Na Nassoro Kitunda
Ni dhahiri siasa zetu zimekuwa zinasukumwa zaidi na shauku ya kutafuta madaraka kuliko ukombozi wa jamii. Ndiyo maana ninakubaliana na Dk. Bashiru Ally aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliposema katika moja ya mihadhara yake akiwa bado mhadhiri wa chuo kwamba ombwe lililopo sasa katika siasa limetokana na wanasiasa wetu kuacha siasa za ukombozi ambazo dira yake ilikuwa kuleta ukombozi na kuilinda jamii dhidi ya mifumo ya unyonyaji.
Chukulia mfano wa Chama cha TANU ambacho ndicho kilichoongoza mapambano ya uhuru. Hakikufanikisha ajenda yake kutokana na msukumo wa kushika madaraka bali mchakato wa kuiunganisha jamii ili kujiletea maendeleo.
Ndiyo maana utaona mapema baada ya uhuru, viongozi wa chama hicho kama Mwalimu Julius Nyerere aliacha madaraka makubwa serikalini ili akakijenge chama kwa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa ajili ya kujenga umoja.
Lakini kutokana na mabadiliko ya mwelekeo wa kisiasa, madaraka ndiyo yamekuwa ajenda namba moja ya vyama vya siasa na si ukombozi wa kijamii.
Ndiyo maana sasa hivi tunaambiwa dhumuni la chama chochote kile ni kutafuta dola, kwa maana ya madaraka. Kuna msemo wa Profesa Issa Shivji anasema wanasiasa hawapendi siasa bali wanapenda madaraka. Hii ina maana kwamba wanasiasa wanatumia siasa kupata madaraka lakini wao hawapendi siasa ya kweli.
Kuhama huku kumesababisha kuwa na ombwe la kiitikadi. Siasa za TANU zilikuwa siasa za ujamaa na kujitegemea, siasa zilizolenga kuondoa unyonyaji wa ubepari chini ya Azimio la Arusha, lakini sasa tuna vyama vingi lakini utofauti wa vyama hivyo zaidi ya 20 inaweza kuwa rangi za vyama lakini si itikadi.
Ukitizama msingi wa vyama vyote vya ukombozi barani Afrika havikuwa vyama vya kutafuta kura, bali ni vyama vya kutafuta uhuru na maendeleo ya kweli.
Lakini sasa tunalo tatizo hili. Kura imekuwa muhimu zaidi kuliko ajenda muhimu za wananchi. Hii inaweza ikatufikirisha zaidi kama tumefanya busara ya kuingia katika siasa hizi za ushindani, kwa kweli kuleta maendeleo au kutafuta kura katika kila miaka mitano ya uchaguzi?
Profesa Shivji katika kitabu chake cha ‘Isha za Mapambano ya Wanyonge’ anasema tumekumbatia siasa za ushindani wa vyama, siasa hii imezaa soko la kura, kura zinauzwa na kununuliwa.
Wakati fulani Professa Shivji anasema tuwe makini tusione kwamba chama ‘A’ ni cha wananchi na chama ‘B’ si cha wananchi, kwa sababu vinaweza vikawa vinawakilisha tabaka lile lile moja la walalaheri.
Kimsingi, siasa hizi ambazo hazina itikadi zinasukumwa zaidi na matukio. Na hili unaweza kuliona Afrika nzima ni siasa za matukio na si masuala.
Nadhani suala hili pia ni sehemu ya dosari au nyufa ndani ya siasa za sasa, kwa sababu wanasiasa watafanya vitu kwa kusukumwa na kura na si vinginevyo.
Ndiyo maana katika historia ya siasa zetu tumeshuhudia kila chaguzi kuja kwa miunganiko ya vyama vya kisiasa na uhamaji wa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda kingine lakini pia kumekuwa na lugha za kusomba watu katika daladala wakati wa kampeni, na kushindana nani kajaza wafuasi katika kampeni, hii inatokana na kutafuta kura, lakini mara baada ya uchaguzi kwisha, makundi hayo nayo huyaoni tena, kwa mfano Ukawa – Tanzania na Nasa – Kenya.
Hakika hizi ni siasa za marekebisho na si mabadiliko.
Siasa zimekuwa za kurekebisha tu na si kuleta mabadiliko. Kwa sababu mabadiliko ya kweli ni kubadilika kwa mfumo wa uchumi (uzalishaji mali).
Dosari au ufa huu umekuwa wa kubadili vyama na kubadili haiba za watu lakini matatizo ya wananchi yanabaki palepale.
Na huu ufa, ukiitazama Afrika unaonekana dhahiri. Nchi kutoka chama tawala kwenda upinzani au kutoka upinzani kwenda chama tawala haya si mabadiliko bali haya ni marekebisho, kwa sababu kinachobadilika pale ni watu na si mfumo wa uzalishaji mali.
Mfano, kilichotokea Zambia, Hakainde Hichilema, kuchukua nchi kutoka kwa Edger Lungu, hii haimaanishi kutakuwa na mabadiliko ya sera za uchumi, kwa sababu kilichobadilika ni rangi ya chama tu, lakini sera ni zilezile za uliberali-mamboleo.
Leo katika mfumo wa uchumi wa kibepari, siasa zinazotawala ni za mfumo huo na zipo kulinda mfumo huo. Na hoja yangu ya juu nilisema kuna ombwe la itikadi inayokusudia tu kuulinda mfumo huo wa kibepari.
Kwa hiyo kinachoonekana hapa tunafanya marekebisho lakini mfumo unabaki uleule wa kibepari. Kwa hiyo muda mwingine tunadhani chaguzi za kisiasa na kubadilishana uongozi ndiyo mabadiliko, kumbe mabadiliko ya kweli ni kubadilika kwa mfumo wa uzalishaji mali, watu wanazalisha nini? Wanazalisha kwa kutumia nini?
Na nani anafaidika na uzalishaji huo? Maswali haya yanaweza kutusaidia kujua mabadiliko ya kweli katika jamii na si siasa ya kubadili haiba za watu.
Siasa za fedha? Ufa huu hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema miaka ya 1995 kwamba siasa zao kwa maana siasa za TANU hazikuwa siasa za fedha, lakini uchaguzi wa mwaka ule wa 1995 alisema ni uchaguzi ambao fedha zitakuwa sifa namba moja ya kumpata kiongozi.
Hii pia inatufanya tutafakari kwamba siasa hizi zimebadilika na mabadiliko yake yamepoteza siasa ya ukweli, Nyerere aliuona huu ufa katika siasa zetu za kununua uongozi kwa fedha.
Kwa hiyo hii imefanya siasa zetu bila fedha imekuwa vigumu kuziendesha, na hii ina maanisha kuwa mtu anaingia kuzitafuta.
Huu ni ufa katika siasa hizi za uliberali – mamboleo. Tumekuwa tukiona walalahai na walalaheri kama vile wafanyabiashara, wanasiasa, wahadhiri na wanaharakati wakiongozana kuingia katika siasa hizi kwa sababu kuna fedha.
Kwa hiyo nani atayazungumza masuala ya bodaboda, mama ntilie au mmachiga, hakuna? Ajenda za wavuja jasho zimekuwa zikiibuliwa na wao wenyewe lakini si mifumo ya siasa iliyopo ya fedha.
Nyufa katika mwafaka wa kisiasa! Pia, kuna hoja hii ya wapinzani kutaka kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan, na wao wanaita ni kuponya taifa au kuleta mwafaka wa taifa, kwamba wanaona hali ilivyo ya kisiasa inahitaji mazungumzo na kukubaliana katika kuleta umoja huo.
Lakini nadhani tunafanya makosa kufikiri kwamba matatizo yaliyopo yanatokana na siasa. Lenin amewahi kusema kuwa katika kila mapambano ya kisiasa, kuna mapambano ya kiuchumi.
Kama hivyo ndivyo, hatupaswi kudhani kwamba siasa italeta nafuu ya jamii pekee bila kutazama hali za kiuchumi za watu.
Pia mwafaka huu unaozungumzwa ni wa nani? Unataka kufikia kundi gani? Kwa sababu dosari iliyopo na makosa tunayoendelea kuyafanya katika siasa zetu Afrika, ni wanasiasa kufikia mwafaka wa kugawana vyeo na kushindwa kuondoa hali za pengo la umaskini na utajiri kwa wananchi wao.
Uzoefu wa kisiasa unaonyesha hivyo kuhusu mgogoro wa Sudan Kusini, Mali, Libya, Guinea na Sudan. Hivyo, hii inaonyesha dhahiri kwamba tumewekeza nguvu kubwa katika umadhubuti wa kujenga vyama vya siasa kuliko ujenzi wa mfumo wa uzalishaji mali ambao ungejenga hizo siasa.
Mwelekeo si tena mfumo upi wa siasa utakaokwenda kutatua matatizo yetu ya hali za wananchi, na tumekuwa tukijadili ujenzi wa vyama na uhuru wa vyama.
Siasa zipi zinahitajika? Siasa zipi zinatufaa? Ni suala la mjadala, na tunahitaji mjadala wa siasa gani zinatufaa baada ya zaidi ya miaka 60 ya uhuru wetu?
Bado tuna uchumi duni, na siasa gani zinahitajika kuainisha vikwazo vinavyotufanya tushindwe kutoka katika shida hii?
Kutanua mjadala huu, ninaweza kusema tunahitaji siasa za ukombozi (siasa za masafa marefu) zinazokuwa na itikadi inayojali walio wengi.
Maana siasa za uliberali-mamboleo (za sasa) ni siasa zilizopo kwa kulinda masilahi ya wachache (walalaheri) wanaozitumia kupenyeza masuala yao katika nyanja mbalimbali.
Hivyo, tunahitaji siasa zisizotenganisha mwananchi na uchumi wake, na mamlaka yake katika uamuzi wa juu wa maisha yake.
Pia siasa itakayotambua kuwa jamii tuliyonayo ina matabaka na yenyewe isiwe na budi kupigania tabaka la walalahoi ambao tafsiri ya siasa kwao ni ugatuzi wa siasa-uchumi, ardhi, maji na rasilimali nyingine.
Mmachinga uhuru wa siasa kwake ni kufanya biashara zake katika eneo litakalomwingizia faida. Ukienda katika maeneo ya madini, mfano Mirerani, kule wachimbaji wadogo wa madini wanahitaji siasa itakayowahahakishia uhuru wa upatikaji wa leseni ya maeneo ya uchimbaji.
Pia mvuvi anahitaji siasa zitakazompa uhuru wa kuvua na kutawala eneo la ziwa au bahari bila vikwazo vya kodi au kuzuiwa asivue. Pia mkulima hali ya uzalishaji wake, masoko na kuondoka katika umaskini wake.
Ipo mifano inayoonyesha kuwa wananchi wamechoshwa na siasa hizi za uliberali-mamboleo zinazosukumwa zaidi na umaarufu, fedha, kura na mengineyo, kuanza hata kususia baadhi ya uchaguzi.
Tunazo changamoto katika uandikishaji wa wapiga kura lakini pia hata wanaopiga kura (turn out) wamekuwa wakipungua barani Afrika.
Hii ni ishara kuwa wananchi wanahitaji siasa zitakazoonyesha ukombozi wa maisha yao, si kila siku wanachagua viongozi lakini jamii ipo palepale. Tafsiri yake wananchi wanahitaji siasa za ukombozi.
Rai yangu, siasa ya kweli haipaswi kuishia katika uchaguzi au kutafuta kura, bali inayoainisha matatizo ya jamii katika mgongano wa kitabaka unaofanya wengi kushindwa kufaidi rasilimali za nchi na wachache kutumia fursa hiyo kuendeleza maisha yao.
Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi katika Kitengo cha Sosholojia na Ustawi wa Jamii ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
+255683961891/+255659639808