DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Mtibwa Sugar wamelifunga dirisha la usajili kibabe sana. Wamesajili majembe ya maana. Msimu ujao siwaoni tena katika nafasi za mwisho kwenye msimamo wa ligi.
Siku moja kijiweni kwetu Kinondoni niliwahi kumwambia mmoja wa wachezaji wa Mtibwa Sugar ambaye ni rafiki yangu kuwa watashuka daraja. Rafiki yangu yule hakunielewa. Alinishangaa na kubaki kucheka.
Sababu yangu ilikuwa nyepesi tu, Mtibwa Sugar haikuwa na wachezaji wa maana katika kikosi chake. Walikuwa na kundi kubwa la makinda wenye vipaji, lakini wakashindwa na mikikimikiki ya ligi. Wamenusurika kushuka daraja mara mbili mfululizo.
Msimu huu wamekuja na sura tofauti. Wamefanya usajili mzito kikosini mwao. Naamini waliosajiliwa watakwenda kuwaongezea kitu pamoja na makinda wao inaowapandisha kila msimu.
Msimu ujao sitegemei kumuona msemaji wao, Thobias Kifaru, akitoka hadharani kuomba waombewe dua ili wasiteremke daraja. Wamesajili mastaa wa kurudisha heshima na makali ya timu.
Umewaza pacha ya Abdi Banda na Ibrahim Ame pale nyuma, kisha katikati ya uwanja wakawapo Steven Nzegemasabo, Said Ndemla na fundi Joseph Mkele?
Usajili walioufanya Mtibwa Sugar msimu huu ndio usajili wa hadhi yao. Tumezoea kuwaona wakiwanunua mastaa kwa bei rahisi kisha wanakuja kuwauza kwa bei ghali.
Nyakati zile walipokuwa wanazilisha mastaa timu za Simba na Yanga hawakuzilisha kwa bahati mbaya, walikuwa na mastaa kweli katika timu yao.
Mtibwa Sugar wana muda hawajafanya biashara na timu za Kariakoo. Angalau msimu uliopita waliwauzia Yanga Dickson Job, Kibwana Shomari. Biashara ya mwisho kabla ya biashara hii waliwauzia Yanga Andrew Vincent ‘Dante.’
Biashara ya kuwauzia wachezaji Simba mara ya mwisho ilikuwa Hassan Dilunga. Miaka mitano iliyopita walifanya nao biashara ya Shiza kuwauzia Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim ‘MO’. Mtibwa Sugar haikuwa hivi.
Kila mwishoni mwa msimu walikuwa wanafanya biashara na matajiri wa Kariakoo.
Unapoona Mtibwa Sugar wanapitisha miaka miwili bila kuuza mchezaji Simba au Yanga, kuna tatizo mahala. Unaona tatizo zaidi unapoona misimu miwili iliyopita wamenusurika kushuka.
Sasa ni wakati wa kuwapa jicho tulivu Mtibwa Sugar. Usajili wao wa msimu huu utakuwa na majibu katika maswali mengi tuliyokuwa nayo.