Maandiko Matakatifu ya dini zote yameeleza bayana jinsi Mwenyezi Mungu alivyoumba ulimwengu na viumbe hai. Yaliyoandikwa katika vitabu hivyo ni ya manufaa kwa wanaoamini, pia kwao wasioamini uwepo wa Mungu.
Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 55 (Surat Ar-Rahmaan), Aya ya 10, Mwenyezi Mungu anasema: “Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe.”
Maana ya Aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameiweka ardhi kwa matumizi ya viumbe wote wakiwamo wanadamu, wanyama, ndege, wadudu wa aina mbalimbali na viumbe wengine.
Katika Biblia Takatifu, Kitabu cha Mwanzo 1:24-28 tunasoma haya kuhusu uumbaji:
24 Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.
25 Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
26 Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.
Spika Job Ndugai, alisikika ‘akimtisha’ Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, kuhusu kukamatwa kwa mifugo inayoingizwa hifadhini. Akafikia hatua ya kusema aangalie yasimpate yaliyowapata watangulizi wake. Alifanya rejea ya yaliyomkuta shujaa wa uhifadhi, Balozi Hamis Kagasheki. Kauli ya Spika Ndugai ilikuwa ya bahati mbaya kutoka kwa kiongozi ambaye kitaaluma ni mhifadhi.
Miaka mitano iliyopita nilifanya utafiti wa mifugo inayoingizwa maeneo ya hifadhi kama Serengeti na Ngorongoro. Nililenga kujua huruma waliyokuwa nayo wabunge wakati wa Operesheni Tokomeza kama ilikuwa huruma ya kweli au kulikuwa na jambo lililofichika.
Nilichobaini ni kuwa wabunge waliopiga kelele ‘kutetea wafugaji’ wenyewe ndio waliokuwa na mamia kwa maelfu ya mifugo inayonenepeshwa ndani ya hifadhi.
Wanasiasa, viongozi wa umma na wafanyabiashara walikuwa wakinunua ng’ombe waliodhoofu kwa bei chee, kisha kuwanenepesha hifadhini kabla ya kuwauza katika masoko ya ndani na nchi jirani.
Mwezi huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Serengeti iliwahukumu kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh milioni tatu wakazi wawili walioingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Mahakama ikaamuru ng’ombe 34 na kondoo 22 wataifishwe.
Baada ya hukumu hiyo wameibuka ‘manabii’ wapinga uhifadhi wakilalamika kuhusu wafugaji kunyanyaswa. Wengine wamediriki kusema mifugo wakati mwingine inachungwa na watoto wadogo wasiojua mipaka ya hifadhi! Utetezi wa hovyo kabisa, kwa sababu kuwatumikisha watoto badala ya kuwapeleka shule ni kosa kisheria.
Kwa miaka ya karibuni, ukiacha Balozi Kagasheki, Dk. Ndumbaro ndiye waziri aliyerejesha matumaini ya uhifadhi baada ya wizara hii kunajisiwa kwa kiwango kisichoelezeka. Kila mpenda uhifadhi anayo sababu ya kumuunga mkono Dk. Ndumbaro na timu yake.
Ndugu zangu, tulipotaka mabadiliko ya Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori hatimaye tukaipata mwaka 2009, tulilenga kuona maliasili ya wanyamapori, misitu na viumbe wengine ikiendelea kuwapo.
Tulipolilia kuudwa kwa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu tulitaka wahuni na wahalifu wa aina hii walioingiza mifugo hifadhini Serengeti wakamatwe na waadhibiwe kisheria.
Jeshi la Uhifadhi limeundwa kwa sababu kuna tishio la kuharibu makazi ya wanyamapori na hata uwepo wao. Tunapolalamika watu ‘wamepotelea’ hifadhini, tuhoji pia walifuata nini humo ndani ilhali wakijua sheria haziruhusu? Tukiacha kila mtu afanye anavyotaka tutabaki na nini?
Ukiyapitia Maandiko Matakatifu unaona kuwa kabla ya kuumbwa kwa mwanadamu, Mungu aliumba viumbe hai wengine wengi, na mwishowe akawaleta wanadamu ili wautawale ulimwengu na viumbe waliomo.
Mwanadamu hakuumbwa kuwamaliza viumbe hai, bali kuhakikisha anawatawala. Kutawala hapa kuna maana ya kuhakikisha waaendelea kuwapo, maana hauwezi kutawala maiti au kutawala vitu visivyokuwapo.
Wanyamapori sharti walindwe, maana uwepo wao hautokani na matakwa au utashi wa kibinadamu, bali ni matakwa ya Mungu. Ni maua mazuri katika bustani hii kubwa na nzuri iliyoumbwa na Mwenyezi Mungu. Wanyamapori hawawezi kuachwa waonewe au wamalizwe kwa sababu tu hawawezi kujitetea. Ni wajibu wetu kujitokeza kuwasemea.
Tunajua ni kwa kiasi gani wanasiasa, viongozi na baadhi ya wafanyabiashara walivyojiandaa kumwandama Dk. Ndumbaro na watumishi waaminifu wa TANAPA, NCAA, TAWA na TFS. Tunatambua walivyojiandaa kujenga chuki alimradi waonekane wanakiuka haki za binadamu.
Miezi hii ya kiangazi kuna ng’ombe wa ndani na wa kutoka nchi jirani wanaingizwa Serengeti na Ngorongoro kwa kigezo cha kutafutiwa majani na maji.
Haiwezekani Tanzania liwe shamba la bibi aliyekufa ambalo mtu yeyote anaingia na kutoka kadiri anavyotaka. Haiwezekani wafugaji waharibu malisho na vyanzo vya maji kisha wakimbilie hifadhini kupata huduma hizo. Haiwezekani.
Naomba Dk. Ndumbaro asitishwe. Naomba wapenda uhifadhi wote tuungane kuwatetea watu wanaokabiliana na hatari za wanyama na majangili, alimradi kuhakikisha rasilimali hii ya wanyamapori na misitu inadumu milele na milele.
Tumemuona Rais Samia Suluhu Hassan akihangaika huku na kule kuvutia watalii wa ndani, hasa wa nje. Ilani ya CCM imeagiza watalii wafikie milioni tano ifikapo mwaka 2025.
Juhudi hizi zitafaa nini kama kwa upande mwingine tunageuza hifadhi kuwa malisho ya punda vihongwe, kondoo, mbuzi na ng’ombe wasio na bei katika soko la dunia? Mtalii gani atoke New York, Paris, Moscow, au Beijing aje kutazama ng’ombe na kondoo hifadhini?
Wapinga uhifadhi ni wahaini kama wahaini wengine. Wanapinga uhifadhi kwa masilahi binafsi. Wachungaji (si wafugaji) wakubali kubadilika. Wafuge kisasa badala ya kuzurura kila mahali nchini. Wanasiasa wenye masilahi binafsi wasiwe mawakala wa kuua uhifadhi.