Mwaka 2013 nikiwa Geita nilibanwa tumbo; hali iliyonifanya niende katika zahanati ya madhehebu ya dini iliyokuwa jirani.
Nilipokewa na kutakiwa nitoe maelezo ya jina, umri, ninakoishi na dini. Hii haikuwa mara ya kwanza kuulizwa swali hilo katika zahanati na hospitali, hasa za aina hiyo.
Tofauti na huko kwingine, hii ya Geita nilijikuta ninahoji faida za dini yangu kuandikwa kwenye karatasi ya matibabu. Nikagoma kutaja dini. Baada ya mvutano wa dakika kadhaa, nikalipa na kuondoka bila kutibiwa.
Nilipomweleza mwenzangu alinishangaa. Akaniambia: “Kujua dini yako ni suala muhimu, kwa sababu mgonjwa unaweza kufa ghafla, na hawajui umetoka wapi, unadhani utazikwa namna gani? Wakijua dini yako utazikwa kwa mujibu wa imani yako.”
Majibu ya huyu rafiki yangu niliyapuuza, na ninashukuru nimeendelea kuyapuuza. Yawezekana dini na makabila vilitumika wakati wa ukoloni kufanya utafiti wao, lakini kwa mwingiliano wa leo sidhani kama sababu hizo bado zina uhalali. Dini inasaidia kujua kwanini unaugua vichomi? Dini inasaidia nini kumtibu mwenye minyoo?
Nilidhani kama ni suala la kusaidia, basi badala ya dini ningeulizwa namba za simu walau mbili za watu walio karibu nami ili likitokea lolote wajulishwe.
Nimekumbuka tukio hili baada ya kukutana na kituko cha aina hiyo katika kituo cha polisi nilikokwenda kuwadhamini ndugu zangu. Pamoja na jina, umri na makazi, nilitakiwa pia nieleze dini na kabila langu! Kwenye dini na kabila nilifanya kama nilivyofanya Geita.
Polisi wanauliza dini yangu ili iwasaidie nini? Wanafanya sensa ya kujua dini gani inajihusisha na uhalifu? Hata kama ni hivyo, wanatafuta takwimu hizo ili zipelekwe wapi na kwa matumizi gani? Hizi ni taratibu za kikoloni.
Watanzania tunajivuna kuwa taifa la pekee miongoni mwa mataifa ya Afrika tuliofaulu mno kwenye suala la kuoleana. Ni kawaida mno kwa mwenyeji wa Songea, ama kuoa, au kuolewa Mara. Haishangazi hata kidogo mwenyeji wa Pemba kumuoa binti kutoka Kigoma. Tumeona vijana wa Kilimanjaro wakipata wenza wao Mtwara. Mifano ya aina hii ni mingi sana.
Haya yamewezekana kutokana na misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu. Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, shule za sekondari za kitaifa, mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na uhuru wa kila Mtanzania kuishi mahali popote nchini alimradi havunji sheria.
Tumekwenda mbali zaidi. Vijana wa madhehebu tofauti waliopendana wakiona dini ni mtihani kwao, wanakwenda bomani – kisha kila mmoja anaendelea na imani yake.
Kwa ufupi, kuoleana kwa Watanzania kumevuka vizingiti vya makabila, kanda, mikoa, rangi, dini na kadhalika. Wale waliozuru mataifa mengine ya Afrika watakiri kuwa vijana wengi wa Tanzania ni vigumu mno kuwatambua makabila yao kwa kuwatazama sura. Hii imetokana na ukweli kuwa wengi ni machotara waliotokana na kuoleana kwa makabila tofauti.
Ni kwa sababu ya kuoleana makabila tofauti, kizazi cha sasa cha Watanzania kimejikuta kikiwa kwenye aina nyingine kabisa ya kijamii. Lugha inayowatambulisha Watanzania hawa wapya imebaki kuwa Kiswahili. Mimi wanangu hawajui lugha ya asili ya upande wangu, pia hawajui lugha ya asili ya upande wa mama yao.
Hapo kwenye kupotea kwa lugha za baba na mama ndipo kwenye hoja yangu inayohoji kigezo cha polisi kuuliza makabila ya Watanzania wa leo.
Kabila ni utamaduni. Lugha ni utamaduni. Mtoto ambaye hajui Kizaramo (lugha ya baba) na Kihaya (lugha ya mama) – huyo si Mzaramo, na wala si Mhaya. Kigezo cha baba kuwa Mzaramo hakiwezi kuhalalisha mtoto kuwa Mzaramo hata kama hajui mila na desturi za Kizaramo.
Waasisi wa nchi yetu walipofika hapo wakaona mtoto aliyezaliwa na wazazi hawa wawili, kwa stahiki zote, huyu ni Mtanzania. Tena sasa tumekwenda mbali zaidi, kwa kuwa tayari hao kizazi chetu tunao wajukuu.
Kama ilivyokuwa kwa sisi wazazi wao, watoto na wajukuu wetu nao wanaoleana na Watanzania wa kutoka sehemu tofauti kabisa na walipo. Kama hivyo ndivyo, hawa watoto na wajukuu nani anaweza kwa usahihi kujua makabila yao?
Fikiria, trafiki anamkamata dereva kwa kosa la usalama barabarani na katika maelezo anataka ajaze hadi sehemu inayotaka kujua dini na kabila la dereva.
Umuhimu hasa wa kujua dini na kabila la dereva kwenye kosa kama hili ni upi? Tunafanya sensa kujua dini na kabila linalovunja sheria za usalama barabarani? Tukishajua, itasaidia nini?
Haya mambo ya udini na ukabila si ya kuyaendekeza. Tayari kuna vituo vya mafuta ambavyo kwa mazingira ni kama vinalazimisha wafanyakazi wawe wa madhehebu fulani. Vipo na vinajulikana.
Tumeanza kuona mabasi ya kampuni fulani fulani yakisimama abiria wapate chakula katika hoteli za madhehebu yanayoendana na wamiliki, au wakati mwingine wafanyakazi wa mabasi hayo.
Haya mambo yapo, yanaonekana na yameachwa yaendelee kana kwamba ni ya maana. Sote tunao wajibu wa kutokomeza vimelea hivi vya udini na ukabila. Itapendeza polisi waanze kuondoa kwenye fomu zao maswali ya kabila la mtu, na hata dini. Vitambulisho vya NIDA vinatosha.