Mfanyabiashara James Rugemalira ameachiwa huru baada ya kuwekwa rumande kwa miaka zaidi ya minne akikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi na mengine kadhaa yaliyokosa ushahidi.

Kuachiwa kwake kumefufua mjadala miongoni mwa Watanzania, hasa wanaokerwa na mfumo wa ucheleweshwaji wa mashauri katika mifumo yetu ya utoaji haki nchini.

Tukio la Rugemalira limepata umaarufu pengine kutokana na ukweli kuwa yeye mwenyewe ni mtu maarufu.

Akiwekwa kwenye mizani na wenzake waliobambikiwa kesi, miaka minne inaweza kuonekana si kitu mbele ya wale walio magerezani kwa miaka hadi 10 au zaidi.

Mara zote katika JAMHURI tumetoa mwito kwa mamlaka ya utoaji haki nchini kufanya kila linalowezekana ili kuwabaini na kuwaachia huru watu wanaoteseka magerezani bila hatia.

Bahati nzuri uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan uliliona jambo hili kama miongoni mwa dosari kubwa katika suala zima la utoaji na upatikanaji haki nchini. 

Tangu aingie madarakani miezi sita sasa, Rais Samia, kupitia kwa mamlaka za kisheria, amesaidia kuachiwa huru watuhumiwa wengi wa kesi za aina mbalimbali.

Pamoja na hatua hiyo, ukweli unabaki kuwa watu wengi sana bado wako rumande wakikabiliwa na kesi za kusadikika. Rais amekwisha kuliamuru Jeshi la Polisi liwaachie huru watu waliobambikiwa kesi, lakini hakuna taarifa za wazi kwa umma juu ya utekelezaji wa maagizo hayo halali kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Tunao ushahidi wa vilio vya watu wanaolalamika kuonewa wakiwa ndani ya magereza. Baadhi yao tumekuwa tukichapisha taarifa zao mara kwa mara. Wapo walioachiwa, lakini wapo wengi bado wanateseka magerezani.

Tunarejea mwito wetu kwa vyombo vya utoaji haki kufanya mapitio magerezani kote ili watu wasio na hatia waachiwe huru wafaidi haki yao ya msingi ya kuwa huru.

Haki isionekane kutazamwa zaidi kwa watu wenye majina na ukwasi, na kuwapita kando wale ambao hawana wa kuwasemea. 

Tunaamini kwa msimamo wa Rais Samia, tutaendelea kushuhudia haki ikitendeka kwa uwazi na kwa kasi ili wote waaoteseka kwa hila na uonevu waachiwe huru.

Tuyafanye haya tukitambua kuwa vitabu vitakatifu vinahimiza suala la haki kwa wanadamu wote. Wenye makosa wahukumiwe kulingana na matendo yao, na wenye haki wawe huru. Mungu Ibariki Tanzania.