Ndugu wananchi, katika waraka wangu uliopita niliomba mnipe nafasi ya kuongoza Taifa hili kubwa Afrika Mashariki na taifa tajiri kwa rasilimali zake, likiwa na kundi kubwa la maskini.
Nazungumzia maskini waliokata tamaa na kukosa muelekekeo wa maisha yao, wamekata tamaa wakiamini lazima wafe maskini.
Nilitoa angalizo la sera zangu, na nilitoa hofu ya kupata nafasi ya kuongoza kutokana na vigezo vya kuwania nafasi hiyo, lakini sina budi kusema kwamba uongozi naamini ni kipaji, uongozi ni kugawa madaraka pasi na shaka ya utendaji, urais naamini ni taasisi ambayo kama mimi zuzu nilivyo napaswa kushauriwa na wataalamu wa kweli katika kufikia malengo ninayoyapanga.
Mtanzania ninayemjua mimi, ukimwacha huyu wa dotcom, ni Mtanzania mzalendo, mpenda haki, mchapa kazi, mwenye upendo na mvumilivu sana. Ni Mtanzania mwenye kiu ya maendeleo ya jamii na siyo yake peke yake, ni Mtanzania mjamaa anayejua kujitegemea.
Mtanzania ninayethubutu kumsemea ni yule ambaye siyo mnafiki, Mtanzania msikivu, Mtanzania mwenye kiu ya maendeleo, ni Mtanzania ambaye kwake uvivu ni aibu, ni Mtanzania ambaye kwake rushwa ni adui wa haki, ni Mtanzania anayejua kuwa cheo ni dhamana na kwamba ofisi ya umma na waajiriwa wa umma wa Watanzania ni ofisi na wafanyakazi wake.
Mimi bado nimepitwa na wakati, siamini katika kuabudu watu wanaoitwa viongozi wa umma, siamini katika kujinafikisha na kupeana nafasi nyeti na ngumu kama ya kiti hicho cha juu kabisa nchini, siamini katika kutumia nguvu ya kupata nafasi hiyo, naamini katika kuombwa na kushauriwa kushika nafasi hiyo, na ndiyo maana nawaomba Watanzania mnipe nafasi japo kwa kuomba kwamba naweza kujitolea.
Tanzania ina miongo mingi kiasi tangu tupate uhuru, suala la elimu bado ni la kubahatisha, wapo wanaopata nafasi ya kuchaguliwa lakini hakuna madarasa wala madaftari, hakuna walimu wala mitaala ya kwetu, hakuna vitendea kazi wala miundombinu ya kuhakikisha huyu mtoto Mtanzania anajivunia Taifa lake kumpa elimu, naitaka Tanzania ile yetu ya vitabu, madawati, kalamu, daftari bure.
Naitaka ile Tanzania yenye walimu wazuri wenye moyo wa kufundisha, naitaka Tanzania ambayo elimu na fedha vilikuwa vitu viwili tofauti kabisa, naitaka Tanzania yangu ya usafiri wa wanafunzi kwa waranti, wanafunzi kupata elimu sawa na elimu ya kujitegemea.
Naitaka Tanzania ya vijiji kupata huduma za jamii kama zahanati na madaktari katika ngazi ya kijiji, wakunga katika ngazi hiyo ya vijiji, wataalamu wa kilimo na wengineo katika ngazi hiyo, tukiweza hiyo Watanzania hatutakuwa tunazungumzia huduma ya hospitali za taifa kuwa mbaya, hatukuwa tunazungumzia wachache wenye uwezo kupata matibabu nje ya nchi na wala elimu nje ya nchi au nje ya mtaala wetu wa elimu.
Hii ndiyo Tanzania ninayotaka kuwapeleka wapiga kura watakaokuja kunishawishi nikae katika kiti hicho, naitaka Tanzania ya huduma za maji na umeme kuwa za wote wenye nchi, lisiwe suala la wachache tena kwa tabaka la wenye nacho, haki ya maji safi na salama ni la wananchi wote watakaokuwa wametuajiri sisi wachache, haki ya nishati hali kadhalika kwa kuwa watunzaji wa mazingira ni Watanzania wote.
Naitaka Tanzania ya maendeleo kwa kulipa kodi, kodi isiwe kwa watu wachache imbane kila anayehusika na mapato, naitaka Tanzania ya mgawanyo wa utumishi, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara, Tanzania ya wanasiasa na wasio wanasiasa, Tanzania ya viongozi na watawaliwa, kiufupi Azimio la Arusha litakuwa na nafasi yake katika uongozi wangu, haiwezekani wafanyabiashara wakawa viongozi, watendaji wa Serikali na watawala.
Naitaka Tanzania yenye viongozi wenye maadili, wanaoogopa waajiri wao, naitaka Tanzania yenye Serikali kali ambayo wanaocheza na mali za umma wawajibike kisheria, naitaka Tanzania ambayo sheria itakuwa msumeno unaokata wote na siyo wachache wasio na uwezo ndiyo iwe hukumu yao ya pili, naitaka Tanzania itakayokuwa na heshima duniani kwa misingi mizuri iliyojiwekea.
Naitaka Tanzania yenye sifa ya kisiwa cha amani, Tanzania isiyokuwa dampo la kila kitu duniani, Tanzania isiyokopa bali inayokopesha, Tanzania inayolinda maslahi ya rasilimali zake, Tanzania ya viongozi mashujaa, Tanzania ya ubunifu kama zama zile za ujana wetu.
Iwapo mtaona nafaa naomba mnishawishi nichukue fomu, kisha mnichague, msione huruma kwa hatua nitakazochukua, tukubali machungu ya kuvuka daraja la moto kuelekea katika nchi ya ahadi, nchi iliyokuwa na sifa zote miaka ya 1960 kimaendeleo. Tukubali kunyooka hata kama tumekomaa, tukubali kurudi katika maagano yetu, kwamba hii ni nchi yetu na maendeleo yatatuhusu sisi na siyo wawekezaji.
Mkiona sifa hazitoshi lakini yupo mwenye sifa zaidi yangu msinionee haya kuniacha na kumpa fomu huyo anayefaa zaidi, hii ni nchi yetu siyo ya wachache, tujikomboe sasa yatosha.
Wasalamu,
Mzee Zuzu
Kipatimo.