ZANZIBAR
Na Rajab Mkasaba
Tangu kuanza kazi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ya Awamu ya Nane Novemba 2020 hadi Julai 2021, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kukusanya miradi 50 yenye jumla ya mitaji ya dola za Marekani milioni 321.
Hali hii inaonyesha kuwapo mwamko mkubwa wa wawekezaji wanaokuja kuwekeza Zanzibar kutokana na mikakati ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ya kuimarisha na kuvutia uwekezaji nchini.
Miradi hii inatarajiwa kutengeneza ajira 3,590 kwa wananchi na kupatikana kwake kutawezesha kufikiwa malengo ya ahadi ya Rais Dk. Mwinyi wakati wa kampeni za uchaguzi ya kuongeza ajira 300,000 kufikia mwaka 2025.
Katika kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji Zanzibar na kupunguza urasimu wa taratibu za kuwekeza, ZIPA imeimarisha kituo kimoja cha huduma (One Stop Center) ndani ya ofisi zake, ambapo huduma zote zinazohusiana na uwekezaji Zanzibar zinapatikana hapo.
Aidha, baadhi ya huduma kama vibali vya kazi (work permit) na vibali vya kuishi nchini (resident permit) kwa sasa zinatolewa kituoni hapo kwa wageni ndani ya siku moja tu, iwapo vigezo vyote vimekamilika.
Katika suala la kuutangaza uwekezaji Zanzibar, ZIPA inajiandaa kushajihisha uwekezaji katika maeneo mbalimbali yakiwamo Uwekezaji wa Uchumi wa Bluu katika uvuvi wa Bahari Kuu, ufugaji wa samaki na mazao mengine ya bahari, utalii, uwekezaji katika visiwa, usafiri wa baharini na biashara, utafiti na maendeleo.
Pia ZIPA imejipanga kuongeza wigo wa mataifa ya Ulaya, Mashariki ya mbali, Afrika Mashariki na Kati na kukaribisha uwekezaji wa viwanda, kilimo, teknolojia ya habari, nishati mbadala na miradi katika maeneo huru ya uchumi.
Hivi karibuni Rais Dk. Mwinyi alifungua mradi wa Hoteli ya Zanzibar Executive Suite (Airport Hotel) Golden Tulip, iliyopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), eneo lililokuwa likimilikiwa na ZIPA kama sehemu ya Bandari Huru.
Kutokana na umuhimu wa mradi huu, serikali kupitia ZIPA, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamisheni ya Ardhi na taasisi nyingine kadhaa, imefanikisha kutolewa kwa eneo hilo kisheria na kupatiwa eneo jingine mbadala kwa ajili ya Bandari Huru.
Dhana nzima ya mradi wa ujenzi wa hoteli hiyo ya kisasa ni kutoa huduma kwa wageni wanaopita kiwanjani hapo (Transit Passengers), wageni wanaoingia nchini kwa shughuli mbalimbali zikiwamo za utalii na wageni wengine wowote watakaohitaji huduma kutoka hotelini hapo.
Hoteli hiyo aliyoizindua Rais ina hadhi ya nyota tano, ambapo pia mradi huo umeingia dhana mpya ya utalii ijulikanayo kwa jina la ‘MICE’, yenye maana ya (Meetings Incentives, Conferences and Exhibitions/Events) yaani utalii wa mikutano, vivutio, mikutano ya kimataifa na maonyesho.
Mradi huo wa ujenzi wa hoteli ya kisasa ulithibitishwa na ZIPA Desemba 31, 2015 awali ukiwa na mtaji wa makisio ya dola za Marekani milioni 7, mradi ambao unamilikiwa na Royal Group of Companies, chini ya umiliki wa Mohamed Raza Hassan (hisa 90%) na Hassan Raza Hassan (hisa 10%); wote ni raia wa Tanzania.
Dhana hii itasaidia kupanua wigo wa sekta ya utalii na kuacha kutegemea utalii wa hoteli za fukwe pekee. Hivyo basi, eneo lililojengwa hoteli hiyo halina fukwe, lakini dhana ya mradi pekee inavutia utalii wa daraja la juu.
Lengo na madhumuni ya ujenzi wa hoteli karibu na maeneo ya uwanja wa ndege ni kusaidia kupata malazi karibu na uwanja wa ndege, hasa kwa wasafiri wa usiku sana au alfajiri, wafanyakazi wa ndege (cabin crew) na abiria ambao ndege zao zinachelewa kuruka (long delays) au safari zao zimefutwa (cancellations).
Kwa wakati uliopo hoteli za kulaza wageni jirani na viwanja vya ndege si chaguo, bali ni sehemu muhimu ya huduma za usafiri wa anga.
Hoteli hii imejengwa kwa kuzingatia masharti na ubora unaohitajika kwa hoteli ya uwanja wa ndege kama kuwapo vioo vya madirisha kuzuia kelele za ndege.
Kuna mfumo wa kuzima moto ambao ni wa kiwango cha kisasa unaokubalika kwa majengo yaliyopo jirani na viwanja vya ndege. Kuna vifaa maalumu vya ukaguzi kwa wageni wanaoingia katika eneo la hoteli kama kwamba wameingia katika eneo la uwanja wa ndege, hii ni kwa ajili ya usalama; suala linalopewa kipaumbele kikubwa.
Katika hotuba yake ya kutimiza siku 100 aliyoitoa Februari 2021, Rais Dk. Mwinyi alieleza jinsi anavyofahamu kwamba ili kuvutia wawekezaji ni lazima kuondolewe urasimu katika utoaji wa huduma wanazozihitaji.
“Kwa msingi huo, ndani ya siku 100 za mwanzo za uongozi wangu, nimeshafanya vikao mbalimbali na uongozi wa ZIPA na wa taasisi nyingine za serikali zinazoshughulikia masuala ya uwekezaji, lengo langu ni kuhakikisha kwamba ZIPA ina uwezo wa kutoa huduma zote za wawekezaji katika sehemu moja na kwa kipindi kifupi.
“Kwa maana ya kwamba inakuwa ‘One Stop Centre’ kivitendo na si kinadharia, nimeshatoa maelekezo kwa wakuu wa taasisi mbalimbali, ikiwamo ZRB, TRA, Uhamiaji na nyinginezo zinazoshughulikia masuala ya Mazingira na Ardhi kwamba wawe na watednaji kwenye Ofisi ya ZIPA wenye uwezo wa kutoa huduma na uamuzi wa kitaasisi kwa wawekezaji bila ya nenda – rudi”, anasema Rais Dk. Mwinyi katika hotuba yake hiyo.
Katika hotuba ya ufunguzi wa hoteli hiyo ya kisasa, Dk. Mwinyi amewataka watendaji wa serikali kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma ili kuhakikisha matatizo yanayowakabili wawekezaji yanapungua au kuondoka kabisa.
Rais Dk. Mwinyi anasema serikali imekuja na sera ya kuvutia wawekezaji, hivyo mtendaji yeyote atakayekwenda kinyume au kukwamisha azima hiyo atalazimika kuwa nje ya serikali.
Anasema hatua ya serikali ya kuleta mabadiliko kiutendaji katika kipindi kifupi kijacho, inalenga kuvutia wawekezaji na kubainisha kuwa wawekezaji wanahitaji utendaji wa kisasa.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi anasema kuwa tayari serikali anayoiongoza imeanza kuchukua hatua hususan kwa taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi pamoja na kuhakikisha utendaji katika sekta binafsi unahamia serikalini.
Anasema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane kwa kushirikiana na sekta binafsi itahakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo ametumia fursa hiyo kuwahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza bila hofu kushirikiana na serikali katika kupanga na kutekeleza miradi kwa njia ya PPP.
“Utaratibu huu umekuwa ukitumiwa sana na kupendwa na wawekezaji katika nchi mbalimbali kwa njia ya Public Private Partneship (PPP) ”, anasema Rais Dk. Mwinyi.
Anasema kuwa ujenzi wa hoteli hiyo unakwenda sambamba na dhamira ya serikali ya kuimarisha sekta ya utalii, usafirishaji pamoja na biashara.
Anaongeza kwamba kwa kipindi kirefu wasafiri wengi wanaotaka kusafiri nyakati za asubuhi wamekuwa wakisumbuka kupata malazi ya uhakika karibu na kiwanja cha ndege kama ilivyo katika viwanja vingine vya kimataifa.
Anasema kuwa hoteli hiyo hivi sasa itaweza kutoa huduma hizo, ikiwa na miundombinu muhimu na ya kisasa itakayowawezesha kupata huduma muhimu zinazotolewa na mashirika ya ndege hapa nchini, hivyo kuongeza idadi ya wageni.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi anaonyesha kufarijika na kusema kwamba mbali ya kuwapo changamoto mbalimbali katika sekta ya utalii zinazotokana na kuzuka kwa maradhi ya COVID 19, bado wawekezaji wa sekta hizo kwa kushirikiana na serikali wameendelea kuwekeza mitaji mikubwa hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi ametoa pongezi kwa Kampuni ya Estim Construction kwa umakini na umahiri mkubwa katika ujenzi wa jengo hilo ambalo pamoja na mambo mbalimbali lina kumbi kubwa za kupendeza kwa ajili ya mikutano ya kitaifa na kimataifa.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi nilikutana na viongozi waliowakilisha sekta binafsi kwa lengo la kujadiliana, kubuni na kutafuta njia bora za kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuijenga nchi yetu.
“Serikali ya Awamu ya Nane itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa, ushirikiano na umoja wetu ndio utakaotuwezesha kutekeleza miradi yenye tija, ikiwamo uendelezaji wa viwanda, utalii na uchumi wa bluu. Ili kufanikisha azima hii, serikali itaweka mifumo rafiki kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi. Kadhalika, serikali itaweka mazingira rafiki kwa wanadiaspora kuja kuwekeza nyumbani kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi tunayoyakusudia kuyafanya,” anasema Rais Dk. Mwinyi.
Hayo ni maelezo aliyoyatoa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wakati akitoa hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi Novemba 11, 2020, ambapo mbali ya hayo aliongeza kuwa ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi dhamira ya kufanya mageuzi ya kiuchumi, lazima pawe la ushirikiano mzuri na wa kuaminiana baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.