ALGIERS, ALGERIA
Rais wa zamani wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Bouteflika ameliongoza taifa hilo la kaskazini mwa Afrika kwa takriban miongo miwili, akaachia ngazi mwaka 2019 baada ya mchakato wake wa kugombea tena urais kwa muhula wa tano kusababisha maandamano makubwa mitaani.
Katika miaka ya 1950 na 1960, alishirki kikamilifu na kwa namna ya pekee katika mapambano ya kugombea uhuru.
Mwaka 1999 wakati Algeria ilipotoka kwenye vita mbaya ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000, jeshi lilimsaidia Bouteflika kuwa rais.
Rais huyu wa zamani na maarufu barani Afrika, amekuwa akionekana kwa nadra sana hadharani tangu alipopata kiharusi mwaka 2013, ugonjwa ulioathiri uwezo wake wa kuzungumza na kutembea.
Ushiriki wake katika siasa ulianza mapema sana. Baada ya Algeria kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1962, Bouteflika akawa mmoja kati ya mawaziri wa mambo ya nje duniani mwenye umri mdogo sana; akiwa na miaka ya kati ya 20, rekodi ambayo hadi sasa haijavunjwa.
Alishikiria nafasi hiyo kwa miaka 16, na alikuwa mwanachama hai na machachari wa Umoja wa Mataifa (UN).
Akiwa Rais wa Baraza Kuu la UN mwaka 1974, alimualika Kiongozi wa Palestina, Yasser Arafat, kulihutubia baraza hilo – kitendo cha kushitukiza na hatua muhimu sana.
Pia ni katika kipindi hicho ambapo alikuwa akisisitiza umuhimu wa China kuwa na kiti UN, huku akiwa pia kinara wa kupinga siasa za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Bouteflika anakumbukwa pia kwa kumwezesha kijana Nelson Mandela kupata mafunzo yake ya kwanza ya kijeshi.
Sehemu ya miaka ya 1980, Bouteflika aliipitisha akiwa uhamishoni, akikwepa mashitaka ya ufisadi ambayo baadaye yalitupiliwa mbali.
Akarejea nyumbani miaka ya 1990 na mwaka 1999 akawa Rais wa Algeria – akiwa rais wa kwanza raia wa taifa hilo kwa zaidi ya miongo mitatu.
Bwana huyo aliyefahamika kwa kifupi kama ‘Boutef’, alifanikiwa kuleta amani kati ya jeshi na wanamgambo wa Kiislamu waliokuwa wakipambana katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Mwaka 2008 alianzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba yaliyoondoa kipengele cha mihula miwili ya ukomo wa urais – kisha mara mbili baaadaye akachaguliwa kuwa rais, mbali na kuwapo kwa madai na mashitaka ya ulaghai.
Wakati machafuko maarufu kama ‘Arab Spring’ yalipoibuka Afrika Kaskazini mwaka 2011, haraka Bouteflika akaongeza ruzuku kwa umma na kuondoa tangazo la hali ya hatari lililodumu kwa miaka mingi nchini Algeria.
Mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa mwaka 2017, miaka minne baada ya kupata kiharusi, alipokuwa akizindua kituo cha mabasi na msikiti uliokarabatiwa wa Ketchaoua jijini Algiers.
Wakati huo, nyuma ya pazia, mdogo wake Said Bouteflika, alichukuliwa kama kiongozi wa taifa hilo.
Ilipotangazwa kuwa rais huyo mgonjwa angesimama tena kugombea nafasi hiyo kwa mara ya tano mwaka 2019, maandamano yakaibuka nchi nzima kupinga hatua hiyo.
Ndani ya wiki moja maandamano hayo yakasambaa nchi nzima katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kabla.
Hata baada ya kuahidi kwamba angeahirisha uchaguzi na kisha ndani ya mwaka mmoja kujiuzulu, wananchi hawakukubali na Bouteflika akalazimishwa kuachia ngazi.
Hiyo ndiyo ikawa mara ya mwisho kwa Waalgeria kumuona mtu aliyewatawala kwa miaka 20.