MBEYA
NA MWANDISHI WETU
Kutokana na ukosefu wa utaratibu wa watu kumuona daktari ili kuchunguzwa na kufanyiwa vipimo mapema (check-up), watu wengi hujikuta wakishindwa kugundulika matatizo yao mapema na kujikuta wakifika hospitalini katika hatua mbaya na za mwisho.
Ili kuthibitisha hilo, unakumbuka ni lini ulifika kwa daktari wa macho kwa ajili ya uchunguzi wa macho bila kuwa na dalili yoyote?
Leo tutakuwa na mada ya ugonjwa wa shinikizo la macho ambalo kwa kitaalamu linaitwa ‘glaucoma’, inayoletwa na Dk. Rajabu Mlaluko, kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.
Tuanze kwa swali: “Ugonjwa wa shinikizo la macho ni nini?”
Daktari Mlaluko anasema: “Ni ugonjwa unaoleta athari kwenye mshipa wa fahamu unaotoa taarifa kwenye macho kwenda kwenye ubongo ili kumfanya mtu kuona, athari hizo zinasababishwa na presha kuwa kubwa ndani ya jicho.
“Kwa kawaida presha ya macho huanzia 9-21mmHg japo baadhi ya watu athari hutokea hata hiyo presha inapokuwa kawaida kulingana na urahisi wa mshipa wa fahamu kuumizwa na presha ndani ya jicho.
“Kuna aina tofauti za shinikizo la macho lakini zaidi ni ile inayotokea hata kona (angle) ya sehemu ya kupitishia maji ya ndani ya jicho (aqueous humor) inapokuwa haijajifunga, kwa kitalaamu inaitwa ‘open angle glaucoma’.
Tofauti na magonjwa mengine ya macho ambayo humfanya mtu kwenda hospitalini kwa haraka, ugonjwa huu mara nyingi hauna dalili yoyote katika hatua za mwanzo kabla ya kufikia hatua ya kupungua uwezo wa kuona hata upofu, hivyo ni rahisi uharibifu kutokea hata bila mgonjwa kugundua kwa haraka kama ana tatizo hili.
“Ndiyo maana tunashauri kufika mara kwa mara kwa daktari wa macho ili kuchunguzwa na kujua hali ya afya ya macho yako.
“Ugonjwa huu huwaathiri wazee kwa watoto, wanawake na wanaume kwa kuleta athari sawasawa japo huwaathiri zaidi wanaume na watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 40 na kuendelea.
“Magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu (presha), matatizo ya uhafifu wa kuona mbali (high myopia) na karibu (high hypermetropia), matumizi ya pombe, uvutaji wa sigara, mtoto wa jicho, matumizi ya dawa za kupanga uzazi na hata unywaji wa kahawa ni baadhi ya sababu za tatizo la shinikizo la macho (glaucoma).”
Daktari Mlaluko anasisitiza kwa kusema: “Ugonjwa huu mbali na sababu nyingine, husafiri katika familia kwa kurithishana. Mfano, baba au mama anapokuwa na tatizo hili anashauriwa kuwakumbusha watoto wake, wazazi wake, kaka zake au dada zake kufika kwa mtaalamu wa macho kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Bahati mbaya ugonjwa huu hauna tiba kabisa isipokuwa kuna dawa za kutumia au hata kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kushusha presha ya macho na kupunguza uwezekano wa uharibifu unaoweza kusababisha upofu wa macho kabisa.”
Dk. Mlaluko, mtaalamu wa macho katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya anashauri watu wote kujenga utaratibu wa kufika hospitalini kuonana na daktari wa macho, kwani kutofanya hivyo inaweza kusababisha ucheleweshwaji wa kugundulika na hata kusababisha upofu kabisa.
Mgonjwa akigundulika kuwa na tatizo la shinikizo la macho anashauriwa kuhudhuria kliniki ya macho na kutumia dawa zake ipasavyo bila kuacha hata siku moja.
Makala hii imeandaliwa na Dk. Rajabu Jumanne Mlaluko kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya. Anapatikana kwa simu namba 0753 938628 au baruapepe: [email protected]