*Wananchi wahoji kwa nini kazi wapewe wenye ufaulu hafifu
*Ni baada ya Jeshi la Polisi kuwakata vijana wenye Divisheni I na II
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Idara ya Uhamiaji nchini imetangza nafasi 350 za ajira kwa vijana waliomaliza kidato cha nne, kigezo kimojawapo kikiwa ni kwa waliofaulu katika Daraja la Nne (Divisheni IV).
Kigezo hiki kimelalamikiwa na wananchi kadhaa, wakidai kuwa kinawakatisha tamaa vijana wanaojituma darasani na kupata ufaulu wa juu.
Katika tangazo la ajira lililotolewa na Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji wiki iliyopita, idara hiyo nyeti inahitaji vijana katika cheo cha konstebo.
Maswali haya yameibuka wiki moja tu tangu Gazeti la JAMHURI liliporipoti malalamiko ya vijana waliokataliwa kujiunga na Jeshi la Polisi kwa sababu tu, ufaulu wao ulikuwa wa juu; yaani Divisheni I na II.
Na sasa Idara ya Uhamiaji nayo haiwataki makonstebo wenye ufaulu wa juu, tangazo likibainisha kuwa nafasi zilizotangazwa ni kwa ajili ya wenye ufaulu wa Daraja la Nne kwa alama 28 hadi 31.
Sifa nyingine ni lazima vijana hao wawe wamefuzu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa upande wa Tanzania Bara au Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa Zanzibar; huku wakiwa na fani katika taaluma mbalimbali.
Na sasa wananchi wanahoji iwapo Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji wameamua kutumia vijana wenye ufaulu hafifu katika kuendesha shughuli zao za kila siku.
Joel Patrobas, muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyerejea nyumbani kwao Tunduru mkoani Ruvuma kujishughulisha na biashara ya mbaazi, anahofu kwamba huenda vigezo hivyo vimewekwa makusudi ili watu wapeane kazi kwa upendeleo.
“Kumekuwapo hisia za muda mrefu kwamba Uhamiaji wanapeana kazi kwa upendeleo, sasa kwa vigezo hivi ni kama wanaimarisha dhana hii, kwani kupitia mwanya huu watoto wa vigogo wasio na sifa ndio wanaweza kufaidika na nafasi hizo,” anasema Patrobas.
Anasema hali hii ikiachwa iendelee, vijana wataanza kuamini kuwa hakuna haja ya kusoma na kufaulu vizuri, kwa sababu serikali haitaki kuajiri watu wenye ufaulu wa juu.
Mbali na hilo, kijana huyo anayepitia misukosuko ya kuzuiwa na serikali kuuza mbaazi katika soko analoamini kuwa ‘linalipa’, anasema kutokana na wimbi la vijana wasomi kujihusisha na kazi zisizo rasmi ili kujiingizia kipato, ipo hatari nyingine ya wasomi kuingia kwenye vitendo viovu kwa kukosa matumaini ya kuajiriwa katika sekta rasmi.
“Kuna mtu amehitimu chuo kikuu tangu 2012 (anamtaja), huyu hana ajira, yumo mitaani. Sasa leo asikie nafasi za kazi zinatolewa serikalini lakini wanaohitajika ni wenye daraja la nne, tena wenye alama 30, unategemea mtu kama huyo atajisikiaje?” anahoji Patrobas.
Mwananchi mwingine, Aziza Omary, Ofisa Maendeleo ya Jamii (mstaafu) na mkazi wa Morogoro, anahoji kuhusu sifa za vijana wanaohitajika katika idara hiyo huku akikosoa mfumo wa utoaji taarifa wa idara za serikali kwa sasa, ingawa pia anaamini kuwa huenda kutangazwa kwa nafasi hizo kumezingatia ikama ya idara husika.
“Kwani askari mwenye cheo cha konstebo anafanya kazi gani ndani ya Idara ya Uhamiaji? Hilo lilitakiwa kuwekwa wazi kwenye tangazo lao la kazi,” anasema Aziza na kuongeza kuwa huenda sifa ya elimu iliyotajwa katika tangazo inawahitaji watu wenye ufaulu wa hali ya chini.
Kwa upande mwingine anasema shida ni namna taarifa zinavyofikishwa kwa wananchi kutoka serikalini ndiyo huibua utata, hasa wahusika wanaotakiwa kuieleza jamii na kuielimisha wakibaki kimya.
“Nadhani wahusika baada ya kutangaza nafasi hizo ingekuwa vizuri kama wangejitokeza na kutoa ufafanuzi kwa nini wameamua kuweka vigezo hivyo.
“Wakikaa kimya maana yake wameruhusu wananchi waendelee kuwaza wanavyojua wenyewe,” anasema Aziza.
Anaongeza kuwa vijana wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi ni wengi mitaani, hivyo inapojitokeza nafasi ya kazi yoyote hata kama itawekewa sifa ambazo wao wanaona hawawezi kupata, wataomba tu ilimradi wajaribu bahati zao.
Mawazo ya Aziza kuhusu ikama yanapingana kwa namna fulani na mtazamo wa Godfrey Maro, mkazi wa Bunju, Dar es Salaam, ambaye anaamini kuwa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi kwa sasa kunahitajika watu wenye weledi na uwezo mkubwa katika teknolojia ya mawasiliano.
“Achana na ikama, nchi nyingi sasa hivi zinateswa na masuala ya wizi wa kutumia mitandao, ukiajiri mtu mwenye ufaulu hafifu atawezaje ‘ku-control’ (kudhibiti) mifumo ya kiteknolojia ambayo inabadilika kila siku? Nchi yetu itakuwa salama ikiwa mikononi mwa watu wenye ufaulu hafifu?” anahoji Maro, mwekezaji na mmiliki wa migodi midagomidogo nchini.
Maro anadai kuwa kuweka kigezo cha wenye ufaulu hafifu ni kutaka kujaza watu ambao watakuwa wanapelekeshwa bila wao kuwa na uwezo wa kuhoji mambo mazito.
“Inashangaza kweli, nadhani jeshini, hasa Jeshi la Polisi kunatakiwa watu wenye uelewa mpana, kwa sababu kazi wanazofanya ziko karibu na jamii, sasa kama watajazwa watu wasio na fikra pana wataleta msuguano baina yao na wananchi kwa kushindwa kuelewana.
“Matokeo ya kuweka wasio na weledi yanaweza kujitokeza pale watakapotumika kisiasa, kwa sababu wao ni watu wa ‘ndiyo mzee’. Mwanasiasa atakuwa na uwezo wa kuwaamuru kufanya hata yaliyo nje ya taaluma zao,” anasema Maro.
Mkurugenzi wa Tiba Asilia na Mazingira nchini, Boneventure Mwalongo, anasema kitendo cha kutangazwa kwa nafasi za kazi serikalini ni jambo la heri kwa vijana kwa sababu ilikuwa imepita miaka sita bila serikali kutangaza nafasi za kazi.
“Tusiangalie kwanza vigezo vya kupata nafasi hizo, kwanza tuipongeze serikali kwa kufikia hatua hiyo,” anasema Mwalongo.
Kwa upande mwingine anasema kitendo cha Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji kuwataka watu wenye ufaulu hafifu ni kudhalilisha kada ya usomi nchini.
Uhamiaji waahidi kutoa ufafanuzi
Wakati hali ikiwa hivyo miongini mwa wananchi wa kawaida, JAMHURI lilibisha hodi Idara ya Uhamiaji, lakini simu ya Kamishna Mkuu, Dk. Anna Makakala, haikupokewa kwa siku mbili mfululizo.
Baadaye, Ofisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, akalieleza JAMHURI kuwa jambo hilo liko wazi na linazungumzika.
Mselle ameahidi kulitolea ufafanuzi suala hilo wiki hii.
Wakati Idara ya Uhamiaji wakitangaza nafasi hizo kwa vijana waliohitimu kidato cha nne peke yake, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetangaza nafasi za kazi 180 huku wanaohitajika wakiwa vijana waliohitimu kidato cha nne, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 wenye astashahada ‘Trade-Test Grade I’.
Katika tangazo hilo wanataka mwombaji awe na fani ya udereva, ufundi wa magari, ushonaji, ufundi bomba, ufundi ujenzi, ufundi umeme na uzamiaji.