*Ameamua kuvunja kikombe, wenye nia na urais wasubiri hadi 2030
*Queen Sendiga: Wanawake tukikosea 2025 tutasubiri kwa miaka 100
*Dorothy Semu ataka kwanza awajengee wanawake uwezo kiuongozi
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Wakati ndoto za kugombea urais mwaka 2025 miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zikiyeyuka, yamekuwapo maoni tofauti miongoni mwa wadau wa siasa nchini.
Kuyeyuka kwa ndoto hizo kumekuja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutamka hadharani kwa mara ya kwanza kwamba sasa atasimama kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Kauli ya Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM inatafsiriwa kama nyundo kwa wana CCM waliokuwa wakijipanga kugombea nafasi hiyo ndani ya chama hicho.
Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wanasiasa wa muda mrefu aliyewahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa ‘The Forum for Restoration of Democracy (FORD)’, Emmanuel Patuka, anasema:
“Pazia ndani ya CCM limefungwa. Ndoto zimezimika na hapa hakuna mjadala. Samia ameamua kuvunja kikombe, hivyo wana CCM wenye nia ya kugombea urais wasubiri hadi mwaka 2030.”
Patuka ambaye chama chake, FORD, kimefutiwa usajili, anasema mustakabali wa mwanachama yeyote wa CCM atakayekaidi kauli ya Samia hautakuwa mwema.
“Ni hatari kupishana njia na mwenyekiti. Tumeshuhudia watu kadhaa wakijaribu kufanya hivyo lakini hawakufanikiwa. Ilitokea Zanzibar mwaka 2005 na kulikuwa na fununu kama hizo mwaka 2010 Tanzania Bara,” anasema bila kutaka kuingia kwa undani.
Patuka anasema hata mwaka 2020 baada ya Mkutano Mkuu wa CCM kumpitisha aliyekuwa Mwenyekiti wake, Dk. John Magufuli, kugombea tena urais, kuna mwanasiasa (anamtaja jina) hakukubaliana na hali hiyo na mustakabali wake hadi sasa haujulikani.
“Kwa hiyo hata wale vijana walioonyesha nia na kuomba uteuzi ndani ya CCM mwaka 2015, wakadhani kwamba wangeingiza tena majina yao mwaka 2025, sasa wasubiri hadi mwaka 2030,” anasema.
Takriban wana CCM 39, miongoni mwao wakiwamo vijana wenye umri chini ya miaka 40, waliomba kupeperusha bendera ya chama kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo Dk. Magufuli alishinda ndani ya chama, hivyo kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM na Samia akawa mgombea mwenza.
Viongozi wanawake wazungumza
Akizungumzia kauli ya Samia kuvunja ukimya kuhusu kugombea urais mwaka 2025, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, anasema licha ya wao kuunga mkono mgombea urais mwanamke, ameipokea kauli hiyo kwa tafsiri tofauti.
“Kama nchi ya demokrasia ya vyama vingi, tunaona urais ni kazi ya kutimiza majukumu ya wananchi, kubadilisha maisha yao na kuwaletea maendeleo chanya na tunaamini tunapochagua Rais tunakwenda kuchagua mtu yeyote kwa uwezo wake; awe mwanamume au mwanamke.
“ACT-Wazalendo tumekuwa na imani kwa wanawake. Tukiwa chama kichanga, tulimsimamisha mgombea urais mwanamke, Mama Anna Mghwira (sasa marehemu) na alifanya kampeni vizuri sana, akaungwa mkono na watu wengi ingawa kura hazikutosha,” anasema Dorothy.
Anasema ACT haitajali jinsia pale atakapotokea mgombea mwenye uwezo; na mgombea mwanamke akishinda, watamuunga mkono ili afanye kazi yake kwa mafanikio.
Akizungumzia maandalizi ya kiuongozi kwa wanawake wa Tanzania, Dorothy, anasema ukitazama kwa makini utafahamu kwamba bado kuna kazi.
“Tulitamani Samia angeutumia wakati huu kuweka misingi imara ya kuondoa sheria kandamizi na kuweka sheria wezeshi za kuwaandaa wanawake kuwa viongozi bora na kuwa na nafasi na fursa sawa pale wanapotaka kuingia katika hatamu za uongozi. Bado jamii yetu ina mfumo dume.
“Bado wanawake wanaonekana si watu wa kushika madaraka, kwa hiyo tunatakiwa kurekebisha hayo na tumuweke mwanamke katika nafasi ya kujitambua na kutambua ndoto zake na kupata nafasi yoyote ambayo angependa kushiriki kuchaguliwa tukiangalia uwezo wake,” anasema.
Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga, anasema Samia ametoa kauli ya kijasiri ikidhihirisha namna anavyojiamini.
“Ni kauli njema na inaleta matumaini. Imetoka kwa mtu anayejiamini, Rais Samia anajua nini anafanya na nini anatarajia kwenda kukifanya.
“Anafahamu nguvu tuliyonayo wanawake. Kiukweli hakuna kiongozi mwanamume aliyepo madarakani ambaye amepita bila kupewa nguvu kubwa na mkono wa mwanamke,” anasema Queen.
Mama huyu mwaka 2020 aligombea urais kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), na baada ya Samia kuchukua urais, akamteua kuwa mkuu wa mkoa. “Wanawake ndio wanapiga kampeni nyumba kwa nyumba; ndio wanasherehesha. Kwa kifupi ameongea kazi ambayo wanawake tunakwenda kuifanya.
“Kwa mtazamo wangu ni kwamba mwaka 2025 kazi ya kumuweka madarakani Samia ni nyepesi. Sidhani kama tutatumia nguvu kubwa kumnadi! Alishafanya kazi kubwa na zinaonekana, ameshasafiri sehemu mbalimbali nje na ndani ya nchi,” anasema.
Queen anasema kazi anayoifanya Samia ni kama alijiandaa kuja kuifanya, hivyo mwaka 2025 ni kumhalalisha tu kwa sababu kura zake ni kama zimekwisha kuhesabiwa.
“Tumeshafunga hesabu ya kura. Sisi wanawake ndio wengi na katika uchaguzi ndiyo tunajiandikisha wengi zaidi. Hata wanaume wasipopiga kura, sisi ni muhimu kwani hata tukipiga kura peke yetu, zinatosha kupata ushindi,” anasema.
Anadai kwamba iwapo wanawake watafanya makosa kutomchagua Samia kuwa Rais mwaka 2025, itawagharimu kwa hadi miaka 100 baadaye kupata mwanamke mwingine.
Kauli ya Samia
Ukweli kwamba kwa sasa ni kama pazia la mbio za urais ndani ya CCM limeshafungwa kwa makada na makundi yao unatokana na kauli iliyotolewa na Rais Samia wakati akizungumza na wanawake katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia.
Samia amesema Tanzania haijafanikiwa kumpata Rais mwanamke anayetokana na Uchaguzi Mkuu kwa kuwa yeye amepatikana kwa ‘kudra za Mungu’ na ‘matakwa ya kikatiba’.
“Rais mwanamke tutamweka mwaka 2025. Ndugu zangu, mwaka 2025 tukifanya vizuri, tutamweka Rais mwanamke, tutakutana hapa tufurahi.
“Wameanza kutuchokoza kwa kuandika katika vigazeti kwamba Samia hatasimama. Nani kawaambia?
“Fadhila za Mungu zikija mkononi, usiziache. Wanawake tumefanya kazi kubwa kuleta uhuru na kujenga nchi hizi, tumewabeba sana wanaume katika siasa za nchi hizi, leo Mungu ametupa baraka mikononi na tukiiachia Mungu atatulaani,” anasema Samia huku akishangiliwa na umati wa wanawake waliohudhuria maadhimisho hayo.
Awali, Aprili Mosi, mwaka huu, akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri kwa mara ya kwanza tangu awe Rais baada ya kifo cha Dk. Magufuli, Samia amenukuliwa akiwaonya wenye nia ya urais mwaka 2025 waache mara moja.
“Nafahamu mwaka 2025 upo karibu na kawaida yetu sijui kama ni Watanzania au kote ulimwenguni inapoingia kipindi cha pili cha Rais aliyepo watu kidogo mnakuwa na hili na lile kuelekea mbele, nataka kuwaambia acheni, twendeni tukafanye kazi,” anasema Samia na kuongeza:
“Hili na lile tutajua mbele, sawa ndugu zangu, tukafanye kazi, ninalotaka kuwaambia jingine ni kwamba rekodi yako inakufuata katika maisha yako. Nitakuwa na jicho kubwa zaidi kuangalia rekodi zenu na safari ya mbele yetu, kuna wengine wamekosa nafasi hizi kwa rekodi zao tu na yule mwenye nia na 2025 aache mara moja.”
Miezi mitano sasa imepita tangu alipotoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza na kuirejea wiki iliyopita huku Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo, naye anasema mwaka 2025 ni rasmi kwa kumuweka Ikulu Rais mwanamke.
“Ni wakati sasa wa wanawake wote kuungana na kutumia fursa hii kufanikisha hili na kuendelea kuandika historia Tanzania. Naamini wanaume pia watatuunga mkono maana nia ya Mama kulitumikia taifa wote tumeiona,” anasema Jokate kupitia akaunti yake ya Twitter na kuongeza:
“Lakini pia kwa kutambua wanawake tumefanya kazi kubwa kuleta uhuru wa nchi yetu, kujenga siasa za nchi yetu. Na pia kama Rais alivyosema tumekuwa chachu nyuma ya wanaume wengi kupata vyeo vya juu. Ni wakati wetu sasa. Namuunga mkono Mama, mwaka 2025 twende na Mama.”
Wengine waliozungumza kuunga mkono uamuzi wa Mama Samia kuweka hadharani nia ya kugombea urais mwaka 2025 ni Katibu wa Wabunge wa CCM, Rashid Shangazi, Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu na aliyewahi kuwa Mbunge wa Misungwi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Kitwanga anasema Watanzania wanapaswa kumuunga mkono Samia kwa nguvu zote kwa sababu ni kiongozi makini, mtulivu na mwenye maono makubwa, akiwaonya wanaotaka kujipendekeza badala ya kumsaidia.
“Kila mmoja kwa nafasi yake aendelee kumuunga mkono. Awe mkulima, mfugaji, au mfanyabiashara. Tusisubiri. Tumsaidie, tumpe ushauri ili uchumi wetu ukue kwa sababu tuna kiongozi anayesimamia sheria, kanuni na taratibu. Tunamuomba Mungu amlinde tufike mwaka 2025,” Kitwanga amenukuliwa akisema.