TABORA

Na Moshy Kiyungi

Miaka 50 ni utu uzima na kuna watu wanapofikisha umri huo huchoka. Lakini hali hiyo haipo kwa Anna Mwaole, mkongwe wa muziki mwenye umri wa miaka 56 sasa.

Ni mwanamuziki aliyepita katika bendi na vikundi mbalimbali, akiimba nyimbo za muziki wa dansi sambamba na taarabu.

Hii ni mbali na vipaji vyake vya ziada vya uigizaji na kucheza ngoma za asili.

Kuna watu yawezekana hawamfahamu mama huyu.

Kwa umbo lake, huwezi kuamini anayoyafanya jukwaani.

Asili yake ni Iringa, lakini historia yake inaanzia Mpwapwa mkoani Dodoma, ambako ndiko alikozaliwa mwaka 1965.

Akiwa kigori, alihusudu uimbaji wa mwanamuziki wa kike wa DRC, Marikirala Mboyo ‘M’bilia Bel’.

Ni huyo ndiye aliyesababisha Anna aanze kujifunza kuimba hadi akafahamu.

Miaka ya 1980 akiwa na mwanamuziki mwingine maarufu, Rahma Shari, walijiunga na kwaya ya kanisa moja la Mpwapwa na kuwa waimbaji wa kutegemewa.

“Jina la awali la Rahma ni Grace. Alikuwa Mkristo akabadili dini alipoolewa na Muislamu,” anasema Anna.

Naye baadaye akaolewa na Rashidi Nyambya, akasilimu na kuchagua jina la Sauda.

Anasema ni Rahma ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa yeye kuingia katika muziki wa dansi baada ya kuhamia Dar es Salaam mwaka 1988.

Wakati huo Rahma alikuwa Maquis du Zaire, akamuombea nafasi ya kazi katika bendi hiyo.

Baada ya usaili ambapo aliimba vema wimbo wa ‘Nakei Nairobi’ wa M’bilia Bel na ‘Kama Umenichoka Mpenzi’ wa Issa Nundu, akapata kazi katika bendi hiyo.

“Kuimba ‘Nakei Nairobi’ ilikuwa rahisi sana kwangu kwa kuwa tayari nilishaziimba sana nyimbo zote za M’bilia Bell tangu  nikiwa Mpwapwa,” anasema.

Anasema aliimba vizuri na kuwaacha midomo wazi wakongwe wa Maquiz, akina Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Nguza Mbangu ‘Vicking’ na Tshimanga Kalala Assosa.

Anakumbuka kuwa siku ya kwanza kupanda stejini na Maquis du Zaire, alitetemeka sana alipoambiwa kuimba mbele ya mashabiki katika ukumbi wa Wapi Wapi’s Bar, Chang’ombe Maduka Mawili.

“Wingi wa mashabiki ulinitisha. Nilitamani ardhi ipasuke,” anasema Anna au Sauda.

Mungu akampa ujasiri na kuimba kwa umahiri mkubwa hata ule wimbo alioshirikiana na Issa Nundu.

Lakini ni wimbo wa ‘Nakei Nairobi’ ndio uliowanyanyua mashabiki vitini wakishangilia na kumtuza pesa nyingi, wakisema wamepata M’bilia Bell wa Tanzania.

Septemba 1989 akajiunga na Polisi Jazz, hivyo kwenda ‘depo’ (mafunzo za kijeshi) kwa miezi mitatu, Kilwa Road jijini Dar es Salaam.

Akiwa na bendi hiyo alitoka na wimbo wa ‘Sitaki Sitaki Visa Vyako’ uliotungwa na Mobari Jumbe.

Muda si mrefua Anna akaondoka Polisi Jazz na kujiunga na Bantu Group chini ya ‘Mzee wa Madongo’ Komandoo Hamza Kalala.

Huko akakutana na akina Muumini Mwinjuma, Musemba wa Minyungu, Rogers na wapiga gitaa Magele Sange na Ali Adinani.

Safari yake haikuishia hapo kwani mwishoni mwa mwaka 1991, alijiunga na Orchestra Makassy ya Mzee Kitenzogu Makassy.

Mwaka mmoja baadaye akajiunga na Legho Stars iliyokuwa na wakali akina Joseph Mulenga ‘King Spoiler’(solo), Anania Ngorika, Kapaya Vivi na Chibanda Sonny.

Bendi hiyo ikasambaratika naye akahamia La Capitale iliyokuwa ikimilikiwa na Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’.

Nyota yake ikamuangazia zaidi Januari 1993 alipojiunga Washirika Stars ‘Watunjatanjata’ ambako akina Madaraka Morris, Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, Eddy Sheggy, Christian Sheggy na Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ walikikuza zaidi kipaji chake.

Kati ya mwaka 1993 hadi 1995, Anna alikuwa Tanza Muzika iliyokuwa ikimilikiwa na Elvis Musiba, mfanyabiashara na mtunzi wa vitabu maarufu wa miaka hiyo.

Huko alikutana na François Makassy ‘Makassy Junior’, Kasongo Ilunga na Chibanda Sonny.

Baadaye akajiunga na Shikamoo Jazz ya jijini Dar es Salaam, ambako aliwakuta akina Salimu Zahoro, John Simon, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ na Majengo Selemani.

Alibahatika kusafiri hadi Kampala, Uganda, lakini baada ya miezi sita aliiacha bendi hiyo na kutimkia Matimila iliyokuwa ikiongozwa na Dokta Remy Ongalla.

Baadaye akajiunga na Super Volcano, iliyokuwa ikiongozwa na Taji Mbaraka, binti wa Mbaraka Mwinshehe Mwaruka.

Sifa zake za kupitia Jeshi la Polisi zilimpa nafasi kubwa ya kupata kazi Magereza Jazz Februari 1998.

Huko alitoa kibao cha ‘Samahani Baba Watoto’ akishirikiana na akina Makoye Kwirukwira, Sharifa Bernard na wengineo.

Safari yake ikimfikisha Vijana Jazz, bendi ya Jumuiya ya Vijana wa CCM na kukutana na akina Suleiman Mbwembwe, Freddy Benjamin, Abdallah Mgonahazelu na mwana dada wakati huo Nuru Muhina ‘Baby White’.

Ilikuwa mwaka 2001 ambapo msanii maarufu wa kucheza na nyoka, Norbert Chenga, alipomchukua Anna katika kikundi cha Muungano Dancing Troupe.

Huko akatakiwa kuzifanyia mazoezi nyimbo za taarabu za ‘Mtu Mzima Ovyo’, ‘Hata Mkisema’, ‘Sanamu ya Michelini’ na nyingine nyingi alizokuwa akiziimba Nasma Hamis aliyekuwa ameondoka Muungano.

Akazitendea haki nyimbo hizo na mashabiki kukubali kuwa pengo la Nasma limezibika.

Mbali na kuimba taarabu akiwa Muungano, Anna a.k.a Sauda pia alikuwa akicheza sarakasi na ngoma za asili ndani ya kikundi hicho.

Mwaka 2004 aliachana na Muungano baada ya kutoelewana katika masilahi mwaka 2006 akaomba kurudi La Capitale ya King Kiki, alikubaliwa japo alifanya kazi kwa muda mfupi akaamua kwenda kupiga muziki katika hoteli za kitalii Unguja mwaka 2007.

Mkataba ulipomalizika, akajiunga na Bana Maquis ya Assosa akiwa na mkongwe Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’.

Anna baadaye akaitwa kujiunga na Super Kamanyola ya Mwanza ambako alikutana na wakali wengine katika uimbaji akina Mukumbule Lolembo ‘Parash’ na Benno Villa Anthony. Alipiga muziki na bendi hiyo kwa miaka miwili, akarejea Bana Maquis.

Sauda (Anna) Mwaole amekwisha kutengeneza albamu ambayo anasema bado ipo jikoni ikikolezwa viungo kabla ya kupakuliwa hivi karibuni.

Huyu ni mama wa watoto watatu; mmoja kati yao amekwisha kutangulia mbele ya haki. Walio hai ni Mariam na Kassim ambaye ni mwimbaji.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba: 0713331200, 0784331200 na 0767331200.