DAR ES SALAAM
Na Regina Goyayi
Mwanamuziki wa ‘hip hop’ na rapa maarufu nchini, Rosary Robert a.k.a Rosa Ree, amesema ubovu wa mazingira ya kazi umemfanya avunje mkataba na lebo moja ya Afrika Kusini.
Rosa Ree ameliambia JAMHURI kuwa mkataba aliokuwa nao ulimfunga, hivyo kumchelewesha kuwa karibu na mashabiki, ambao kwa upande mwingine ndio waajiri wake.
“Kuna wakati nilifika nikaona kuwa nitakuwa ninachelewa kuwapa mashabiki kile wanachokitaka. Hii ni kwa sababu unapofanya kazi chini ya mtu, hata kipaji unachotaka kukionyesha kwa mashabiki kinalazimika kuendana na mipango ya hao walio juu yako na si wewe mwenyewe.
“Pia katika kampuni yao kulikuwa na vinaendelea miongoni mwao vilivyosababisha mimi kuchelewa kuwaletea mashabiki vitu wanavyotamani kutoka kwangu.
“Kwa hiyo nikaona ni vema tukae chini kujadiliana na hao watu wa Afrika Kusini. Nikawaomba, kwa kuwa muziki kwangu ndiyo kila kitu, kwa hiyo siwezi kuwachelewesha mashabiki. Hawa ndio mabosi wangu.
“Tukafikia makubaliano, tukaweka mambo sawa na mimi nikaendelea na michongo yangu ninayoifanya hadi sasa,” anasema Rosa Ree.
Anasema kuvunja mkataba ni suala zito kidogo, lakini baada ya kujitafakari kwa makini, aliona ni vema kufanya hivyo kuliko kupotea kabisa kwenye tasnia ya muziki ndani na nje ya nchi.
“Ukiwa na mkataba na watu huwa si rahisi sana kuuvunja hadi mtakapokuwa mmekubaliana na kila upande kuridhia makubaliano hayo.
“Mara nyingi mikataba ina vitu vingi na ule mkataba wangu kuna vitu vilivyokuwa vinanichelewesha huku mashabiki wakiniuliza sababu ya kuchelewa kutoa vitu vipya, nikaona ni bora nifanye kazi zangu mwenyewe,” amesema.
Kwa sasa Rosa Ree anasema hafahamu kama yupo tayari au hapana kufanya kazi chini ya lebo yoyote, akitilia mkazo umuhimu wa kufanya kazi kwa uhuru zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
“Lakini inategemea. Unaweza kufanya kazi na lebo fulani kama makubaliano yanatoa faida stahiki kwa kila upande. Kila mtu anafaidika kulingana na kile anachokifanya. Kikubwa ni makubaliano,” anasema.
Kuhusu chanzo cha yeye kuimba nyimbo zilizozoeleka kuimbwa na wanaume, maarufu kama ‘hardcore’, Rosa Ree amesema ni kutokana na watu kumwambia kuwa kwa kuwa yeye ni mtoto wa kike, hawezi kuimba nyimbo ‘ngumu’.
“Ni hisia tu. Kwamba walinichukulia kuwa kwa kuwa mimi ni msichana siwezi au sifai kuimba nyimbo hizi. Lakini mimi ninajiamini. Nikasema ninaweza, pia nikawa tayari kuweka ushindani kwa walionitangulia.
“Nashukuru Mungu, nilipotoa wimbo wangu wa kwanza mashabiki wakanikubali na kunipa nafasi, kitu ambacho kimefanya niwape nafasi mabinti wengine ambao wanatamani kufanya muziki kama mimi.
“Wale waliokuwa wananinyooshea kidole wakisema mtoto wa kike hawezi kufanya muziki wa aina hii, sasa nimeondoa fikra hizo potofu zilizokuwa vichwani mwao,” anamaliza Rosa Ree.