TABORA
Na Moshy Kiyungi
Wahenga walinena kwamba kilichotundikwa na mrefu, mfupi hawezi kukitungua. Usemi huo ulijidhihirisha baada ya mwanamuziki nguli, Franco Luambo Luanzo Makiadi, kufariki dunia mwaka 1989.
Baada ya hapo bendi yake; T.P.OK Jazz, ikatoweka katika anga la muziki licha ya kuwapo wanamuziki wengi wenye vipaji vikubwa.
Walibaki watu kama Simaro Lutumba Massiya, Kiambukutu Josky, Ndombe Opetum, Serge Kiambukuta, Shakembo Batangunu, Lokombe Nkalulu, Elba Kuluma, Jerry Dialungana, Makosso Kidundi, Flavien Makabi, Henri Weteto na Henri Bofando.
Wengine ni Ndilu Kanda, Nsona Bruno, Malage de Lugendo, Baniel Mbambou na Madilu ‘Multi Systeme’.
Sasa imepita miaka 32 tangu Franco afikwe na mauti Oktoba 12, 1989 katika Hospitali ya Namur, Ubelgiji, alikokuwa amelazwa.
Wakati wa uhai wake alitumia talanta alizopewa na Mwenyezi Mungu kutunga na kuimba nyimbo zilizohamasisha wananchi kulijenga taifa lao, DRC (Zaire).
Nyimbo zenye maudhui ya siasa, mapenzi na hata kukemea mienendo mibovu iliyokuwa ikifanywa na baadhi ya viongozi, akiwamo Rais Mobutu Sese Seko.
Kifo chake kilipokewa kwa majonzi makubwa na mashabiki wa muziki wa rhumba Afrika nzima. Mwili wake ulirejeshwa Zaire, ukatembezwa mitaa ya Kinshasa kuagwa na wananchi chini ya ulinzi mkali wa polisi kabla ya mazishi ya kitaifa.
Baadhi ya viongozi na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali walijumuika, serikali ikiwakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Leon Kengo wa Dondo.
Serikali ilitangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa, radio ikipiga nyimbo za Franco hadi siku alipowekwa kaburini, Oktoba 17, 1989.
Serikali ya DRC kwa kuthamini kazi zake ikiwamo kuinua uchumi wa taifa hilo, ilifukua kaburi la Franco lililokuwapo kwenye makaburi ya Gombe na kuyazika upya mabaki yake katika makaburi mapya ya Kinkole, Nsele, nje kidogo ya Jiji la Kinshasa.
Oktoba 17, 2015, wakati wa maadhimisho ya miaka 26 ya kifo chake, Waziri Mkuu wa DRC wakati huo, Augustine Matata, alizindua mnara wa sanamu ya Franco kama kuenzi mchango wake, huku barabara iliyokuwa ikifahamika kama Jean Bendel Bokassa Avenue ikibadilishwa jina na kuwa Lwambo Makiadi Avenue.
Bokassa alikuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na swahiba wa Rais Mobutu.
Baadaye serikali ya Rais Joseph Kabila ikaazimia kujenga studio kubwa ya kurekodi muziki na kupewa jina la Franco; na kujenga nyumba ya makumbusho na kuwekwa vitu vyote alivyokuwa akitumia Franco enzi za uhai wake.
Franco alizaliwa Julai 6, 1938 katika Kijiji cha Sona Bata, magharibi mwa Jamhuri ya Kongo Leopoldville, akijulikana kama Luambo Makiadi Lokanga La Dju Pene Francois au Franco Yogo.
Akiwa mdogo, wazazi wake walihamia Leopoldville, mji ambao sasa unaitwa Kinshasa ambako baba yake, Joseph Emongo, alikuwa mfanyakazi wa shirika la reli huku mama yake akioka na kuuza mikate sokoni.
Franco alitengeneza gitaa la kienyeji akiwa na umri mdogo ambalo alilitumia kupiga muziki kando mwa mama yake kuwavutia wateja kununua mikate.
Magitaa yake likiwamo la ‘galaton’ aliloanzia kujifunza kupiga, gari, viatu pamoja na nguo alizokuwa akivaa vimo kwenye nyumba ya makumbusho.
Ni mpiga gitaa Paul Ebengo Dewayon ndiye aliyegundua kipaji chake na kumfundisha kupiga vema ala hiyo.
Mwaka 1950 akiwa na miaka 12, alitengeneza jina akiwa katika bendi ya Watam ya Ebengo Dewayon.
Miaka mitatu baadaye, alirekodi wimbo wake wa kwanza uliokuwa na jina la Bolingo na Ngai na Beatrice (mpenzi wangu Beatrice), alioutunga akiwa na bendi iliyokuwa inamilikiwa na Studio za Loningisa.
Kiongozi wa bendi hiyo, Henri Bowane, ndiye aliyeanza kufupisha jina lake la François akimuita Franco, jina alilokuja kujulikana katika maisha yake yote na mwaka 1955 alianzisha bendi akishirikiana na Jean Serge Essous, iliyozinduliwa katika ukumbi uliokuwapo katika Baa ya OK.
Bendi hiyo ilitoa zaidi ya albamu 150 katika kipindi cha miaka 30 iliyodumu, wakibuni jina la TP OK Jazz kuthamini Baa ya OK.
Katika kipindi kifupi Franco akiwa na mwimbaji Vicky Longomba katika bendi hiyo, waliibua upinzani mkubwa dhidi ya Bendi ya African Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’ Pepe Kalle.
Serikali ya Zaire ilimtunuku heshima kubwa ya Grande Maitre, ambayo ilikuwa mahususi kwa ajili ya majaji na wasomi.
Pamoja na umaarufu aliokuwa nao, mwaka 1958 alifungwa gerezani kwa kosa la ajali ya barabarani.
Aidha, purukushani za kisiasa nchini Zaire zilisababisha ahamie Ubelgiji hadi mambo yalipotulia chini ya Mobutu, aliporejea na kuandaa tamasha kubwa ‘Festival OK Jazz African Arts’ mwaka 1966.
Mwaka 1970 Franco alipata pigo kwa kufiwa na mdogo wake, Bavon Marie Marie, baada ya kupata ajali ya gari alilokuwa akiliendesha kwa hasira.
Chanzo cha hasira ni ndugu hao; Franco na Bavon, kukorofishana sababu ikiwa ni Marie Josee, mwanamke mpenzi wa Bavon.
Ilimchukua muda mrefu kurejea katika hali ya kawaida baada ya kifo cha mdogo wake.
Mwaka 1973, T.P.OK Jazz walitembelea Tanzania na kufanya maonyesho kabambe Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na baadaye Arusha.
Katika onyesho la Dar es Salaam, T.P.OK Jazz walifyatua papo kwa papo santuri zilizokuwa na nyimbo zilizopigwa kupitia mitambo yao na kuzigawa kwa mashabiki waliokuwapo uwanjani hapo.
Mwaka 1978, Luambo akawekwa tena gerezani kutokana na utunzi wa nyimbo za Helein na Jackie ambazo zilituhumiwa kuwa na maneno machafu yasiyo na maadili kwa umma, sheria ikachukua mkondo wake kupiga marufuku zisipitishwe kwenye radio na TV ya taifa.
Mwenyewe akajitetea akisema zilikuwa bado hazijaingia sokoni japokuwa zilikuwa zikisikika wakati wa maonyesho kwenye ukumbi wake wa 1.2.3 Kinshasa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Leon Kengo wa Dondo, akaamuru atupwe katika Gereza la Luzubu lililopo Mkoa wa Bas Kongo alikozaliwa Franco.
Akiwa gerezani, Franco, kwa masikitiko, alikuwa akishangaa kwanini rafiki yake, Rais Mobutu, hataki kumsaidia!
Msongo huo wa mawazo ulimuathiri na kumsababishia ugonjwa wa ‘hemorrhoid’.
Miaka michache baadaye Leon Kengo wa Dondo akaondolewa kwenye nafasi yake na kupelekwa kuwa Balozi nchini Ubelgiji, kitendo kilichomfurahisha sana Franco.
Misukosuko ya tunzi zenye ujumbe ulioonekana kutowaridhisha wenye mamlaka za kusimamia muziki DRC ilimkumba Franco mara kwa mara na kujikuta akitupwa gerezani na hata kuzuiwa kutoka nje ya nchi.
Siku zote Franco hakuona soni kusifia mazuri wala kuonya yaliyo mabaya; akitumia tafsida kufikisha ujumbe ukichagizwa na maelezo mujarabu.
Pamoja na urafiki kati yake na Rais Mobutu Sese Seko, mara kadhaa serikali ilizipiga marufuku baadhi ya nyimbo zake na kumsweka rumande hata akalazimika yeye na T.P. OK Jazz kukimbilia Brazzaville.
Baadaye Mobutu akamtumia wajumbe kumshawishi arudi Kinshasa, akimuahidi usalama wa maisha yake.
Akarudi DRC kama alivyoombwa, lakini alipokanyaga ardhi ya Kinshasa tu, akajikuta matatani tena kwa kupokewa na kikosi cha wanajeshi, wakawapakia kwenye gari lao hadi Gereza la Ndolo walikokaa siku mbili.
Baadaye wakahamishiwa Kambi ya Jeshi ya Tshatshi, walikoshikiliwa kwa siku kadhaa hadi Rais Mobutu alipokwenda kuzungumza na Franco na kumwambia:
“Kuanzia leo hadi nitakapoondoka madarakani, utakuwa ukiniimbia mimi. Utafanya kazi zangu zote kila nitakapokuhitaji.”
Tangu siku hiyo Franco akawa kiungo kikuu katika kampeni zote za Mobutu, akitunga nyimbo za kumsifia kama ule wa ‘Candidate Mobutu’, kukidhi matakwa ya rais.
Akanufaika sana na utawala wa Mobutu kuliko wanamuziki wengine wote.
Lakini hata kabla ya kulazimishwa kuwa ‘chawa’ wa Mobutu miaka ya 1980, tayari Oktoba 1971 Franco alishaonyesha kukubaliana na sera za rais huyo za kubadili majina yote ya Kizungu na kuweka majina ya kienyeji.
Ni Franco Luambo Makiadi ndiye aliyekuwa wa kwanza kutangaza kubadilishwa jina kwa Jamhuri ya Kongo Leopoldville na kuitwa Zaire kupitia wimbo wake wa ‘Republique Du Zaire’.
Akiwa na uzito mkubwa (kilo 136), wakati huo ugonjwa wa ukimwi ukiitikisa dunia, Franco aliibuka na wimbo wa ‘Attention na SIDA ’(jihadhari na ukimwi).
Septemba 22, 1989, Franco alifanya onyesho la mwisho maishani mwake katika Ukumbi wa De Melkweg jijini Amsterdam, Uholanzi, akiwa amedhoofika kiafya, akisaidiwa kupanda jukwaani na hata kuketi na mshirika wake wa tangu mwaka 1957, mpiga saksafoni wa bendi ya T.P. OK Jazz, Isaac Musekiwa.
Akiwa ameketi, Franco alishindwa hata kupiga gitaa kwa umahiri uliozoeleka na kulazimika kuondoka jukwaani huku baadhi ya mashabiki na wanamuziki wakibubujikwa machozi.
Siku 20 baada ya onyesho hilo, Oktoba 12, 1989, Luambo Makiadi Lokanga La Dju Pene Francois ‘Franco Yogo’, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 51.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali na mwandishi anayepatikana kwa namba 0767331200, 0713331200, 0736331200 na 0784331200.