*Kambi ya Upinzani yaanika bungeni uozo wa kutisha
*Familia ya Chavda yavuna mabilioni na kutokomea
Hii ni sehemu ya hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, aliyoitoa bungeni wiki iliyopita, akieleza namna ardhi ya Tanzania inavyohodhiwa na wafanyabiashara na matajiri matapeli…
MASHAMBA YALIYOBINAFSISHWA AMBAYO HAYAJAENDELEZWA
Mheshimiwa Spika, wakati akihitimisha bajeti ya ardhi mwaka jana, Waziri wa Ardhi aliliahidi Bunge lako Tukufu kwamba baada ya Bunge la bajeti wizara ingekwenda kufanya ukaguzi huru wa nani ametelekeza mashamba. Alisisitiza kwamba wawekezaji wote waliotelekeza mashamba “the honeymoon is over.”
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka kupata idadi ya mashamba yaliyokaguliwa na wizara na mahali yalipotoka hadi husika ilipotolewa na ni hatua gani ambazo zimeshachukuliwa na serikali dhidi ya wawekezaji husika.
Mheshimiwa Spika, wakati Kambi ya Upinzani ikisubiri taarifa kutoka kwa Waziri wa Ardhi juu ya ukaguzi huru iliyofanywa na wizara kuweza kuwabaini waliotelekeza mashamba, Kambi ya Upinzani inataka Serikali itoe msimamo juu ya taarifa ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda vya bidhaa na kilimo iliyofanyiwa kazi na CHC (Shirika Hodhi), kutokana na maelekezo waliyopewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
Taarifa husika imebainisha kwamba mashamba 13 yenye ukubwa wa hekta 71,184 yalikuwa yameendelezwa kwa kiasi, wakati mashamba 14 yenye ukubwa wa hekta 44,764 yalikuwa hayajaendeleza kabisa/yametelekezwa! Mengi ya mashamba yakiwa ni mashamba ya mkonge. Mashamba hayo ni:-
1) Ndungu Sisal Estate, shamba hili lenye ukubwa wa hekta 1,230. 9 liliuzwa kwa L.M Investiment ya Tanga mwaka 1997 kwa bei ya shilingi milioni 278 . Mpaka sasa 2012, miaka 15 baada ya kukabidhiwa shamba, mwekezaji ameendeleza 52% tu ya shamba lote!
2) Mkumbara Sisal Estate, shamba hili lenye ukubwa wa hekta 1,734 liliuzwa mwaka 1997 kwa M/S D.D Ruhinda & Company LTD kwa bei ya shilingi 100 milioni. Mpaka sasa (miaka 15 baada ya kukabidhiwa shamba) mwekezaji ameendeleza 52% tu ya shamba lote.
3) Toronto Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 6,023 lililobinafsishwa kwa Highland Estate Limited kwa bei ya shilingi milioni 265.4 mwaka 1998, mpaka Septemba 2011, ni 50% tu ya shamba ilikuwa limeendelezwa! Taarifa zilizopo ni kwamba mwekezaji husika hana hatimiliki ya shamba kutokana na kudaiwa riba, hivyo kushindwa kupata mkopo wa kuliendeleza shamba.
4) Magunga Sisal Estate, shamba lipo Wilaya ya Korogwe, lina ukubwa wa hekta 6,520. Katika shamba hili ambalo linamilikiwa kwa ubia na kuendeshwa kwa kilimo cha mkataba kati ya wakulima wadogo wa mkonge na Katani Limited limeendelezwa kwa 19% tu.
5) Ngombezi Sisal Estate, shamba liko Wilaya ya Korogwe na lina ukubwa wa hekta 6,480 ambapo hekta 3881 zimegawiwa kwa wakulima. Shamba linaendeshwa kwa kilimo cha mkataba kati ya wakulima wakubwa na wa kati. Eneo lililopandwa mkonge ni hekta 1301.6 tu!
6) Hale Mruazi Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hekta 4,180, ambapo hekta 1,136 tu ndizo zilizopandwa Mkonge.
7) Manza Bay Sisal Estate, shamba liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998. Mwekezaji alitumia hatimiliki kupata mkopo ambapo hakutumia mkopo husika kuendeleza shamba, shamba husika lilishikiliwa na CRDB mpaka mwaka 2001 alipoiuzia Mbegu Technologies ambaye naye amelikodisha kwa Omari Mduduma. Shamba halijaendelezwa!
8) Kwashemshi Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hetka 1498.5, shamba liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, mwekezaji alitumia hatimiliki ya shamba kupata mkopo, ambao hakuutumia kuendeleza shamba. Shamba hilo lilishikiliwa na NBC mpaka 2003 lilipouzwa kwa Mathew Upanga Mnkande. Shamba limeendelezwa kwa 35% tu.
9) Ubena Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 4,227 ambalo lipo Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani liliuzwa kwa Highlands Estates Ltd mwaka 2007 kwa kiasi cha shilingi 278 milioni. Jumla ya hekta 499 ambayo ni sawa na 12% tu imepandwa mkonge.
10) Kingolwira/Pangawe Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 3703 liko Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro, liliuzwa kwa Highland Estates Limited kwa bei ya shilingi milioni 210.2 kupitia PSRC mwaka 2007. Jumla ya hekta 800 kati ya hekta 3703 ambazo ni sawa na 22% ya eneo lote ndio limepandwa mkonge!
11) Msowero Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 5200 lipo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, shamba liliuzwa na Mamlaka ya Mkonge Tanzania kwa Kampuni ya Noble Azania Agricultural Enterprises mwaka 1993. Shamba limepandwa mkonge hekta 900 tu ambazo ni 17% ya shamba lote na alizeti na mtama zimepandwa hekta 200 tu. Hekta 4100 hazijaendelezwa toka mwaka 1993!
12) Rudewa Sisal estate, shamba lina ukubwa wa hekta 6351, liliuzwa kwa kampuni ya Farm Land mwaka 1992. Kampuni husika iliuza shamba kwa kampuni ya China State Farms Agribusiness (Group) Corporation Tanzania Limited (CSFACOT) kwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.2 mwaka 2000. Mwekezaji ameweza kuendeleza 32% tu kwa kupanda mkonge hekta 2018!
13) Kimamba Fibre Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 5743 liliuzwa kwa kampuni ya ANCO Ltd mwaka 1998. Mwaka 2009 Kampuni ya ANCO Ltd iliuza hekta 3,043 kwa kampuni ya Sino na kubakiwa na hekta 2,700. Mustakabali wa shamba walilouziwa Sino haujulikani, ila shamba lililobaki ANCO Ltd limeendelezwa kwa 46.3% tu!
Mheshimiwa Spika, mashamba ambayo hayajaendelezwa kabisa ni:
1) Kikulu Sisal estate, lenye ukubwa wa hekta 5900 lililouzwa kwa Chavda Group, mwekezaji aliweka dhamana shamba, kama kawaida yake akachukua mkopo hakuendeleza shamba.
2) Kibaranga Sisal Estate lenye ukubwa wa hekta 6,900, liliuzwa kwa Kampuni ya Katani Ltd, iliposhindwa kuendeleza serikali ililiweka chini ya PSRC na Bodi ya Mkonge.
3) Kwamgwe Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 3700, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, alichukua mkopo, hakuendeleza shamba.
4) Kwafungo Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2,310, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, mwekezaji alitumia hatimiliki ya shamba kuchukua mkopo, ambapo hakutumia kwa kusudi la kuendeleza shamba. Shamba hilo bado linashikiliwa na CRDB.
5) Bombuera Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2,370 lipo Korogwe, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998. Mwekezaji alitumia hatimiliki ya shamba kupata mkopo. Hakuliendeleza shamba. Mwaka 2002 CRDB iliuza shamba kwa AMC Arusha Ltd.
6) Hale Mwakiyumbi Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 4,309. Shamba liliuzwa kwa Chavda Group, 1998. Alitumia hatimiliki kupata mkopo ambao hakuutumia kwa kusudi la kuendeleza shamba na kulitelekeza. Shamba linashikiliwa na CRDB.
7) Allidina Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2,300 liliuzwa kwa Noble Azania Agriculture Enterprises mwaka 1993. hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!
8) Msowero (Godes) Farm, lenye ukubwa wa hekta 5,000, lilikuwa linasimamiwa na Wizara ya Kilimo chini ya Tanzania Livestock Research Organization (TALIRO) mwaka 1993 Serikali ya CCM ilipanga kujenga chuo cha mifugo. Mpango ambao haukukamilika, shamba likabaki bila usimamizi wowote.
9) Rutindi Sisal Estate, lina ukubwa wa hekta 1,087. Shamba liko Morogoro, linamilikiwa na kampuni ya Noble Azania Agricultural Enterprises. Shamba halijaendelezwa na mwekezaji toka amelinunua.
10) Magole Sisal Estate, lina ukubwa wa hekta 1,149. Lipo Dumila, kilometa 65 kutoka Kilosa. Lilikuwa la Serikali chini ya Mamlaka ya Mkonge Tanzania. Japo halijabinafsishwa liko katika hali mbaya.
11) Mauze Sisal Estate, lina ukubwa wa hekta 2,842.5. Shamba lilikuwa na deni la shilingi milioni 1.36 kutoka Benki ya NBC. Benki ilishikilia hatimiliki na kuliweka chini ya ufilisi wa LART kutokana na kuongezeka kwa deni mpaka milioni 10. Kwa sasa kuna vijiji vya Kilangali na Mabwembele vilivyoanzishwa na vimesajiliwa ndani ya shamba. Halmashauri za vijiji hivyo zinakodisha maeneo katika shamba hilo kwa wanavijiji na watu kutoka nje ya vijiji kwa gharama ya shilingi 3,000 kwa ekari moja!
12) Myombo na Kilosa Sisal Estates. Mashamba haya yenye ukubwa wa hekta 2,024 (Kilosa) na 1843 (Myombo). Mashamba yalibinafsishwa na Mamlaka ya Mkonge kwa Kampuni ya Katani mwaka 1998. Baada ya kampuni ya Katani Limited kushindwa kuyaendesha, iliyakodisha kwa kampuni ya Agro-Focus. Mwaka 2005 Baraza la Mawaziri liliagiza kuwa mashamba haya yatafutiwe mwekezaji mwenye uwezo kwani kampuni ya Agro- focus Ltd imeshindwa kuyaendeleza. Hata hivyo, kinyume na maagizo mwaka 2009 Bodi ya Mkonge iliyauza mashamba haya kwa Agro-Focus. Matokeo yake mpaka sasa hakuna uwekezaji wowote uliofanywa. Sehemu kubwa ya shamba ni pori na sehemu iliyobaki imekodishwa kwa wananchi kwa ajili ya kulima mahindi.
13) Madoto Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hekta 3,200. Shamba lilinunuliwa na kampuni ya Sumagro Ltd ambayo nayo ililiuza kwa East African Breweries mwaka 2009. Hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!
14) Kivungu Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hekta 2,200. Shamba lilinunuliwa na kampuni ya Sumagro Ltd. Mwaka 1998 ililiuza kwa East African Breweries mwaka 2009. Hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuyarejesha mashamba yote ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza, kama ambavyo taarifa hii imevyoainisha. Hali kadhalika, kwa wale wawekezaji ambao wameweza kuendeleza sehemu ndogo na hawana uwezo wa kuendeleza shamba zima, warejeshe sehemu ya mashamba waliyoshindwa kuendeleza ili wapewe wananchi wenye uhitaji.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza serikali iangalie hatua za kuchukua dhidi ya wawekezaji katika mashamba 13 ambao wafuatao wameshindwa kuendeleza mashamba kwa 100%. Pamoja na wawekezaji katika mashamba 14 ambao wameshindwa kabisa kuendeleza mashamba waliyonunua, kama ambavyo yameorodheshwa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, kwa tathmini hii fupi iliyofanywa na CHC utaona ni kwa namna gani zoezi la ubinafsishwaji mashamba lilifanywa holela na kwa hujuma, pasipo kuzingatia maslahi ya umma. Katika hali ya kawaida, watu wote walioshiriki katika zoezi hilo wana kila sababu ya kuchukuliwa hatua, hakika hawana tofauti na wahujumu uchumi. Kwa mfano huyu ‘mwekezaji’ anayejiita Chavda Group, aliuziwa shamba kwa bei ya kutupa -mashamba saba, yenye ukubwa wa hekta 25,000, katika maeneo tofauti ya nchi hii. Kikubwa alichokifanya ni kutumia hati za shamba kuchukulia mikopo, kisha kutelekeza mashamba! Hivi kweli unahitaji kuwa na akili nyingi kuyaona haya? Nyuma ya Chavda Group wako akina nani?
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe ni familia hii hii ya Chavda (V.G Chavda na kaka yake P.G Chavda), waliojitwalia mkopo wa dola 3.5m mwaka 1993 chini ya DCP (Debt Conversion Program) wakiahidi kufufua mashamba ya mkonge Tanga ndani ya miaka 10, na kupata dola 42 milioni. Walipopata hayo mapesa, hawakufanya lolote, na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao. Kwa utaratibu huu, lazima tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni ‘waporaji’ na hawana tofauti na majambazi yanayoiba benki kwa kutumia nguvu!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali, kupitia Wizara ya Ardhi yenye jukumu pana la kusimamia sekta ya ardhi, kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji yanarejeshwa serikalini bure bila fidia kwa ajili ya kutafuta wawekezaji wengine wenye mtaji wa kutosha watakaoyaendeleza mashamba hayo.
Hali kadhalika, kwa yale mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo wanaoendesha shughuli zao za kilimo, Serikali ipange utaratibu wa kuwamilikisha wananchi maeneo husika ili kuondokana na ile dhana ya ‘uvamizi’ au kukodishwa ardhi kwa ajili ya kilimo. Zoezi hili lazima lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu uliotokea katika maeneo mengine ya nchi. Huko vigogo na watu wenye nafasi zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya wanakijiji.
MASHAMBA YALIYOPENDEKEZWA KURUDISHWA KWA WANANCHI MKOA WA ARUSHA
Mheshimiwa Spika, tarehe 17/6/1997 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Ndugu Daniel ole Njoolay aliitisha kikao kilichohudhuriwa na Ndugu Kileo – Katibu Tawala Mkoa, Ndugu P. H Muhale – Afisa Maendeleo ya Ardhi (M), Ndugu E. K. E Makere – Afisa Ardhi na Ndugu Z.M.S Meirish – Afisa Ardhi. Kikao husika kilichofanyika saa 4.35 asubuhi kilikuwa mahsusi kwa kuchambua mapendekezo yaliyoletwa kutoka wilayani kuhusu taarifa za mashamba makubwa mkoani Arusha.
Mheshimiwa Spika, mashamba yaliyojadiliwa na kufikia uamuzi mbalimbali yalihusisha wilaya sita:
a) Wilaya ya Arumeru – mashamba 18
b) Wilaya ya Ngorongoro – mashamba 10
c) Wilaya ya Babati – mashamba 11
d) Wilaya ya Simanjiro – mashamba 2
e) Wilaya ya Karatu – mashamba 6
f) Wilaya ya Monduli – mashamba 36
(Nakala ya majina ya mashamba pamoja na hatua zilizopendekezwa nimeziambatanisha kama sehemu ya hotuba hii). Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili Tukufu nini mustakabali wa mashamba 83, na hatua zilizochukuliwa kufuatia kikao husika.
Mheshimiwa Spika, mwaka 1999, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kupitia barua yenye kumb. Na. RC/AR/ CL 2/3 Vol IV/19 ilimwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Arumeru ikimtaarifu juu ya mashamba 11 ambayo yamepata kibali cha Rais kufuta miliki, taarifa ambayo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilipata toka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi kwa barua yenye kumbukumbu namba CL/46/VOL III ya tarehe 1 Juni 1999.
Mashamba hayo:
1) Shamba namba 78 na 79 – NAIC, Usa River
2) Shamba namba 90 na 91- Madiira Coffee Ltd
3) Shamba namba 98/2/1 – Duluti New – Duluti Lodge
4) Shamba namba 218/2 – Maua Limited
5) Shamba la Oljoro – Salama Estate
6) Shamba la Unit 15 Oljoro – Iman Estate
7) Karangai Sugar Estate (Tanzania Plantation)
8) Shamba Namba 3 – Milimani Pharmacy
9) Shamba la Nduruma – Lucy Estate
10) Shamba la Nduruma – Umoja Sisal Estate
11) Shamba la Dolly – Dolly Estate – Flycatchers (ambalo limegeuzwa uwanja wa gofu na shamba la wanyama kinyume na maagizo ya Rais)
Kambi ya upinzani inaitaka serikali itupe maelezo ya kina kuhusu mashamba haya.
MIGOGORO YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, kama tulivyofanya katika mwaka wa fedha 2011/12, Kambi ya Upinzani itakuwa na utaratibu wa kila mwaka wa fedha kuianishia Serikali migogoro mbalimbali ya ardhi inayolikumba taifa letu! Ni jukumu la Serikali kupitia vyombo vyake kuhakikisha kwamba inafuatilia migogoro hii kwa kina na hatimaye kuyatafutia ufumbuzi:
BAGAMOYO – MKOA WA PWANI
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Milo chenye vitongoji vitano – Milo, Relini, Kengeni, Kisiwani na Migude – kilichoandikishwa chini ya Sheria ya Vijiji (chenye shule ya msingi na zahanati na kijiji) wanailalamikia Kampuni ya Noble-Azania Agricultural Enterprises Limited ambayo inadai ni wamiliki halali wa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 3,000, eneo ambalo limekimeza Kitongoji cha Migude na sehemu ya Kijiji cha Milo. Kwa upande mwingine, Kampuni ya Azania inadai wanakijiji hao ni wavamizi kwa kuwa wao wana umiliki halali wa eneo husika kupitia umiliki namba 36911.
WILAYA YA MPANDA – KATAVI
Mheshimiwa Spika, Mkoa mpya wa Katavi anakotoka Waziri Mkuu, ni kati ya maeneo yenye migogoro mingi sana ya ardhi, mingi ikiwa ni migogoro sugu, ambayo imeshindwa kutafutiwa ufumbuzi licha ya malalamiko kufika ngazi za juu serikalini pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Migogoro inazihusu kata za Kabwe na Korogwe, Kijiji cha Nkungwi, Kijiji cha Kabange, Kijiji cha Mbuguni, mgogoro baina ya hifadhi ya Ubende na vijiji 18.
Mheshimiwa Spika, nitawasilisha mezani kwako nyaraka mbalimbali za migogoro hii, kama serikali itaona inafaa, iyafanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, nitaelezea mgogoro mmoja sugu ambao unahusisha watendaji serikalini. Mgogoro huu unaambatana na vitisho kwa wananchi hadi kufikia hatua wananchi kufunguliwa kesi za jinai ili kuwatisha. Wananchi wa Kata ya Sibwesa, Wilaya ya Mpanda wanalalamikia mtandao ambao umeundwa na watumishi wa serikali, ambao ni waajiriwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda wanaofahamika kama Cletus Siwezi, Andrea Malando (Kitengo cha Ardhi) na Bwana Galus Kasonso (Meneja wa mradi wa maji katika Halmashauri ya Mpanda).
Mheshimiwa Spika, watumishi hawa wanalalamikiwa na wananchi wakituhumiwa kuwanyang’anya mashamba yao kwa kutumia nafasi zao.
Mheshimiwa Spika, mtumishi huyu wa Serikali (kupitia kwa Bwana Ramadhani), alishindwa kuthibitisha umiliki wake katika Baraza la Ardhi la Kata, walikimbilia Baraza la Ardhi na Nyumba la Sumbawanga ambako ilitolewa hukumu ya upande mmoja!
Baada ya hukumu hiyo ya upande mmoja kumekuwa na hujuma dhidi ya wananchi na kuna malalamiko kwamba kuna mbinu ya kuandikwa hati ya kukamata heka mia tatu na sitini (360) kutoka mbuga ya Mwamapuli, Kijiji cha Kabage na mbinu yake ya kuendelea kufanya mipango ya kukamata watu bila ya kuwa na kosa kwa kutambua kuwa hawana uwezo wa kukabiliana na kesi za jinai. Jeshi la Polisi linahusishwa pia katika mazingira mawili, la kwanza kufungua kesi za kubambikiza, hali kadhalika kumlinda mhalifu!
Mheshimiwa Spika, yanayotokea Mpanda, yanafanyika pia kwenye maeneo mengi ya nchi hii, kwa watu ambao wamepewa dhamana kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, kutumia fursa hiyo kujilimbikizia ardhi, na pale wananchi wa kawaida wenye uhitaji wa huduma hiyo kukumbana na urasimu mkubwa uliotawaliwa na rushwa!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ijipime kwa kuangalia ni hatua gani stahili itawachukuliwa watumishi hao wa halmashauri, kama ushahidi ulivyotolewa na pengine inaweza pia kubaini mambo mengi mazito yaliyojificha.
MKOA WA MANYARA – BABATI
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu unahusu hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Vijiji vya Gijedabung, Ayamango na Gedamar. Vijiji hivi vilikaliwa na wananchi tangu miaka ya 1960. Hifadhi ya Tarangire ilianzishwa mwaka 1970 kwa kuzingatia tangazo la Serikali (GN) Na. 160. Mipaka yake ilitambulishwa kwa barabara iliyozunguka hifadhi nzima na kuipatia umbo linaloonekana katikati yake kupitia Sheria ya mwaka 1974 ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa, mpaka ambao wananchi wote waliutambua na kuuheshimu.
Mheshimiwa Spika, mgogoro ulianza baada ya uongozi wa Hifadhi ya Tarangire ulipotekeleza zoezi lake la kuhakiki mipaka yake kwa nia ya kufanya tafsiri yakinifu kwa kutumia vifaa vya kisasa. Wataalamu walibaini kwamba ule mpaka wa miaka yote wa barabara, uliowekwa na Mamlaka ya Hifadhi yenyewe haukuzingatia vipimo halisi na hivyo kusababisha eneo lenye ukubwa wa ekari 16,249.10325 kuingizwa kwenye mamlaka ya vijiji kimakosa.
Kwa mantiki hiyo, hifadhi iliamuru wananchi waliokuwa wakiishi kwenye ardhi hiyo kuhama mara moja na kusitisha matumizi yote juu ya ardhi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na amri hiyo, wananchi wengi wa maeneo haya wako katika hali mbaya sana kiuchumi kutokana na ardhi waliyokuwa wanaitegemea kuchukuliwa na Serikali! Wananchi wamezuiwa kufanya kitendo chochote cha kufanyia matengenezo makazi yao walioishi kwa zaidi ya miaka 50. Ikumbukwe kwamba wananchi hawa hawakuvamia eneo hili bali waliwekwa na mamlaka ya wilaya kwa makosa pasipo kukusudia. Pamoja na serikali kutaka kuwahamisha wananchi hao haijafanikiwa kuwapatia makazi mapya na mashamba ya kulima.
Mheshimiwa Spika, usumbufu wa askari wa Hifadhi ya Tarangire wanaofanya vitendo vya unyanyasaji ni kero kubwa kwa usalama, utulivu na ustawi wa wananchi wa maeneo husika. Kambi ya Upinzani haidhani kwamba hifadhi ni muhimu zaidi kuliko Watanzania walioiweka CCM madarakani. Ni rai yangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano awatazame wananchi wa maeneo haya kwa jicho la huruma!
Awatazame wananchi wa maeneo haya kwa jicho la huruma kutokana na kwamba hawana maeneo mbadala ya kuishi ili kuendeleza maisha yao. Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka ya kuhawilisha ardhi ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inayokaliwa na wananchi wa vijiji tajwa ili iwe ardhi ya kijiji, ombi ambalo lilishawasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, lakini mpaka leo hakuna majibu.
MKOA WA KAGERA – Wilaya ya Karagwe
Mheshimiwa Spika, muda sasa Kambi ya Upinzani, pamoja na wabunge wengi, wamekuwa wakizungumzia juu ya mgogoro baina ya wakulima na wafugaji, kutokana na serikali kutokuwa na mpango endelevu wa kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji. Mwaka jana katika hotuba ya Kambi, tulielezea juu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamaasai katika eneo la vijiji vya Izava (Chamwino) na Chitego (Kongwa).
Mgogoro huu mpaka leo hujapatiwa ufumbuzi. Kimsingi mgogoro ulisababishwa na ubabe na uamuzi mabovu wa mkuu wa wilaya. Katika hotuba hii, Kambi ya Upinzani inafikisha mbele ya Bunge lako Tukufu kilio cha wana-vitongoji wa Karugwebe, Kijiji cha Iteera na Kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Chanya, Karagwe.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanalalamikia kufukuzwa kwenye maeneo yao ya kilimo na kupewa wafugaji matajiri bila wao kuhusishwa. Baada ya kufukuzwa hawakupewa hifadhi, kitu ambacho kimewafanya wawe wahamiaji wasio rasmi ndani ya nchi yao. Ikumbukwe wananchi hawa walikuwa wanafanya shughuli za kilimo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20. Madiwani walipohoji katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika tarehe 31/2/12, walipata vitisho kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Misenyi aliyekuwa anakaimu ukuu wa Wilaya ya Karagwe!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kauli ya Serikali kuhusiana na matukio haya mawili; hali kadhalika Serikali ilitaarifu Bunge lako Tukufu ni lini itaandaa mpango rasmi wa matumizi ya ardhi kwa wakulima na wafugaji ili kuepuka migogoro isiyokwisha.
MKOA WA DAR ES SALAAM
Maeneo ya Pembezoni
Mheshimiwa Spika, miaka ya hivi karibuni serikali imekuwa na mikakati inayoitafsiri kama mikakati kabambe ya kuendeleza maeneo yaliyomo pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam. Mipango hiyo imeleta msiba mkubwa sana kwa wananchi wa maeneo hayo. Kwa sababu ya muda, tutazungumzia miradi ya Luguruni na Kwembe Kati, Kinondoni Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo haya, wananchi wameporwa ardhi yao yote kwa fidia ndogo sana, wamebomolewa makazi yao na kutimuliwa kutoka kwenye ardhi yao kwa nguvu ya dola, wakiwa “wamemaskinishwa” kupindukia baada ya kuporwa rasilimali ardhi yao, na wakiwa na fidia duni mkononi, wakihamia kwingineko kuanzisha makazi yasiyopimwa na ya kimasikini kupindukia!
Miradi hiyo imegubikwa na utendaji wenye kupindisha sheria, ubabe, usio na utawala bora, ulioteteresha viwango vya ramani na upimaji uliochakachua fidia, uliofanya ofa na hatimiliki kuwa uyoga, uliojaa dhuluma na hujuma dhidi ya hakiardhi ya wananchi. Hapo Luguruni tarehe 22/5/2007 Mkurugenzi wa Makazi na Ardhi alitangaza utwaaji wa ardhi wa asilima 5 ya ardhi kwa ajili ya miundombinu. Hali hii ilibadilika kufikia asilimia 100 na waliofanya hivyo ni watendaji wa mradi baada ya mkurugenzi husika kustaafu.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kinachofanyika Kwembe-Kati, kwa maeneo ya miundombinu, biashara na makazi yalitwaliwa na mradi na kutangazwa kuwa mali ya serikali, licha ya tamko la Waziri wa Ardhi Mhe. Chiligati Bungeni la tarehe 18/06/2009 na tamko la Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Goodluck ole Medeye bungeni tarehe 12/11/2011 kusisitiza ya kwamba baada ya Rais kutwaa ardhi na miundombinu albaki ya ardhi kwa ajili ya makazi na biashara, ibakie mikononi mwa wananchi wamiliki wa ardhi, waiendeleze wao wenyewe ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Katika maeneo yote hayo, baada ya ardhi yote ya wananchi kutwaliwa kwa fidia duni chini ya asilimia 20 ya bei ya soko kinyume hata na matakwa ya Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, sehemu ya II, kifungu cha 3 kinachoelezea misingi mikuu ya Sera ya Ardhi ya Taifa, wananchi walitimuliwa kimabavu baada ya makazi yao kubomolewa kwa tingatinga.
Mfano dhahiri ni wa eneo la Luguruni; fidia iliyolipwa kwa mita moja ya mraba ilikuwa ni shilingi 1,977, ardhi hiyo hiyo iliuzwa kwa shilingi 30,000 mita moja ya mraba bila maendelezo yoyote! Hivyo kuzalisha faida ya asilimia 1500. Huu ni wizi na unyonyaji mkubwa.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana pale watendaji wa Wizara ya Ardhi wanapotumia mgongo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutengua toleo la hatimiliki halali za wananchi wamiliki wa ardhi, kupora ardhi yao kwa mtindo huu, kupima viwanja vipya juu ya viwanja vya awali.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka Serikali hii ya CCM kuacha kufanya mambo kibabe, na kusitisha kile kinachoendelea katika maeneo ya Luguruni na Kwembe-Kati. Ulipaji fidia unakuwa na mianya lukuki ya ubadhirifu wa fedha, hivyo kuhitaji ukaguzi na udhibiti makini sana wa masuala yote ya malipo na matumizi ya fedha kwenye miradi ya Luguruni na Kwembe-Kati.
Viwango vya fedha vinavyohusika hapa ni vikubwa sana kutokana na wingi wa watu wanaohitaji kufidiwa, na kutokana na mauzo ya viwanja vilivyopatikana katika mchakato mzima wa kutwaa na kuuza ardhi, kuna uhitaji mkubwa wa ukaguzi na udhibiti mahsusi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu. Suala la ukaguzi ni muhimu kutokana na tuhuma kwamba malipo ya fidia yamefanywa bila kutumia nyaraka halali za matayarisho na ulipaji fedha.