DAR ES SALAAM
Na Abdul Dendego
Ni kawaida kwa viongozi wakuu wa kitaifa kufanya ziara za kila mwaka na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Septemba 18, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan, ametekeleza suala hilo kwa kufanya safari Marekani na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 76 wa UNGA, uliofanyika Septemba 23, 2021.
Rais amehutubia Mkutano Mkuu wa 76 wa UNGA na kurejea nchini mara baada ya mkutano huo.
Hebu tuitazame hotuba ya Rais Samia aliyoiwasilisha siku hiyo kuanzia majira ya saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, pamoja na mengine aliyoyafanya au kuchuma akiwa Marekani.
Mama Samia aliondoka nchini Septemba 18, mwaka huu kuelekea Marekani na kutua salama katika Uwanja wa Ndege wa John F. Kennedy, New York, siku iliyofuata, yaani Septemba 19, 2021.
Wanadiplomasia wa Tanzania wanaofanya kazi nchini Marekani walikuwapo uwanjani kumlaki kongozi wao mpendwa.
Akiwa huko alikutana na kuzungumza na Watanzania waishio Marekani (Diaspora) na kufanya mazungumzo nao, na kuwaeleza kuwa, pamoja na Mkutano Mkuu wa 76 wa UNGA, pia atahudhuria mikutano mingine kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Siku iliyofuata, Septemba 20, Rais akahudhuria Mkutano wa UN uliojadili athari za mabadiliko ya tabia nchi duniani ambapo akasisitiza umuhimu wa kutopuuza juhudi za kukabiliana na janga hilo.
Mkutano huu ulikuwa maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 26 wa Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) unaotarajiwa kufanyika Glasgow, Scotland, Novemba 2021 mwaka huu; Tanzania itashiriki.
Katika mkutano huo, Rais Joe Biden wa Marekani aliahidi kuongeza mara dufu mchango wake kwenye mfuko wa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi duniani.
Dola za Marekani bilioni 100 huhitajika kila mwaka, zikichangiwa na nchi zenye nguvu kiuchumi, kuzisaidia nchi nyingine katika kukabiliana na athari hizo.
Nia hii ya Marekani ni dalili nzuri itakayoongeza matumaini kwa jumuiya ya kimataifa, msimamo tofauti na wa uongozi uliopita chini ya Donald Trump alioutoa katika Mkataba wa Paris mara tu alipoingia madarakani.
Msimamo wa Trump uliyumbisha malengo ya Mkataba wa Paris kwa kuwa Marekani ni mshirika mkubwa na muhimu katika mapambano haya.
Kisha Samia akakutana na kuzungumza na viongozi akiwamo Rais wa Comoro, Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Rebecca Nyandeng Garang, akakubaliana nao kukuza uhusiano kati ya Tanzania na mataifa yao.
Rais aliwaagiza watendaji wake kuunda haraka tume za kudumu za ushirikiano ili kukuza uhusiano wa kidiplomasia na mataifa hayo.
Kisha akazungumza na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi, na kukubaliana kuimarisha ushirikiano hasa katika kusaidia wakimbizi waliopo Tanzania.
Grandi akapendekeza kuandaliwa jopo la wataalamu kutoka UNHCR na serikalini kutatua changamoto zilizopo katika kuhudumia wakimbizi nchini.
Tanzania ipo mstari wa mbele katika kutoa ardhi na kuhifadhi wakimbizi kutoka nchi mbalimbali duniani tangu ilipopata uhuru mwaka 1961.
Siku tatu baada ya Samia kutua Marekani, akashiriki UNGA, pia mkutano maalumu na wakuu wa nchi na serikali ambao ni wanawake walioshiriki mkutano huo.
Hapo akaihakikishia dunia kuwa chini ya uongozi wake kutakuwapo usawa wa kijinsia, licha ya vikwazo vilivyopo.
Akasema katika utawala wake ameteua viongozi wanawake kwenye ngazi mbalimbali, hasa katika nafasi ambazo zilizoeleka kushikwa na wanaume tu.
Akatoa mfano wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, nafasi inayoshikiliwa na Dk. Stergomena Tax.
Katika mkutano huo mkubwa zaidi duniani, Mama Samia ameweka ahadi ya kuunda timu ya wataalamu itakayoleta mapendekezo ya kuwainua wanawake kiuchumi.
Akatoa wito kwa washiriki kutotoa fursa kwa UVIKO-19 kuwa kikwazo cha mafanikio kwenye usawa wa kijinsia, akatilia msisitizo kuwa ili Malengo 17 ya Milenia kufanikiwa, lengo namba tano linalohusu usawa wa kijinsia ni lazima lifanikiwe.
Baadhi ya malengo hayo 17 ni kutokomeza umaskini, kutokomeza njaa, afya bora, elimu bora, usawa wa kijinsia, upatikanaji wa maji salama, upatikanaji wa nishati kwa unafuu, upatikanaji wa ajira zenye utu na ukuaji uchumi, ugunduzi na ujenzi wa miundombinu na kuleta usawa katika uchumi.
Katika mazungumzo yake na Rais wa Benki ya Dunia (WB), David Malpass, ameahidiwa na rais huyo kuwa WB itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi, hasa kupitia mabadiliko ya kidijitali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kutokana na mazungumzo hayo, tumeshuhudia ujio wa Makamu wa Rais wa WB, Dk. Hafez Ghanem, aliyefika Tanzania na kuzungumza na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Septemba 28, 2021 Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Akiwa Marekani, Mama Samia akakutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo Iweala, wakikubaliana kuwezesha biashara kwa kuimarisha upatikanaji wa chanjo, usimamizi wa uvuvi na kilimo.
Siku ya nne akiwa Marekani, Rais alihudhuria na kuhutubia mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani.
Katika mkutano huo, Rais alionyesha uwiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Marekani, kwa kutoa takwimu za mwaka 2019, zinazoonyesha bado Watanzania hawatumii fursa zilizopo kufanya biashara na Marekani, ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi wa Marekani.
Ametoa mfano kwamba mwaka 2019, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 241 na kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 46.
Sambamba na hayo, Rais ametekeleza vilivyo dhana ya diplomasia ya uchumi kwa kuvutia uwekezaji zaidi kutoka kwa wafanyabiashara wa Marekani, kwa kuwaonyesha wigo wa soko lilopo nchini.
Akawaonyesha wafanyabiashara kuwa kuwekeza ndani ya Tanzania ni kujihakikishia kupata soko la watu milioni 450, ambao ni zao la Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Tanzania pia imesaini na kufanya kuwa sheria Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCTA), ambapo nchi wanachama zitanufaika kwa masharti rahisi bila vikwazo vya kuingiza bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine, hivyo kuwa na uhakika wa soko lenye watu takriban bilioni 1.3 barani Afrika.
Pia Samia amekutana na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), Charles Michel, wakazungumzia masuala ya UVIKO-19, mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa Msumbiji na mapinduzi ya kidijitali.
Baadaye akahudhuria maadhimisho ya miaka 20 ya Tamko la Durban kuhusu kupinga ubaguzi wa rangi na aina zote za unyanyasaji.
Kilele cha ziara yake Marekani ilikuwa Septemba 23, 2021 (siku tano baada ya kufika), alipohutubia UNGA kwa mara ya kwanza tangu kuapishwa kwake kuwa Rais wa Tanzania.
Mbali na hilo, akakutana na Mtendaji Mkuu wa kampuni za Grumeti, Mikael Andrea, anayemuwakilisha mmiliki wa kampuni hizo, Paul Tudor Jones II na kukubaliana kuendelea kufanya kazi na serikali pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii.
Mtu mwingine muhumu aliyekutana na kuzungumza naye kwa muda mfupi tu aliokuwa Marekani kuhudhuria UNGA, ni Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres.
Sasa tugeukie hotuba ya Mama Samia UNGA. Hotuba yake imejikita katika masuala yanayohusu ushirikiano wa pamoja kwa mataifa yote katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa, UVIKO-19 na athari zake pamoja na hatua ambazo Tanzania imechukua kukabiliana na janga hilo.
Akazungumzia changamoto zilizopo katika upatikanaji wa chanjo kwa mataifa yanayoendelea, masuala yanayohusu usawa wa kijinsia, mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya vijana.
Hotuba hii imeibua maswali mengi na sintofahamu katika jamii ambayo wengi wangependa kupata majibu yake ili kuendana sawa na utekelezaji wa kile kilichowasilishwa na Rais.
Tukumbuke kuwa hotuba hii inatoa dira ya vipi ni vipaumbele vyake katika sera ya mambo ya nje kipindi cha awamu yake, pia yapi malengo yake katika siasa za kimataifa.
Kwa mfano, Rais ameeleza kuwa kwenye upatikanaji wa chanjo za UVIKO-19, hakuna usawa au uwiano baina ya nchi tajiri, zilizoendelea na nchi maskini.
Akaonyesha kuwa nchi zilizoendelea zimepatiwa chanjo ya UVIKO-19 kwa kiwango kikubwa zaidi, zikiwapa chanjo raia wake zaidi ya mara moja wakati nchi zinazoendelea bado zinapata changamoto kupata chanjo hiyo, hali inayosababisha kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa na Shirika la Afya duniani (WHO).
WHO inataka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, nchi zote ziwe zimefikia asilimia 40 ya uchomaji wa chanjo kwa watu wake, na asilimia 70 ya uchomaji chanjo itakapofika nusu ya mwaka 2022 kwa nchi zinazoendelea.
Swali na je, Tanzania ina mahitaji ya chanjo za UVIKO-19 kwa kiasi hicho hata kumsukuma Rais kuchangia wazo hilo UN?
Je, Tanzania itaweza kufikia malengo ya WHO? Kwa kweli hakukuwa na haja kwa Rais kupendekeza hayo hasa kwa Tanzania, kwa kuwa tayari tumenufaika na chanjo takriban milioni moja kupitia mpango wa COVAX.
Lakini ajabu hadi sasa muamko ni mdogo miongoni mwa wananchi kujitokeza kuchanja, kinyume cha matarajio ya serikali, wakati muda wa matumizi ya chanjo hizo ukikaribia kufikia ukomo wake.
Sasa hata tukiletewa chanjo nyingi zaidi, hazitaharibika bila watu kuzitumia? Hii itakuwa ni hasara kwa wahisani na kwa serikali.
Hadi Septemba 26, 2021, inakadiriwa ni Watanzania 400,000 tu ndio walikuwa wamekwisha kupata chanjo ya UVIKO-19 (kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali).
Huenda sera ya ‘chanjo ya hiari’ ndiyo kikwazo kitakachosababisha hata msaada wa chanjo utakaoletwa kuishia kuharibika kwenye bohari za dawa.
Hamasa ya kugomea chanjo iliyoachwa nyuma na Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli, huku Samia akiwa makamu wake, nayo ni tatizo, kwani hata sasa wananchi wanaamini katika dawa za kienyeji kuliko chanjo.
Jingine linaloweza kuibua maswali katika hotuba hiyo ni hoja ya usawa wa kijinsia, hasa aliponena kuwa suala hilo kwake ni mzigo ambao anahitaji kusaidiwa ili aweze kufikia malengo aliyojiwekea.
Wengi walitarajia angeweza japo kwa uchache kuonyesha jitihada za serikali zilizopita katika kumnyanyua mtoto wa kike katika jamii.
Labda nimkumbushe Mama Samia jitihada ambazo serikali zilizotangulia zilifanya kuimarisha usawa wa kijinsia.
Serikali zilizopita zimetoa fursa kwa wanawake kushiriki shughuli mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.
Mfano mzuri, taifa lina nafasi za ubunge na udiwani wa Viti Maalumu kwa muda mrefu sana sasa.
Kama hiyo haitoshi, kumekuwapo uteuzi katika nyadhifa tofauti za kiuongozi nchini ambapo wanawake wamekuwa wakijumuishwa; mfano wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na hata watendaji wa ngazi mbalimbali kwenye taasisi za umma na vyombo vya uamuzi.
Serikali zilizopita zilizoongozwa na wanaume, kumekuwapo na upendekezaji wa wanawake katika taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, tukimshuhudia Dk. Asha-Rose Migiro akiwa Naibu Katibu Mkuu wa UN!
Getrude Mongela amewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika, huku akina mama kadhaa wakishika nafasi nyeti za kimataifa kama Profesa Anna Tibaijuka (Mkurugenzi Mkuu wa UN Habitat).
Katika orodha hii wapo pia akina Anna Makinda, Dk. Tulia Ackson pamoja na Mama Samia mwenyewe aliyekuwa Makamu wa Rais wa serikali iliyopita.
Katika vyombo vya dola, kuna kumbukumbu ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuamua kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebecca Z. Gyumi (2017) C.A.T No. 204.
Kwenye shauri hili, mahakama ilitoa tamko kuwa vifungu vya sheria, kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa kinachompa mzazi au mlezi uwezo wa kumuozesha binti aliyefika miaka 15 kuwa ni batili na ni kinyume cha Katiba, hivyo kuzitaka mamlaka za serikali kupitia upya na kurekebisha sheria, ili sasa binti aweze kuolewa akiwa na miaka 18 na zaidi.
Hii ni michango ya awamu zilizopita katika kuhakikisha Tanzania inavuka Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kusimamia lengo namba tano kwa nguvu.
Jingine linaloleta maswali ni suala la maendeleo kwa vijana. Rais hakuelezea chochote kuhusu hili kwenye hotuba yake UNGA.
Serikali zilizotangulia ziliweka mikakati na misingi kumuinua kijana wa Kitanzania, ikiwamo ulazima wa halmashauri kutenga asilimia ya mapato yake kwa ajili ya vijana.
Awamu zilizopita pia zimepitisha sera ya vijana na sheria inayohusu vijana, inayotoa fursa ya kuundwa Baraza la Vijana la Tanzania, litakalowakutanisha vijana bila kujali itikadi ya vyama vyao vya kisiasa, na kuwaweka pamoja kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Sasa nitumie nafasi hii kupendekeza baadhi ya mambo ambayo Rais angeweza kuyapa kipaumbele kwenye hotuba yake.
Mambo hayo ni kama kukuza uhusiano wa kikanda (regional integration) katika kushughulikia changamoto zinazoukabili ulimwengu leo hii; angesisitiza pia kukuza uhusiano baina ya taifa moja na jingine, na taasisi za kimataifa.
Kuhusu chanjo ya UVIKO na mwitikio duni, Rais inabidi abadilishe au kuboresha sera yake ya ‘chanjo kwa hiari’ kwa sababu itaathiri mwenendo wa utoaji chanjo.
Iwe lazima, kwa mfano, kwa watumishi wa umma, kisha sekta zinazohudumia watu wengi kama vile sekta ya mabenki, uchukuzi, afya, elimu na nyinginezo ambazo hukusanya watu wengi kwa mkupuo. Kwa kushindwa kufanya hivi, basi ni wazi kuwa sera yake haitakuwa na mashiko na kwa maana hiyo, huenda ikashindwa kutekelezeka au isipate mafanikio yaliyotarajiwa.
- 1. Pia katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, Rais ni vema hotuba ingejikita kwenye kutoa msisitizo kwa mataifa yenye nguvu duniani, na mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa yenyewe, Umoja wa Ulaya, Mashirika ya fedha kama Benki ya Dunia (W.B) na I.M.F, pamoja na Shirika la Biashara Duniani (W.T.O), kuondosha vikwazo vya kiuchumi kwa nchi zinazoendelea ili yaweze kukabiliana na changamoto za ukuaji uchumi ambazo zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na Janga la UVIKO-19. Katika hili pia angezitaka nchi izo tajiri na mashirika ya maendeleo kutoa mikopo yenye masharti nafuu, mikopo isiyo na riba, misamaha ya madeni, na misaada ya kifedha kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kufufua uchumi wao ulioathiriwa na janga la UVIKO-19. Lakini itasaidia kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya 2030 dunia iliyojiwekea.
- 2. Hoja nyingine ya msingi ni kuhusu hali ya usalama katika Bara la Afrika, hususan nchi za maziwa makuu na nchi jirani kama Msumbiji, Burundi, Somalia, Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ni matarajio yangu kuwa hotuba ya Rais ingeeleza kwa undani kuhusiana na hali ya usalama katika maeneo hayo. Ambayo kumekuwapo na vita ya wenyewe kwa wenyewe ya muda mrefu bila kupata ufumbuzi, pia kumekuwapo na kesi mpya za matukio ya kigaidi katika nchi hizo, huku hali za watu zikiendelea kuwa mbaya zaidi, hivyo kuongeza idadi ya watu maskini na wakimbizi duniani. Kutokana na ukosefu wa amani katika nchi hizo kumesababisha idadi kubwa ya wakimbizi katika nchi jirani ya nchi hizo, hali inayozidi kudumaza maendeleo ya nchi hizo kutokana na kuelemewa mzigo wa wakimbizi kutoka nchi jirani.
- 3. Hoja nyingine ya msingi ilikuwa ni matarajio yangu kuona Rais kwenye hotuba yake akieleza umuhimu wa Bara la Afrika kupewa kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSCO). Hali ambayo italihakikishia Bara la Afrika kuwa na uwakilishi wa kudumu kwenye chombo hicho cha juu kabisa katika Umoja wa Mataifa. Chombo hiki ni muhimu sana katika mustakabali wa masuala yote nyeti ulimwenguni, na lingekuwa jambo la faida sana kama Bara la Afrika lingeweza kupata kiti cha kudumu katika chombo hicho, kwa mustakabali wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Mwisho kabisa, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Samia kwa kitendo chake cha kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake, sambamba na Bara la Afrika katika Mkutano Mkuu wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Kwa kufanya hivyo, Rais ameweza kufanikiwa kukuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni, sambamba na kuitekeleza vema sera yetu mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, inayosisitiza uendelezaji na ushiriki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
E-mail: [email protected]
Simu: +255762476738/ +255714065453