DODOMA
Na Javius Byarushengo
Ule usemi usemao ya kale ni dhahabu si wa kupuuza hata kidogo. Ulikuwa na maana, unaendelea kuwa na maana na utaendelea kuwa na maana.
Katika miaka ya nyuma, hususan katika Awamu ya Kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na Awamu ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi, palikuwapo mifumo ya balozi wa nyumba kumi.
Kimsingi, Mwalimu Nyerere kuasisi mifumo ya namna hiyo mbali na malengo ya kujenga umoja wa kijamaa, lakini ilisaidia pakubwa kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
Nasema mifumo hiyo ilisaidia kuimarisha usalama kwa maana kwamba balozi alikuwa anao uwezo wa kuwamudu watu wake katika nyumba kumi.
Ni kupitia mfumo huo wahusika wa nyumba hizo chini ya kiongozi wao ambaye ni balozi waliishi kwa umoja huku wakijuana mmoja baada ya mwingine.
Ni mfumo ambao ulisaidia kuelewa changamoto za kila mmoja, ikiwamo kutatua migogoro ya familia pamoja na usalama wao.
Kwa kutumia mfumo huo ilikuwa ni rahisi kuelewa mienendo ya kila mmoja kitabia na kimaadili na hata kama angelikuwa mgeni familia inayohusika na mgeni huyo ililazimika kutoa taarifa za mgeni huyo huku ikijulikana amekuja kufanya nini na atakaa kwa muda gani.
Endapo angejitokeza mgeni aliyekosa maelezo ya kujitosheleza, hatua fulani fulani zilichukuliwa dhidi yake, ikiwamo kuelewa malengo yake na ikiwezekana kumtia chini ya ulinzi.
Baada ya mfumo huo wa balozi wa nyumba kumi kupigwa teke, kwa nyakati tofauti pamekuwa pakiibuka matukio ya uhalifu ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara.
Wizi, ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha ni miongoni mwa matukio mabaya kabisa ya uhalifu kwani hulenga mali za wahusika na wakati mwingine watu kupoteza uhai kwa kuuawa na majambazi hayo.
Wakati mwingine uhalifu huu huibuka kwa kasi ya ajabu kutokana na mfumo wa nyumba kumi kutokuwapo.
Leo hii mtu anaweza kwenda kutembea kijijini tena sehemu ya ugenini lakini ajabu hakuna mtu anayemuuliza kuwa anakaa kwa nani na amekuja kufanya nini, hivyo kutoa nafasi kwa mgeni kuyasoma mazingira, hivyo kupanga michongo ya wizi, ujambazi au unyang’anyi wa kutumia nguvu.
Si vijijini peke yake kuna hali ya kutowahoji wageni bali hata mijini na huko hali ndiyo mbaya zaidi, kwani watu walio wengi wako ‘bize’ kujitafutia riziki bila ya kufuatilia masuala ya usalama wao.
Ndiyo siku hizi kuna watendaji wa vijiji lakini sina uhakika kama wanao uwezo wa kutambua mtu mmoja mmoja anakaa wapi na anafanya nini kwa kuzingatia kuwa baadhi ya familia zinao watu wengi.
Sina uhakika kama mtendaji anaweza kuwatembelea watu wake kila siku kuelewa changamoto zao kama ilivyokuwa rahisi kwa balozi kuongoza nyumba kumi.
Sina uhakika kama siku hizi wageni wanaokuja katika himaya ya ofisa mtendaji wa kijiji wanakwenda kuripoti kwake kama ilivyokuwa kwa siku za nyuma kipindi mabalozi wa nyumba kumi wakiwa na nguvu.
Ndiyo, siku hizi kuna polisi jamii lakini sina uhakika kama mfumo huo unajitosheleza kulingana na wingi wa watu waliopo.
Ndiyo, serikali kwa kiasi fulani imejitahidi kujenga vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali, lakini na hilo halitoshi kwani idadi ya maofisa na askari polisi haiendi sambamba na wingi wa watu waliopo nchini.
Si kazi rahisi serikali kuwa na uwezo wa kuweka polisi wa kutosha walau kila watu 100 kuwa na polisi mmoja na likitokea itachukua muda mrefu.
Je, nini kifanyike ili kuondoa changamoto hii ya kiusalama hususan katika nyakati hizi ambazo watu wanaongezeka kwa kasi, ajira kiduchu na teknolojia inayoweza kuongeza uhalifu ikikua kwa kasi?
Jibu si rahisi, lakini kinachoweza kufanyika ni kurejea matumizi ya mifumo ya nyuma hata kama si kuanzisha upya uwepo wa mabalozi wa nyumba kumi.
Watu wanaokaa katika eneo moja, iwe majirani, shinani au kijiji hawana budi kujuana na kufuatiliana mienendo yao.
Watu hao wanaoishi kwa pamoja hawana budi kujiwekea utaratibu wa kutambulisha wageni katika mamlaka husika kwa lengo la kuzuia uhalifu.
Kwa mgeni wasiyemuelewa au wanamtilia shaka, hawana budi kutoa taarifa zake kwa mamlaka husika, ikiwamo uongozi wa serikali ya kijiji au kwenye vyombo vya ulinzi na usalama hususan kwenye vituo vya polisi vilivyo karibu nao lakini hata kama vituo viko mbali kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano kupitia simu za mkononi wanaweza kupiga simu.
Wananchi wanaoishi kwa pamoja hawana budi kufuatilia tabia na mienendo ya watu wao na ikiwezekana wakimtilia shaka mtu fulani hata kama anao umaarufu, watoe taarifa kwenye mamlaka husika ili uchunguzi ufanyike dhidi yake, kwani serikali ina mkono mrefu.
Ni dhahiri Mwalimu Nyerere aliposema kila raia awajibike kulinda usalama wa nchi alikuwa na malengo mazuri.
Mwananchi anapotoa taarifa za uhalifu mapema katika mamlaka husika tayari naye anakuwa ni askari kwa kitendo hicho kwani kupitia taarifa hiyo uhalifu utadhibitiwa.
Mwananchi anapofuatilia mienendo ya mtu fulani na kubaini kuwa anayemfuatilia anatenda uhalifu, hivyo akatoa taarifa anakuwa amegeuka askari kwa taarifa hizo ambazo zitachochea usalama.
Wananchi hususan wazazi katika familia wanapowajibika kukemea vitendo vya uhalifu kwa watoto wao, wanakuwa wamegeuka askari kwa kuzuia uhalifu huo usitendeke.
Viongozi wa dini wanapotoa mahubiri yao yakasaidia kupunguza uhalifu wanakuwa wamegeuka askari wa kulinda usalama wetu.
Tukio lililotokea Jumatano Agosti 25, 2021 ambapo mtu mmoja jijini Dar es Salaam katika eneo la Ubalozi wa Ufaransa aliwaua kwa kuwashambulia risasi askari polisi watatu na askari mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, hakika tukio hilo mbali na kutuhuzunisha lakini pia liamshe hisia, fikira na mitazamo yetu kuhusu ulinzi na usalama wetu.
Ni dhahiri licha ya jukumu la ulinzi na usalama wa nchi kuwa mikononi mwa vyombo vya dola, lakini na wananchi kwa upande wao wakiongeza ushiriki, itasaidia kutokomeza uhalifu.
[email protected], 0756 521 119