RIO DE JANEIRO, BRAZIL

Afya ya mwanasoka maarufu duniani, Pele, imedorora baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe tumboni,  kisha kulazwa ICU.

Hata hivyo,Kely Nascimento, binti wa nguli huyo wa soka, amesema hali yake inaimarika.

“Ni kama amepiga hatua mbele. Anaendelea vizuri. Alirejeshwa ICU wiki iliyopita, siku tatu baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani,” anasema Kely.  

Picha za video zilizotumwa na Kely kupitia Instagram zinamwonyesha Pele akiwa mwenye tabasamu huku akifanya mazoezi madogo madogo. 

“Wanafamilia wa Instagram, naona mngependa kufahamu hali ilivyo kwa leo.  

“Kwanza amefanya mazoezi ya viungo chini ya mtaalamu wake, Dk. Adriano Barroco na msaada wa timu ya ‘Kely & Flavia Show’.

“Amepiga hatua mbili mbele leo! Asanteni sana kwa kuonyesha kujali na ujumbe unaoonyesha mapendo yenu kwetu,” anaandika Kely.

Katika picha hizo za video, Pele anaonekana akirusha ngumi hewani huku akiendesha baiskeli ya mazoezi, huku Kely akimtania. 

Mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia alitarajiwa kurejea nyumbani mara baada ya kutoka ICU katika Hospitali ya Albert Einstein, Sao Paulo, Jumanne iliyopita, lakini Ijumaa akarejeshwa tena ICU. 

Jumapili, Pele amewaandikia ujumbe mashabiki wa soka kupitia Instagram akiwataarifu akisema: “Rafiki zangu, leo nimetembelewa na ndugu zangu na kila siku ninaendelea kutabasamu. Ninawashukuru nyote kwa upendo mnaonionyesha.”  

Baadaye Kely akatuma picha akiwa na baba yake kama ushahidi kwa mashabiki wa soka kwamba anaendelea vizuri.

“Kuna wasiwasi umetapakaa duniani na sisi hatutaki kuwa sababu ya watu kuwa na hofu zaidi. Picha hii nimeipiga sasa hivi. Hapendi kuvaa fulana hii, lakini humu (ICU) kuna baridi,” anasema binti huyo.

Katika miaka ya karibuni afya ya Pele imekuwa ikikumbwa na misukosuko na mwaka 2015 alifanyiwa upasuaji wa tezi dume na kulazwa hospitalini mara mbili ndani ya miezi sita.

Alilazwa tena mwaka 2019 kutokana na matatizo ya njia ya mkojo na Februari mwaka jana mwanaye wa kiume, Edinho, alisema Pele anashindwa kutoka ndani kutokana na maumivu ya tishu za pajani. 

Mwanasoka huyo mashuhuri wa Brazil ameapa kupambana na matatizo yake ya afya kwa tabasamu la siku zote.

“Kila siku ninaendelea kuwa na furaha ile ile ya kuwa tayari kucheza dakika 90 na za nyongeza,” anasema.

Hadi sasa Pele ndiye mchezaji maarufu zaidi duniani na nchini kwake anasalia kuwa mfungaji kinara wa muda wote, akiwa na mabao 77 katika mechi 92. 

Alijitambulisha kimataifa mwaka 1958 alipoisaidia Brazil kushinda Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 17 tu; akafanya hivyo tena mwaka 1962 na 1970. 

Katika muda wa uchezaji wake wa soka, Pele amefunga mabao rasmi 757 – Klabu ya Santos inadai kuwa jumla ya mabao aliyofunga yanakaribia 1,000 – akiachwa nyuma na Cristiano Ronaldo na Josef Biscan pekee.

Kama nyongeza, wiki iliyopita Lionel Messi aliivunja rekodi yake ya mabao kwa Amerika Kusini baada ya kufunga ‘hat-trick’ kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.