji wote ndani ya mkoa bila kubagua. Anasema soko hilo ni fursa kwa wachimbaji kuuza madini bila usumbufu.

Hata hivyo, Mhandisi Hango anakiri kuwapo kwa changamoto chache kwenye soko hilo ambalo linatekeleza majukumu yake kikamilifu.

“Zipo changamoto chache kwenye soko letu la Ruangwa ambalo ndilo linalotegemewa na wachimbaji. Hata hivyo, changamoto hizo hazizuii wachimbaji kuuza madini yao,” anasema Injinia Hango.

Amezitaja changamoto kuwa ni pamoja na uchache wa  vifaa vya kupimia madini (XRF mashine). Ameeleza kuwa taarifa ya uhitaji wa mashine hizo imepelekwa kwa uongozi wa Tume ya Madini  na kuwa fedha zilikwisha kupatikana na taratibu za  manunuzi zinaendelea.

Changamoto nyingine ni uchache wa wanunuzi kwenye soko hilo, jambo ambalo linafanya wakati mwingine wachimbaji kukosa mnunuzi wa madini yao. Hali hii husababisha madini yanayouzwa kwenye soko hilo kukosa bei nzuri.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, kaimu meneja huyo amesema kuna juhudi za kuwashawishi wanunuzi zaidi waweze kuja katika soko hilo.

“Katika hili kunatakiwa jitihada za kuwashawishi wanunuzi kuja Ruangwa kwani kuna madini mengi. Nitoe wito wanunuzi kujitokeza kuja kununua madini. Wasihofu, usalama ni mkubwa,” anasema Injinia Hango.

Mhandisi Hango amebainisha kuwa licha ya changamoto hizo bado mkoa umeweza kuvuka lengo la kukusanya maduhuli ya serikali kupitia sekta hiyo, ambapo hadi mwezi Aprili mwaka huu walikuwa wamekusanya Sh bilioni 2.4, ambazo ni zaidi ya lengo walilojiwekea la kukusanya  Sh bilioni 2 hadi mwisho wa mwaka wa fedha.