*Mtandao wa kumpinga Rais Samia ‘wafukiziwa moshi’
*Waahirisha vikao vya kupinga chanjo, waanza kuogopana
*Askofu Gwajima atwishwa msalaba, Rais Samia aonya 2025
*Katibu Mkuu asema hakuna mkubwa kuliko chama, watajuta
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Baada ya kuchapisha habari za uwepo wa mtandao uliojengwa na Rais John Magufuli bila kujua akidhani anakijenga Chama Cha Mapinduzi (CCM- Mpya), JAMHURI limebaini kuwa ‘mamluki’ waliojipenyeza kwenye mtandao huo bila kuwa na nia thabiti ya kuitumikia nchi wameanza kubanwa.
Viongozi waandamizi wawili walioomba wasitajwe majina, kwa nyakati tofauti wameliambia JAMHURI kuwa CCM haiwezi kuwavumilia watu wanaoanzisha makundi yenye malengo binafsi ndani ya chama.
“Tunafahamu kuwa kuna watu walipewa madaraka na vyeo vinavyowazidi uwezo. Hadi sasa wapo wasiojua hatima yao itakuwaje. Ndiyo maana walianza vikao kwa kushawishiwa na wachache waliowaahidi kuwa watalinda masilahi yao.
“Chama kimekusanya orodha na kinawafahamu wote kwa majina. Kama alivyosema Katibu Mkuu, Daniel Chongolo, kwenye mkutano na waandishi wa habari Agosti 12, 2021 tayari kazi kubwa imeanza kufanyika. Hawa wameyataka wenyewe. Watafukiziwa moshi kwenye shimo hadi watoke wenyewe,” amesema ofisa mmoja mwandamizi.
Ameliambia JAMHURI kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kuendelea na “viongozi hawa waliopeana nafasi, wakati mwingine bila Rais Magufuli kujua kama nilivyokwambia wiki iliyopita. Rais hawezi kufahamu kila mtu. Wasaidizi wake walipenyeza watu wengi wasio na sifa. Sasa ndio hao wanaojiunda kukusanya fedha wakidhani wataweka mtu wao atakayelinda masilahi yao mwaka 2025.
“Hawapendi kuona utawala wa sheria unafanya kazi. Wengi walizoea vya kunyonga, hivyo vya kuchinja hawaviwezi. Matukio kama ya Sabaya (aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai) na Mwakabibi (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Temeke) kufikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka yanawaweka matumbo joto.
“Sasa hivi wanasubiri saa, dakika na sekunde. Hawana uhakika nani atafikishwa mahakamani lini, iwapo walitumia vibaya nafasi walizopewa. Wangependa kuendelea hivyo hivyo kuumiza watu na kutisha watu, ila sasa wanaona nchi inatawaliwa kwa mujibu wa sheria chini ya Rais Samia, hili linawakera. Linawakosesha fursa ya kutisha watu wakapata fedha,” ameongeza.
Ofisa mwingine amesema: “Hapa tatizo kubwa ni moja tu. Tunao baadhi ya viongozi, tena katika ngazi ya wizara, mikoa na wilaya, ambao nyadhifa walizonazo na uwezo wao tofauti ni dunia na mbingu. Kinachowasibu sasa ni jambo moja tu. Wanajiuliza hizi nafasi wataendelea nazo? Badala ya kuthibitisha uwezo wao, wanajiingiza katika hujuma, hili litawagharimu.
“Nadhani fursa aliyowapa Mama [Rais Samia] sasa imetosha. Rais apange vizuri serikali yake. Mawaziri wangeangalia Waziri Mkuu [Kassim Majaliwa] anavyochapa kazi nao wakaiga utendaji wa namna hii. Hivi sasa ukiniuliza kuna mawaziri ambao kazi yao ni kugombana na manaibu wao tu wizarani. Kila jambo analoanzisha Naibu Waziri hata kama ni zuri kiasi gani, wao wamejipanga kulipinga. Bahati mbaya, hawana mawazo mbadala… Mama [Rais Samia] anapaswa kubadili gia haraka,” kimesema chanzo chetu kingine.
Mbunge anayetoka katika moja ya majimbo ya Dar es Salaam, ambaye kwa miaka mitano hakuwa chaguo la uongozi uliopita kutokana na msimano wake, amesema: “Kaka, hapa kinachotokea ni sawa na msiba wa Uswahilini. Akifa baba mwenye nyumba wapangaji wote wanalia. Maana unakuta baba mwenye nyumba ndiye anafahamu kula ya wapangaji wake, ada za watoto, matibabu, kimsingi wao wanaona maisha bila baba mwenye nyumba nao hawapo.
“Lakini ngoja nikwambie jambo. Hawa unaoona wanaunda mtandao, wakati wa uongozi wa Rais [John] Magufuli hawakuwa pamoja na Mama Samia. Walikuwa wanamdharau, hawamsalimii, wanasusa ziara zake, akiwaelekeza jambo wanamgomea… hata yeye aliishasema kuwa kuna jambo alipolieleza akaona limemzidi kimo akakaa kimya.
“Hawakupata kuwaza kuwa ipo siku Rais Magufuli angeondoka na walikuwa na uhakika kuwa akiondoka, basi atawaachia mwingine wa kuwashika mkono. Sisi wanadamu hatuwezi kuingilia mapenzi ya Mungu, ila sasa hawa wenzangu na mimi, wanapaswa kufahamu na kukubali kuwa Rais Magufuli ameishafariki dunia. Wasimsononeshe huko aliko. Wamheshimu Mama Samia na waache harakati za siasa, sasa hivi wachape kazi. Huu ni muda wa kutekeleza Ilani ya CCM si wa kuwaza madaraka ya 2025.
“Lakini pia ingawa si jukumu langu, naomba niwashauri hawa wenye nia ya 2025. Jambo moja wanapaswa kulifahamu ni kuwa kama alivyosema yeye Rais Samia, kwa neema na mapenzi ya Mungu 2025 katika vikao vya uamuzi ndiye atakuwa mwenyekiti wa vikao vya uamuzi ndani ya CCM. Sasa hizi harakati wanazofanya watapita wapi? Inahitaji akili ya kawaida tu, kulifahamu hilo,” amesema mbunge huyo.
Sehemu ya kilichoandikwa wiki iliiyopita
Kuna fukutoa kubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa kutokana na mtandao uliojengwa na Rais John Magufuli wakati wa uongozi wake wa miaka mitano na miezi minne Ikulu, ambao kwa sasa unaamini ‘tonge’ linawatoka mdomoni kutokana na mwelekeo mpya wa siasa nchini, JAMHURI limebaini.
Chanzo cha kuaminika kinasema mtandao huo uliopenyezwa katika siasa na nafasi nyeti katika utumishi wa umma unajipanga kwa nguvu kubwa na sasa unamchimba chini kwa chini Rais Samia Suluhu Hassan, ukitaka kujenga upya himaya yao iliyobomoka baada ya kifo cha Rais Magufuli Machi 17, 2021.
“Hawa mamluki waliotoka kusikojulikana wakapewa nafasi kubwa na madaraka katika siasa na utumishi wa umma ndio hatari kubwa kwa sasa. Matukio tunayoyaona yenye lengo la kumhujumu Rais Samia, walianza kujipanga siku nyingi. Kwanza hawakufahamu kuwa Rais Magufuli angefariki dunia kabla ya kumaliza muda wake.
“Pili, walidhani hata kama angekuwapo ukwasi walioukusanya wangeutumia kumweka madarakani mtu wao wanayemtaka. Tumesikia mara kadhaa wanajigamba kujenga ngome ya kikanda. Wanatukuza ukabila na kuutumia kama nguvu ya kuwaunganisha. Mwalimu [Julius] Nyerere alikemea kwa nguvu kubwa ukabila, lakini kwa bahati mbaya watu aliowaamini Rais Magufuli walikuwa wanaitumbukiza nchi hii katika ukabila.
“Hesabu idadi ya watu waliowapa madaraka katika vyombo na taasisi mbalimbali. Ukisikia Rais ameteua, si kweli kwamba watu wote anakuwa anawafahamu, hapana. Wengine analetewa majina mezani yakiwa yamepambwa kwa sifa nyingi na kutokana na mambo mengi anayokuwa nayo anajikuta ameteua watu kwa ukabila au udini bila yeye kujua. Wasaidizi ni watu hatari sana.
“Wakati wa Uchaguzi Mkuu ilikuwa kufuru. Wapo watendaji wawili ndani ya CCM waliotumia muda huo kukusanya mabilioni. Zaidi ya asilimia 40 ya wabunge na madiwani walipita kwa nguvu na walikusanya fedha kutoka kwao. Ilikuwa wanawahakikishia kuwa ukitoa ‘mzigo’ unapata ubunge au udiwani, na wengi walifanya hivyo.
“Hizi fedha ilikuwa wanazikusanya na kumkabidhi [jina linahifadhiwa] ambaye ni mfanyabiashara mkubwa Kanda ya Ziwa. Na sasa hivi wamefanya vikao wamekubaliana wawe na mradi wa mgombea wao 2025. Ndio hao unasikia kila wanapokuwa wanatoa maagizo na matamko… hawa ni shida kubwa kwa sasa. Ukitaka kufahamu vema mpango mzima mtafute yule kijana aliyetimuliwa pale CCM kwa kukataa kushiriki hujuma. Sasa hivi ameajiriwa katika ofisi nyeti, anayafahamu vema madudu yao hawa watu,” anasema mtoa habari wetu.
Waahirisha vikao vya kupinga chanjo, waanza kuogopana
JAMHURI limefuatilia kwa karibu kundi lililokuwa limeandaliwa kusimama kidete kupinga chanjo na kubaini kuwa limeanza kusambaratika. Gazeti hili limefahamishwa kuwa moja ya mkakati wa kumsumbua Rais Samia, kundi hili lililokuwa linajiunda ndani ya CCM lilitaka baadhi ya wabunge na mawaziri watumie majukwaa kadhaa kupinga chanjo.
“Walitaka chanjo ionekane haifahi, ni hatari. Wanafanya hivyo kutetea msimamo wa aliyewateua kuwa kujifukiza na maombi vinaondoa corona nchini. Wanaona kama Rais Samia kukiri kuwa corona ipo nchini amepingana na msimano wa Rais Magufuli aliyefariki dunia, wakati uhalisia Rais Samia amesimamia dhana ya ukweli na uwazi.
“Kwa hiyo katika vikao vyao walijipanga kuwa ‘wanalipuka’ iwe kwenye nyumba za ibada au kwenye sherehe katika sehemu mbalimbali za nchi. Baada ya kuona mpango wao umefahamika sasa wanaogopana kama ukoma. Hata wakipigiana simu za kawaida hawapokei, utasikia wanaambizana ‘whatsapp, whatsapp, whatsapp’. Hii ina maana wameingiwa hofu na hata kukutana hawakutani tena sasa,” amesema mtoa habari wetu.
Askofu Gwajima atwishwa msalaba
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa Bunge Ijumaa, ilimtaka Mbunge wa Kinondoni (CCM), Askofu Josephat Gwajima kufika mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge bila kukosa ajitetee. Gazeti la Mzalendo Jumapili lilibainisha kuwa Gwajima anaitwa bungeni kujibu tuhuma za kusema uongo na kulidhalilisha Bunge.
JAMHURI limemtafuta Askofu Gwajima kuzungumzia tuhuma hizi bila mafanikio. “Askofu Gwajima kuitwa bungeni ametwishwa msalaba wa kwanza… acha akajieleze, ila akibainika kuwa naye yupo katika kundi la wanaompinga Rais Samia, basi ujue naye atafukiziwa moshi,” alisema mbunge mwingine.
Kupitia mahubiri kwa waumini wake juzi Jumapili, Gwajima alisema wanaompotosha Rais Samia ni Waziri na Naibu Waziri wa Afya katika suala la chanjo. Alisema angekwenda Dodoma mbele ya Kamati ya Bunge kujitetea jana. Amesisitiza kuwa anamuunga mkono Rais Samia tofauti na maelezo yanayotolewa kuwa anampinga.
Aliwaombea Rais Samia, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Naibu Spika na viongozi wa ngazi zote hadi kwenye kata.
Alisema amefunga mjadala wa chanjo hatazungumzia tena suala la chanjo isipokuwa labda akichokozwa, ndipo atarejea. Aliwataka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima na Naibu Waziri wake, Dk. Godwin Mollel, wajiuzulu kwani walimshauri vibaya Rais kuwa watu wasichanjwe na sasa watu wale wale hawawezi kushauri watu wachanje wakaeleweka.
Rais Samia aonya 2025
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita amepokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ambapo ameungana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage kusema kuwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 yaanze sasa.
Katika kuashiria kuwa ana nia ya kugombea urais mwaka 2025, Rais Samia alitumia maneno “wagombeaji wenzangu,” akimaanisha kuwa naye yumo mwaka 2025 tofauti na ilivyoandikwa na Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Uhuru la Agosti 12, 2021 kuwa hana mpango wa kugombea urais mwaka 2025.
“Mwisho wa uchaguzi mmoja, ni mwanzo wa uchaguzi mwingine. Hivyo twende tukajipange kwa uchaguzi wa mwaka 2025. Na ninavyosema tukajipange si kujipanga kugombea, kujipanga tume iweze kufanya kazi zake vizuri na kupanga mipango yake. Kwa hiyo wale wagombeaji wenzangu, sisemi tukajipange kugombea mapema. Atakayejipanga sheria zipo. Niombe uchaguzi ujao uwe bora na mzuri zaidi, kwa kuzingatia mapendekezo yatakayotolewa na wadau…”
Awali Rais Samia alitaka Sheria ya Uchaguzi wa Taifa Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura 292 kupitiwa kuangalia uwezekano wa Uchaguzi Mkuu na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na mamlaka moja kama ilivyopendekezwa na tume.
Suala la kuwa na watendaji wa tume mpaka kwenye ngazi ya halmashauri na serikali kutoa fedha kwa asasi za kiraia zinazotoa elimu kwa mpigakura, alisema hayo yaangaliwe kwa uangalifu kwani yanaweza kuwa na gharama kubwa isiyohimilika.
“Mapendekezo yote haya ni ya msingi… Hatuna budi kuziangalia sheria zetu, ili zisitumike kuwanyima watu haki kwa masuala ya kiufundi. Mathalani pale mtu anapokosea kuandika herufi za jina lake au herufi za chama chake. Nadhani mipango ingewekwa vizuri zaidi, ili (makofi), nilijua vyama vya siasa mtashangilia hilo. Nilijua mtashangilia hili kwa sababu tuliwashughulikia kweli kweli kwenye uchaguzi uliopita. Kila mlipokosea, tuliwaweka chini, na mkatupa fursa ya kupita bila kupingwa. Tutaliangalia vizuri hili. Lakini na nyie muwe makini basi. Muwe makini, vinginevyo…” Rais Samia alitaka vyama vya siasa kuwapa nafasi wanawake katika nafasi za kugombea kwa nia ya kuongeza idadi ya wanawake wanaochaguliwa.
Katibu Mkuu asema hakuna mkubwa kuliko chama, watajuta
Akizungumza na waandishi wa habari, Agosti 12, 2021, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema anaufahamu mtandao wote unaojipanga kumhujumu Rais Samia, ila hautafika popote. Wakati anajibu swali la mwandishi wa Dar Mpya, alisema:
“Umeeleza kuhusu kauli kinzani, dhidi ya msimamo wa chama na serikali. Serikali zote hizi ni za Chama Cha Mapinduzi. Niseme, chama ni kikubwa kuliko mtu yeyote. Hata mimi Katibu Mkuu wa chama hiki, nimepewa dhamana tu. Sina mamlaka ya kuweka ya kwangu na kubeba ajenda zangu.
“Chama hiki kimeweka utaratibu wa kuhangaika na mimi, nikianza kufanya mambo ya hovyo. Sasa sijui kwenye chama hiki leo hii baada ya mwenyekiti na makamu wa Zanzibar na Tanzania Bara, anayefuata kwa ukubwa ni nani? Ni mimi. Kama mimi nina fursa ya kuchukuliwa hatua, nani mkubwa zaidi?
“Kwa hiyo mtu asifikirie hapa kuna mtu ana uwezo wa kuota pembe, zikawa ndefu kuliko waliowahi kuota huko nyuma. Na ninyi mnajua historia, chama hiki kimekuwa kikichukua hatua, katika mazingira ambayo kila mmoja anapanua mdomo na kushangaa. Na hao unaofikiria wanaweza wakafikiria fikiria hivi, kushindana au kukijaribu chama hiki, chama hiki kina utaratibu, na taratibu zimeanza, subiri matokeo.”
Baadhi ya wanachama waliozungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, waliomba viongozi wa kisiasa watulie wamuunge mkono Rais Samia ambaye ameonyesha kuongoza chama kwa utratibu wa kufuata sheria, huku akiwa na huruma kwa wanyonge, wameomba asisumbuliwe.