Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa kuboresha Shirika la Umeme nchini (Tanesco). 

Amemteua Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco. Amemteua Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco. Kabla ya uteuzi huo Chande alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa Multichoice Afrika. Chande anachukua nafasi ya Dk. Tito Mwinuka.

Aliyepata kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Felschemi Mramba, amemteua kuwa Kamishna wa Nishati Jadidifu. 

Pia amemteua Hassan Seif Said kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Nishati Vijijini (REA). Naye Michael Minja ameteuliwa kuwa Kamishna wa Petroli na Gesi, Wizara ya Nishati.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba, ameteua wajumbe wa Bodi ya Shirika la Tanesco, ambao ni Nehemia Mchechu, Zawadi Nanyaro, Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmas Massawe, Balozi Mwanahidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim, Abubakar Bakhressa na Christopher Gachuma.

Sisi tunaomba kukiri kuwa uteuzi huu umewahusisha watenda kazi bora. Nchi hii ilifika mahala majungu yakatawala kazi na ndiyo maana tumeshindwa kupiga hatua. 

Yalikuwapo maneno ya chini kwa chini kuwa baadhi ya watu walikataliwa uteuzi au kufanya kazi fulani kwa sababu ya makabila yao. Tulipokuwa tunaelekea ilikuwa ni kubaya.

Sasa hivi Watanzania wana hamu ya kusikiliza uteuzi. Ukiacha ukweli kwamba uteuzi unajenga umoja wa kitaifa kwa vijiji, wilaya na mikoa kujisikia kuwa vimewakilishwa serikalini, sisi tulishindwa kuelewa jinsi nchi hii ilivyowaweka pembeni watu makini kama Mchechu na Mafuru. 

Watu wasio na maana yoyote kiutendaji zaidi ya ubora wa kupika majungu, walisikilizwa na kuwafitini Mchechu na Mafuru hadi dunia ikapata habari.

Wafitini hawajakoma, hata sasa bado wapo kazini wanaendelea kufitini watu kwa dini zao, vyama vyao vya kisiasa, makabila yao na mambo mengine mengi ya kipuuzi yasiyo na tija kwa nchi hii. 

Uteuzi uliofanywa TANESCO kuanzia mkurugenzi mkuu na wajumbe wa bodi, akiwamo Mama Maajar, unaleta imani kubwa kuwa shirika hili sasa litafufuka.

Hakuna asiyefahamu kazi ya kupigiwa mfano aliyoifanya Mchechu akiwa National Housing. Tunaamini ubunifu aliouonyesha NHC atauhamishia TANESCO kupitia Bodi ya Wakurugenzi na tutashuhudia mabadiliko makubwa katika kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme nchini. Tunatarajia utafika wakati TANESCO itabaki na kazi moja tu ya usafirishaji.

Uzalishaji na usambazaji wataruhusu ushindani kama ilivyo kwa simu za mkononi, hali inayoboresha huduma. Mungu awatangulie. 

Hongera Mama Samia kwa kutimiza ahadi yako ya kufanya kazi na watu kwa kuangalia uwezo wao, na si maneno mengine yasiyopimika. Mungu ibariki Tanzania.