BRUSSELS, UBELGIJI

Wanachama wa Jumuiya ya Ulaya wameanza kuvurugana baada ya baadhi yao kukataa kuutambua mkataba unaounda umoja huo kuwa una nguvu kuliko sheria zao za ndani.

Poland ndiyo inayoongoza kupinga ukuu wa mkataba wa Jumuiya ya Ulaya dhidi ya sheria zake na wanachama wengine wanaiona hatua hiyo kama usaliti, hasa katika kipindi hiki ambacho umoja huo unakabiliwa na changamoto baada ya Uingereza kujitoa.

Wiki iliyopita katika kikao kilichofanyika jijini Brussels, wanachama wa jumuiya hiyo walipiga kura kulaani kitendo cha Mahakama ya Kikatiba ya Poland kutoa uamuzi uliosisitiza kuwa mkataba wa EU hauna nguvu kisheria juu ya sheria za nchi hiyo.

Hukumu hiyo ya mahakama ya Poland imezishitua nchi nyingine wanachama wa EU ambao wanasema inadharau misingi ya kisheria ya kuundwa kwa jumuiya hiyo.

Wanachama wengi wanaamini kuwa hukumu hiyo ni mwanzo wa safari ya Poland nayo kujitoa EU.

Wiki iliyopita wabunge wa Bunge la Ulaya waliagizwa kuandaa mashitaka dhidi ya Kamisheni ya Ulaya inayotuhumiwa kushindwa kuwaadhibu wanachama wanaokiuka sheria za jumuiya.

Rais wa Bunge hilo, David Sassoli, alisema kuwa kamisheni imekuwa ikikataa kuweka mfumo uliokubaliwa mwaka jana ambao utaiwezesha EU kuzuia fedha zake za bajeti kwenda kwenye nchi ambazo zinakiuka sheria.

“Wakati umefika sasa wa kuchukua hatua,” alisema na kuongeza: “Jumuiya ya Ulaya ni jumuiya iliyojengwa juu ya misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria. Iwapo mambo haya hayaheshimiwi na mmoja wa wanachama, EU inalazimika kuyalinda.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki, alinukuliwa akisema kuwa kamwe nchi yake haitakubali kuwekwa mateka hata kama nchi zote zitakuwa dhidi ya hatua yake.

Alisema yupo tayari kutafuta ufumbuzi wa suala hilo ingawa watu wengi wana wasiwasi kuwa nchi hiyo yenye msimamo mkali inaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa katika jumuiya hiyo.

‘Siku chache zilizopita msingi wetu wa sheria wa jumuiya ulitikiswa. Hii haikuwa mara ya kwanza, na haitakuwa mara ya mwisho. Lakini haijawahi kutokea kwa jumuiya kutikiswa kiasi hiki,” alisema katika barua aliyowaandikia viongozi wenzake waliokuwa wanakutana Brussels.